Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Ndg. Amos Maka
Kadama Malunde na Dotto Kwilasa – Dodoma
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza rasmi kuwa kikao cha mwisho cha uteuzi wa wagombea wa nafasi za Ubunge na Udiwani kimepangwa kufanyika tarehe 28 Julai, 2025, badala ya Julai 19, kama ilivyotangazwa awali.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Ndg. Amos Makalla, amesema mchakato wa ndani wa uchaguzi unaendelea kwa mafanikio huku ukihitaji umakini mkubwa kutokana na idadi kubwa ya wagombea.
“Maandalizi ya mchakato wa uchaguzi ndani ya CCM yanaendelea vizuri. Kikao cha mwisho cha uteuzi wa wagombea sasa kimepangwa kufanyika Julai 28, 2025 hapa Dodoma, badala ya leo Julai 19, 2025,” amesema Makalla.
Amefafanua kuwa idadi kubwa ya wagombea imepelekea chama kuongeza muda wa uchambuzi ili kuhakikisha haki inatendeka kwa kila mmoja.
“Wagombea ni wengi sana. Kwa mfano, nafasi za udiwani zina zaidi ya wagombea 27,000, huku ubunge ukiwa na zaidi ya wagombea 10,000. Kazi ya kuchambua ni kubwa. Tunataka tutende haki kwa umakini na utulivu,” amesema.
Makalla amewataka wagombea wote waendelee kuwa watulivu wakati mchakato ukiendelea kufanyika kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa.
“Wagombea watulie, wa relax wakati tunaendelea na mchakato mpaka tarehe 28,” amesisitiza.
Mchakato huu wa ndani wa CCM ni sehemu ya
maandalizi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, ambapo chama hicho
tawala kimesema kitaibua wagombea bora watakaowania nafasi mbalimbali kwa
tiketi ya CCM, kuanzia ngazi ya serikali za mitaa hadi taifa.


No comments:
Post a Comment