Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) tarehe 13/6/2024. |
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) tarehe 13/6/2024 |
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA, MHESHIMIWA DKT. MWIGULU LAMECK NCHEMBA MADELU (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAPENDEKEZO
YA SERIKALI KUHUSU MAKADIRIO YA
MAPATO NA MATUMIZI KWA
MWAKA 2024/25
13 Juni 2024 Dodoma
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lipokee, lijadili na kukubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka 2024/25. Bajeti hii inawasilishwa kwa mujibu wa Ibara ya 137 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ikisomwa pamoja na Kifungu cha 23 (3) cha Sheria ya Bajeti, Sura 439 na Kifungu cha 124 (4) cha Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Februari 2023.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hotuba hii ninawasilisha vitabu vinne vinavyoelezea kwa kina makadirio ya Bajeti ya Serikali. Kitabu cha Kwanza ni Makadirio ya Mapato; Kitabu cha Pili ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Wizara, Idara Zinazojitegemea na Wakala wa Serikali; Kitabu cha Tatu ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa; na Kitabu cha Nne ni Makadirio ya Matumizi ya Maendeleo kwa Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala wa Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2024 pamoja na Muswada wa Sheria ya Matumizi ya Serikali wa Mwaka 2024 kwa pamoja ni sehemu ya bajeti hii.
Mheshimiwa Spika, niruhusu kwa moyo wa simanzi nitoe pole kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, waheshimiwa wabunge pamoja na watanzania kwa ujumla kwa kuondokewa na wapendwa wetu Hayati Alhaj Ali Hassan Mwinyi, aliyekuwa Rais wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Hayati Edward Ngoyai Lowassa, aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Monduli na Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, natoa pole kwa kuondokewa na Mheshimiwa Francis Leonard Mtega, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mbarali, na Mheshimiwa Ahmed Yahya Abdulwakil, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kwahani, pamoja na Viongozi wengine wa Serikali waliofariki katika mwaka huu wa fedha. Mwenyezi Mungu azilaze roho zao mahala pema peponi. Amina!
Mheshimiwa Spika, niruhusu pia nitumie fursa hii kutoa pole kwa wananchi wote walioathiriwa na majanga mbalimbali ikiwemo ajali na mafuriko yaliyotokea maeneo mbalimbali nchini kutokana na mvua za El-Nino. Majanga haya yamesababisha athari mbalimbali ikiwemo vifo, majeruhi pamoja na uharibifu wa mali na miundombinu. Nawapa pole wananchi wote waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki pamoja na mali zao kutokana na majanga hayo na nawaombea kwa Mwenyezi Mungu majeruhi wote wapone haraka na kurejea katika majukumu yao na awajalie marehemu wote pumziko jema la milele. Amina!
BAJETI YA MWAKA 2024/25
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, naomba niwasilishe makadirio ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/25 ambayo imeandaliwa kwa kuzingatia: Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2020; Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 - 2025/26); Dira ya Maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki 2050; Ajenda ya Maendeleo ya Afrika 2063; Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030; pamoja na nyaraka, miongozo na makubaliano mengine ya kikanda na kimataifa ambayo Tanzania imeridhia.
Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2024/25 ni ya nne katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 - 2025/26), wenye dhima ya Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu. Aidha, dhima kuu ya Bajeti ya Mwaka 2024/25 kama ilivyokubaliwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni “Mageuzi Endelevu ya Kiuchumi kupitia Uimarishaji wa Sera za Kibajeti na Uwekezaji katika Kuhimili na Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi kwa Maendeleo ya Wananchi”.
Shabaha za Uchumi Jumla
Mheshimiwa Spika, kutokana na nyaraka na miongozo iliyozingatiwa katika uandaaji wa Bajeti hii, shabaha za uchumi jumla ni kama ifuatavyo:
Kuongeza kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa kufikia asilimia 5.4 mwaka 2024 kutoka ukuaji wa asilimia 5.1 mwaka 2023;
Kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja ya wastani wa asilimia kati ya 3.0 - 5.0 katika muda wa kati;
Mapato ya ndani kufikia asilimia 15.8 ya Pato la Taifa mwaka 2024/25 ikilinganishwa na matarajio ya asilimia 15.4 mwaka 2023/24;
Mapato ya kodi kufikia asilimia 12.9 ya Pato la Taifa mwaka 2024/25 kutoka matarajio ya asilimia 12.6 mwaka 2023/24;
Kuwa na nakisi ya bajeti (ikijumuisha misaada) isiyozidi asilimia 3.0 ya Pato la Taifa; na
Kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne (4).
Misingi ya Bajeti
Mheshimiwa Spika, uandaaji wa shabaha za uchumi jumla kwa mwaka 2024/25 umezingatia misingi (assumptions) ifuatayo:
Kuongezeka kwa ushiriki wa sekta binafsi kwenye shughuli za uwekezaji na biashara;
Kuendelea kuhimili athari za majanga ya asili na yasiyo ya asili ikiwemo ukame, vita, magonjwa ya mlipuko, mafuriko;
Kuimarika kwa uchumi wa dunia na utulivu wa bei katika masoko ya fedha na bidhaa;
Kuendelea kuimarika kwa upatikanaji na usalama wa chakula nchini; na
Uwepo wa amani, usalama, umoja na utulivu wa ndani na nchi jirani.
Maeneo ya Vipaumbele kwa Mwaka 2024/25
Mheshimiwa Spika, bajeti ya Serikali ya mwaka 2024/25 imelenga kutekeleza vipaumbele vilivyozingatia maeneo yaliyoainishwa kwenye Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 - 2025/26 wenye dhima ya “Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu” pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2024/25. Maeneo ya vipaumbele yaliyoainishwa katika Mpango ni pamoja na: kuchochea uchumi shindani na shirikishi; kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma; kukuza biashara na uwekezaji; kuchochea maendeleo ya watu; na kuendeleza rasilimali watu.
Mheshimiwa Spika, baadhi ya maeneo mahsusi yatakayopewa kipaumbele ni pamoja na: kukamilisha miradi ya KIELELEZO na ile ya KIMKAKATI; kuimarisha sekta za UZALISHAJI; kuimarisha rasilimali watu hususani katika sekta za HUDUMA ZA JAMII; kuongeza matumizi ya TEHAMA; na kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji wa sekta binafsi. Aidha, maeneo mengine ya muhimu katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2024/25 ni kugharamia: mishahara ya watumishi wa umma; deni la serikali; Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2024; maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025; maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050; na maandalizi ya michuano ya mpira wa miguu ya mataifa ya Afrika (AFCON) ya mwaka 2027 ikiwa ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa viwanja.
Mheshimiwa Spika, miradi mahsusi katika maeneo ya kipaumbele ambayo Serikali itatekeleza kupitia Bajeti ya mwaka 2024/25 imeainishwa kwa kina katika hotuba iliyowasilishwa leo asubuhi na Mheshimiwa Prof. Kitila Alexander Mkumbo (Mb), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Mipango na Uwekezaji, alipokuwa akiwasilisha taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2024/25.
Usimamizi wa Matumizi ya Fedha za Umma
Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwenye mifumo ya uendeshaji wa shughuli zake ili kudhibiti matumizi ya fedha za umma. Hata hivyo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amekuwa akitoa hoja zinazohusu matumizi ya fedha za umma. Nipende kulihakikishia Bunge lako Tukufu na watanzania wote kuwa, Serikali makini ya Chama Cha Mapinduzi itaendelea kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti, Sura 439; Sheria ya Fedha za Umma, Sura 348; Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290; Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura 410; na Sheria ya Matumizi ya Fedha za Umma ya Mwaka 2024. Aidha, Serikali itaendelea kuhakikisha Sheria hizo zinasimamiwa na kutekelezwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kujibu hoja zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na hoja za wakaguzi wa ndani. Na endapo itabainika Afisa Masuuli wa Fungu husika ameshindwa kutekeleza matakwa ya Sheria hizo, hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa.
Mheshimiwa Spika, niendelee kuwasisitiza Maafisa Masuuli kuzingatia Waraka wa Mkuu wa Utumishi wa Umma Na. 2 wa mwaka 2021 kuhusu utaratibu wa kutumia magari, aina na stahili za magari kwa viongozi katika utumishi wa umma kwa lengo la kupunguza matumizi. Aidha, hatua nyingine zitakazochukuliwa ni pamoja na kupunguza safari za ndani na nje na kupunguza ukubwa wa uwakilishi kwenye mikutano ya ndani na nje ya nchi. Vilevile, niendelee kuwasisitiza Maafisa Masuuli wote kuendelea kufanya vikao/mikutano kwa njia ya mtandao na kupunguza matumizi ya karatasi.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuchukua hatua kwa taasisi za Serikali zinazokiuka taratibu za ununuzi ikiwemo kufanya ununuzi bila kupata ridhaa ya bodi za zabuni. Nitoe wito kwa taasisi zote za Serikali kufuata taratibu za ununuzi wa umma na kuhakikisha kuwa ununuzi wote unaidhinishwa na Bodi za Zabuni. Hii itaongeza uwazi na uwajibikaji katika mchakato wa ununuzi na hivyo, kudhibiti matumizi mabaya ya rasilimali za umma. Aidha, nawaelekeza Maafisa Masuuli kuendelea kutumia Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma katika ununuzi wa bidhaa, huduma na kandarasi pamoja na kuzingatia bei ya soko wakati wa ununuzi.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutekeleza Mkakati wa Kugharamia Miradi ya Maendeleo kwa Kutumia Vyanzo Mbadala (Alternative Project Financing - APF) ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kupunguza utegemezi wa bajeti ya Serikali Kuu. Mfano halisi wa utekelezaji wa mkakati huo ni kufanikiwa kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga (TANGA UWASA) kutoa hatifungani ya kijani yenye thamani ya shilingi bilioni 53.1. Aidha, Serikali itaendelea kutoa mafunzo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, sekta binafsi na taasisi za fedha kuhusu ugharamiaji wa miradi kwa njia mbadala ikiwemo utekelezaji wa miradi kwa ubia baina ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP).
Mheshimiwa Spika, utakumbuka kuwa, mwaka 2023/24, Serikali ilianzisha vitengo vya ufuatiliaji na tathmini katika wizara na taasisi zake ili kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa majukumu ya taasisi husika. Nipende kuwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuviongezea nguvu vitengo hivyo kwa kuvipatia rasilimali watu, fedha na vitendea kazi ili kuhakikisha shughuli zinazotekelezwa zinaakisi thamani halisi ya fedha.
Mheshimiwa Spika, tukitekeleza hatua hizo za kudhibiti matumizi ya fedha za umma, tutaokoa fedha ambazo zitaweza kuelekezwa kwenye miradi itakayosaidia jamii kama vile ujenzi wa barabara, vituo vya afya, miundombinu ya maji na shule. Aidha, niwasihi viongozi wenzangu kuona umuhimu wa kusimamia matumizi ya fedha za umma ili kuweza kuleta maendeleo kwa wananchi. Na niwaonye wale wachache wanaotumia vibaya fedha za umma waache mara moja! Na wale watakaobainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
MAFANIKIO YA SERIKALI YA AWAMU YA SITA
Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa uongozi wake shupavu ambao umedhihirishwa wazi na majira ambayo nchi imepitia. Ikumbukwe kuwa, Mheshimiwa Rais alipokea usukani wa kuiongoza nchi ikiwa imepatwa na tukio la huzuni la kuondokewa na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, tukio ambalo halikuwahi kutokea hapa nchini lakini MAMA hakuyumba na hata sasa tunasonga mbele, nchi haijakwama kwenye jambo lolote, Nchi inasonga mbele!
