BENKI ya NMB imetoa msaada wa Madawati, vifaa vya afya, mabati, mbao na vifaa ya ujenzi kwa shule wilayani Korogwe na Kilindi mkoani Tanga vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 60. Pamoja na vifaa hivyo vya kupaulia, pia NMB imekabidhi madawati 200 kwaajili ya kupunguza uhaba wa madawati katika wilaya hizo.
Shule zilizofaidika na msaada huo kwa upande wa Korogwe ni Shule ya Msingi Mtonga iliyopata madawati 100, Shule ya Sekondari Semkiwa viti 50 na meza 50, Shule ya Msingi Semangube mabati, kofia na misumari vyenye thamani ya sh. milioni tano, Shule ya Msingi Kwamngumi mabati yenye thamani ya sh. milioni tano, Shule ya Sekondari ya Wasichana Korogwe mabati ya sh. milioni tano na Shule ya Msingi Kijungumoto ya Halmashauri ya Mji Korogwe mabati ya sh. milioni tano.
Kwa upande wa wilaya ya Kilindi, Shule ya Sekondari Kimbe imepata viti na meza 100, shule za msingi za Mafisa, Nkama na Songe zimepata mabati vyote vikiwa na thamani ya sh. milioni 20. Lakini pia kutoa vifaa tiba kwa zahanati mbili kila moja sh. milioni tano na vifaa vyote kuwa na gharama ya sh. milioni 30.
Mkuu wa Wilaya ya Korogwe - Kissa Kasongwa ameishukuru Benki ya NMB baada ya kutoa msaada wa madawati na vifaa vya ujenzi wilayani kwake na kusema msaada huo wa kijamii umewasaidia kukabiliana na changamoto za uhaba wa madawati na vifaa vya ujenzi wa madarasa kwenye sekta ya elimu.
Akizungumza jana kwenye hafla ya kukabidhiwa madawati na mabati kutoka Benki ya NMB kwenye Shule ya Msingi Mtonga, Bi Kasongwa alisema pamoja na maendeleo makubwa yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kwenye Sekta ya Elimu kwa elimu bila malipo, bado ni muhimu wadau kuchangia elimu. Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilindi - Sauda Mtondoo amesema vifaa tiba, madawati walivyopewa na Benki ya NMB vitasaidia kuboresha miundombinu ya shule na kuboresha afya za wananchi.
Serikali yetu ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli, ipo kwenye maboresho makubwa ya huduma za jamii, lakini peke yake haitoshi mpaka kuwe na ushirikiano na wadau. Na leo hii NMB wamejidhihirisha kuwa ni wadau wetu wakubwa kwenye suala hili la huduma za jamii.
Naye Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini - Cosmas Sadat, alisema NMB imekuwa ikisaidia miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi kwa kujikita zaidi kwenye elimu kwa kutoa madawati na viti, huku kwenye sekta ya afya wakichangia vitanda na magodoro, na kusaidia majanga yanayoipata nchi yetu.
"Tunatambua kuwa ni kupitia jamii ndipo wateja wetu wengi wanapotoka, hivyo kurudisha sehemu ya faida kwa jamii ni utamaduni wetu. Kwa maana hiyo tumeamua kushirikiana na serikali ya wilaya ya Korogwe na Kilindi na kuwapatia madawati Zaidi ya 200, vifaa vya afya na vifaa vya ujenzi kwa shule Zaidi ya 10 na hospitali na kuonyesha kuwa tunajali. "Ingawa NMB inapokea maombi mengi sana kuchangia miradi ya jamii, benki imejikita zaidi katika maeneo ya elimu, afya na msaada wa hali na mali katika nyakati ngumu kama za majanga.
Kwa mwaka 2018, NMB imetenga zaidi ya sh. bilioni moja kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya wananchi ikiwemo kusaidia sekta ya afya na elimu. Kiasi hiki kinatufanya kuwa benki ya kwanza katika kuchangia maendeleo kuliko benki yeyote nchini. Benki ya NMB kwa mwaka 2018 ilitenga zaidi ya shilingi bilioni 1 kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya wananchi ikiwemo kusaidia sekta ya afya na elimu ambapo mpaka sasa, Zaidi ya shilingi milioni 900 zimeshatumika kusaidia jamii kwa Tanzania bara na Zanzibar.
Kwa kiasi hicho, Zaidi ya madawati 5500 yameshanunuliwa na kugawiwa kwenye shule 110 nchini kote, Zaidi ya vituo 60 vya afya vimenufaika kwa kupatiwa vitanda vya kujifungulia, vitanda vya kawaida na pia vifaa mbalimbali vya tiba. Kiasi hiki kinatufanya kuwa benki ya kwanza katika kuchangia maendeleo kuliko benki yoyote nchini. Kwa taarifa tu, NMB ndiyo benki inayoongoza nchini kwa kuwa na matawi mengi kwani ina matawi 228, ATM Zaidi ya 800 na NMB Wakala zaidi ya 6,000 nchi nzima pamoja na idadi ya wateja inayofikia milioni tatu hazina ambayo hakuna benki yenye nayo.
No comments:
Post a Comment