UJENZI OFISI ZA WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO MJI WA SERIKALI IHUMWA DODOMA WAENDELEA KWA KASI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 14 January 2019

UJENZI OFISI ZA WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO MJI WA SERIKALI IHUMWA DODOMA WAENDELEA KWA KASI

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Susana B. Mkapa (kulia), akisalimiana na Mbunifu Majengo wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Msafiri Msaki, alipofika kukagua ujenzi wa Ofisi za Wizara hiyo Katika Mji wa Serikali eneo la Ihumwa Jijini Dodoma.

Muonekano wa Jengo la Ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango Katika Mji wa Serikali eneo la Ihumwa Jijini Dodoma.

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dk. Philip Isdor Mpango (Mb), (kulia), akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Susana B. Mkapa, alipotembelea na kukagua ujenzi wa Ofisi za Wizara hiyo Katika Mji wa Serikali eneo la Ihumwa Jijini Dodoma.
Na Peter Haule, WFM, Dodoma
WAZIRI wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango amelitaka Shirika la Nyumba lililopewa kandarasi ya kujenga Jengo la Ofisi za Wizara hiyo katika Mji wa Serikali-Ihumwa, Jijini Dodoma, kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati na ofisi hizo zinaanza kutumika mapema mwezi Februali Mwaka huu.
Dk. Mpango ametoa rai hiyo alipofaya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Ofisi hizo zitakazogharimu zaidi ya shilingi bilioni moja.
Amesema kuwa licha ya kuwa ujenzi unakwenda vizuri lakini ni lazima Mkandarasi aongeze bidii ya ujenzi kwa kuwa vifaa vyote vinavyohitajika vipo ikiwemo pia raslimali watu ambayo ipo tayari kufanya kazi na kujiongezea kipato.
"Nataka kutumia Ofisi hii ifikapo Februari na nitakuja na kiti changu hapa tayari kuchapa kazi" alisema Dk. Mpango
“Kwangu mimi ujenzi unaoendelea una umuhimu mkubwa kwa kuwa watu wanapata ajira, hivyo ni vema kuendelea kuhakikisha kunakuwa na raslimali hiyo kwa idadi inayotakiwa itakayosaidia kuhakikisha ifikapo Januari, 31, mwaka huu ujenzi uwe umekamilika,” alisema Dk. Mpango.
Aidha amepongeza jitihada zinazofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa hatua waliyofikia, kwa kuwa tayari hatua ya ujenzi wa kuta ipo katika hatua za mwishoni na kilichobakia ni kupiga plasta na baadae kupaua.
Kwa upande wake Mbunifu Majengo wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Msafiri Msaki, ameahidi kuhakikisha kazi hiyo inamalizika kwa muda uliopangwa kwa kuwa kwa sasa hatua ya ujenzi ipo ndani ya muda.
Hata hivyo ameitaja changamoto iliyojitokeza kuwa ni pamoja na maji kutopatikana kwa wakati kwa baadhi ya siku kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni kupasuka kwa mabomba.
Dk. Mpango aliagiza wasimamizi wa ujenzi huo kuhakikisha tatizo hilo linatafutiwa ufumbuzi haraka iwezekanavyo ili kutokua kikwazo katika ukamilishaji wa ujenzi wa ofisi hizo.
Baadhi ya vijana wa kike na wa kiume wameelezea kufurahishwa na ajira zinazopatikana kwenye eneo la ujenzi wa majengo ya ofisi za Serikali katika eneo hilo la Mji wa Serikali Ihumwa, na kuwataka vijana wenzao kuchangamkia fursa mbalimbali za ajira katika eneo hilo.

No comments:

Post a Comment