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipokea nchi katika kipindi ambacho dunia ilikuwa inapita katika msukosuko wa kiuchumi kufuatia UVIKO – 19 na baadae kidogo mzozo wa kisiasa kule Ulaya ya mashariki, msukosuko wa kiuchumi ambao uliyumbisha hata chumi za mataifa makubwa, sababu ambazo zingetosha kuachana na miradi mikubwa ya maendeleo, lakini bado Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, akasema ataendeleza miradi yote iliyokuwa inatekelezwa na awamu zilizopita na ataleta miradi mingine mipya.
Mheshimiwa Spika, licha ya misukosuko hiyo, Serikali ya Chama Cha Mapinduzi chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeendelea kuboresha maeneo yafuatayo: sekta za uzalishaji ikiwemo kilimo, mifugo, uvuvi na madini; miundombinu wezeshi hususan utekelezaji wa miradi ya reli, barabara, viwanja vya ndege, usafiri wa anga na mawasiliano; na huduma za kijamii ikiwemo maji, afya na elimu. Kwa ujumla, Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa na mafanikio makubwa katika kipindi hiki cha miaka mitatu ambayo hayahitaji “VAR” kuyang’amua. Mheshimiwa Spika, naomba uniruhusu sasa nielezee baadhi ya mafanikio hayo kama ifuatavyo:
Sekta ya Uchukuzi
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema, Mheshimiwa Rais aliahidi kuendeleza utekelezaji wa miradi ya awamu zilizopita na kuleta miradi mipya. Ni dhahiri sasa, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan hakusema tu bali ametekeleza kauli hiyo. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipokea mradi wa reli ya kisasa (SGR) ukiwa umetekelezwa kwa asilimia 83.55 kwa Lot 1 na asilimia 57.57 kwa Lot 2 ambazo sasa zimekamilika na kufanyiwa majaribio. Sasa hata nauli zimeshatangazwa Dar es Salaam - Dodoma bei ya jogoo wawili tu yaani shilingi 31,000. Hii inatuambia nini Mheshimiwa Spika? Dkt. Samia Suluhu Hassan, Ameweza pasipo mashaka kuiongoza Tanzania.
Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliahidi kuanzisha miradi mingine mipya. Hilo hakuliahidi tu, limetekelezwa kikamilifu kwani alianzisha ujenzi wa reli Lot 3 (Makutupora -Tabora), Lot 4 (Tabora -Isaka), Lot 6 (Tabora - Kigoma) na Lot 7 (Uvinza - Musongati) ambazo hazikuwepo wakati Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea kijiti. Kazi kwenye vipande vyote hivi inaendelea kwa usimamizi wa upatikanaji wa fedha kupitia Standard Chartered Bank kwa Lot 3, Lot 4 na Lot 5, na Benki ya Maendeleo ya Africa (AfDB) kwa Lot 6 na Lot 7 ikiwa ni ushiriki wa kwanza kwa benki hii kushiriki kwenye mradi kama huu kwenye ukanda wetu.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya bandari ikiwemo kuongeza kina kufikia mita 15.5 na upana mita 200 katika lango la kuingia na kugeuza meli kwa ajili ya kupokea meli kubwa katika bandari ya Dar es Salaam. Kadhalika, Serikali inaendelea na ujenzi wa Bandari Kavu ya Kwala ambapo utekelezaji umefikia asilimia 96.0.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha usafiri wa anga ikiwemo: ujenzi wa kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Msalato ambapo ujenzi umefikia asilimia 56.9 kwa Package I - Miundombinu na asilimia 22.56 kwa Package II - Majengo. Aidha, Serikali inaendelea na ukarabati, upanuzi na uboreshaji wa viwanja vya ndege vya Iringa, Musoma, Tabora, Shinyanga, Sumbawanga na Moshi ambavyo vipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Vilevile, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya hali ya hewa nchini kwa kukamilisha ufungaji wa rada mbili (2) za hali ya hewa katika Mikoa ya Mbeya na Kigoma. Kadhalika, ndege mpya saba (7) zimenunuliwa na hivyo kuifanya ATCL kuwa na jumla ya ndege 16.
Sekta ya Ujenzi
Mheshimiwa Spika, ili kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji nchini pamoja na kuwawezesha wananchi kutekeleza shughuli zao za kiuchumi na kijamii, Serikali ya awamu ya sita imeendelea na ujenzi na ukarabati wa barabara kuu, barabara za mikoa na madaraja kupitia TANROADS pamoja na barabara za mijini na vijijini kupitia TARURA. Ni dhahiri MAMA hasemi tu, bali anatekeleza! Niwape mfano mmoja, utekelezaji wa ujenzi wa Daraja la Kigongo – Busisi lenye urefu wa kilomita 3 na barabara unganishi yenye urefu wa kilomita 1.66 kwa kiwango cha lami umefikia asilimia 88.0 na jumla ya shilingi bilioni 426.1 zimetumika. Mradi huu unatarajiwa kukamilika mwaka 2024/25.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua kuwa barabara za vijijini ni maisha, uchumi na usalama kwa watanzania tulio wengi, Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuiongeza bajeti ya TARURA kutoka shilingi bilioni 710.31 mwaka 2022/23, shilingi bilioni 825.09 mwaka 2023/24 hadi kufikia shilingi bilioni 841.19 kwa mwaka 2024/25. Bajeti hii itawezesha TARURA kuendelea na ujenzi, matengenezo pamoja na ukarabati wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji wa vijijini na mijini. Hii nayo inatuambia nini Mheshimiwa Spika? Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Anatosha kuiongoza Tanzania.
Sekta ya Nishati
Mheshimiwa Spika, MAMA alipokea Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Maji wa Julius Nyerere (JNHPP) utakaozalisha jumla ya MW 2,115 ukiwa na takribani asilimia 37 ambapo hadi Aprili 2024 utekelezaji ulikuwa umefikia asilimia 97.43 na kuanza uzalishaji kupitia mtambo namba tisa (9) unaoingiza katika Gridi ya Taifa jumla ya MW 235 na hivyo, kuimarisha upatikanaji wa umeme. Hadi kufikia hatua hii jumla ya shilingi trilioni 6.01 zimetumika. Kwa sasa kazi inaendelea ili kukamilisha ufungaji wa mitambo saba (7) yenye uwezo wa kuzalisha MW 235 kila mmoja. Aidha, Serikali imekamilisha Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Rusumo kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Kagera ambapo mradi huu unahusisha nchi tatu (3) za Tanzania, Burundi na Rwanda ambao unachangia MW 26.7 katika Gridi ya Taifa. Kwa upande wa mwingine, Serikali imeanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme wa MW 150 kwa kutumia nguvu ya jua katika eneo la Kishapu mkoani Shinyanga. Vilevile, Serikali inaendelea na ujenzi na ukarabati wa njia za kusafirisha na kusambaza umeme ambazo zinaunganisha maeneo mbalimbali nchini na nchi jirani.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita imekamilisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa Kilovoti 400 na kituo kipya cha kupoza umeme cha Chalinze cha Kilovoti 400/220/132 na kimeanza kutumika kuingiza umeme katika Gridi ya Taifa. Kwa upande mwingine, Serikali imekamilisha Mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa Kilovoti 400 yenye urefu wa kilomita 414 kutoka Singida hadi Namanga kupitia Babati na Arusha. Gharama za mradi huu ni dola za Marekani milioni 258.82. Aidha, miundombinu yote ya kusafirisha umeme imekamilika na umeme unasafirishwa kutoka Singida hadi Arusha. Mradi huu utawezesha kuiunganisha Gridi ya Taifa na Nchi za Afrika Mashariki (Eastern Africa Power Pool - EAPP).
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa Kilovoti 400 kutoka Iringa kupitia Mbeya, Tunduma hadi Sumbawanga pamoja na ujenzi wa vituo vya kupoza umeme vya Kisada (Iringa), Iganjo (Mbeya), Tunduma na Sumbawanga umefikia asilimia 27 ya utekelezaji. Gharama za mradi huu ni dola za Marekani milioni 615. Mradi huu unalenga kuunganisha Gridi ya Taifa na nchi za Kusini mwa Afrika (Southern Africa Power Pool – SAPP). Kwa upande mwingine, Serikali imeanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa Kilovoti 132 kutoka Malagarasi hadi Kidahwe mkoani Kigoma. Kazi hii inaenda sambamba na kazi ya ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme wa MW 49.5 kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Malagarasi.
Mheshimiwa Spika, hadi Mei 2024, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeunganisha umeme katika vijiji 11,973, sawa na asilimia 97.2 ya vijiji vyote nchini na wakandarasi wanaendelea kukamilisha uunganishaji wa umeme katika vijiji vilivyobaki. Vilevile, vitongoji 32,827 kati ya 64,359 nchi nzima vimefikishiwa huduma ya umeme. Kazi hiyo inaendelea hadi vitongoji vyote vitakapopata umeme.
Mheshimiwa Spika, katika Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki, Serikali kupitia TPDC inamiliki asilimia 15 ya hisa. Hadi mwezi Mei 2024, Serikali imelipa jumla ya Dola za Marekani milioni 307.3, sawa na asimilia 99.8 ya kiasi kinachotakiwa kulipwa cha Dola za Marekani milioni 308. Kazi mbalimbali zinaendelea kutekelezwa ambapo shehena za mabomba ya mradi yenye jumla ya urefu wa kilomita 600 zimewasili nchini na mradi unatarajia kuendelea kupokea shehena ya mabomba yenye jumla ya urefu wa kilomita 100 kila mwezi kwa miezi 11 ijayo. Kazi ya kulaza mabomba inatarajiwa kuanza mwezi Agosti 2024 na mradi kukamilika Desemba 2025. Mafanikio haya katika sekta ya nishati ni ishara kwamba MAMA amedhamiria upatikanaji wa umeme wa uhakika nchi nzima. Hakika MAMA Mitano Tena!
