Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William
Lukuvi (wa pili kushoto) akisitiza msimamo wa Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii, Japhet Hasunga (wa pili kulia) alioutoa leo kuhusu umuhimu wa kuheshimu
mipaka ya msitu wa Hifadhi ya Kazimzumbwi kwa Wananchi wanaouzunguka msitu
huo katika eneo la Zingiziwa wilayani Ilala mkoani Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa
Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga akitoa msimamo kwa wananchi wanaozunguka
Msitu wa Hifadhi wa Kazimzumbwi kuhusu umuhimu wa kuheshimu mipaka ya Hifadhi
wa Misitu huo kwa ajili ya manufaa ya wananchi wote wakati alipokuwa
akizungumza na wananchi hao katika eneo la Zingiziwa wilayani Ilala mkoani Dar
es Salaam.
SERIKALI
imewataka wananchi wanaoishi kuzunguka Hifadhi ya Msitu wa Kazimzumbwi
waliokuwa wamefungua kesi na baadaye kushindwa waendelee kuheshimu mipaka ya
Msitu huo huku Chama Cha Mapinduzi kikiangangalia namna bora ya
kuwasaidia.
Hatua
hiyo inakuja kufuatia Wananchi hao waliokuwa na mgogoro wa Ardhi ndani ya Msitu
huo kufungua kesi mwaka 2017, kwenye Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi na
maamuzi ya shauri la madai hayo yaliipa serikali ushindi, baada ya wananchi hao
kushindwa kuonyesha ushahidi wa umiliki wa ardhi ikiwa ni ushahidi wa manunuzi na
urithi wa ardhi hiyo katika Msitu wa Hifadhi ya Kazimzumbwi.
Akizungumza
kwenye mkutano na wananchi katika eneo la Zingiziwa wilayani Ilala mkoani Dar
es Salaam, Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi amewaambia
wananchi hao kuwa hawana haki kwenye ardhi hiyo kwa mujibu wa hukumu
iliyotoka.
Aliongeza
kuwa mipaka ya msitu huo ipo sahihi na si vinginevyo hali iliyopelekea
wananchi hao kushindwa kukata rufaa.
Hata
hivyo Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi
amejipa siku 30 kuangalia namna ya kuwasaidia wakazi hao walioshindwa kesi.
Ameongeza
kuwa tayari ameshaunda kamati iliyopewa muda wa miezi miwili na tayari
imeshamaliza mwezi mmoja na hivyo itatoa majibu ndani ya siku 30 lengo likiwa
ni kuwasaidia wananchi hao ambao kisheria walishindwa kesi.
"Mgogoro
huu ulishafika mahakamani na uamuzi ukatolewa kuwa mmevamia hilo lipo wazi na
sisi hatupingani na uamuzi wa mahakama. Ila kwa kuwa nyie ni wananchi wetu, CCM
imeamua kununua kesi, sio kwa maana ya kupinga mahakama Bali ni kwa kuangalia tunawasaidia
vipi," alisema Lukuvi.
Kwa
upande wake, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga amesema wizara
yake haina tatizo na wakazi hao zaidi ya kuhakikisha msitu huo uko salama. Amesema
katika kipindi ambacho msitu huo ulivamiwa athari kubwa zilijitokeza.
"Msitu
huu tunaweza kusema ndio mapafu ya Dar, sasa ukivamiwa kwa kuwekwa Makazi au
shughuli za kibinadamu mambo yanakuwa mabaya,”
Tunategemea
tupate hewa nzuri kutoka huku lakini wao walivamia na kutengeneza hewa chafu.
Sisi tunachosimamia ni kuhakikisha msitu unatunzwa na kubaki kuwa msitu," amesema.
Baadhi
ya wawakilishi wa kundi hilo la wananchi waliokuwa wamevamia msitu huo
wameeleza kuwa wanachotaka ni kuonyeshwa mipaka ya kitaalam ya unapoanzia msitu
huo.
No comments:
Post a Comment