Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba akifafanua vifungu
vya Sheria ya Mazingira mbele ya Watendaji na Viongozi wa Mkoa wa Singida juu
ya maeneo lindwa. Wengine katika picha ni viongozi wa Mkoa wa Singida
wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Rehema Nchimbi (wa pili kutoka kushoto).
Ziwa Singidani ambalo liko
hatarini kutoweka kutokana na shughuli zisizo endelevu za kibinadamu. Waziri
Makamba yuko katika ziara ya kikazi ya kukagua na kuona namna bora ya kunusuru
Ziwa hilo pamoja na mengine kwa mustakabali wa nchi yetu.
WAZIRI
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. January Makamba
amesema Ofisi yake inaangalia uwezekano wa kutangaza Ziwa Singidani na Ziwa
Kindai katika Halmashauri ya Singida kama maeneo lindwa kimazingira kwa kuwa
yako hatarini kutoweka.
Waziri
Makamba ameyasema hayo hii leo Mkoani Singida ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara
yake katika Mikoa 9 hapa nchini yenye lengo kukagua, kutathmini na kuzungumza
na viongozi, wataalam, watendaji na wananchi kuhusu maeneo yanayopendekezwa
kuhifadhiwa kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira kifungu namba 51.
Aidha,
Waziri Makamba amesema kuwa mara baada ya kutoa tangazo hilo katika gazeti la
Serikali matumizi sahihi ya maziwa hayo yataainishwa ikiwa ni pamoja na kupanda
miti rafiki kuzunguka maeneo yote na kuzingatia makatazo yatakayotolewa.
“Ziwa Singidani liko hatarini kutoweka kutona
na shughuli za kibinadamu, hivyo kwa kutumia Sheria ya Mazingira nitashauriana
na wataalamu wangu kuona namna bora ya kunusuru maziwa haya ikiwa ni pamoja na
kuyatangaza kwenye gazeti la Serikali kama maeneo lindwa kimazingira.” Makamba
alisisitiza.
Imebainika
kuwa, lengo la kuainisha na kutangaza maeneo hayo ni kulinda mifumo muhimu ya
kiikolojia (ikiwemo vyanzo vya maji, mito, maziwa, mabwawa, milima na vilima,
chemichemi, ardhi oevu, mazalia ya samaki na misitu) ambayo hayana ulinzi wa
Sheria nyingine.
Waziri
Makamba pia ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Singida kwa utayari na uwezo wao
katika kusimamia uhifadhi mara maeneo hayo yatakapotangazwa na kuwataka
kuwasiliana na Ofisi yake ili waweze kupatiwa rasimu ya Sheria ndogo ndogo
watakazozitumia katika Halmashauri zao ili kukabiliana na changamoto za
uharibifu wa mazingira katika ngazi zote.
Nae Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amesema Mkoa wake uko tayari kuingia
makubaliano na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC)
yenye lengo la kuhuisha Sheria ndogo ndogo zitakazosaidia hifadhi ya Mazingira
mkoani kwake pamoja na kuundwa kwa Kamati za Mazingira katika ngazi zote.
Jumla ya maeneo 77 yamependekezwa
kutoka Mikoa mbalimbali kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa kwa mujibu wa Sheria
na katika awamu ya kwanza, maeneo takriban 20 yanatarajiwa kuhifadhiwa kwa
kutumia Sheria ya Mazingira.

No comments:
Post a Comment