Sekta ya Maji
Mheshimiwa Spika, sio tu kwamba, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendeleza miradi ya kimkakati na kuleta mipya, bali ameweza kuweka historia ya kukwamua miradi sugu ya maji iliyoshindikana kwa miaka mingi. Katika kutimiza azma ya kumtua mama ndoo kichwani, Serikali imeendelea kutekeleza miradi mikubwa na ya kimkakati yenye lengo la kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji mijini na vijijini. Kwa msisitizo zaidi Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imekamilisha Mradi wa ujenzi wa tekeo (intake) Kigoma na Mradi wa Maji wa Orkesumet Manyara. Aidha, Serikali iliendelea na utekelezaji wa: Mradi wa Ujenzi wa mtambo wa kutibu maji Butimba ambao utekelezaji umefikia asilimia 99; Mradi wa Maji Mugango - Kiabakari - Butiama asilimia 99; Mradi wa Maji Same - Mwanga - Korogwe asilimia 92; Mradi wa Maji kutoka Mto Kiwira kwenda jijini Mbeya asilimia 20; Mradi wa Maji wa Miji 28 asilimia 25; na Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Kidunda asilimia 20. Mheshimiwa Spika, napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu na wananchi kwa ujumla kuwa hadi Desemba 2023, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama ulifikia asilimia 79.6 katika maeneo ya vijijini na asilimia 90.0 mijini. Kwa ujumla, mafanikio hayo yamechangiwa na kukamilika kwa utekelezaji wa miradi 1,633 ya maji vijijini na miradi 213 ya maji mijini. Hii inatwambia nini Mheshimiwa Spika? Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, anajali mahitaji ya lazima ya wananchi wa Tanzania.
Sekta ya Kilimo
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa sekta ya kilimo, Mheshimiwa Rais alipokea nchi ikiwa na eneo la umwagiliaji la ukubwa wa hekta 726,000 tokea tunapata uhuru. Kwa kipindi chake takribani miaka mitatu anatekeleza miradi mipya yenye ukubwa wa hekta 543,366 yenye thamani ya shilingi trilioni 1.18 na ameanza ujenzi wa mabwawa makubwa 14 na kukamilisha upembuzi yakinifu wa mabonde 22. Kwa upande wa sekta ndogo ya mbegu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokea nchi ikiwa inajitosheleza kwa mahitaji ya mbegu bora kwa asilimia 22 tu na sasa ndani ya miaka mitatu ya uongozi wake tumefikia utoshelevu wa asilimia 78 na ifikapo 2026/27 tutakuwa tumejitosheleza kwa asilimia 100. Kwa upande wa uhifadhi wa chakula, nchi ilikuwa na uwezo wa tani 250,000 tu sasa katika kipindi cha miaka mitatu tumefikia tani 500,000. Mauzo ya nje yalikuwa wastani wa dola za Marekani bilioni 1.2 leo tuna wastani wa dola za Marekani bilioni 2.3. Utoshelevu wa chakula umefikia asilimia 124 mwaka 2023/24 na kutarajiwa kufikia asilimia 130 mwaka 2024/25. Hii nayo inatwambia nini Mheshimiwa Spika? Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, anapambana kwa vitendo kuondoa umasikini wa watanzania.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa sekta ya kilimo, Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo kutoka shilingi bilioni 294.0 mwaka 2021/22 hadi shilingi bilioni 970.8 mwaka 2023/24. Kuongezeka kwa bajeti hiyo kumewezesha kuendelea na utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) yenye lengo la kuboresha sekta ya kilimo ili kuongeza tija katika kilimo ikijumuisha kuinua wakulima wadogo, kuimarisha usalama wa chakula na lishe pamoja na kuongeza mchango katika Pato la Taifa. Aidha, Serikali ilitoa ruzuku ya mbolea kiasi cha shilingi bilioni 389.9.
Sekta ya Mifugo na Uvuvi
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuongeza Bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutoka shilingi bilioni 66.8 mwaka 2020/21 hadi bilioni 295.9 mwaka 2023/24. Ongezeko hilo ni mara 4 zaidi ya bajeti iliyokuwa ikitengwa awali. Kutokana na ongezeko hilo na utekelezaji mzuri wa sera na miongozo iliyopo, mafanikio mbalimbali yamepatikana ikijumuisha: kuongezeka kwa mauzo ya mazao ya mifugo na uvuvi nje ya nchi; ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya mifugo na uvuvi ikiwemo Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko ambapo ujenzi umefikia asilimia 53; ujenzi wa miundombinu ya ukuzaji viumbe maji, mialo na masoko ya samaki, ujenzi wa miundombinu ya maabara ya uzalishaji wa chanjo za mifugo, minada ya kisasa 51; ujenzi wa majosho 746 na mabwawa 15; uzalishaji wa malisho na pembejeo ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa maeneo ya malisho hadi kufikia hekta milioni 3.5; kuboresha huduma za ugani nchini kwa kutoa mafunzo na vitendea kazi kwa wataalamu; uboreshaji wa mbari za mifugo na upatikanaji wa vifaranga vya samaki; kuboresha shughuli za uvuvi katika bahari kuu; na kuwawezesha wakulima wa mwani, wafugaji na wavuvi kupata mikopo ya vitendea kazi na fedha taslimu.
Sekta ya Afya
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na jitihada za kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya katika ngazi zote za utoaji huduma nchini. Jitihada hizo zinahusisha uboreshaji wa miundombinu ya vituo vya kutolea huduma vilivyopo pamoja na ujenzi wa vituo vipya zaidi ya 1,324. Waheshimiwa Wabunge na watanzania wenzangu, sote ni mashahidi kuwa katika kipindi cha mwaka 2023/24, vituo vya kutolea huduma za afya viliongezeka na kufikia 12,266 kutoka vituo 11,040 vilivyokuwepo mwaka 2022/23.
Mheshimiwa Spika, sote tunafahamu kuwa, huduma za uchunguzi wa magonjwa ni nguzo muhimu katika utoaji wa huduma za tiba ya magonjwa kwa wananchi. Kwa kutambua hilo, Serikali imeendelea kuimarisha huduma hizo kwa kufanya uwekezaji mkubwa katika upatikanaji wa vifaa vya uchunguzi wa magonjwa ambapo digital X – ray zimefikia 346, ultrasound 677 na mashine za CT scan 31 ambazo zimeanza kutumika kutoa huduma katika Hospitali za Rufaa za Mikoa. Aidha, Serikali imekamilisha usimikaji wa MRI 4. Kuanza kupatikana kwa huduma hizo kumewawezesha wananchi kuokoa gharama za kufuata huduma hizo umbali mrefu ikiwemo kwenda nje ya nchi. Haya ni mapinduzi makubwa yaliyofanywa na Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutoa kipaumbele katika upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vinavyomilikiwa na Serikali. Aidha, katika kuijengea uwezo Bohari ya Dawa (MSD) kuwa na dawa na bidhaa za afya za kutosha, kwa mara ya kwanza na katika historia ya Tanzania Serikali imetoa jumla ya shilingi bilioni 100 ikiwa ni sehemu ya mtaji wa MSD. Fedha hizo zimewezesha upatikanaji wa bidhaa muhimu za afya.
Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto ya uhaba wa wataalam wa afya, katika kipindi hiki, Serikali imetoa kibali cha kuajiri jumla ya watumishi 13,187. Aidha, katika kuimarisha na kuzisogeza huduma za kibingwa na ubingwa bobezi karibu zaidi na wananchi, Serikali imeendelea kutoa ufadhili wa masomo katika fani hizo. Mathalan, kupitia Mpango wa Dkt. Samia Afya Scholarship, jumla ya wataalam 1,251 wanaosomea ubingwa na ubingwa bobezi katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi walipata ufadhili wa masomo kwa gharama ya shilingi bilioni 9 zilizotolewa na Serikali. Hii nayo inatwambia nini Mheshimiwa Spika? Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ana upendo wa dhati kwa watanzania.
Sekta ya Elimu
Mheshimiwa Spika, sasa naomba nizungumzie mageuzi makubwa kwenye sekta ya elimu ambayo yameanza kutekelezwa mwaka huu kwa awamu. Awali ya yote naomba kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka kipaumbele kwenye sekta ya elimu. Katika kipindi cha takribani miaka mitatu cha uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali imeongeza uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu ikiwemo uwekezaji kwenye miundombinu, vitendea kazi, ajira, maslahi ya wanafunzi na kuanzisha mageuzi makubwa ya elimu. Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuimarisha utoaji wa elimu ya msingi na sekondari kwa kuboresha miundombinu ya elimu ikijumuisha ujenzi na ukarabati wa vyumba vya madarasa, mabweni, mabwalo na uzio wa shule ambapo jumla ya shilingi trilioni 1.29 zimetolewa.
Mheshimiwa Spika, uwekezaji katika elimu umeelezwa vizuri katika hotuba za Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia - kwa hiyo sitarudia kwa undani. Hata hivyo, tukumbuke hiki ndicho kipindi ambacho ujenzi na ukarabati wa shule za awali, shule za msingi na shule za sekondari umeongezeka kwa kasi kubwa. Kwa mfano, kama ilivyoelezwa na Mawaziri hao wa sekta ya elimu, Serikali itaanza kujenga shule mia moja za sekondari za mkondo wa amali kuanzia mwaka ujao wa fedha. Mafunzo ya amali yatakayotolewa ni ya nyanja ya ufundi, yaani technical secondary schools, kama ilivyo Tanga Technical School, Moshi Technical School na kadhalika. Na huu ni mwanzo tu. Kadhalika, ujenzi wa vyuo 64 vya VETA katika wilaya 64 ambazo zilikuwa hazina vyuo hivyo pamoja na ujenzi wa chuo cha VETA cha Mkoa wa Songwe unaendelea.
Mheshimiwa Spika, chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, siyo tu kwamba mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu imeongezwa, lakini pia kiasi cha fedha anachopata mwanafunzi kimeongezeka na zaidi ya hapo sasa Serikali imeanza kutoa mikopo hata kwa wanafunzi wanaosoma vyuo vya kati. Hadi Aprili 2024, jumla ya shilingi trilioni 1.98 zimetolewa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu na vyuo vya kati. Kadhalika, Serikali imeondoa ada ya wanafunzi kwa kidato cha tano na cha sita sambamba na kufuta ada ya mitihani. Aidha, Serikali imeendelea kugharamia Programu ya Elimumsingi na Sekondari bila Ada ambapo jumla ya shilingi bilioni 766.1 zimetolewa.
Mheshimiwa Spika, kati ya jambo ambalo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan atakumbukwa nalo daima katika historia ya Taifa letu ni jinsi alivyoagiza na anavyosimamia mageuzi makubwa ya elimu hapa nchini. Mageuzi haya ni makubwa sana, ni magumu sana na yatakuwa na uhitaji mkubwa wa fedha, rasilimali watu na umakini mkubwa. Matunda ya mageuzi haya ni makubwa sana lakini hatutayaona haraka. Haya ni mageuzi ambayo kiongozi anaeangalia tu uchaguzi ujao angeogopa kuyaanzisha. Ni mageuzi ambayo kiongozi anaeangalia maslahi ya vizazi vijavyo angeyapa kipaumbele. Kuna msemo usemao kuwa “a politician looks at the next election but a stateman looks at the next generation”. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan siyo tu kwamba ni mwanasiasa shupavu bali pia ni kiongozi jasiri mwenye maono makuu ya kulijenga Taifa letu kwa vizazi na vizazi.
