| Sehemu ya washiriki wa uzinduzi wa nakala za kitabu cha ‘She Creates Changes’ kilichozinduliwa na.Shirika la Room To Read. |
| Sehemu ya wageni waalikwa na wanafunzi wakifuatilia matukio kwenye hafla ya uzinduzi wa nakala za kitabu cha ‘She Creates Changes’. |
Na Mwandishi Wetu, Dar
ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake
Tanzania (UWT), Jokate Mwegelo amelipongeza Shirika la Room To Read- Tanzania
kwa program zake zinazochochea wanafunzi nchini kusoma vitabu mbalimbali.
Alisema juhudi za shirika hilo kupitia program za hamasa za usomaji
vitabu kwa kuanzisha maktaba na zile za mtandaoni, zimehamasisha wanafunzi
kupenda kujisomea vitabu jambo ambalo linachochea hali ya ufaulu, na kuunga
mkono juhudi za Serikali katika maboresho ya elimu nchini.
Kiongozi huyo mdau wa maendeleo ya elimu, ametoa kauli hiyo juzi jijini
Dar es Salaam kwenye maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike yaliyoenda
sambamba na uzinduzi wa Kitabu cha ‘She Creates Changes’ na video zinazoangazia
mafanikio ya msichana aliyepitia changamoto mbalimbali.
“Juhudi za Shirika la Room To Read- Tanzania
za kuweka maktaba zaidi ya 1,500 na kuwasaidia maelfu ya wasichana katika mikoa
ya Pwani, Tanga, Morogoro na Dar es Salaam zimeacha alama za kudumu katika
jamii,” alisema, Bi. Jokate Mwegelo katika hotuba yake.
Aidha aliipongeza Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
jitihada mbalimbali za kuboresha elimu ikiwemo kutoa elimu bila malipo na
ujenzi wa hosteli za wasichana jambo ambalo linapunguza vikwazo vya wanafunzi
wa kike kwenye elimu.
“…Kupitia ushirikiano wa Shirika
la Room To Read na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na
Taasisi ya Elimu Tanzania, wamewezesha walimu kupata mafunzo ya ufundishaji
unaozingatia jinsia na hivyo kuunda mazingira bora ya kujifunzia kwa wanafunzi
wote,” alisisitiza kiongozi huyo aliyewahi pia kuwa Mkuu wa Wilaya za Kisarawe,
Temeke pamoja na Korogwe,
Awali Mkurugenzi wa Shirika la Room To Read- Tanzania, Bi. Joan Minja aliishukuru
serikali chini ya Uongozi wa Rais Samia kwa kuimarisha elimu kwa watoto
wakiwamo wa kike kupitia mipango mbalimbali.
Alisema mipango mizuri ya serikali kama vile elimu
hadi ngazi ya sekondari bila malipo, sera ya kuruhusu wasichana waliopata
ujauzito kurudi shuleni na maboresho anuai ya sekta ya elimi inayofanya
imechangia kuleta
mabadiliko makubwa na kuwa ukombozi kwa wasichana na jamii kwa ujumla.
Bi. Joan, alibainisha kuwa kwa Tanzania, Room to Read imefanya kazi tangu mwaka 2012 katika mikoa
ya Morogoro, Pwani, Tanga na Dar es Salaam ikilenga programu mbili za msingi
ambazo ni usomaji na maktaba pamoja
na elimu kwa msichana.
“Kwa
Programu ya Elimu kwa Msichana, tunawasaidia wasichana kuanzia Darasa la 5 hadi
Kidato cha 4 kukamilisha elimu yao ya sekondari wakiwa na stadi za maisha
zinazohitajika ili kufanya uamuzi sahihi kufikia malengo binafsi na ya jamii
zao,” alisema.
Bi. Joan, alisema
nchini Tanzania Room to Read imefanikiwa kufikia wasichana takriban 16,000
kwa kuwajengea uwezo wa kupambana na changamoto mbalimbali vinazosababishwa na
mila na desturi zikiwamo mimba na ndoa za utotoni, unyanyasaji wa kijinsia na umaskini.
“…Aslimia 100 ya wasichana wanufaika wa mradi
wameweza kuendelea na masomo kila mwaka, asilimia 90 ya wanufaika wa wameweza
kufaulu mitihani ya taifa kidato cha pili na kidato cha nne, kupunguza mdondoko
wa wanafunzi kutoka asilimia 18 mradi ulipoanza hadi asilimia 3 na asilimia 79
ya wasichana waliomaliza kidato cha nne wamejiunga na elimu ya juu…”
alibainisha kiongozi huyo wa Room to Read nchini Tanzania.

No comments:
Post a Comment