Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika mazungumzo na Makamu
wa Rais wa Benki ya Dunia kwa Kanda ya Afrika Hafez Ghanem Ikulu jijini Dar es
Salaam.
|
BENKI ya Dunia imeridhia kutoa Dola za Marekani Milioni 300 sawa na shilingi Bilioni 680.5 kwa Tanzania kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kuongeza ubora wa elimu ya sekondari unaokusudiwa kujenga vyumba vya madarasa, mabweni, maabara, nyumba za watumishi na kununua vifaa vya kufundishia.
Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika Dkt. Hafez Ghanem aliyekutana na Mhe. Rais Magufuli tarehe 16 Novemba, 2018 Ikulu Jijini Dar es Salaam amesema pamoja na kuridhia kutoa fedha za mradi huo, Benki hiyo inaendelea kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania yenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni 5.2 sawa na zaidi ya shilingi Trilioni 13 na kwamba miradi hiyo inatekelezwa kutokana na uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati yake na Tanzania.
Dkt. Hafez Ghanem amesema katika mazungumzo hayo wamejadili juu ya maendeleo ya miradi hiyo na kazi nzuri ambayo inafanywa na Tanzania kuimarisha uchumi, na pia amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa matokeo mazuri ya mapambano dhidi ya rushwa na kuimarisha huduma za kijamii.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Benki ya Dunia kwa ushirikiano na uhusiano mzuri na Tanzania na ameahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza na kukuza uhusiano huo, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha fedha zote zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinatumika kwa miradi iliyokusudiwa.
“Namshukuru Dkt. Hafez Ghanem na Benki ya Dunia kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya Tanzania, hizo Dola Milioni 300 ambazo baadhi ya watu wasiotutakia mema walisema zimefyekelewa mbali, anasema zitaletwa, na pia Benki ya Dunia imetoa Dola Bilioni 5.2 ambazo zinafadhili miradi mbalimbali ya elimu, nishati, barabara, kilimo, afya na maji, ni miradi mikubwa na mingi.
“Kwa hiyo amekuja kututhibitishia kuwa Benki ya Dunia haitatuacha” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James ameitaja baadhi ya miradi inayoendelea kutekelezwa kwa ushirikiano na Benki ya Dunia kuwa ni mradi wa uboreshaji wa bandari ya Dar es Salaam ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 24, ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya barabara eneo la Ubungo Jijini Dar es Salaam, mradi wa ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (BRT) kwa awamu kwana na ya pili na miradi mingine mbalimbali.
Mazungumza kati ya Mhe. Rais Magufuli na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Dkt. Hafez Ghanem yamehudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu na Mwakilishi wa Benki ya Dunia hapa nchini Bi. Bella Bird.
No comments:
Post a Comment