Mheshimiwa Spika, katika mageuzi haya ya elimu, ifikapo mwaka 2027 kila mtoto wa Kitanzania atalazimika kusoma mpaka kidato cha nne. Kwa maana hiyo kila mtoto itabidi akae shuleni si chini ya miaka kumi. Labda niseme tu, sasa hivi vijana wetu wanamaliza elimu ya lazima, yaani darasa la saba, wakiwa na miaka 13 - umri ambao hawawezi kujiajiri wala hawaajiriki. Kwa mageuzi haya, sasa mtoto wa Kitanzania atamaliza elimu ya lazima akiwa na miaka kumi na sita. Hatua hii inaendana na nchi nyingi duniani na ni hatua nzuri kiuchumi kuandaa nguvu kazi. Zaidi ya hapo, sasa elimu ya kidato cha kwanza mpaka cha sita itakuwa imegawanyika katika mikondo miwili, mkondo wa elimu jumla na mkondo wa elimu ya amali. Wale watakaopitia mkondo wa elimu ya amali watapata elimu ya sekondari sambamba na ujuzi kama unaotolewa kwenye vyuo vya VETA na vyuo vya ufundi. Haya ni baadhi tu ya mambo yaliyoko kwenye mageuzi ya elimu na mitaala.
Mheshimiwa Spika, swali ambalo kila mtu anauliza ni je, tutatenga fedha za kuwezesha utekelezaji wa mageuzi haya ya sera ya elimu na mitaala mipya? Napenda kuwahakikishia waheshimiwa wabunge na watanzania wote kwamba mageuzi haya ni maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, hivyo sisi na Mawaziri wote tunatoa kipaumbele katika kutekeleza mageuzi haya. Fedha zitapatikana na zitatolewa kwa wakati. Tunaharakisha kutumia fedha za Programu ya Kuboresha Upatikaji Fursa Sawa katika Ujifunzaji Ngazi ya Elimu ya Awali na Msingi (BOOST) na Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) ili tuwe na miundombinu ya kutosha kuhakikisha ifikapo mwaka 2027 watoto wote watasoma mpaka kidato cha nne na mafunzo ya amali yatatolewa kwa wanafunzi wengi kwa viwango vinavyotakiwa. Bajeti ya sekta ya elimu kwa mwaka ujao imeongezwa ili kuweza kugharamia mageuzi haya makubwa. Tutafanya kila tuwezalo kufanikisha mageuzi haya makubwa ambayo ni kielelezo hata kwa nchi nyingine za Afrika. Mheshimiwa Spika, hii ndio Tanzania ijayo inayojengwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Sekta ya Madini
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Awamu ya Sita kumekuwa na mafanikio katika sekta ya madini ikiwemo: kuendelea kuongezeka kwa mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa kutoka asilimia 7.3 mwaka 2021 hadi asilimia 9.0 mwaka 2023; kuongezeka kwa vituo vya ununuzi wa madini kutoka 61 mwaka 2020/21 hadi vituo 100 mwaka 2023/24; pamoja na kuanzishwa kwa soko jipya moja (1) la madini hivyo kufikia masoko 42. Aidha, Serikali imenunua mitambo mitano (5) ya uchorongaji kwa ajili ya wachimbaji wadogo inayotumika katika maeneo mbalimbali nchini. Vilevile, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania imeanzisha utaratibu wa kununua dhahabu kwa ajili ya akiba ya Taifa (National Gold Reserve) kwa lengo la kuimarisha akiba ya fedha za kigeni na kusaidia katika utekelezaji wa Sera ya Fedha. Hadi Aprili 2024, Benki Kuu ya Tanzania imenunua dhahabu yenye thamani ya dola za Marekani milioni 26 ambapo malengo ya Serikali ni kununua tani sita (6) za dhahabu yenye thamani ya dola za Marekani milioni 400. Kadhalika, Serikali inaendelea kuhamasisha viwanda vya ndani vya kuchenjua dhahabu kufanya taratibu za kupata Ithibati ya London Bullion Market Association (LBMA) ili kuwezesha dhahabu inayosafishwa kutambuliwa kwenye masoko ya kimataifa na kuweza kununuliwa kwa ajili ya kuhifadhiwa kama fedha.
Sekta ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
Mheshimiwa Spika, sekta ya viwanda imepata mafanikio mbalimbali ikiwemo: kuendelea na ulipaji wa fidia kwa wananchi wanaopisha Mradi Unganishi wa Mchuchuma na Liganga; kukamilisha maandalizi ya kuanza utekelezaji wa mradi wa Magadi Soda Engaruka; kufufua kiwanda cha Kilimanjaro Machines Tools Company (KMTC); kufanya usanifu na kuendeleza utengenezaji wa vifaa tiba na kuvisambaza katika hospitali mbalimbali nchini; kukamilisha utafiti na kutengeneza teknolojia kwa ajili ya kuchakata alizeti itakayosaidia kupunguza uhaba wa mafuta ya kula; kusimamia utekelezaji wa mfumo wa stakabadhi za ghala kwa waendesha ghala na meneja dhamana wa mazao mbalimbali; na kuratibu majadiliano ya kikanda na kimataifa ili kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Sekta ya Maliasili na Utalii
Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kutangaza utalii ndani na nje ya nchi ikiwemo programu ya Tanzania - The Royal Tour ili kuongeza mapato yatokanayo na utalii. Kutokana na mikakati hiyo, idadi ya watalii walioingia nchini iliongezeka hadi 1,808,205 mwaka 2023 kutoka watalii 922,692 mwaka 2021. Aidha, mapato ya utalii yameongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 1.31 mwaka 2021 hadi dola za Marekani bilioni 3.37 mwaka 2023. Ni matumaini yangu kuwa, filamu ya Amazing Tanzania iliyozinduliwa mwezi Mei 2024 itaongeza zaidi mapato yatokanayo na sekta ya utalii.
Sekta ya Mawasiliano
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa sekta ya mawasiliano katika kuhakikisha uwepo wa jamii yenye habari sahihi na iliyowezeshwa kidijitali kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, mafanikio mbalimbali yamepatikana katika sekta hii ikiwemo: kufanyika kwa operesheni ya anwani za makazi ambapo anwani za makazi takribani 12,810,353 zimesajiliwa; na kuongeza wigo wa miundombinu ya mkongo wa Taifa wa mawasiliano kwa kujenga kilomita 3,000 na kufanya jumla ya kilomita 11,319 za mkongo wa Taifa ambazo zitawezesha upatikanaji wa mawasiliano ya kasi na ubora na uhakika katika Wilaya 99 nchini hivyo kuchochea maendeleo ya jamii na uchumi.
Sekta ya Ardhi
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuongeza kasi ya upangaji, upimaji na umilikishaji wa ardhi ambapo hatua mbalimbali zimechukuliwa. Hatua hizo ni pamoja na: utekelezaji wa Mradi wa Usalama wa Milki za Ardhi; kutekeleza Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi kwa kushirikiana na sekta binafsi na taasisi za umma; na kuendelea kuboresha mifumo ya TEHAMA katika utoaji wa huduma. Aidha, kwa kuzingatia umuhimu wa upangaji, upimaji na umilikishaji wa ardhi nchini, Serikali imeridhia kurejeshwa kwa matumizi ya akaunti ya Mfuko wa Maendeleo ya Ardhi ambapo Serikali imetoa mtaji wenye thamani ya shilingi bilioni 15.4 na imeridhia marejesho ya fedha kiasi cha shilingi bilioni 50 za kupanga, kupima na kumilikisha zinazodaiwa kwenye mikopo ya halmashauri ziingizwe kwenye Mfuko huu. Hatua nyingine iliyochukuliwa ni uendeshwaji wa kliniki za ardhi katika mikoa 22 nchini. Kliniki hizi zimekuwa na mafanikio makubwa kutokana na wananchi wengi kujitokeza kusikilizwa kwa uhuru na uwazi changamoto zao na kupatiwa ufumbuzi ambapo hadi Mei 2024, wananchi 35,963 walihudumiwa. Aidha, migogoro na malalamiko 7,444 yalipokelewa ambapo migogoro 4,565 ilitatuliwa na migogoro 2,879 inaendelea kushughulikiwa.
Utawala Bora, Ulinzi na Usalama
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Chama Cha Mapinduzi chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeendelea kuimarisha mifumo ya utoaji haki ikijumuisha ujenzi wa miundombinu na kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika uendeshaji wa mashauri ya mahakama. Aidha, kutokana na umahiri wa Serikali katika kujali haki za binadamu na kuheshimu utawala wa sheria nchini, Tanzania imefanikiwa kuwa mwenyeji wa mikutano ya kimataifa ya masuala haya ikiwemo Kikao cha 77 cha Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu pamoja na Mkutano wa Mawaziri wa Sheria wa nchi za Jumuiya ya Madola. Vilevile, katika jitihada za kukuza na kuimarisha demokrasia nchini, Bunge lako Tukufu lilitunga Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya Mwaka 2024 na Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2023 pamoja na kufanya marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura 258.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha na kusimamia hali ya ulinzi na usalama wa mipaka ya nchi yetu. Katika kuimarisha usalama wa raia na mali zao, Serikali imejenga jumla ya vituo 26 vya polisi vya daraja A, B na C kwa gharama ya shilingi bilioni 9.63; ofisi 6 za makamanda wa polisi wa mikoa shilingi bilioni 9.46; na ujenzi na ukarabati wa nyumba 57 za mapumziko na makazi shilingi bilioni 7.2. Aidha, Tanzania imeendelea kutoa mchango katika ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa na jumuiya za kikanda kupitia Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Jukumu hili limeongeza sifa kwa nchi kimataifa, kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na nchi mbalimbali pamoja na kulipa jeshi letu uzoefu wa kimataifa.
Michezo, Sanaa na Burudani
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita inatambua umuhimu wa michezo, sanaa na burudani katika kukuza ajira hususani kwa vijana. Kwa kuzingatia hilo, Serikali imeendelea kuwaunganisha wasanii wa Tanzania na soko la kimataifa kupitia mikutano na matamasha mbalimbali na kuhakikisha kuwa kazi za ubunifu wao zinalindwa. Aidha, kwa upande wa michezo, Serikali ya awamu ya Sita imeendelea kujenga misingi ya uibuaji na uendelezaji wa vipaji kuanzia mashuleni ambayo imesaidia kuongeza ajira na kipato kwa wachezaji wanaosajiliwa katika timu mbalimbali ndani na nje ya nchi. Kufuatia hatua hiyo ya uendelezaji wa vipaji, imewezesha timu ya taifa ya mpira wa miguu Taifa Stars kushiriki mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa mara ya tatu katika historia ya Taifa letu na Timu ya Taifa ya wanawake ya mpira wa miguu Twiga Stars kufuzu kucheza mashindano ya WAFCON ambayo yatafanyika mwaka 2024 nchini Morocco.
Mheshimiwa Spika, kufuatia jitihada za makusudi za MAMA katika kuimarisha sekta ya michezo nchini, Tanzania itakuwa mwenyeji wa michuano ya kombe la AFCON ya mwaka 2027 kwa kushirikiana na nchi za Uganda na Kenya. Nipende kuwahakikishia kuwa, Serikali imejipanga vyema juu ya maandalizi ya michuano hiyo ikiwemo ujenzi wa uwanja wa mpira wa Samia jijini Arusha kama alivyowasilisha Mheshimiwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Nitoe rai kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania kuanza maandalizi ya timu yetu ya Taifa mapema ili hatimaye tulibakize kombe hilo hapa nyumbani.
