BARAZA LA 13 LA UONGOZI CHUO CHA MIPANGO LAZINDULIWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 20 November 2024

BARAZA LA 13 LA UONGOZI CHUO CHA MIPANGO LAZINDULIWA

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) akizindua Baraza la 13 la Uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, ambapo amelitaka Baraza hilo kuwa walinzi wa dira, dhima na mwelekeo wa Chuo, hafla iliyofanyika katika Chuo hicho, Kampasi ya Dodoma.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) akiagana na Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Prof. Hozen Mayaya, baada ya kuzindua Baraza la 13 la Uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, ambapo amelitaka Baraza hilo kuwa walinzi wa dira, dhima na mwelekeo wa Chuo, hafla iliyofanyika katika Chuo hicho, Kampasi ya Dodoma.

Na Peter Haule, WF, Dodoma

 

NAIBU Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) amelitaka Baraza la 13 la Uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kuwa walinzi wa dira, dhima na mwelekeo wa Chuo.

 

Alitoa rai hiyo jijini Dodoma wakati akizundua Baraza hilo la Uongozi uliofanyika katika Chuo cha Mipango ya Maendeleo vijijini, Kampasi ya Dodoma.

 

Mhe. Chande alisema kuwa kulingana na Sheria ya Chuo, Baraza la Uongozi wa Chuo linapaswa kuhakikisha kuwa dira, dhima, na mwelekeo wa taasisi vinasimamiwa kwa weledi na uwajibikaji mkubwa ili kufikia matokeo chanya ya taasisi kwa manufaa ya wadau wote wa ndani na wa nje.

 

“Kufanya kazi kwa bidii, maarifa na umakini na hali ya juu kunakiwezesha Chuo kutoa huduma bora inayokidhi matakwa ya wadau wetu na hasa katika zama hizi za kidijiti. Mnatakiwa kuwekeza kwenye kujitoa, kujituma, na kutumia muda mwingi kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowasilishwa kwenu na menejimenti”, alisema Mhe. Chande.

 

Mhe. Chande alilitaka Baraza la uongozi wa Chuo kuishauri Menejimenti ipasavyo juu ya mipango ya maendeleo ikiwemo kujadili na kupitisha bajeti ya taasisi, mpango mkakati na mambo mbalimbali yanayoletwa na Menejimenti kwenye Baraza.

 

Vilevile amelitaka Baraza hilo la uongozi kusoma na kutekeleza kwa vitendo Sheria, Taratibu, Kanuni na Miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali mara kwa mara hususani katika kutekeleza falsafa ya 4R, Reconcilliation (Maridhiano), Resillience (Ustahimilivu), Reforms (Mageuzi) na Rebuilding (Kujenga upya) iliyotolewa na Mhe. Dkt. Samia Suhulu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

 

Alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, imedhamiria kuipaisha nchi kiuchumi kupitia elimu ya juu, katika kutekeleza hilo imekuja na programu mahususi ya kutumia Elimu ya Juu kuleta Mageuzi ya Kiuchumi yaani Higher Education for Economic Transformation - HEET.

 

Aidha, alikipongeza Chuo kwa kupitia mitaala 15 na kuanzisha mitaala mingine mipya saba (7) kwa kuwa kwa kufanya hivyo kumesaidia kutekeleza dhima ya kuandaa wataalaamu wa kada adhimu ya mipango na pia kutekeleza R 2 za Mageuzi (Reforms) na Kujijenga upya (Rebuilding).  

 

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Prof. Hozen Mayaya, alimshukuru kwa namna ya pekee Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumteua Mwenyekiti wa Baraza la 13 la Uongozi wa Chuo Profesa Joseph Andrew, hivyo kukamilisha Baraza la Uongozi wa Chuo kufuatia uteuzi wa wajumbe wa Baraza ulioufanya tarehe 01 Oktoba, 2023.

 

Prof. Mayaya, alisema majina ya Uongozi wa Baraza la 13 la Uongozi wa Chuo kuwa ni pamoja na Prof. Joseph Kuzilwa ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza, CPA. Dkt. Samwel Werema, Makamu Mwenyekiti wa Baraza na Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi, Dkt. Francis Mwaijande, Mwenyekiti wa Kamati ya Taaluma ya Baraza la Uongozi wa Chuo na Bw. Benjamin Chilumba, Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha, Mipango, Ajira na Maendeleo ya Wafanyakazi.

No comments:

Post a Comment