NAIBU Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye amefanya ziara ya kukagua
maendeleo ya mradi wa upanuzi wa bandari, ujenzi wa magati na kuongeza kina cha
kupakia na kupakua mizigo kwenye Bandari ya Dar es Salaam.
Nditiye amesema kuwa
ameridhishwa na hatua iliyofikiwa ya maendeleo ya mradi huo kwa kufikia kiwango
cha asilimia 42 ya mradi huo ambapo mradi huo ulitegemewa ukabidhiwe mwezi
Oktoba mwaka huu 2018. Amefafanua kuwa ilibidi mradi huo ufanyiwe maboresho ili
kuendana na matakwa ya mradi ili uweze kubeba mizigo mizito na utakamilika
mwezi Juni mwakani, 2019.
Pia, ameongeza kuwa,
ili kuweza kwenda sambasamba na muda wa mkataba wa mradi huo, ujenzi wa gati
namba moja ulikuwa unaendelea na unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka
huu, 2018 badala ya mwezi Aprili mwakani 2019, “hivyo tuko ndani ya muda wa
mkataba,” amesema Nditiye.
Naye Naibu Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Mhandisi Karim Mataka
amemweleza Nditiye kuwa maendeleo ya mradi ni mazuri japo walikumbana na
changamoto ya kukukutana na udongo laini baharini kwenye eneo la ujenzi wa
mradi huo ambapo iliwalazimu kuimarisha eneo hilo ili bandari iweze kubeba
mzigo wa kontena mpaka tano zikiwa zimepandana kutokea chini kwenye eneo la
kupakia na kupakua mizigo.
Mataka ameongeza kuwa Mamlaka
ya Usimamizi wa Bandari Tanzania imejipanga ili kuhakikisha kuwa mradi huo
unakamilika kwa wakati ndani ya kipindi cha miezi 36 kuendana na matakwa ya
mkataba wa mradi huo ambao ulianza rasmi tarehe moja Julai mwaka 2017 na
unatarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka 2020. Mataka amesema kuwa mradi huo
unagharimu jumla ya shilingi bilioni 336 na unajengwa na mkandarasi wa kampuni
ya kutoka China ya CHEC (LYU wei).
Amefafanua kuwa mradi
wa upanuzi wa bandari, ujenzi wa magati na kuongeza kina cha kupakia na kupakua
mizigo, utaiwezesha bandari kuhudumia meli kubwa zaidi ambapo hivi sasa hamna
kina cha mita 12 ambapo inazifanya meli nyingi kuwa kwenye foleni na kulazimika
kusogeza meli moja moja ambapo mradi huu ukikamilika, bandari itakuwa na uwezo
wa kushusha mizigo ya kutoka kweye meli kubwa saba kwa wakati mmoja.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments:
Post a Comment