Mheshimiwa Spika, maandalizi ya timu yanahitaji uwepo wa viwanja bora. Serikali imejiandaa kujenga viwanja vipya na kukarabati baadhi ya viwanja vilivyopo. Kuhusu ubora wa eneo la kuchezea, yaani pitch kwenye viwanja mbalimbali, tayari Serikali ilitunga sheria inayotoa msamaha kwenye uingizaji wa nyasi bandia na vifaa vyake. Mheshimiwa Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa, msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania tutaanza kutumia ''VAR'' ili kuhakikisha matokeo yanayopatikana uwanjani yanakuwa ya haki maana kuna timu zimezidi - msimu mmoja penati 10, halafu zikifungwa zenyewe magoli yanakataliwa. Na ili tuwe na ''VAR'' za kutosha katika viwanja vyote, naleta pendekezo la kutoa msamaha kwenye uingizaji wa mashine za ''VAR'' na vifaa vyake kwa ufafanuzi utakaotolewa hapo baadae. INAWEZEKANA!
Maslahi ya Watumishi na Wastaafu
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa malimbikizo ya kimshahara na yasiyo ya kimshahara ya watumishi wa umma yanalipwa kwa wakati. Katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita, jumla ya shilingi bilioni 98.63 zimelipwa kama malimbikizo mbalimbali ya watumishi wa umma. Aidha, katika kipindi hicho, Serikali imelipa jumla ya shilingi bilioni 160.04 kwa ajili ya kugharamia upandishwaji wa vyeo kwa watumishi wa umma wapatao 126,814 katika kada mbalimbali. Hata hivyo, kumekuwa na kilio kikubwa kutoka kwa wastaafu kuhusu kikokotoo. Kama asemavyo Naibu Waziri wa Fedha Mheshimiwa Chande kuwa mara zote mtoto akilia mama hujua kwa sauti kuwa hapo mtoto analilia nini. Akilia anasema hapo ameshiba, akilia anasema hapo ana usingizi, akilia anasema hapo nguo zimembana au akilia anasema apelekwe hospitali.
Mheshimiwa Spika, mabadiliko ya kikokotoo yalishusha kundi la wafanyakazi waliokuwa wakipokea mkupuo wa asilimia 50 mpaka asilimia 33 , na kundi waliokuwa wakipokea asilimia 25 walipandishwa mpaka asilimia 33.
Mheshimiwa Spika, Serikali yetu sikivu inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imesikia kilio hicho na imekifanyia kazi kwa maslahi mapana ya wastaafu wetu na wanaotarajiwa kustaafu. Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameelekeza kuongezwa malipo ya mkupuo kutoka asilimia 33 iliopo sasa hadi asilimia 40. Hili ndio kundi kubwa la watumishi wanaofanya kazi nzuri sana kwa taifa letu wakiwepo, Walimu, kada ya afya, Polisi, Magereza, Uhamiaji, Zimamoto na makundi mengine yalioko Serikali kuu na Serikali za Mitaa. Vilevile, Mheshimiwa Rais ameelekeza kuongezewa zaidi kundi lililokuwa likipokea asilimia 25 hapo awali na kupandishwa kwenda asilimia 33 sasa itakuwa asilimia 35 kuanzia mwaka wa fedha huu. Watumishi takriban 17 walioathirika na mabadiliko haya watazingatiwa katika mabadiliko haya. Serikali itaendelea kuangalia maslahi ya wastaafu kwa kuzingatia tathmini ya uhai na uendelevu wa mifuko.
Mheshimiwa Spika, mafanikio hayo yote yamepatikana chini ya uongozi mahiri na thabiti wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, kupitia mchango wa watanzania wakiwemo wakulima, wafanyakazi, wafanyabiashara na wazalishaji. Hii inadhihirisha kuwa MAMA anawapenda sana watanzania, hivyo basi na sisi watanzania Tusimame na MAMA kwa kumpatia wasaidizi makini kutoka Chama Cha Mapinduzi watakaoendeleza gurudumu la maendeleo kupitia uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 2024.
Kuimarisha Upatikanaji wa Fedha za Kigeni
Mheshimiwa Spika, kama ilivyokuwa kwa nchi nyingi duniani, nchi yetu pia ilikabiliwa na changamoto ya upungufu wa fedha za kigeni mwaka 2023/24. Changamoto hii ilisababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo: athari za UVIKO–19; vita vinavyoendelea nchini Ukraine na katika ukanda wa Gaza; mabadiliko ya tabianchi; na kubadilika kwa sera za fedha katika nchi zilizoendelea. Changamoto hizo zilisababisha kupanda kwa riba za fedha kwenye nchi zilizoendelea na masoko ya kimataifa ili kukabiliana na mfumuko wa bei kwenye nchi hizo. Hali hiyo ilipunguza ukwasi na mzunguko wa fedha za kigeni katika uchumi wa dunia kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto hii kuwa kubwa katika nchi nyingi duniani, Serikali ilifanikiwa kukabiliana nayo kwa kushirikiana na sekta binafsi na washirika wa maendeleo ili kuendelea kuwa na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni. Hadi Machi 2024, akiba ya fedha za kigeni ilikuwa dola za Marekani bilioni 5.3, kiasi ambacho kinakidhi uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa miezi 4.4, ambacho kiko juu ya lengo la nchi la muda usiopungua miezi 4.0. Aidha, Serikali iliendelea kutekeleza mkakati wa kupunguza nakisi ya urari wa biashara uliopelekea kupungua kwa nakisi hiyo kutoka dola za Marekani bilioni 5.3 mwaka 2022 hadi dola za Marekani bilioni 2.7 kwa mwaka ulioishia Februari 2024 kwa kuongeza mauzo nje na kupunguza uagizaji wa bidhaa zinazozalishwa nchini.
Mheshimiwa Spika, pamoja na sababu nilizozitaja hapo awali, sisi watanzania pia tunalikuza tatizo la upungufu wa dola kwa baadhi ya watu kudai malipo au kufanya malipo ya bidhaa na huduma zinazotolewa ndani ya nchi kwa kutumia fedha za kigeni yaani, dollarization. Taasisi ipo Tanzania na pengine hata taasisi ya Serikali, inamuuzia huduma mtanzania inamwambia alipe kwa dola, taasisi zingine zinataka mtanzania alipe ada kwa dola, alipe kodi ya nyumba kwa dola, vibali vya kazi, leseni na kadhalika kwa dola. Tunawafanya watanzania wahangaike kuitafuta fedha ya kigeni kununua huduma zinazotolewa ndani ya nchi yao badala ya kuwafanya wageni wahangaike kuitafuta shilingi ya Tanzania wanapotaka huduma ndani ya nchi. Jambo hili linasababisha kuongezeka kwa mahitaji yasiyo ya lazima ya fedha za kigeni na kuwanyima fursa watu wanaohitaji fedha za kigeni kwa ajili ya kulipia bidhaa na huduma muhimu kutoka nje ya nchi. Kitendo cha kuuza bidhaa au huduma za ndani kwa kutumia fedha za kigeni ni kosa kwa mujibu wa kifungu cha 26 cha Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006, ambacho kinabainisha kwamba Shilingi ya Tanzania ndiyo fedha halali pekee kwa malipo ya ndani ya nchi.
Mheshimiwa Spika, kuanzia tarehe 1 Julai, 2024, naelekeza wadau wote wa ndani, taasisi za umma, wafanyabiashara, asasi za kiraia, mashirika ya kimataifa na watu wote waliopo nchini Tanzania wenye tabia ya kuweka bei kwenye huduma au kuuza bidhaa kwa fedha za kigeni kuacha mara moja na kuhakikisha bei za bidhaa na huduma hizo zinatangazwa na kulipwa kwa Shilingi ya Tanzania. Aidha, nazielekeza taasisi zote za Serikali zinazotoza ushuru, ada na tozo mbalimbali kwa fedha za kigeni kurekebisha kanuni zao ili tozo hizo zilipwe kwa shilingi. Hata mgeni akija na fedha za kigeni ni vyema akaibadilisha kuwa fedha ya kitanzania ili aweze kupata huduma. Tunafanya kila malipo kwa fedha za kigeni, halafu shilingi ikishuka thamani tunajiuliza tumekosea wapi.
Mheshimiwa Spika, nawahimiza watanzania wenzangu na wadau wote waliopo nchini kuacha kununua/kulipia vitu vilivyomo nchini kwa fedha za kigeni, hususan vifaa vya kielektroniki, ada za shule/chuo, kodi za nyumba, viwanja, na bidhaa au huduma mbalimbali kwa kuwa ni haki yetu kisheria kulipa bidhaa na huduma kwa sarafu yetu, na ukikubali kulipa kwa fedha za kigeni ni kosa la uhujumu uchumi. Endapo una fedha za kigeni, unatakiwa kuzibadilisha kupitia benki au maduka halali ya kubadilishia fedha ndipo ufanye malipo kwa kutumia shilingi ya Tanzania. Naielekeza Benki Kuu pamoja na vyombo vingine vinavyohusika kuendelea kudhibiti suala hili, kufuatilia kwa ukaribu ili kubaini wote wanaoendelea kufanya makosa hayo, na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Spika, pamoja na sababu za upungufu wa fedha za kigeni nilizozitaja, takribani asilimia 80 ya bidhaa zinazozalishwa nchini kwa ajili ya soko la nje ni bidhaa ghafi. Hali hii inadhihirisha kuwa nchi yetu bado haitumii ipasavyo fursa ya kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini kabla ya kuuzwa nje ili kuongeza fedha za kigeni. Kwa upande mwingine, uzalishaji wa bidhaa na huduma nchini haukidhi mahitaji ya ndani na hivyo kulazimika kutumia kiasi kikubwa cha fedha za kigeni kuagiza bidhaa kutoka nje.
Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha upatikanaji wa fedha za kigeni, Serikali imeandaa Mkakati wa Taifa wa Kuimarisha Upatikanaji wa Fedha za Kigeni wenye malengo ya: kuimarisha uzalishaji na kuongeza thamani ya bidhaa na huduma ili kuongeza mapato ya fedha za kigeni; kuzalisha bidhaa na huduma mbadala zinazoagizwa kutoka nje ili kupunguza matumizi ya fedha za kigeni; na kuimarisha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji kutoka nje ya nchi na sekta binafsi. Nitoe rai kwa sekta husika kutekeleza Mkakati huo ili kufikia matokeo yanayotarajiwa. Aidha, nisisitize taasisi zote za Serikali kuzingatia matakwa ya kifungu cha 60 cha Sheria ya Ununuzi wa Umma Namba 10 ya Mwaka 2023 kinachoelekeza kutoa kipaumbele kwa bidhaa au huduma zinazotengenezwa au kuzalishwa ndani ya nchi katika mikataba inayotolewa kwa misingi ya ushindani wa zabuni za kitaifa au kimataifa ili kupunguza matumizi ya fedha za kigeni na kukuza viwanda vya ndani.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hatua nilizoziainisha hapo juu, napenda pia kuwakumbusha wananchi kuwa suluhisho la kudumu katika kuimarisha thamani ya sarafu yetu ni kuongeza uzalishaji na ubora wa bidhaa na huduma tunazouza nje ya nchi na kukubali kutumia zaidi bidhaa na huduma zinazozalishwa hapa nchini. Ikumbukwe kuwa, thamani ya sarafu ni kielelezo cha uwezo wa uchumi kukidhi mahitaji yake ya msingi, ikiwemo kulipia mahitaji ambayo hayana budi kuagizwa kutoka katika nchi nyingine. Hivyo, kwa kutekeleza hayo, tutakuwa tumechangia kuimarisha sarafu yetu. Kila mmoja wetu ana mchango wa kutoa katika suala hili.
