![]() |
1.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya
Maliasili na Utalii, Bw. Lusius Mwenda (kushoto) akiwa ameongoza na Watumishi
zaidi ya 50 wa Wizara hiyo wakipanda kilima kwenda kuangalia michoro ya
miambani katika kituo cha Utalii cha Kolo kilichopo wilayani Kondoa
mkoani Dodoma jana ikiwa lengo la ziara hiyo ni kuhamasisha utalii wa ndani kwa
Watumishi wa Serikali. Wa pili ni Mkuu wa Kituo cha Kolo, Zuberi Mabie.
![]() |
1.
Mkuu wa Kituo cha Utalii, Kolo chenye michoro ya miambani, Zuberi
Mabie akiwa na watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii akiwaonesha michoro
ya miambani katika kituo cha Utalii cha Kolo kilichopo wilayani Kondoa
mkoani Dodoma jana ikiwa lengo la ziara hiyo ni kuhamasisha utalii wa ndani kwa
Watumishi wa Serikali.
NA LUSUNGU HELELA-DODOMA
MKURUGENZI wa Utawala na Raslimali Watu wa Wizara ya
Maliasili na Utalii, Bw. Lusius Mwenda ametoa wito kwa watumishi wa
Serikali kuwa mstari wa mbele kutembelea vivutio vya utalii
vilivyopo nchini kwa ajili ya kujifunza mambo mapya ikiwa pamoja na
kupumzisha akili.
Pia amewataka watumishi hao kujenga utamaduni wa kutembelea
vivutio hivyo ili waweze kuona na kuchangamkia fursa mbalimbali za
kiuchumi ambazo wanaweza kuanza kuzifanya kwa ajili ya kujiingizia kipato ikiwa
ni njia mojawapo ya kuanza kujiandaa kwa ajili ya kustaafu.
Amefafanua kuwa kila mtumishi wa Serikali anatakiwa kuanza
kujiandaa kwa ajili ya kustaafu kuanzia ile siku ya kwanza aliyoajiriwa.
Amesema watumishi walio wengi mara baada ya kustaafu hali zao za
kiuchumi huteteleka kwa vile katika kipindi cha utumishi wao walikuwa
hawatembelei maeneo tofauti na yale waliyoyazoea kwa ajili ya
kujifunza na kukutana na watu tofauti.
Ametoa Rai hiyo jana katika kituo cha utalii Kolo
kilichopo wilayani Kondoa mkoani Dodoma
alipokuwa ameongozana na Watumishi zaidi ya 50 kutoka Wizara ya
Maliasili na Utalii , Ikiwa ni moja ya jitihada za Wizara hiyo kuhamasisha
utalii wa ndani kwa Watumishi wa Serikali kwa kuanza na Watumishi wa Wizara
yenye dhamana.
Kivutio cha Utalii, Kolo kipo ni kivutio mashuhuri sana kwa michoro yake ya miambani
kwa vile inafanana na michoro ya Afrika Kusini na kimebeba tamaduni za
waafrika.
" Tunataka Watumishi muwe mabalozi wazuri kuanzia kwenye
ngazi ya familia hadi ngazi ya taifa kwa kuhamasisha jamii kuona umuhimu wa
kutembelea vivutio vya utalii ikiwemo maeneo ya kihistoria ambavyo
yamesheheni chimbuko la tamaduni zetu pamoja na harakati za binadamu katika
kupambana na mazingira yake." alisema
Akizungumzia kuhusu lengo la ziara hiyo, Bw.Mwenda amesema ziara
hiyo ya siku moja imejikita kuhamasisha Utalii wa ndani kwa kauli mbiu "
Utalii wa ndani unaanza kwako na kwangu"
Aidha, Amesema Wizara ya Maliasili na Utalii inaandaa utaratibu
maalum wa kuwawezesha watumishi wengine wa Wizara nyingine pamoja na taasisi za
serikali waanze kutembelea vivutio vya utalii ili kujenga utamaduni kwa
watumishi wa Umma kutembelea vivutio vya utalii nchini kwa ajili ya kujifunza
na kufurahia maisha.
Awali, Mkuu wa Kituo cha Kolo, Zuberi Mabie alieleza kuwa Kolo
ni kivutio cha Utalii cha aina yake chenye michoro ya miambani iliyochorwa na
jamii ya Wasandawe miaka 10,000 hadi miaka 6,000 iliyopita.
Amesema eneo hilo ni miongoni mwa maeneo manne ya Idara ya
Mambokale yaliyopo katika orodha ya Urithi wa dunia
Alisema inaonesha kuwa kabla ya ugunduzi huo watu walikuwa
wanaweka kumbukumbu ya kuchora vitu na matukio waliyokuwa wanayaona katika
mazingira yao.
Akizungumzia kuhusu idadi ya watalii wanaotembelea, alisema kila
mwezi hupata watalii zaidi ya 200 kutoka ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake, Afisa Utalii, Heda Chale mara baada ya
kutembelea kituo hicho alisema ameifurahia safari hiyo na amejifunza vitu
mbalimbali ikiwa pamoja na kujionea madhari ya aina yake katika kivutio hicho.
Naye, Mhifadhi Mkuu wa Mambo Kale, Wiliam Mwita alitoa wito kwa
jamii kutembelea vituo vya maeneo ya kihistoria yaliyotapakaa nchi nzima
ili jamii iweze kujifunza historia ya binadamu pamoja na mapambano yake katika
kuyamudu mazingira.
Pia, Alitoa wito kwa Wawekezaji kuchangamkia fursa ya kuwekeza
kwenye vivutio vya Mambokale kwa vile nafasi zipo wazi lengo likiwa ni
kuviendeleza kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.
Amesema maeneo hayo yanahitaji uwekezaji wa nguvu ili kuyafanya
yawe na mvuto ili kuwavutia wageni kutika nje na pia Watanzania
Kivutio cha Utalii Koli kipo kilomita 150 kutoka jiji la Dodoma
na ni michoro ya kwanza kwa bara la Afrika kutokana na uwingi wake na kutapakaa
kwake katika eneo kubwa.



No comments:
Post a Comment