| Kulia ni mmoja wa washiriki katika Kongamano la 5 la Kimataifa la Elimu Bora (IQEC) 2025 akipata maelezo kutoka kwenye Banda la HakiElimu alipotembelea banda hilo. |
Na Mwandishi Wetu, Dar
WADAU mbalimbali wanaoshiriki kwenye Kongamano la 5 la Kimataifa la Elimu Bora (IQEC) 2025 linaloendelea jijini Dar es Salaam wamejadili suala la elimu jumuishi na kushauri kuwa ipo haja ya Serikali kwa kushirikiana na wadau kuiangalia upya kwa lengo la kuboresha utekelezaji wa mkakati huo.
Wakizungumza kwenye moja ya mjadala kwa nyakati tofauti, wadau hao wamesema suala la elimu jumuishi ni pana linaloitaji kuangalia kwa kina ili utekelezaji wake uendane na uhalisia wa jambo lenyewe na kuleta mafanikio zaidi kwa makundi yote ya walengwa.
Mshauri Mwelekezi wa Masuala ya Elimu kutoka Hakielimu, Dk. Wilberforce Meena amesema dhana ya elimu jumuishi ndani yake ina makundi mbalimbali yenye uhitaji, ambayo yote yanatakiwa yanufaike kiufasaha katika utekelezaji wa mkakati wa elimu jumuishi wa mwaka 2022-2026, lakini utekelezaji wa sasa unayaacha baadhi ya makundi hayo kunufaika kielimu.
"Kimsingi tunapozungumzia elimu jumuishi ni aina ya elimu ambayo inatolewa kuhakikisha kwamba kila mwanafunzi anapata fursa ya kujifunza, bila kujali changamoto tofauti za wanafunzi hao, na hatua ya pili ni kuhakikisha hata wale wengine ambao wanakosa fursa ya kuingia katika mfumo wa elimu nao wanajifunza, jambo ambalo kwa sasa ni kikwazo," alisema Dk. Meena.
Alisema elimu jumuishi lazima iangaliwe katika hatua mbili yaani walengwa katika mkakati huo wanajifunza na pia kutoa fursa hata katika makundi mengine ambayo yanaachwa nje ya mfumo wa elimu nayo yananufaika na elimu hiyo. Alitolea mfano makundi ya watoto wanaotoka katika jamii ya wafugaji, au umaskini uliopitiliza wanaweza wasipate fursa ya kuingia katika mfumo wa elimu ya shule lakini bado wanatakiwa kunufaika na mkakati wa elimu jumuishi.
Alisema yapo maeneo ambayo elimu jumuishi inatolewa kwa kuunganisha makundi yote yenye uhitaji maalum pamoja na kupewa elimu jambo ambalo bado wadau wa elimu wanaamini si makundi yote yananufaika kutokana na kutofautiana katika changamoto za ujifunzaji wa kundi hadi kundi.
Kwa upande wake mdau mwingine wa elimu, kutoka Shirika la OCODE, Bi. Digner Mushi ambao wanatekeleza mradi wa elimu 'Sauti Zetu' unaofuatilia utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa elimu jumuishi, alisema utekelezaji wa elimu jumuishi unaenda sambamba na uwepo wa vituo vya kutosha vya upimaji na utambuzi watoto (ESRACs) suala ambalo bado ni changamoto za uwepo wa vituo vya kutosha.
Alibainisha kuwa maeneo mengi hayana vituo vya upimaji na utambuzi kwa watoto jambo ambalo linawalazimu kuunganishwa kwa pamoja katika makundi na kufundishwa bila kujali changamoto za ujifunzaji za kila kundi. "Mwongozo unasema wazi kuwa kila halmashauri ijitahidi kutengeneza kituo cha utambuzi na upimaji watoto kuweza kutambua changamoto kabla ya kuingizwa katika utoaji elimu jumuishi, utafiti wetu unaonesha vituo ni vichache sana...kuna vituo kama 51 nchi nzima, tuna jumla ya halmashauri 184 nchi nzima lakini ni 24 tu ndio zilizo na vituo hivyo sasa hii ni changamoto kubwa," alieleza Bi. Mushi.
Alisema uchache wa vituo vya upimaji umesababisha watoto wengi kupelekwa katika madarasa pasipo kufanyiwa upimaji jambo ambalo linakosesha fursa ya kujifunza kwa ufasaha wawapo darasani, hivyo kuishauri Serikali kwa kushirikiana na wadau wa elimu kuhakikisha kunakuwa na vutuo vya kutosha kukabiliana na changamoto hiyo.

No comments:
Post a Comment