Uendelezaji wa Sekta ya Fedha
Mheshimiwa Spika, sekta ya fedha imeendelea kukua na watumiaji wa huduma rasmi za kifedha wameendelea kuongezeka. Utafiti wa Finscope wa mwaka 2023 unaonesha kuwa asilimia 76 ya watanzania wanatumia huduma rasmi za kifedha ikilinganishwa na asilimia 65 ya mwaka 2017. Pamoja na mafanikio haya, kumekuwa na changamoto mbalimbali katika sekta ya fedha, ikiwemo utoaji wa mikopo yenye riba kubwa inayowaumiza wananchi na kuwarudisha nyuma kimaendeleo (maarufu kama mikopo-umiza, mikopo kausha-damu, mikopo kuzimia, mikopo chuma ulete na kadhalika). Wako baadhi ya watanzania wenzetu wasio na huruma na ambao wanawapa wenzao mikopo yenye masharti ya dhuluma ikiwemo riba kubwa sana na kuuza mali za wakopaji bila kufuata taratibu za kisheria. Aidha, wako baadhi ya watu wanaotoa mikopo hii kwa njia ya vitu badala ya fedha, ila kwa masharti yanayoumiza pia.
Mheshimiwa Spika, wako watu wanaowakopesha wakulima kopo la mbegu la kilogramu 2 halafu wanamtaka mkulima atakapovuna alipe gunia la mazao lenye takribani kilogramu 100, hii ni sawa na riba ya asilimia 5,000. Hii ni dhuluma na ni wizi kama wizi mwingine. Aidha, wapo watu wanaokopeshana fedha kwa makubaliano ya riba ya shilingi 800,000 kwa mwezi ambapo ukikopa shilingi milioni 4 utatakiwa urudishe shilingi milioni 28 baada ya miezi 30, hii ni sawa na riba ya asilimia 240 kwa mwaka. Hii nayo ni dhuluma na ni wizi kama wizi mwingine. Viwango hivi ni vikubwa sana na vinawarudisha nyuma wananchi ambao wakati mwingine wanafanya makubaliano bila kuwa na elimu ya fedha. Hii si huruma, ni dhuluma, ni kuiba kwa kutumia matatizo aliyonayo mtanzania mwenzako.
Mheshimiwa Spika, natoa onyo kwa watu binafsi na kampuni zinazojihusisha na utoaji wa mikopo ya namna hii kuacha mara moja kwani jambo hili linarudisha nyuma wananchi wetu kiuchumi na kuwaingiza katika lindi la umaskini. Aidha, nawakumbusha wananchi wote kuwa na nidhamu ya fedha ikiwemo: kukopa kwa ajili ya mahitaji yenye tija na ikiwezekana kuchukua mikopo kwa ajili ya shughuli za uzalishaji mali badala ya matumizi ya kawaida; kuwa makini katika masharti ya mikataba ya mikopo mnayoingia; na kuhakikisha mikopo mnayopewa inarejeshwa kwa wakati ili msiingie katika mitego ya wakopeshaji wenye nia mbaya ya kuuza dhamana zao. Vilevile, naielekeza Benki Kuu na taasisi zote zinazohusika katika usimamizi wa sekta ya fedha ikiwemo: kamati zote za ulinzi na usalama kuendelea kufuatilia suala hili kwa ukaribu; kuchukua hatua kali dhidi ya wote wanaotoa huduma za fedha bila kuwa na leseni; na kuwanyang'anya leseni wote watakaobainika kuwa wanatoa mikopo bila kuzingatia masharti ya leseni na kuwaumiza wananchi.
Mheshimiwa Spika, katika kutatua changamoto hiyo, Serikali imeendelea kutekeleza programu ya Elimu ya Fedha kwa Umma ya mwaka 2021/22 - 2025/26 pamoja na kuhamasisha usajili na kutoa elimu ya uendeshaji wa vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha. Hadi Februari 2024, Serikali imesajili jumla ya vikundi vya kijamii 49,168 vya huduma ndogo za fedha na wahamasishaji 500. Aidha, Serikali imeteuwa maafisa dawati 212 katika ngazi ya wizara, mkoa, na halmashauri na kuwapatia mafunzo ya uratibu na usimamizi wa biashara ya huduma ndogo za fedha katika maeneo yao. Vilevile, Serikali imetoa leseni kwa watoa huduma za fedha daraja la pili wapatao 1,726 na Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo 759. Mheshimiwa Spika, sekta ya fedha inasimamiwa na sheria mbalimbali ikiwemo Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya Mwaka 2006 na Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018. Kwa msingi huo, ili kampuni au taasisi iweze kutoa mikopo kwa wananchi inapaswa kukidhi matakwa ya sheria tajwa. Hivyo, nasisitiza watanzania kutumia watoa huduma za fedha waliosajiliwa
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuwezesha upatikanaji wa mikopo yenye riba rafiki. Hatua hizo ni pamoja na: kufanya mashauriano na benki ili kupunguza gharama za uendeshaji; Benki Kuu kuimarisha mazingira ya ushindani katika sekta ya fedha; na kuimarisha kanzidata ya taarifa za wakopaji na mwenendo wao katika urejeshaji wa mikopo. Aidha, Serikali itaendelea kutoa elimu ya fedha kwa wananchi ikiwemo umuhimu wa kupanga bajeti pamoja na usimamizi wa fedha binafsi na mikopo ili kuwaepusha kukopa bila kuwa na mipango madhubuti.
Matumizi ya Mifumo ya Malipo ya Kidijitali
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ina lengo mahsusi la kuupandisha hadhi uchumi wa nchi yetu ili kuwa uchumi wa kidijitali. Mojawapo ya hatua kubwa tunazochukua ni kuhakikisha tunakuwa na mifumo madhubuti ya kidijitali, itakayowawezesha wananchi kufanya malipo kwa urahisi popote walipo na kwa gharama nafuu. Katika kutekeleza azma hiyo, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania iliunda na kuzindua Mfumo wa Malipo ya Papo kwa Papo (Tanzania Instant Payment System - TIPS) katika mwaka 2023/24. Lengo la kuundwa kwa TIPS ni kuwezesha miamala kutoka benki na mitandao ya simu kufanyika kwa urahisi zaidi (interoperability), kuongeza ufanisi katika kufanya miamala na kupunguza gharama za miamala. Mheshimiwa Spika, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa, benki zote za biashara na kampuni zote zinazotoa huduma za fedha kwa njia ya simu zimejiunga kwenye mfumo wa TIPS. Hadi sasa, TIPS inawezesha kufanyika kwa miamala yote ikiwemo kati ya mtu na mtu, mtu na biashara, na biashara na biashara. Serikali imeanza hatua nyingine ya utekelezaji wa TIPS itakayowezesha kufanya malipo ya bidhaa na huduma kwa njia ya msimbo wa haraka (QR code).
Mheshimiwa Spika, watumiaji wa mitandao ya kielektroniki kutuma na kupokea fedha walifikia milioni 51.7 mwaka 2023 kutoka watumiaji milioni 38.3 mwaka 2022. Kwa kutumia mfumo wa TIPS, miamala milioni 364.4 baina ya mtu na mtu ilifanyika mwaka 2023 ikiwa na thamani ya shilingi bilioni 11,323.78 ikilinganishwa na miamala milioni 235.5 yenye thamani ya shilingi bilioni 7,369.3 mwaka 2022. Aidha, miamala iliyofanywa na watumiaji wa mitandao ya kielektroniki kununua bidhaa na huduma (mtu na biashara) ilifikia milioni 1,350.8 yenye thamani ya shilingi bilioni 18,250.3 mwaka 2023 kutoka miamala milioni 788.1 yenye thamani ya shilingi bilioni 10,819.7 mwaka 2022. Miamala iliyofanywa na wananchi kupata huduma zinazotolewa na Serikali (mtu na Serikali) ilifikia milioni 10.54 yenye thamani ya shilingi bilioni 426.28 mwaka 2023 ikilinganishwa na miamala milioni 9.5 yenye thamani ya shilingi bilioni 357.2 mwaka 2022.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa pia na ongezeko la mashine za kituo cha mauzo (Point of Sales - POS) kufikia 8,652 zilizofanya miamala milioni 9.9 yenye thamani ya shilingi bilioni 1,922.2 mwaka 2023 ikilinganishwa na mashine 7,317 zilizofanya miamala milioni 6.7 iliyokuwa na thamani ya shilingi bilioni 1,343.9 mwaka 2022. Matumizi ya mifumo ya kielektroniki yameendelea kuboreshwa ambapo sasa unaweza kutumia simu yako kulipia huduma popote ulipo kwa kutumia mfumo wa “lipanamba” (merchant payment). Mfumo huu wa lipanamba sasa unapatikana nchi nzima na idadi ya watoa huduma hii wamefikia 657,346 na miamala iliyofanyika kupitia lipa namba ilikuwa milioni 301.2 yenye thamani ya shilingi bilioni 17,918.12 mwaka 2023 ikilinganishwa na watoa huduma 393,977 na miamala milioni 166.4 mwaka 2022 ikiwa na thamani ya shilingi bilioni 12,103.43. Takwimu hizo zinatuonesha kwamba kuna mwamko mkubwa wa wananchi kufanya miamala kwa kutumia mifumo ya kielektroniki kwani inarahisisha upatikanaji wa huduma.
Mheshimiwa Spika, kumekuwepo na changamoto ya watu kushindwa kufanya miamala kwa kisingizio kuwa mtandao uko chini. Hata hivyo, matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika kufanya miamala yameendelea kuboreshwa ambapo sasa unaweza kutumia simu yako kulipia huduma popote ulipo kwa kutumia mfumo wa “lipanamba” (merchant payment) ambao hauhitaji kuwa na mtandao wa intaneti. Hivyo, napenda nitoe rai kwa watanzania wote kujiunga na mfumo huo wa lipa namba ili kurahisisha ufanyaji wa miamala kiganjani mwako.
