Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Katavi Mhandisi
Martin Mwakabende, akitoa taarifa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga, kuhusu hatua zilizofikiwa katika ujenzi wa barabara ya Mpanda-Vikonge
yenye urefu wa KM 35 kwa kiwango cha lami, mkoani humo.
KATIBU
Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi
Joseph Nyamhanga, ameuagiza Wakala wa Barabara (TANROADS), kuhakikisha wanatuma
mapendekezo Wizarani ili barabara ya Mpanda -Vikonge yenye urefu wa KM 35
inayojengwa kwa kiwango cha lami iongezwe urefu wa KM 3.
Katibu
Mkuu huyo amesema hivyo lengo likiwa ni kuifikisha
barabara hiyo katika kijiji cha Vikonge badala ya kuishia porini.
Agizo
hilo amelitoa mkoani Katavi, mara baada ya kukagua ujenzi wa barabara
hiyo inayojengwa na mkandarasi
China Railway Seventh Group kwa gharama
ya shilingi zaidi ya bilioni 57 ikiwi ni fedha za Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100.
"Nimeridhishwa
na hatua zinazoendelea za ujenzi lakini barabara hizi zinajengwa kwa ajili ya
wananchi hivyo lazima ujenzi wake uwanufaishe wananchi hao kwa kufika
katika kijiji chenyewe", amesema Mhandisi Nyamhanga.
Amesema
ujenzi wa barabara hiyo umefikia asilimia 66 ambapo mpaka sasa KM 15
zimeshakamilika kwa kiwango cha lami na kazi zingine zinaendelea kukikamilisha
kipande kilichobaki.
Aidha,
Mhandisi Nyamhanga amefafanua kuwa mradi
huu umetoa huduma kwa wananchi wake kwa kuwajengea visima vya maji pamoja na matenki ya uwezo mkubwa wa kubeba
maji katika shule mbili za sekondari.
"Mradi
huu ni mfano mzuri kwa miradi mingine tutaangalia namna ya kuweka katika
mikataba huduma kama hizo kwa jamii", amesisitiza Mhandisi Nyamhanga.
Kwa
upande wake, Kaimu Meneja wa TANROADS mkoa wa Katavi, Mhandisi Martin Mwakabende,
amesema kuwa atamsimamia mkandarasi huyo kukamilisha sehemu iliyobaki kwa
viwango na ubora uliopangwa.
Mradi
wa ujenzi wa barabara ya Mpanda-Vikonge ni sehemu ya barabara kuu ya Ukanda wa
Magharibi yenye urefu wa KM 1042 ambapo Sera ya Serikali ya Awamu ya Tano ni
kuhakikisha inaunganisha mikoa yote nchini kwa barabara za lami pamoja na nchi
jirani.
Imetolewa na Kitengo
cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment