WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini wafuatilie utendaji kazi wa watumishi kwenye maeneo kubaini kama wanakwenda kwa wananchi na kuwahudumia ipasavyo.
‘Serikali inahitaji kuona watumishi wa umma wanakwenda kwa wananchi kusikiliza kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili ili kushirikiana nao katika kuzipatia ufumbuzi’’.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo Januari 3, 2019 wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Lugagala, wilayani Songea akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma.
“Rais wetu Dkt John Magufuli ni muumini wa maadili na mchapakazi ,ndio maana amesisitiza umuhimu wa watumishi wa umma kwenda kuwahudumia wananchi katika maeneo yao, kwani baadhi yao hawana uwezo wa kufikia maeneo ya kutolea huduma.”
Waziri Mkuu aliongeza kuwa ni vema kwa watumishi wa umma wahakikishe wanapanga muda wa siku tatu kwa wiki kutoka maofini kwenda kuwahudumia wananchi hususani waishio maeneo ya pembezoni.
Alitumia fursa ya mkutano huo kuwataka wananchi waendelee kuiamini Serikali yao pamoja na watendaji wake waliopo kwenye maeneo mbalimbali nchini kwani Serikali inatambua matatizo yao na kuahidi kuwa yatapatiwa ufumbuzi kwa wakati.
Waziri Mkuu aliongeza kuwa Serikali haina msamaha na watumishi wazembe, hivyo wananchi waendelee kuwa watulivu na imani kwani watahudumiwa na ahadi zote zilizotolewa na Rais Dkt Magufuli katika maeneo yao zitatekelezwa.
Kadhalika, Waziri Mkuu alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Songea asimamie zoezi la kuwaondoa wananchi wote wanaoishi na kufanya shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo katika maeneo ya vyanzo vya maji kwa sababu watasababisha vyanzo hivyo vikauke.
Awali, Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi katika mradi wa maji wa Luyehela kwenye kijiji cha Muungano Zomba, kuzindua kituo cha kuchotea maji cha kijiji cha Lugagala na kukagua mradi wa ujenzi ya zahanati wa kijiji hicho.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenister Mhagama ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Peramiho na Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga.
Wengine ni Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, Naibu Waziriwa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme na maafisa wengine wa Serikali.
No comments:
Post a Comment