Naibu Waziri wa
Ujenzi, Mhe. Elias Kwandikwa, akitoa maelekezo kwa Meneja wa TANROADS Mkoa wa
Kilimanjaro, Mhandisi Nkolante Ntije alipokagua ujenzi wa barabara ya Sanya
Juu-Elerai KM 32.2, katika eneo la mto simba mkoani humo.
Naibu Waziri wa
Ujenzi, Mhe. Elias Kwandikwa, akitoa maelekezo kwa Mkandarasi wa Kampuni ya
China Geo-Engineering Corporation Bw. Wang Tuquan anayejenga barabara ya Sanya
Juu-Elerai KM 32,2, alipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo.
Mafundi wa Kampuni ya
China Geo-Engineering Corporation inayojenga barabara ya Sanya Juu-Elerai KM 32.2,
wakiendelea na kazi ya ujenzi wa tabaka la lami katika barabara hiyo, Mkoani
Kilimanjaro.
IMEELEZWA kuwa ushirikishwaji, ushirikiano na uzalendo baina ya wadau wote wa ujenzi wa barabara nchini utawezesha unafuu wa gharama za ujenzi na ubora wa barabara zinazojengwa kukamilika kwa wakati.
Naibu Waziri wa
Ujenzi, Mhe. Elias Kwandikwa amesema hayo Wilayani Siha, Mkoani Kilimanjaro
alipokagua ujenzi wa barabara ya Sanya Juu-Kamwanga Kilomita 74 na kusisitiza
kuwa ni wakati sasa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), wananchi na
Mkandarasi kufanya kazi pamoja ili kuwezesha tija na ufanisi kufikiwa kwa
haraka katika mradi huo.
“Wananchi wa Wilaya za
Siha, Longido na Rombo nawaomba mtoe ushirikiano kwa TANROADS na Mkandarasi ili
kuwezesha kupatikana kwa urahisi wa kokoto, mchanga na nguvu kazi ili kuwezesha
mradi huo kukamilika kwa wakati” amesema Naibu Waziri Kwandikwa.
Barabara ya Sanya
Juu-Kamwanga ni sehemu ya barabara ya Boma Ng’ombe hadi Kamwanga yenye urefu wa
KM 98 ambapo ujenzi wake umegawanywa katika sehemu tatu ambazo ni SanyaJuu-
Elerai KM 32.2, Elerai-Kamwanga KM 42 na
Bomang’ombe-Sanya Juu KM 24.
“Kukamilika kwa
barabara hii kutachochea kasi ya uzalishaji katika mashamba, kutoa fursa mpya
za ajira na kuongeza kasi ya utalii katika eneo la Mkoa wa Kilimanjaro”
amesisitiza Naibu Waziri Kwandikwa.
Naye Meneja wa
TANROADS Mkoani Kilimanjaro, Mhandisi Nkolante Ntije amesema zaidi ya shilingi
bilioni 52 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo sehemu ya kwanza
inayohusisha madaraja makubwa mawili, makalvati ya kati 110 na makalvati madogo
32 na ujenzi wake unatarajiwa kukamilika februari mwakani.
Mkandarasi anayejenga
barabara hiyo China Geo-Engineering Corporation kutoka China , Bw Wang Tuquan
amemhakikishia Naibu Waziri Kwandikwa kuwa licha ya barabara hiyo kujengwa kwa
kiwango cha juu cha ubora itamalizika kwa wakati.
Naibu Waziri Kwandikwa
yuko katika ziara ya siku tatu kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu katika Mkoani Kilimanjaro.
Imetolewa na Kitengo
cha Mawasiliano Serikalini,Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

No comments:
Post a Comment