Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS),
mkoa wa Mwanza Mhandisi Marwa Rubirya
(watatu kushoto), akimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Elias John Kwandikwa
(wapili kushoto) eneo litakapojengwa daraja jipya linalounganisha
Kigongo-Busisi mkoani Mwanza, daraja hilo litakuwa na urefu wa KM 3.2 (kulia)
ni mkuu wa kivuko cha Kigongo-Busisi mhandisi Abdala Atiki.
NAIBU Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Elias John Kwandikwa amewataka wakazi wa mikoa ya Mwanza na Geita kuchangamkia fursa za kiuchumi na kijamii zitakazojitokeza wakati wa ujenzi wa daraja litakalounganisha eneo la Kigongo na Busisi Mkoani Mwanza.
Amesema maandalizi kwaajili ya ujenzi wa daraja
hilo la aina yake hapa nchini yako katika hatua ya usanifu wa kina hivyo ujenzi
wake utaanza mara baada ya mkandarasi wake kutangazwa na linatarajiwa kuwa na
urefu wa kilomita 3.2, litakapokamilika.
“Hakikisheni mnatoa ushirikiano kwa mkandarasi ili
kazi ya ujenzi iwe nyepesi na wale watakaopata fursa za ajira fanyeni kazi kwa weledi,
bidii na nidhamu,” amesisitiza Naibu Waziri Kwandikwa.
Amesema Serikali inatumia fedha nyingi katika
miradi ya maendeleo ya muda mrefu hivyo ni jukumu la wananchi kujiandaa na
kubaini fursa za kiuchumi na kijamii na kuzitumia.
Naye Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa
Mwanza Mhandisi Marwa Rubirya amesema daraja hilo litakuwa na njia nne za kupitisha magari, njia ya waenda kwa miguu
ambapo pia litakuwa na kina kitakachoruhusu meli kupita chini ya daraja hilo.
Mhandisi Rubirya amesisitiza umuhimu wa wananchi
wenye maeneo yatakayotumika kupisha ujenzi huo kutoa ushirikiano ili
kuharakisha kazi hiyo.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kwandikwa amekagua
kivuko cha Kigongo-Busisi na kuagiza Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA),
kuhakikisha elimu inatolewa kwa wananchi kuhusu usalama na matumizi sahihi ya utumiaji
wa vivuko.
Amezungumzia umuhimu wa TEMESA kuweka mifumo ya
kielektoniki ili kuwezesha waendesha vivuko, wakusanya mapato na wasimamizi kuwa
na mawasiliano ya pamoja na hivyo kuwezesha vivuko kuwa na abiria na mizigo
inayokubalika wakati wote.
Mkuu wa kivuko cha Kigongo –Busisi Mhandisi Abdala
Atiki amesema kivuko hicho kwa sasa kinahudumiwa na Mv- Mwanza na Mv- Misungwi ambapo
zaidi ya abiria elfu sita na mia tano huvushwa kwa siku.
Zaidi ya mikoa 12 nchini ina maeneo yenye mahitaji
ya vivuko ambapo takriban vivuko 30 vinatoa huduma nchini kote.
IMETOLEWA
NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO,
(NOVEMBA 23, 2018).
No comments:
Post a Comment