ZUNGU ACHAGULIWA KUWA SPIKA WA BUNGE LA 13 LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 11 November 2025

ZUNGU ACHAGULIWA KUWA SPIKA WA BUNGE LA 13 LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

Spika Mpya wa Bunge la Tanzania, Mussa Azzan Zungu.

Na Dotto Mwaibale, Dodoma

​BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limemchagua Mbunge wa jimbo la Ilala mkoani Dar es Salaam kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe.Mussa Azzan Zungu kuwa Spika wa Bunge la 13 akichukua nafasi ya mtangulizi wake Dk.Tulia Ackison.

Mhe Zungu ambaye katika Bunge la 12 lililopita alikuwa Naibu Spika kuchaguliwa kwake kuwa Spika ni wazi kuwa amepanda ngazi kwa kushika nafasi hiyo ambayo awali ilikuwa ikishikiliwa na Dk.Tulia  ambaye alijitoa katika kinyang’anyiro hicho.

Mhe. Zungu ameibuka kidedea baada ya kupata kura 378 kati ya kura 383 zilizopigwa na hivyo kuwashinda wagombea wa vyama vingine vitano waliojitosa katika kinyang’anyiro hicho.

Wagombea hao ni Veronica Charles kutoka Chama cha NRA, Anitha Mgaya wa NLD, Chhrisant Ndege wa Chama cha DP, Ndonge Said Ndonge kutoka Chama cha AAFP na Amin Yongo kutoka Chama cha ADC.

Kabla ya zoezi la kupiga kura kufanyika, wagombea wa nafasi ya Spika wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waliomba kura mbele ya wabunge wateule kila mmoja akieleza nia yake ya kuliongoza Bunge lenye uwajibikaji, ushirikiano na kuwatumikia wananchi.

Mgombea wa kwanza kujinadi kwa wabunge ni Veronica Charles kutoka Chama cha NRA, ambaye alisema akichaguliwa kuwa Spika atalifanya Bunge  liwe la usawa na la wananchi.

Veronica alisema ataondoa kambi rasmi ya upinzani na kuanzisha kambi ya majadiliano kwa lengo la kuimarisha umoja na ushirikiano bungeni.

Aidha, alimpongeza Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mfano wa kuigwa, akisema ni kiongozi aliyempa ujasiri wa kuwania nafasi hiyo.

Naye Anitha Mgaya kutoka Chama cha NLD amesema dhamira yake ni kuhakikisha nidhamu, heshima na utulivu vinatawala mijadala yote bungeni.

Mgaya alisema kama kijana ataweka mkazo kwa  kuwaelimisha vijana juu ya thamani ya amani, upendo na utulivu.

Kwa upande wake, Chrisant Ndege wa Chama cha DP amesema ana nia ya kusimamia Bunge litakalokuwa na uwezo wa kuishauri na kuisimamia Serikali kwa mujibu wa Katiba.

 Amesema  kuwa mihimili mitatu ya dola ambayo ni Serikali, Bunge na Mahakama  inapaswa kufanya kazi kwa ushirikiano, huku kila mhimili ukitekeleza majukumu yake kwa uadilifu.

Ndege amesema atahakikisha sheria zinazotungwa zinakuwa na tija kwa maendeleo ya wananchi.

Ndonge Said Ndonge kutoka Chama cha AAFP ameanza kwa kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa ushindi alioupata.

 Aidha, Ndonge alitumia falsafa ya neno KIONGOZI kueleza misingi yake ya uongozi akisema K ni kukubali kukosolewa, I kujua tabia za unaowaongoza, O kuonyesha kwa vitendo, N kunena kauli thabiti, G kugawa madaraka, O kuondoa uonevu, Z kuzuia migogoro na I kuinua kipato.

Kwa upande wake Amin Yongo, kutoka Chama cha ADC amesema endapo atachaguliwa kuwa Spika, atahakikisha Bunge linasimamia amani, umoja wa kitaifa na katiba ya nchi. 

Kwa upande wake,Mhe. Musa Azan Zungu kutoka CCM amesema akipata nafasi ya Uspika, ataunganisha Bunge kwa maslahi ya wananchi na kuhakikisha linafanya kazi kwa ufanisi ili kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.

Zungu alisema ataendelea kuimarisha uhusiano kati ya Bunge na wananchi ili kuhakikisha hoja zinazojadiliwa bungeni zinagusa moja kwa moja maisha ya Watanzania.

No comments:

Post a Comment