Eneo
la Fuga ni sehemu ambayo mizigo itakuwa ikitelemshwa kwa njia ya reli
itakayotumika kwa ajili ya ujenzi wa mradi kufua umeme katika mto Rufiji katika
Pori la Akiba la Selous katika Kanda ya Matambwe mkoani Morogoro. (PICHA
ZOTE NA LUSUNGU HELELA).
NA LUSUNGU HELELA, MOROGORO
SERIKALI imesema
maandalizi ya miundombinu wezeshi kabla ya kumkabidhi Mkandarasi aliyepewa kazi
katika Mradi wa kufua umeme wa Mto Rufiji tayari imekamilika kwa asilimia
themanini.
Miundombinu hiyo ni
pamoja na maji, umeme, barabara pamoja na nyumba za kukaa wafanyakazi.
Kauli hiyo imetolewa
jana na Mawaziri wa Wizara tano kutoka Nishati, Maliasili na Utalii,
Nyumba, Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Ofisi ya
Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Fedha na Mipango baada ya
kutembelea na kujionea miundombinu hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa
imeshakamilika.
Ziara hiyo katika Pori
la Akiba la Selous kanda ya Matambwe mkoani Morogoro iliongozwa na Waziri wa
Nishati, Dkt.Medard Kalemani ikilenga kukagua hatua zilizofikiwa katika ujenzi
wa miundombinu wezeshi ili kumuwezesha Mkandarasi kuanza kusafirisha mizigo kwa
ajili ya ujenzi wa mradi huo.
Alisema kukamilika kwa
miundombinu hiyo kutamuwezesha Mkandarasi huyo kuanza maandalizi ya awali
ikiwemo kuanza kusafirisha mizigo kuileta katika maeneo ya ujenzi wa bwawa.
Aliongeza kuwa
kutokana na Mkataba uliopo Mkandarasi huyo ataanza kazi rasmi Juni 15 mwaka huu
na ataukamilisha mradi huo ifikapo mwezi April 2022.
Katika upande
wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu alitoa
tahadhari kwa wafanyakazi wanaokuja kufanya kazi katika mradi huo wasiende
kupumzika vichakani kuna wanyama wakali kama vile Simba, Nyati pamoja na
tembo.
" Wale wenye
tabia ya kujipumzisha vichakani baada ya kufanya kazi chonde chonde jiepusheni
na haya mazoea la sivyo mtaliwa na Simba.
Aidha, Mhe.Kanyasu
alitumia fursa hiyo kuiomba Wizara ya Utumishi kutoa kibali cha kuajiri Askari
Wanyamapori zaidi ya 200 ambao watatoa ulinzi kwa Wafanyakazi wa mradi huo,
Ombi hilo linakuja
kufuatia Askari wanyamapori 115 kutoka mapori mengine kuhamishiwa kwa
muda katika Pori hilo katika kanda ya Matambwe kwa lengo la
kuongeza nguvu baada ya askari 115 waliokuwepo kuonekana hawatoshi.
Hata hivyo ,
Mhe.Kanyasu alisema hatua za haraka zimeanza kuchukuliwa ikiwa ni
pamoja kutengeneza vyoo, malazi pamoja na maji kwa vile miundombinu
iliyokuwepo katika Kanda hiyo ilikuwa na uwezo wa kuhudumia Askari Wanyamapori
85 tu lakini hadi hivi sasa kuna jumla ya askari 230.
Kukamilika kwa mradi
huo wa kufua umeme, Bwawa hilo la Rufijin litakuwa la nne kwa ukubwa kwa Afrika
na la kwanza kwa Afrika Mashariki, Duniani ni la 60 katika ya mabwawa sabini
makubwa.
No comments:
Post a Comment