Mbunge wa Jimbo la Hanang’ Mhe. Asia Halamga akila kiapo cha Utii na Uaminifu na kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kikao cha kwanza cha mkutano wa kwanza wa Bunge la 13, leo Novemba 11, 2025 Jijini Dodoma.
Na Dotto Mwaibale, Dodoma
MBUNGE Mteule wa Jimbo la Hanang’ kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Manyara Asia Halamga ameendelea kung’ara katika medani za siasa na kuwa gumzo katika mkoa huo na Tanzania kwa ujumla.
Halamga ni mbunge msikivu, mnyenyekevu, mpole, mwenye maono na mpenda maendeleo ambaye amekuwa akiguswa na changamoto za wananchi pasipo ubaguzi.
Nyota yake ya kisiasa ilianza kuchipuka kupitia Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) na hasa baada ya kugombea ubunge wa Vijana Taifa kupitia CCM ambapo alishinda kwa kupata kura za kutosha.
Akiwa mbunge kupitia Vijana Halamga alifanya kazi kubwa nzuri ya kuwatumikia wananchi kwa nguvu zake zote liwake jua, inyeshe mvua alikuwa bega kwa bega na wananchi jambo lililomfanya aendelee kupendwa na nyota yake kung’ara.
Uchaguzi Mkuu wa 2025, Halamga aligombea Ubunge wa Jimbo la Hanang’ na katika kura za maoni ndani ya chama alishinda kwa kupata kura 7,092 na kuwashinda wagombea wenzake watano, akiwemo aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo Dkt. Mary Nagu aliyepata kura 5,237.
Mary Nagu anatajwa kuweka rekodi ya kushika nafasi za Uwaziri katika wizara mbalimbali kwa muda mrefu.
Uchaguzi huo wa kura za maoni ulihusisha wajumbe 21,094 na wajumbe 16,384 walijitokeza kushiriki zoezi hilo na matokeo ya kura Halamga aliibuka mshindi kwa kupata kura 7,092, Mary Nagu – 5,237, Samwel Hhayuma 2,995, Franklin Sumaye 399, John Lory 189 na Qambemeda Nyangura kura 152.
Wahenga walisema nyota njema uonekana mapema asubuhi hivyo basi kwa ushindi huo alioupata ndani ya chama ulionesha safari ya mafanikio yake katika siasa kuelekea uchaguzi mkuu ambapo alishinda kwa kura nyingi.
Mhe. Asia Halamga akikabidhiwa vitendea kazi.

No comments:
Post a Comment