Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa tatu kulia) akisikiliza
kwa makini taarifa kutoka kwa Afisa Mtendaji Kata ya Katwe, Wilaya ya
Sengerema, Mwanza, Deus Ngodagula Masasi (aliyenyoosha kidole) kuhusu ukosefu
wa mawasiliano kwenye kisiwa cha Maisome wakati wa ziara yake ya kukagua hali
ya mawasiliano wilayani humo. Naibu Katibu Mkuu – Sekta ya Mawasiliano Dkt. Jim
Yonazi (aliyeshika ramani) akiwa na Mkurugenzi wa Uendeshaji, UCSAF, Mhandisi
Albert Richard (wa kwanza kushoto).
Naibu Katibu Mkuu –
Wizara Ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Sekta ya Mawasiliano Dkt. Jim Yonazi
(katikati) akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano
Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza kulia) wakati wa ziara yake ya kukagua
changamoto ya mawasiliano kisiwani Maisome, Mwanza. Anayesikiliza wa kwanza
kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya TCRA, Dkt. Jones Kilimbe.
MKURUGENZI Uendeshaji
wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Mhandisi Albert Richard amemweleza
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye kuwa UCSAF
imeleta changamoto chanya kwa kampuni za simu za mkononi zinazotoa huduma za
mawasiliano nchini.
Richard ameyasema hayo
wakati wa ziara ya Nditiye ya kukagua changamoto za mawasiliano kwenye maeneo
mbali mbali wilayani Sengerema mkoani Mwanza.
Richard amefafanua kuwa awali kampuni za simu za mkononi nchini zilisita
kuwekeza kwenye vijiji mbali mbali ambavyo havina mawasiliano nchini kwa kuwa
havina mvuto wa kibiashara ambapo kampuni hizo zilikuwa zinakwenda maeneo ya
mijini yenye mvuto wa kibiashara.
“Ila sasa Serikali
kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano tunashirikiana na kampuni za
simu za mkononi kufikisha huduma za mawasiliano vijijini na kampuni zimepata
mwako,” amesema Richard. Ameongeza kuwa Serikali imekuwa inatoa ruzuku kwa
kampuni hizo ili waweze kujenga minara kwa lengo la kuhakikisha kuwa wananchi
wanapata huduma za mawasiliano.
Nditiye amesema kuwa
amefanya ziara ya siku tatu ya kukagua mawasiliano kwenye maeneo mbali mbali
wilayani Sengerema ili kuona changamoto za mawasiliano ambapo amekiri uwepo wa changamoto
za mawasiliano kwenye Wilaya hiyo kwenye baadhi ya kata ambapo ina jumla ya
kata 21 na kubaini uwepo wa ukosefu wa mawasiliano kabisa kwenye baadhi ya maeneo,
mawasiliano ya kusuasua na mahitaji ya kuongeza nguvu ya usikivu wa mawasiliano
kwenye baadhi ya maeneo.
Pia, amekiri kuwa
wameshindwa kufika moja kwa moja kwenye kata ya kisiwa cha Maisome ambapo kuna
wananchi wengi wanaoishi huko na hawana mawasiliano kwa kuwa kisiwa hicho
kinasomeka kwenye ramani kuwa ni hifadhi ya misitu ambapo kampuni ya Halotel
wamepata ruzuku kutoka UCSAF ya kujenga minara ya kufikisha mawasiliano kwenye
kisiwa hicho.
“Nimemwelekeza Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Sekta ya Mawasiliano,
Dkt. Jim Yonazi aonane na Wizara husika ya Maliasili na Utalii na taasisi ya
misitu ya TFS ili waweze kupata kibali cha kuiwezesha Halotel kujenga minara,”
amesema Nditiye.
Nditiye ameilekeza
UCSAF na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wafanye tathmini ya hali halisi
ya mawasiliano wilayani Sengerema. Pia, washirikiane kwa pamoja na kampuni za
simu za mkononi kuongeza nguvu za mawasiliano kwenye maeneo mbali mbali ambayo
hayana mawasiliano, kujenga minara kwenye maeneo ambayo hayana mawasiliano
kabisa au kuweka minara mingine ya ziada kwa kuwa mawasiliano ni ulinzi na
usalama, mawasiliano ni uchumi.
Naye Dkt. Yonazi
amesema kuwa amezingatia maelekezo na wataboresha mawimbi ili wananchi
waendelee kupata mawasiliano katika eneo la Buchosa na tutaendelea kuboresha
usikivu wa mawasiliano na kufikisha
mawasiliano kwenye maeneo ambayo hakuna mawasiliano kabisa. Ameongeza kuwa
tutaendelea kutoa elimu kwa wananchi na tutashirikiana na TCRA ili kuhakikisha
ubora wa mawasiliano kwa wananchi unaboreshwa.
Mwenyekiti wa Bodi ya
TCRA, Dkt. Jones Kilimbe amesema kuwa tumefika Buchosa na tumeshuhudia wenyewe
hali ya mawasiliano Buchosa na tumeona kuna baadhi ya sehemu hakuna mawasiliano
kabisa na kwingine nguvu ya mawasiliano ni ndogo na ziara hii itatuwezesha
kufanyia kazi changamoto hizi sehemu mbali mbali nchi nzima.
“Ni jukumu letu
kuhakikisha wananchi wanapata huduma za mawasiliano hususani kuwahudumia
wananchi wanaoishi vijijini,” amesema Kilimbe. Ameongeza kuwa mawasiliano ni
maendeleo na ni uchumi, watu wanatumia huduma za mawasiliano ikiwa ni pamoja na
kutuma na kupokea pesa.
Richard ameongeza kuwa
hadi sasa asilimia 94 ya watanzania wanapata huduma za mawasiliano na asilimia
6 iliyobaki ni ya watu wachache ambapo Serikali inaendelea kupata ufumbuzi wa
teknolojia rahisi ya kufikisha mawasiliano na kwa maeneo ya Buchosa ambayo yana
changamoto za mawasiliano zitajumuishwa kwenye zabuni za mwaka 2019 ili maeneo
hayo yapate mawasiliano.
No comments:
Post a Comment