Mheshimiwa Spika, katika kurahisisha ufanyaji wa malipo ya kidijitali kwa wananchi, Serikali ilifanya marekebisho kwenye tozo za uwekaji wa miundombinu kwenye hifadhi ya barabara (Right of Way) kwa kupunguza ada ya awali (Initial Fee) ya usimikaji wa nyaya za mawasiliano kutoka dola za Marekani 1,000 kwa kilomita hadi dola za Marekani 200 kwa kilomita na ada ya mwaka (annual fee) kutoka dola za Marekani 1,000 kwa kilomita hadi dola za Marekani 100 kwa kilomita. Lengo la hatua hii ni kufanikisha usambazaji wa miundombinu ya mawasiliano kutoka mkoani kwenda wilayani na kutoka wilayani kwenda kwa wateja ili kuwezesha upatikanaji wa huduma za mawasiliano zilizo bora. Hivyo, natoa rai kwa wananchi kuongeza matumizi ya mifumo ya kidijitali katika kufanya malipo na kupunguza matumizi ya fedha taslimu. Serikali itaendelea kuboresha na kuimarisha mifumo ya malipo ya kidijitali, na kuweka mazingira rafiki ya kufanya malipo, biashara na uwekezaji inayotumia teknolojia za kidijitali kwa ajili ya maendeleo ya watu wetu.
Masuala ya Muungano
Mheshimiwa Spika, ili kuendeleza ustawi wa watanzania na kukuza uchumi wa nchi yetu, umoja wa kitaifa, amani, mshikamano na undugu ni jambo muhimu sana. Serikali inatambua kuwa muungano wetu ndio utaifa wetu. Bila Tanzania Bara hakuna Taifa linaitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na vivyo hivyo, bila Zanzibar hakuna Taifa linaitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndio utambulisho wetu duniani. Mheshimiwa Spika, zaidi ya hayo yote, sasa muungano umepiga hatua zaidi kutoka kwenye karatasi na mchanga vilivyofanyika wakati ule wa ishara ya muungano na kwenda kwenye muungano wa damu, sasa watanzania wameoleana kabila kwa kabila, hakuna kabila moja sasa ambalo hawajaoleana na kabila lingine na wala hakuna upande mmoja wa muungano ambao upande huo watu wake haujaoleana na upande mwingine wa muungano.
Mheshimiwa Spika, sasa kumezuka baadhi ya wanasiasa, kwa sababu za kufilisika kisiasa na kutotambua unyeti wa suala hili wamekuwa wakitoa lugha zinazopandikiza chuki dhidi ya watanzania. Sote tumeshuhudia lugha za kibaguzi zikitolewa na baadhi ya viongozi wakuu wa vyama vya siasa ambazo zinahatarisha muungano wetu. Kauli hizi zikiachwa bila kukemewa na kila mmoja wetu zina uelekeo wa kuvunja muungano wetu na zinatishia kuvunja utaifa wetu na undugu wetu.
Mheshimiwa Spika, tukumbuke, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alituasa kuwa, dhambi ya ubaguzi ni kama dhambi ya kula nyama ya mtu, ukila mara moja hauachi. Tutamaliza kubaguana kwa misingi ya muungano na baada ya hapo tutahamia kubaguana kikabila, tutachomeana vibanda, tutanyang'anyana viwanja, tutafukuziana mifugo, tutavunja utaifa wetu. Tuzikatae wote agenda za viongozi wabaguzi hawa waliofilisika kisera, hawana agenda inayoweza kuwapa uhalali kwa watanzania mpaka watoe lugha za kibaguzi. Lugha hizo ni za hovyo kabisa na za aibu kutolewa na viongozi wa vyama vya siasa. Ikumbukwe kuwa, vyama hivyo vya siasa vimesajiliwa kwa sharti la lazima kuwa viwe vimeungwa mkono na pande mbili za muungano.
Mheshimiwa Spika, inawezekana wenzetu hawa kwa tamaa za madaraka hawajatilia maanani suala hili. Viongozi hao wanafikiri kuwa lugha hizo za kuhatarisha muungano zina mashiko kwa wapiga kura wao na kana kwamba hawajawahi kunufaika na uwepo wa muungano. Kuligawa Taifa kwa ajili ya kufanikisha agenda ya kisiasa ni jambo la hatari sana. Ndugu watanzania, viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani wanaotaka kuligawa Taifa letu kwa maslahi mepesi hawastahili kuaminiwa kupewa uongozi wa nchi, ukiwajaribishia hawa watauvunja muungano wetu, wataiua nchi yetu. Hawafai kabisa!!
Mheshimiwa Spika, narejea tena, kwa hawa wanasiasa wanaotafuta uhalali wa kisiasa kwa misingi ya ukabila au utanganyika au uzanzibar, ni wanasiasa waliofilisika kisera, hawafai, na jambo hili ni la hatari sana kwa Taifa letu. Jambo hili halikubaliki hata kidogo na wala halina afya kwa demokrasia yetu. Vyombo na mamlaka zote zinazohusika zitoe onyo kali kwenye kauli hizi na zichukue hatua kali haya mambo yakijirudia. Tutaulinda muungano kwa gharama yeyote, tutailinda nchi yetu kwa gharama yeyote wala Serikali hatutatoa nafasi kwa yeyote mwenye chokochoko kama hii kufanikisha agenda ovu kama hizo. Mheshimiwa Spika, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa, Serikali zote mbili zina nia ya dhati na thabiti katika kuhakikisha kuwa, hoja za muungano zilizopo na zitakazojitokeza zinashughulikiwa kwa wakati na kuufanya muungano kuwa na maslahi kwa kila mmoja ili kuulinda na kuudumisha muungano wetu adhimu.
Usalama Barabarani
Mheshimiwa Spika, takwimu zetu za ajali zitokanazo na vyombo vya moto zinaashiria hatari kubwa sana ambayo kila mtu anapaswa kuongeza umakini. Watanzania wengi bado hatuheshimu sheria za barabarani, hatuna nidhamu na matumizi ya vyombo vya moto na alama za barabarani. Madhara yake tunapoteza nguvu kazi ya nchi yetu kutokana na ajali za barabarani ambazo zinatuondolea watu wanaotegemewa katika jamii zetu, wakati mwingine kwa uzembe unaoweza kuepukika. Katika kipindi cha miaka mitano yaani kutokea mwaka 2019 hadi Mei 2024, ajali za barabarani zilikuwa 10,093 ambapo vifo vilikuwa 7,639 na majeruhi 12,663 miongoni mwao wakipata ulemavu wa kudumu. Hebu fikiria, magari binafsi - ajali 3,250, vifo 2,090, majeruhi 3,177. Hebu fikiria, mabasi - ajali 790, vifo 782, majeruhi 2,508. Hebu fikiria, daladala - ajali 820, vifo 777, majeruhi 1,810. Hebu fikiria, taxi - ajali 93, vifo 97, majeruhi 173. Hebu fikiria, magari ya kukodi (sherehe, misiba, na shughuli maalum) - ajali 326, vifo 263, majeruhi 302. Idadi hii kubwa ya majeruhi na vifo vya watu kutokana na ajali utadhani nchi iko kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe. Jambo Hili Halikubaliki!
Mheshimiwa Spika, ilivyo sasa wengi huona usumbufu na wakati mwingine mpaka tunaweka chuki na uadui tunapokumbushwa kuhusu usalama wetu na Jeshi la Polisi tuwapo barabarani. Tunavunja sana sheria barabarani, hata magari ya Serikali hivyo hivyo, wakati mwingine tunawagonga waenda kwa miguu. Ni wakati sasa jambo hili kuazimiwa na jamii nzima ya watanzania kwa kuweka mtazamo wa kuchukia ajali. Hatuwezi kuendelea kushuhudia nguvu kazi yetu ikipukutika kirahisi tu kama nyumbu anavyouawa mbugani. Askari barabarani msiwe na huruma hata kidogo kwa wazembe wote wanaokiuka sheria hata kama gari ina usajili wa namba za Serikali. Mheshimiwa Spika, kama sheria zetu ni rafiki sana, tuyaondoe makosa yote ya ajali barabarani kwenye inayoitwa traffic case, tupeleke kwenye makosa makubwa zaidi ikiwezekana huu uwe ni uuaji kama uuaji mwingine kwa maana mtu anayekufyatulia risasi kwa kukusudia ana uhakika kuwa atakujeruhi au kukuua na hata anayefanya uzembe na vyombo vya moto ana uhakika wa kukujeruhi au kuua kwa makusudi kabisa.
Sheria ya Ununuzi wa Umma
Mheshimiwa Spika, utakumbuka Bunge lako tukufu lilitunga upya Sheria ya Ununuzi ya Umma Na.10 ya Mwaka 2023. Baadhi ya mambo yaliyozingatiwa katika sheria hii mpya na kanuni zake ni pamoja na maboresho katika masharti yahusuyo upendeleo wa kitaifa (National Preference), upendeleo wa kipekee kwa watu au kampuni za ndani (Exclusive Preference) pamoja na maeneo mengine ya upendeleo wa ndani.
Mheshimiwa Spika, moja ya maboresho hayo, ni ukomo wa upendeleo (Margin of Preference) kwa bidhaa zilizochimbwa au kuzalishwa ndani ya Tanzania kuendelea kuwa asilimia 15 pamoja na kuwekwa masharti mapya yatakayohakikisha uzingatiwaji wa sharti hili. Aidha, kiwango cha upendeleo wa kipekee (Exclusive Preference) kwa wauzaji wa bidhaa, wakandarasi au watoa huduma wa ndani kimepandishwa kwa kiasi kikubwa hadi kufikia shilingi bilioni 50. Hivyo, zabuni zote zinazohusu bidhaa, kandarasi na huduma ambazo thamani yake haizidi shilingi bilioni 50 zimetengwa kwa wazawa pekee.
Mheshimiwa Spika, Kanuni za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2024 zimeweka masharti mahsusi kuwa upendeleo wa kipekee utatumika kwa wauzaji wa bidhaa, wakandarasi au watoa huduma wa ndani na ushirika wa ndani na wa kigeni ikiwa mchango wa wauzaji wa bidhaa, wakandarasi, au watoa huduma wa ndani katika ushirika ni zaidi ya asilimia 75. Aidha, Sheria imeweka masharti mahsusi yatakayopaswa kuzingatiwa na wazabuni ili kunufaika na upendeleo huu na hivyo kuziba mianya ya matumizi mabaya ya masharti haya.
Mheshimiwa Spika, kwa zabuni ambazo Kampuni za kigeni zitaruhusiwa kushiriki, Kanuni mpya za ununuzi wa umma pia zimetoa upendeleo maalum kwa kampuni za kigeni ambazo zinatoa mikataba midogo (Sub-contracts) kwa kampuni ndogo za ndani. Katika zabuni hizo, Kanuni mpya za Ununuzi wa Umma zimeweka sharti kwa Taasisi nunuzi kulipa moja kwa moja kwa kampuni ya ndani malipo ya mkataba mdogo ulioingiwa baina ya kampuni ya ndani na kampuni ya kigeni kwa kuzingatia masharti ya Mkataba husika.
