WANAFUNZI WANAPASWA KUSOMA NA KUTUMIA VIFAA KIDIJITALI - MTHIBITI UBORA WA SHULE - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 30 September 2025

WANAFUNZI WANAPASWA KUSOMA NA KUTUMIA VIFAA KIDIJITALI - MTHIBITI UBORA WA SHULE

Baadhi ya wanafunzi wakitoa burudani kwenye hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Usomaji Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 8 Septemba.

Mthibiti Ubora Mkuu wa Shule wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Bi. Lilian Kazenga n mgeni rasmi akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Usomaji Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 8 Septemba.


Mthibiti Ubora Mkuu wa Shule wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Bi. Lilian Kazenga n mgeni rasmi akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Usomaji Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 8 Septemba.

Na Mwandishi Wetu

MTHIBITI Ubora Mkuu wa Shule wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke amesema ipo haja ya kuhakikisha watoto katika shule mbalimbali wanafundishwa kusoma na kutumia vifaa vya kidijitali kama vile vijitabu vya kielektroniki (e-books), programu za kielimu, majukwaa ya kidijitali na maktaba mtandao.

Kauli hiyo imetolewa juzi jijini Dar es Salaam na Mthibiti Ubora Mkuu wa Shule wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Bi. Bi. Lilian Kazenga alipokuwa akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Usomaji Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 8 Septemba.

“Katika ulimwengu wa sasa unaoongozwa na teknolojia ya kidijitali na Ulimwengu wa TEHAMA, ni wazi kuwa usomaji haupaswi kubaki katika mfumo wa vitabu vya karatasi pekee. Tunapaswa kuhakikisha kuwa watoto wetu wanafundishwa kusoma na kutumia vifaa vya kidijitali kama vile vijitabu vya kielektroniki (e-books), programu za kielimu, majukwaa ya kidijitali ya kusomea, na maktaba mtandao,” alisema Bi. Kazenga.

Aidha alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano imeendelea kuboresha elimu kwa kuchukua hatua kadhaa, ikiwemo kuboresha mitaala sambamba na uhamasishaji wa matumizi ya vifaa vya TEHAMA., jambo ambalo limechangia kupunguza tatizo la watu kutojua kusoma na kuandika.

“Kimsingi Juhudi hizi zinaenda sambamba na jitihada za wadau wa Elimu kama Room to Read kuanzisha mifumo mbalimbali inayorahisisha na kuhamasisha matumizi ya vifaa vya TEHAMA. Mathalan, wameanzisha Maktaba Mtandao ambayo inarahisha upatikanaji wa vitabu vya kujisomea kwa watoto. Matumizi sahihi ya vifaa vya kidijitali hupelekea kujengwa na kuimarishwa tabia ya usomaji miongoni mwa wasomaji wa leo na wa kesho.” Alisema katika hotuba yake.

Alibainisha kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote katika kuhakikisha elimu bora, jumuishi na yenye kumuwezesha mtoto wa Kitanzania kufikia ndoto zake ukizingatia kuwa Usomaji wa Kidijitali ni Nguvu ya Wasomaji wa Leo na kesho.

Naye Mkurugenzi wa Room to Read Tanzania, Bw. Joan-Ndaambuyo Minja awali akizungumza alisema shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali na mashirika washirika ili kutoa matokeo chanya kwa watoto wengi zaidi, huku akibainisha kuwa kwa zaidi ya miaka 24 wamefanikiwa  kunufaisha zaidi ya watoto milioni 39 ulimwenguni, katika jamii zaidi ya 182,000 wakiwezesha ujifunzaji nje ya darasa kwa kutumia njia mbadala.

Alifafanua kuwa Room to Read ilianza kufanya kazi nchini Tanzania mwaka 2012 katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero mkoa wa Morogoro. Baadaye ikaongeza wigo wa utekelezaji wa shughuli zake katika Halmashauri za Wilaya za Bagamoyo, Chalinze, Kibaha, Mkuranga na Kibaha Mji mkoa wa Pwani; na Halmashauri za Wilaya za Handeni na Muheza, Korogwe Mji na Tanga jiji mkoa wa Tanga; na Manispaa za Ubungo na Temeke mkoa wa Dar es Salaam.

“Kupitia Mradi wa Usomaji na Maktaba, Room to Read tunaamini kuwa maktaba ndio sehemu pekee ambayo mtoto huweza kupata fursa ya kuimarisha stadi za KKK na kujenga tabia ya usomaji. Room to Read imefanikiwa kujenga na kuwezesha unazishwaji wa maktaba 392 na Maktaba mtandao 01. Kupitia mafunzo na usaidizi kwa walimu, Room to Read tunamsaidia mtoto kwa kumjengea msingi bora wa kumudu stadi za kusoma na kuandika kwa wakati katika ngazi ya darasa la kwanza na la pili, kisha, kutumia stadi hizo kujisomea vitabu vya hadithi za watoto kwenye maktaba.  Kupitia maktaba tunamjengea mtoto mazingira rafiki yanayochochea ukuaji wa tabia ya usomaji kwa kusoma hadithi nzuri na za kufurahisha, zilizoandikwa na Room to Read au wachapishaji wa Kitanzania,” alisema

Siku ya Usomaji Duniani huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 8 Septemba. Kama tunavyofahamu, Siku hii ni matokeo ya tamko la shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (UNESCO) lililotolewa tarehe 26 Oktoba 1966.  Kauli mbiu ya mwaka huu kitaifa ni: "Kukuza Kisomo katika Zama za Kidigitali kwa Maendeleo ya Taifa Letu"

No comments:

Post a Comment