Na Josephine Majura, WF, Dodoma
WATUMISHI wa Wizara ya Fedha wametakiwa kuanza kujiandaa mapema kwa maisha ya baada ya kustaafu kwa kuwekeza katika miradi mbalimbali ya maendeleo, ili kuendelea kuwa na tija kwa familia na taifa hata baada ya kumaliza utumishi rasmi.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu, Bi. Fauzia Nombo, wakati akizungumza kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu – Utawala, Bi. Jenifa Christian Omolo, katika hafla ya kuwaaga Waandishi Waendesha Ofisi waliostaafu, iliyofanyika katika Ukumbi wa Simba Hoteli jijini Dodoma.
Bi. Fauzia alisisitiza kuwa mtumishi wa umma anapaswa kujiwekea malengo ya kiuchumi, kijamii na kiafya mapema kabla ya kufikia ukomo wa ajira, ili aweze kuishi kwa furaha, heshima na utulivu.
Alieleza kuwa maandalizi ya awali yanasaidia kupunguza msongo wa mawazo na hujenga msingi wa maisha yenye matumaini.
“Kustaafu ukiwa umejiandaa ni baraka, lakini kustaafu bila maandalizi ni mzigo. Watumishi mliobaki, ni muhimu kuanza safari ya maandalizi maisha baada ya kustaagu mapema ili kuwa na kesho iliyojaa utulivu na mafanikio,” alisisitiza Bi. Fauzia.
Alifafanua kuwa utumishi wa umma ni safari ndefu yenye changamoto na furaha, na kwa wale waliovuka salama hadi kustaafu, ni ushahidi wa moyo wa kujitolea, uvumilivu na mshikamano wa kweli.
Aidha, alisema kuwa kustaafu si jambo la kawaida bali ni heshima kubwa na somo kwa watumishi waliobaki, akiwataka wajifunze kutoka kwa waliostaafu kwa mafanikio.
“Kwa niaba ya viongozi wetu wa Wizara, tunawapongeza kwa utumishi wenu uliotukuka, hongereni sana,” alisema Bi. Fauzia.
Akizungumza kwa niaba ya wastaafu, Bi. Agness Kanola, ambaye ni mmoja wa Waandishi Waendesha Ofisi waliostaafu, alitoa shukrani kwa uongozi wa wizara kwa kutambua mchango wao na kuwaandalia hafla ya heshima.
“Tumetumikia taifa kwa moyo na kujitolea kwa miaka mingi, na leo tunajivunia kuona kazi zetu zikithaminiwa, tunawasihi watumishi waliobaki waendelee kufanya kazi kwa bidii, lakini pia waanze kujiandaa mapema kwa maisha ya baadaye, kwani maisha baada ya kustaafu yanahitaji maarifa, mipango na utulivu wa fikra,” alisema Bi. Agness.
Hafla ya kuwagaa wastaafu wanne Waandishi Waendesha Ofisi waliomaliza utumishi wao kati ya mwaka 2024 hadi 2025, ambao ni Grace Swale, Hilda Kibona, Agness Kanola na Jitihada Lulela ilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa wizara, watumishi wa sasa na wageni waalikwa.

.jpg)

No comments:
Post a Comment