Na Mwandishi Wetu - Dodoma
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Jimbo la Kibakwe, Mhe. George Simbachawene ameonya matumizi ya gari ya wagonjwa (ambulance) iliyotolewa na Serikali katika Kituo cha Afya cha Ipera lisitumike kubeba nyumba ndogo badala ya itumike kwa ajili ya malengo yaliyokusudiwa
Pia amesema gari hiyo isitumike kibiashara kwa kuanza kubeba abiria au mazao bali itumikwe kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa hususani akina mama wajawazito
Waziri Simbachawene ametoa kauli hiyo leo wakati wa hafla ya kukabidhi gari hiyo mara baada ya kufanya mkutano wa hadhara katika Kata ya Ipera, Kibakwe iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa jijini Dodoma ambapo amewataka wananchi wawe walinzi wa gari hiyo.
‘‘Msisitizo wangu gari hii ya wagonjwa ni gari la Serikali na ni gari ya wananchi hivyo nitawashangaa kuiona gari hii ikibeba abiria au magunia ya mazao, Naombeni kila mmoja wetu awe mlinzi wa gari hii kwani ni yetu sote,’’ amesisitiza Mhe.Simbachawene.
Amefafanua kuwa azma ya Serikali ya kutoa gari hiyo ni kuhakikisha inasaidia kuwafikisha wagonjwa katika hospitali ya Rufaa kwa muda muafaka pale ambapo mgonjwa anapewa rufaa ya matibabu.
‘‘Tunataka tukiliona gari hili likiwa linatembea barabarani liwe limebeba mgonjwa au linaenda kumfuata mgonjwa na sio vinginevyo,’’ amesisitiza Mhe. Simbachawene.
Katika hatua nyingine, Mhe. Simbachawene amesema wanaangalia utaratibu wa kuwatafuta madereva wa gari za wagonjwa viliko vituo vya afya ili magari hayo yasikae makao makuu ya Halmashauri ya wilaya badala yake magari hayo yakae kwenye maeneo husika ambako kuna Vituo vya afya.
Amesema hali hiyo itasaidia kutoa huduma ya haraka kwa wagonjwa mara tu pale gari linapohitajika.
Aidha, Mhe.Simbachawene ametoa wito kwa akina mama wajawazito kuwahi katika vituo vya afya mara waonapo dalili za kuanza kwa uchungu ili kuepuka vifo visivyo vya lazima huku akiwasihi manesi kuwahudumia wagonjwa kwa upendo kama viapo vyao vinavyowataka.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Mhe. George Fuime amesema atahakikisha wanafuatilia kwa ukaribu matumizi ya gari hilo ili liweze kuwa msaada kwa wananchi wote wa Kata ya Ipera na wilaya nzima ya Mpwapwa.
No comments:
Post a Comment