WAZIRI MKUU ATETA NA MWENYEKITI WA BODI YA CITIBANK - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday 26 September 2024

WAZIRI MKUU ATETA NA MWENYEKITI WA BODI YA CITIBANK

 



Yaahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imekuwa inafanya kazi na benki ya Citibank ya Marekani kwa zaidi ya miaka 35 na imekuwa ikipokea ushauri wa mambo ya kifedha kupitia Benki Kuu ya Tanznaia (BoT).

Amesema hayo Septemba 24, 2024 mara baada ya kukutana na Mwenyekiti wa Bodi ya Benki hiyo, Bw. John Dugan, kwenye makao makuu ya benki hiyo, jijini New York, Marekani.

“Serikali ya Tanzania inaishukuru sana Benki ya Citibank kwa kuwa imeshiriki katika ujenzi wa uchumi ikiwemo na upatikanaji wa fedha za mikopo, kuishauri Serikali katik amasuala ya fedha na kufadhili miradi mikubwa inayoendelea kujengwa nchini,” alisema.

“Benki hii imekuwa ikikopesha makampuni yanayojenga reli yetu ya SGR na ili kuhakikisha wanachangia ujenzi wa uchumi wa Tanzania, na wao pia wamechukua lot moja ya ujenzi wa reli hiyo na kufadhili ujenzi wake. Hali kadhalika uendelezaji wa uwanja wa ndege wa Pemba.”

Alisema Tanzania ilipokabiliwa na uhaba wa mafuta ya kuendeshea mitambo na magari, benki hiyo ilitumika kuwasaidia wafanyabiashara kupata mafuta kwa bei nafuu,” alisema.

Mbali na ushauri wa masuala ya kiuchumi, Waziri Mkuu amesema benki hiyo kwa kushirikiana na taasisi ya kimataifa ya maendeleo ya Marekani, (U.S. International Development Finance Corporation) pia ilitoa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo huku ikiwapatia fursa zaidi akina mama na wadada wanaomiliki biashara zao binafsi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Citibank ya Marekani, Bw. John Dugan amesema wataendelea kushirikiana na Serikali katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo kama walivyofanya katika mika 40 iliyopita.

No comments:

Post a Comment