![]() |
Ujenzi wa daraja la Kikamba wilayani Songwe linalounganisha
Mkoa wa Songwe na Katavi ukiendelea daraja hilo linatarajiwa kukamilika
mwishoni mwa mwaka huu.
|
SERIKALI imesema haitamwongezea mkataba mkandarasi
China Railway 15 Bureau Group Corporation anayejenga barabara ya Chunya
–Makongolosi kwa kiwango cha lami muda wake utakapomalizika.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Elias John Kwandikwa
amesema muda wa miezi 27 aliyopewa kujenga barabara hiyo yenye urefu wa KM 39 unatosha na hivyo ni jukumu lake
kuhakikisha kuwa anakuwa na vifaa na wafanyakazi wa kutosha wakati wote.
“Mkishindwa kukamilisha barabara hii kwa wakati
hamtapata tena kazi hapa nchini kwani mtakuwa mmeshindwa kazi kwa kukiuka
mkataba na kuiongezea Serikali gharama”, amesema Mhe. Kwandikwa.
Naye Kaimu meneja wa wakala wa barabara (TANROADS)
mkoa wa Mbeya Mhandisi Selemani Lawena amesema barabara ya Chunya –Makongolosi ni
sehemu ya barabara ya Mbeya-Rungwa yenye urefu wa KM 293 ambayo inaunganisha
kwa njia fupi mkoa wa Mbeya na mikoa ya Singida na Tabora.
“Barabara hii ikikamilika itafungua uchumi wa mikoa
ya Mbeya na Songwe na kuhuisha shughuli za kilimo,mifugo, uchimbaji madini na
ufugaji nyuki na hivyo kuongeza fursa za maendeleo kwa jamii na serikali kwa
ujumla”, amesema mhandisi Lawena.
Mhandisi lawena amesema sehemu ya Mbeya- Chunya KM 72
imekamilika na ujenzi wa Chunya –Makongolosi KM 39 unatarajiwa kukamilika Januari
2020.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kwandikwa amekagua
ujenzi wa barabara ya mchepuo ya Iwambi-Mbalizi KM 6.5 jijini Mbeya ambayo itatumiwa na magari madogo ili
kupunguza msongamano na ajali katika mlima Mbalizi na kusisitiza umuhimu wa
wadau wote wa usafiri kushirikiana ili kupunguza ajali na hivyo kulinda maisha
na mali.
IMETOLEWA NA
KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO


No comments:
Post a Comment