NAIBU WAZIRI SANGU: TAKUKURU IJIPAMBANUE KWA KUTENDA HAKI NA UADILIFU - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday 23 September 2024

NAIBU WAZIRI SANGU: TAKUKURU IJIPAMBANUE KWA KUTENDA HAKI NA UADILIFU

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu akizungumza na watumishi wa TAKUKURU  mara baada  kukagua Mradi wa ujenzi wa ofisi za TAKUKURU Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu akipata maelezo kutoka kwa Kamanda wa TAKUKURU Wilaya ya Nzega...  mara baada  kukagua Mradi wa ujenzi wa ofisi za TAKUKURU Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Mhe. Naitapwaki Tukai (kushoto).

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu akiwa ameongozana na na Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Mhe.  Naitapwaki Tukai akisalimiana na baadhi ya Watumishi wa TAKUKURU kabla ya kuanza   kukagua Mradi wa ujenzi wa ofisi za TAKUKURU Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora.

Na Lusungu Helela - Tabora

NAIBU, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuwa mfano kwa kujipambanua kutenda haki na kuonesha  uadilifu katika jamii huku akisisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa Mtumishi yeyote wa TAKUKURU atakayebainika kuwa  sio muadilifu

 

Mhe. Sangu ametoa kauli  hiyo leo mara baada ya kukagua Mradi wa ujenzi wa ofisi za TAKUKURU Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora uliogharimu kiasi cha Sh. Milioni 314.2  hadi kukamilika kwake.

 

Amesema TAKUKURU ni chombo kinachohitaji watumishi wenye uadilifu wa hali ya juu hivyo kwa Mtumishi yeyote ambaye sio muadilifu TAKUKURU si mahali sahihi kwa yeye kufanya kazi.

 

Amesema ni jambo lisilokubalika kwa chombo hicho nyeti cha kuzuia rushwa halafu kukawa na Watumishi  mabingwa  wa kupokea. 

 

Akizungumzia ujenzi wa ofisi hizo, Mhe. Sangu ameipongeza TAKUKURU kwa kuonesha mfano namna fedha za Watanzania zinavyotakiwa kutumika  kwani  thamani ya fedha iliyotumika kwenye ujenzi wa ofisi hizo unaonekana.

 

‘‘ TAKUKURU ni chombo kinachosimamia uadilifu na kinatakiwa kiwe cha kwanza kuonesha uadilifu kwa matendo yake, kwa  namna nilivyokagua jengo hili nimeridhishwa mno naamini wateja wetu watakaokuja hapa kwa ajili ya kuchunguzwa hili jengo litumike kama mfano kwa kuonesha thamani ya fedha iliyotumika, niwapongeze sana kwa jambo kubwa mlilolifanya hapa’’ amesisitiza Mhe. Sangu

 

Hata hivyo, Mhe. Sangu ameiagiza TAKUKURU kuhakikisha inahamia katika ofisi hizo za kisasa ndani ya mwezi huu ikizingatiwa kuwa ofisi wanazozitumia kwa sasa katika Wilaya hiyo kodi yake ya  pango itafikia ukomo mwezi huu.

 

Amesema kukamilika kwa Ofisi hizo  kunaonesha dhamira ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha TAKUKURU inawajibika ipasavyo kwa wananchi.

 

Kufuatia hatua hiyo, Mhe. Sangu ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake  makubwa ya kukubali kutoa fedha hizo ili kuhakikisha Watumishi wa  Takukuru  katika Wilaya ya Nzega wanatimiza  wajibu wao kwa kufanya kazi  katika Ofisi za  kisasa.

 

Katika hatua nyingine, Mhe. Sangu ameitaka TAKUKURU kuzifanyia kazi kwa wakati nyaraka za mikataba ya miradi ya maendeleo ambazo huwasilishwa kwao kutoka kwa Wateja wao   

 

Amesema kama jambo limekamilika au halina uchunguzi wowote ni muhimu nyaraka hizo zikarudishwa haraka kwa wahusika badala ya kukaa nazo kwa kipindi cha muda mrefu kwani lengo la TAKUKURU kupewa nyaraka hizo ni kuzuia rushwa  ili  kuhakikisha miradi hiyo ya maendeleo inapoanza kutekelezwa isiharibike

 

Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa nyaraka hizo za mikataba kufanyiwa kazi ipasanyo ili kuhakikisha miradi hiyo ya maendeleo inakamilika kwa viwango vinavyotakiwa kwa kuonesha thamani ya fedha.

No comments:

Post a Comment