WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameahidi kupokea kundi la watalii wasiopungua 300 ambao wanatarajiwa kuwasili nchini Machi, mwaka huu. Watalii hao ni kundi la kwanza miongoni mwa watalii 10,000 wanaotarajiwa kuwasili nchini katika mwaka 2019 chini ya mpango unaosimamiwa baina ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Bodi ya Utalii Tanzania na kampuni ya TouchRoad International Holding Group ya China.
Ametoa ahadi hiyo Januari 19, 2019 alipokutana na Mwenyekiti wa Touchroad Group, Bw. Liehui He na Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii, Jaji Thomas Mihayo ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma. Waziri Mkuu amefikia uamuzi huo baada ya kuelezwa na Bw. He huyo kwamba kundi hilo la watalii likiwa Djibouti litapokelewa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo na likienda Zimbabwe, litapokelewa na Rais wa nchi hiyo.
“Tanzania imeamua kuweka mkakati wa kuongeza idadi ya watalii nchini kwa kuboresha miundombinu ya usafiri na kukuza utalii kupitia vivutio vya vyakula vya asili, mavazi ya asili, wanyama, fukwe za bahari na milima. Kwa hiyo, ujio wa kundi hili kubwa, unatoa fursa mpya ya kutangaza vivutio vya nchi yetu,” amesema.
“Nitoe wito kwa Watanzania wanaoishi maeneo ya jirani na vivutio vyetu, wachangamkie fursa ya ujio wa watalii hawa katika maeneo mbalimbali. Wakifika Dar es Salaam, wanaweza kwenda Kigoma kuona Ziwa Tanganyika, mbuga zilizoko Nyanda za Juu Kusini, Arusha au vivutio vya Zanzibar. Tujiandae, tuwe tayari kuwauzia bidhaa mbalimbali,” amesema.
Pia amesema amefurahishwa na wazo lao la kuifanya Dar es Salaam iwe kitovu cha utalii (tourist hub) kwa makundi ya watalii ambayo yatakuja Tanzania na baadaye kutoka Tanzania kwenda Lusaka, Harare, Johannesburg na Djibouti.
Mwenyekiti huyo ambaye aliwasili nchini juzi, ameambatana na ujumbe wa watu 31 ambao unajumuisha waandishi wa habari, wasanii, wanamuziki na watu mashuhuri.
Akiwa Beijing, China, wakati akishiriki mkutano wa Jukwaa la Biashara baina ya Tanzania na China lililofanyika Septemba mwaka jana, Waziri Mkuu alikutana na uongozi wa kampuni ya TouchRoad ambayo ilionesha nia ya kutangaza fursa za utalii zilizopo hapa nchini. Ziara ya Bw. He ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano yaliyoingiwa kati ya kampuni ya TouchRoad na Bodi ya Utalii ya Tanzania, Novemba 2018.
Mapema, Bw. He alimweleza Waziri Mkuu nia ya kampuni hiyo kutekeleza makubaliano yao ya kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania katika soko la China ili kuvutia watalii wapatao 10,000 waitembelee Tanzania katika mwaka 2019.
“Tumepanga kuleta watalii 10,000 kwa mwaka huu wa 2019 na tumeweka lengo la kuongeza idadi hiyo kwa asilimia 20 kila mwaka kwa muda wa miaka mitano. Pia tuna lengo la kuitumia ndege ya ATCL ili ilete watalii moja kwa moja kutoka Shanghai, China,” alisema.
Akielezea ujio wa kundi la kwanza la watalii, Bw. He alisema kundi hilo litakaa Djibouti kwa siku moja, Tanzania siku nne (tatu za kulala) na Zimbabwe siku tatu (mbili za kulala) na kisha kurejea China.
Alisema wanapanga kila mwezi wawe na kundi kubwa la watalii ambao watakuwa wanafikia Tanzania na kupelekwa nchi nyingine kwa sababu Wachina wengi hupenda kufanya utalii kwa siku walau 10, lakini wapelekwe maeneo matatu au manne tofauti kuona vivutio vya aina nyingine badala ya kukaa sehemu moja kwa kipindi chote hicho.
“Watalii hawa wakija kwa siku tatu au nne, wana uhakika wa kutumia dola za Marekani zaidi 2,000, wakienda eneo jingine watatumia fedha pia, namna hiyo tuna uhakika wa kuongeza pato la Taifa, lakini pia tuna uhakika wa kutengeneza ajira kwa Watanzania,” alisema.
No comments:
Post a Comment