WAZIRI wa Ujenzi,
Innocent Bashungwa (Mb) amewataka Wapangaji wanaokaa kwenye nyumba na majengo
ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi ya pango
ili fedha hiyo itumike kujenga majengo mapya na kuboresha huduma katika majengo
mengine ya Wakala huo.
Bashungwa ametoa agizo
hilo leo Julai 23, 2024 katika hafla ya ufunguzi wa jengo la makazi ya
watumishi wa umma la Magomeni Kota Awamu ya Pili B la ghorofa saba katika Halmashauri
ya Manispaa ya Kinondoni, Mkoani Dar es Salaam.
“Serikali itaendelea
kufanya kila jitihada za kujenga makazi bora ya watumishi, lakini Watumishi
mliopata fursa ya kukaa kwenye nyumba za TBA, kulipa kodi ni wajibu. Mkilipa
kodi inatupa uwezo wa kuboresha huduma ya makazi bora”, amesisitiza Bashungwa.
Bashungwa ameielekeza
TBA kusimamia ukusanyaji wa madeni kwa wadaiwa sugu kulingana mikataba
waliyojiwekea ili kodi hizo ziweze kukamilisha ujenzi wa jengo la tatu na nne
(Block C na D) yanayoendelea katika eneo la Magomeni ambapo utekelezaji wake
umefikia asilimia 15.
Aidha, amesema Serikali
imerekebisha Sheria za TBA na kutoa fursa kwa kuingia ubia na sekta binafsi ili
kurahisisha ushirikishwaji wa Sekta Binafsi na Taasisi za fedha kwa ajili ya
uendelezaji wa milki, kuwahudumia watumishi wa umma wenye uhitaji wa makazi.
Bashungwa ameeleza kuwa
ujenzi wa jengo la makazi ya watumishi wa umma la Magomeni Kota Awamu ya Pili B
lililogharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 5.6 ni utekelezaji wa Ilani ya Chama
Cha Mapinduzi ya 2020 - 2025 na ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Awamu ya
Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha Makazi
bora.
Kadhalika, Bashungwa
ameipongeza TBA kwa matumizi bora ya ardhi na mipango mizuri ya majengo ya
kisasa katika eneo la Magomeni lenye ekari 32,000 lililokuwa na wakazi zaidi ya
645 kwa kuweza kutumia ekari 9 kutosheleza wakazi hao.
Kwa upande wake, Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameeleza kuwa Mkoa huo unatakiwa
kupangwa upya kwa kuwa na mikakati ya pamoja kwa kushirikiana na Mashirika ya
Kiserikali na Sekta Binafsi ili kuuwezesha Mkoa huo kuwa miongoni mwa miji mikubwa
Afrika kufikia mwaka 2030.
Akitoa taarifa ya
mradi, Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro ameeleza kuwa kazi zote katika
mradi huo za ubunifu, ujenzi na usimamizi zimetekelezwa na TBA kwa kutumia
Wataalam wake wenyewe kwa kuzingatia mabadiliko chanya ya ukuaji katika Sekta
ya Uchumi, Mipango Miji na Teknolojia ya Ujenzi, Mawasiliano na Miundombinu.
Kondoro ameeleza kuwa jengo hilo limefungwa mfumo wa kisasa wa ‘Payless’ ambapo itakapofika wakati wa kulipa kodi ya pango na mpangaji akawa hajalipa, moja kwa moja anakosa huduma ya umeme na maji katika nyumba yake na akilipa kodi ya pango, muda huo huo huduma ya umeme na maji inarejea.
No comments:
Post a Comment