TAKUKURU SINGIDA: UFINYU WA NAFASI CHANZO CHA RUSHWA VYUONI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday, 22 November 2025

TAKUKURU SINGIDA: UFINYU WA NAFASI CHANZO CHA RUSHWA VYUONI

Afisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Singida, Benjamin  Masyaga  akitoa Elimu kuhusu Mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa vyuoni wakati akizungumza na wanafunzi walioanza msimu wa masomo wa 2025/ 2025 Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Kampasi ya Singida Novemba 19, 2025.

Na Dotto Mwaibale, Sindida

IMEELEZWA kuwa ufinyu wa kupata nafasi katika vyuo bora ni moja ya chanzo kinachowafanya baadhi ya wanafunzi wasio na sifa kutoa rushwa ili kupata nafasi.

Hayo yamebainishwa na Benjamin  Masyaga Afisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Singida wakati akitoa Elimu kuhusu Mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa vyuoni wakati akizungumza na wanafunzi walioanza msimu wa masomo wa 2025/ 2025 Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Kampasi ya Singida.

“Ufinyu wa kupata nafasi (udahili) katika vyuo bora baadhi ya wanafunzi wasiokuwa na sifa hutumia mbinu za kihalifu ikiwemo kutoa rushwa kupata nafasi hizo,” alisema Masyaga.

Masyaga alisema sababu za kuwapo kwa rushwa vyuoni kwa mujibu wa taarifa za utafiti ni pamoja na ufinyu wa kupata nafasi katika vyuo husika, baadhi ya viongozi wa vyuo kutochukua hatua zozote dhidi ya walalamikiwa pale wanafunzi wanapotoa taarifa.

Alitaja sababu nyingine ni wanafunzi wasiokuwa na ufaulu au sifa za kutosha kutumia kila mbinu ikiwemo rushwa ili kufaulu mitihani kwa maelezo kuwa shahada hizo ndiyo mlango wa kupata ajira.

“Sababu nyingine za kuwapo kwa rushwa vyuoni ni kupata majibu ya mtihani kabla ya wakati ambapo wanafunzi wanapewa au wanagundua maswali ya mtihani kabla ya muda wa mtihani kwa malipo ya fedha au zawadi,” alisema Masyaga.

Alisema eneo lingine la rushwa ni kupata alama za miradi (Tafiti) kw rushwa ambapo wanafunzi hujaribu kutoa rushwa kwa walimu wa mradi ili kupewa alama nzuri.

Masyaga alitaja sababu nyingine ya rushwa vyuoni ni baadhi ya wanafunzi kukosa uelewa wa mapambano dhidi ya rushwa kwa kutohudhuria semina au mafunzo husika.

Akizungumzia kuhusu TAKUKURU alisema ni kifupi cha jina Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na kuwa inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11/2007 {PCCA Na. 11/2007}

 Afisa Utumishi na Msimamizi wa Huduma za Rasilimali Watu na Utawala wa Taasisi hiyo, Sanula Mohamed, akizungumza.

Mwalimu wa Michezo wa TIA Singida, Mwanahamisi Mkwizu akichangia jambo.

Mtaalamu wa Huduma Rafiki kwa Vijana katika Vituo vya Afya Manispaa ya Singida Dkt. Fatuma  Ndoile, akizungumza.

Wanafunzi wakishiriki tukio hilo.
 

No comments:

Post a Comment