Na Mwandishi Wetu, Arusha
MFANYABIASHARA maarufu jijini Arusha na mmiliki wa viwanda vya Hans Poul, Kamaljit Hanspoul (58) pamoja na wafanyakazi wake watatu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa kwa madai ya kuajiri wafanyakazi (raia wa kigeni) bila vibali vya kazi na kufanya kazi kinyume cha sheria ya uratibu ajira za wageni.
Akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake, Kaimu Afisa Kazi Mfawidhi, mkoani hapa, Willfred Mdumi alisema walikuwa kwenye Operesheni ya kazi walipofika kwenye kiwanda cha Hanspoul walibaini kuwepo wafanyakazi wakigeni wanaofanya kazi kinyume cha sheria kwenye viwanda vya mfanyabiashara huyo.
Aliwataja wafanyakazi hao watatu kuwa ni Shivkumar Vemula (27) raia wa India, Vinoth Krishanth Sathsivam (29) raia wa Sirlanka pamoja na Raiph Leopold Hruscka( 54) raia wa Ujerumani ambao wanashikiliwa kwenye kituo kikuu cha polisi jijini Arusha tayari kufikishwa mahakamani.
Mfanyabiashara huyo ambaye ni miongoni mwa wafanyabiashara waliopo kwenye kamati ya kusaidia shughuli za maendeleo ikiwemo ujenzi wa nyumba 18 za polisi zilizoungua mkoani hapa anadaiwa kutenda kosa hilo kinyume na sheria sura namba 1 ya mwaka 2015 kifungu cha 9 cha sheria za kuratibu ajira za wageni.
Katika Operesheni hiyo inayosimamiwa na Kamishna wa kazi nchini, Gabriel Malata inaendelea katika maeneo mbalimbali mkoani hapa lengo ni kuhakikisha kwamba sheria za kazi hazikiukwi na wote wanafanyakazi kwa mujibu wa sheria za hapa nchini.
Wakati huo huo mmiliki wa kampuni ya Utalii Tyche&Toya Ltd, Ricardo Gramono Reto anatarajiwa kupandishwa kizimbani November 30 kwa tuhuma za kuajiri wafanyakazi wasio na vibali kinyume cha sheria za nchi.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa amethibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao na kesho watapandishwa kizimbani kujibu tuhuma mbali mbali zinazowakabili.
No comments:
Post a Comment