BENKI ya NMB Plc
imesema itashirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili kusaidia
kilimo cha zao la michikichi mkoani Kigoma.
Mpango huo ulielezwa jana
na Mkuu wa Idara ya Wateja Wakubwa na Serikali wa Benki ya NMB, Bw. Filbert
Mponzi wakati wa mazungumzo mafupi na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotembelea
banda la benki hiyo kwenye Mkutano Mkuu wa
34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) unaoendelea jijini Dodoma.
Mponzi alisema kwa sasa
NMB inawasaidia zaidi ya wakulima wadogo wadogo milioni moja nchi nzima, na kwamba
benki itaendelea kutenga fedha za kutosha ili kusaidia wakulima wengi zaidi.
“Kwa sasa, NMB
imetenga zaidi ya shilingi billioni 500 kwa ajili ya kusaidia wakulima hapa nchini
lengo likiwa kusaidia jitihada za serikali ya awamu ya tano ya uchumi wa viwanda
kupitia sekta ya kilimo.
Katika mazungumzo hayo,
Waziri Mkuu alisema kwa sasa Serikali inapeleka nguvu zake katika kukuza kilimo
cha zao la mchikichi mkoani Kigoma, na hivyo akaitaka benki ya NMB kuisaidia Serikali
katika kufanikisha azma hiyo kwa kuwasaidia wakulima wa michikichi mkoani humo.
“Tumekuwa tukiwashawishi
wakulima mkoani Kigoma kujikita katika kilimo cha michikichi lakini kwa bahati mbaya
wakulima wengi hawana mitaji ya kulima michikichi kwa wingi. Nitafurahi kama benki
yenu kupitia mikakati yake itawawezesha wakulima wa michikichi,” alisema.
Aidha, Waziri Mkuu ameomba
kukutana na uongozi wa benki ya NMB mapema wiki ijayo mkoani Kigoma ili kwa pamoja
waweze kupanga mkakati kazi wa kuwasaidia wakulima mkoani humo kulima michikichi
kwa ufanisi na wingi zaidi.
“Kwa sasa tunapambana ili
kuhakikisha mazao yote ya biashara yanayostawi hapa nchini yanalimwa kwa kiwango
kikubwa ili kuchochea kasi ya uchumi wa viwanda kupitia rasilimali za ndani.
Ningependa tukutane Kigoma ilituone namna ya kuwezesha zao la michikichi kulimwa
kwa wingi,” Majaliwa alieleza.
Akielezea mikakati mingine
ya benki, Mponzi alisema NMB itaendelea kutanua wigo wa huduma zake ili kuhakikisha
watanzania wengi zaidi wananufaika na huduma mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo.
“Hivi karibuni tumezindua
mfumo ambao unamwezesha mteja au mwananchi yeyote kufungua akaunti kupitia simu
yake ya mkononi, ambapo namba yake ya simu ndiyo inakuwa namba yake ya akaunti.
Ni matarajio yetu kwamba kwa kupitia mfumo huu shirikishi watanzania wengi zaidi,
hususani wakulima wa vijijini,” aliongeza.
Pamoja na hayo,
alieleza kuwa NMB itaendelea kushirikiana na mamlaka za Serikali za mitaa hapa nchini
katika kuleta maendeleo chanya. NMB imekuwa mdhamini mkuu
wa mikutano ya mwaka ya ALAT, na kwa mwaka huu, benki imetoa kiasi cha shilingi
milioni 100 kwa ajili ya kuwezesha mkutano huo muhimu uliyowakutanisha zaidi ya
wajumbe 500 kutoka mikoa mbalimbali.


No comments:
Post a Comment