Mheshimiwa Spika, katika eneo hili, Sheria mpya ya ununuzi wa umma imeruhusu watu au kampuni binafsi za ndani kuingia katika ushirika na kampuni za nje endapo hazina uwezo wa kutekeleza mikataba ya ununuzi wa umma hususan miradi mikubwa ya ujenzi. Endapo ushirika utakaoanzishwa utahusisha kampuni ya kigeni, Sheria imeelekeza kuwa kampuni ya ndani itakuwa ndiyo kampuni kiongozi katika utekelezaji wa mradi husika. Hatua hii inatarajiwa kuleta mageuzi makubwa ikiwemo kujenga uwezo kwa kampuni za ndani ili kuwa sawa na nchi nyingine ambazo miradi mikubwa ya ujenzi katika nchi hizo hufanywa na kampuni za wazawa ambazo zina uwezo mkubwa wa kutekeleza miradi hiyo. Nitoe rai kwa ndugu zangu wakandarasi na watoa huduma pamoja na wauzaji wa bidhaa kutumia fursa hii adhimu na kuitekeleza kwa uaminifu. Sasa sheria imeruhusu wazawa kupata kazi kubwa na kutoa sub contracts kwa wageni, msione woga kuwapa kazi kubwa wazawa ili wao ndio waajiri wageni kwani hata mbuyu ulianza kama mchicha!. Itakuwa ni jambo la kusikitisha sana endapo tutamuangusha Mheshimiwa Rais aliyetupa fursa hii, kwa kutekeleza miradi chini ya kiwango na isioendana na thamani ya fedha.
Mheshimiwa Spika, ili kuongeza uwajibikaji na ufanisi katika ununuzi wa umma, sheria na kanuni za ununuzi wa umma zimeweka viwango vya uidhinishaji kwa Bodi za Zabuni. Ununuzi wowote ambao thamani yake inaangukia chini ya ukomo huo utashughulikiwa na Afisa Masuuli. Viwango hivyo vinategemea ukubwa wa kiwango cha ununuzi wa mwaka kwa taasisi husika (Annual Procurement Volume) na pia umezingatia mahitaji mahsusi ya Taasisi zinazojiendesha kibiashara.
Mheshimiwa Spika, eneo lingine muhimu lililozingatiwa katika Sheria na Kanuni za ununuzi wa umma ni uwepo wa sehemu mahsusi ya usimamizi wa mikataba ya ununuzi inayohusu: uhakiki wa ubora wa bidhaa na huduma; udhibiti wa ongezeko la gharama na muda; mabadiliko na usitishwaji wa mikataba; mgawanyo wa majukumu; na utaratibu wa malipo. Aidha, PPRA imepewa jukumu la kuandaa bei kikomo kwa bidhaa, huduma na kandarasi zenye viwango na vigezo vya kiufundi kwa kuzingatia taarifa za bei kutoka kwa taasisi husika zenye mamlaka ya kuandaa bei hizo. Aidha, Mtendaji yeyote wa Serikali atakayefanya ununuzi juu ya bei kikomo, atachukuliwa hatua za kinidhamu pamoja na kutakiwa kulipa tofauti kati ya gharama halisi ya ununuzi na gharama ambayo ingepatikana kupitia bei kikomo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu upendeleo kwa makundi maalum, kila Taasisi nunuzi itatoa upendeleo wa kipekee wa asilimia 30 katika ununuzi wake wa mwaka kwa ajili ya makundi maalumu yaliyopo katika eneo lake. Kwa kuzingatia utekelezaji hafifu katika eneo hili, Kanuni za Ununuzi wa Umma zimetamka bayana kuwa Afisa masuuli ambaye atakiuka kanuni hii atawajibika kwa hatua za kinidhamu kwa mamlaka husika. Aidha, PPRA itatoa miongozo kwa ajili ya utekelezaji wa masharti ya Sheria na kanuni ikiwemo upendeleo kwa makundi maalum.
Mheshimiwa Spika, maeneo mengine muhimu yaliyozingatiwa katika sheria na kanuni mpya za ununuzi wa umma ni pamoja na: sharti la lazima la matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa ununuzi wa umma, ambapo yeyote atakayekiuka atakuwa ametenda kosa la jinai na atawajibika binafsi baada ya kutiwa hatiani; na kupunguzwa kwa muda wa utekelezaji wa shughuli za ununuzi ili kuongeza ufanisi. Kuhusu masharti ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi kwa utaratibu wa force account, kanuni mpya za ununuzi wa umma zimeweka ukomo wa thamani ya shilingi milioni 100 ambapo ununuzi wowote unaozidi thamani hiyo hautatumia njia hiyo ya force account. Aidha, Sheria na Kanuni za ununuzi wa umma zimeweka masharti madhubuti yanayopaswa kuzingatiwa katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi kwa utaratibu wa force account.
Mheshimiwa Spika, lengo la hatua hizi ni kujenga sekta binafsi iliyo imara na kutengeneza walipa kodi wakubwa hapa nchini. Sheria ni hatua moja, utekelezaji ni hatua nyingine, nitoe rai kwa kamati zetu za ununuzi kuzingatia mwongozo huu. Utaratibu wa kuwapa masharti ya upendeleo wageni na kuwapa masharti yanaoumiza wazawa yanafanya nchi yetu kuendelea kuwa na sekta binafsi changa yenye wigo mdogo wa walipakodi wakubwa. Tunatekeleza miradi wakati mwingine kwa fedha za mikopo, tunapogawa kazi hizo zote kwa wageni tunafanya fedha hiyo ipitilize kwenda nchi nyingine na kuwaachia watanzania mzigo wa deni. Hivyo, nitoe rai pia kwa Maafisa Masuuli wote mnapoingia mikataba hakikisheni mnalinda maslahi ya watanzania.
Mheshimiwa Spika, umekuwepo utaratibu inapoingiwa mikataba na wageni, inawekwa kwenye mkataba, muda wa kulipwa hati za madai zilizoiva na kwamba ikichelewa hata siku moja inatengeneza riba. Hata hivyo, mikataba hiyo haioneshi wazi wajibu wa makandarasi hawa kulipa riba pindi watakapochelewesha malipo ya makandarasi wazawa walio chini yao (sub contract). Na hivyo, tunakuwa na shinikizo la kuwalipa wageni fedha ambazo wao wanapitisha hata miezi minne mpaka sita bila kuwalipa wazawa. Maafisa Masuuli wote mnapoingia mikataba na makandarasi wageni, wekeni masharti ambayo yatatumika pia kwa wakandarasi wazawa kwenye mikataba midogo wanaopata kutoka kwao.
Ushiriki wa Wazawa katika Shughuli za Kiuchumi
Mheshimiwa Spika, pamoja na Serikali kutenga kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, bado sehemu kubwa ya fedha hizo haziwanufaishi wazawa ipasavyo. Sababu kubwa zinazochangia kuwepo kwa hali hiyo ni uwezo mdogo wa kifedha kwa makandarasi wa ndani, mitambo na wataalam ikilinganishwa na kampuni za nje. Kwa kutambua changamoto hizo, Serikali itaendelea kutoa elimu ili kuwajengea uwezo wazawa kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali hasa katika sekta ya ujenzi hapa nchini. Aidha, Serikali imedhamiria kuwawezesha makandarasi wazawa kushiriki kwenye kazi kubwa za ujenzi katika hatua na taratibu zote kuanzia mipango, usanifu, ununuzi, ujenzi na ukarabati. Katika kufanikisha hilo, Serikali imeandaa mkakati wa kuongeza ushiriki wa wazawa katika utekelezaji wa miradi (Local Content Strategy) pamoja na kufanya marekebisho katika Sheria ya Ununuzi wa Umma Namba 10 ya Mwaka 2023 kwa kuongeza wigo wa thamani ya miradi ya kutekelezwa na wazawa peke yao. Nitoe rai kwa sekta zote kuhakikisha kuwa zinazingatia Sheria hiyo na pia mikataba inayosainiwa na makampuni ya nje ihakikishe inazingatia sera ya uwezeshaji ikiwemo kutumia huduma na rasilimali zinazopatikana hapa nchini pamoja na kutoa ajira za moja kwa moja kwenye utekelezaji wa miradi husika. Vilevile, Serikali itaanzisha utaratibu wa Mfuko wa Mtaji (Venture Capital Fund) kwa lengo la kutoa mtaji kwa biashara zinazoanza na ndogondogo (Start-ups na SMEs) kwa utaratibu utakaowekwa.
Mheshimiwa Spika, uwezeshaji wa wazawa utaleta manufaa ikiwemo: faida inayopatikana kutokana na utekelezaji wa miradi kubaki nchini na kutumika kukuza biashara za wazawa; kupunguza matumizi ya fedha za kigeni; kuongeza ajira na ujuzi kwa wataalam wa ndani pamoja na kujenga uwezo wa kampuni za ndani kuweza kushindana kimataifa.
Mabadiliko ya Tabianchi
Mheshimiwa Spika, mabadiliko ya tabianchi yameendelea kuleta athari za kijamii na kiuchumi hasa kwa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania. Hivi karibuni, tumeshuhudia mafuriko nchini yaliyosababisha uharibifu wa miundombinu pamoja na kuathiri shughuli za uzalishaji. Athari hizo zimeendelea kuongeza gharama za utekelezaji wa bajeti, kupunguza kasi ya ukuaji wa uchumi na kuathiri maisha ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua athari za mabadiliko ya tabianchi, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kutenga bajeti kwa ajili ya kutekeleza programu za uhifadhi na usimamizi wa mazingira pamoja na kufanya mazungumzo na Washirika wa Maendeleo ili kupata fedha za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Mathalan, kwa sasa Serikali ipo katika majadiliano na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ili kunufaika na mkopo nafuu kupitia dirisha la Resilience and Sustainability Facility (RSF) kwa ajili ya kuimarisha uwezo wa nchi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Aidha, nitumie fursa hii kuzielekeza taasisi zote kujumuisha masuala ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira wakati wa kupanga na kutekeleza sera na programu mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, katika kuunga mkono juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, napenda nitambue juhudi zinazochukuliwa na Serikali yetu ikiongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kupunguza uchafuzi wa mazingira kupitia hewa ya kaboni. Mheshimiwa Rais katika mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi uliofanyika Dubai mwaka 2023 (COP 28) alizindua rasmi mpango wa utekelezaji wa Mradi wa Nishati Safi ya kupikia kwa Wanawake Afrika (African Women Clean Cooking Support Programme - AWCCSP) ambao una lengo la kuleta mageuzi ya nishati ya kupikia na kumkomboa mwanamke na kulinda mazingira yetu. Aidha, Mheshimiwa Rais alizindua Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024 - 2034) ikiwa ni moja ya hatua za awali za kitaifa za utekelezaji wa programu hiyo. Mkakati huu unalenga kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa watanzania kwa kuimarisha upatikanaji wa malighafi na miundombinu ya uhakika ya nishati safi ya kupikia. Hivyo, napenda kutoa rai kwa wananchi na wadau wote kumuunga mkono Mheshimiwa Rais katika jitihada za kufanikisha utekelezaji wa mkakati huu.
Mwenendo wa Deni la Serikali
Mheshimiwa Spika, hadi Machi 2024, deni la Serikali lilikuwa shilingi bilioni 91,708.28. Kati ya kiasi hicho, deni la nje ni shilingi bilioni 60,954.31 na deni la ndani ni shilingi bilioni 30,753.97. Tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika Desemba 2023 imeonesha kuwa deni ni himilivu katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu. Katika tathmini hiyo, viashiria vinaonesha kuwa kwa mwaka 2023/24: thamani ya sasa ya deni la Serikali kwa Pato la Taifa ni asilimia 35.6 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 55; thamani ya sasa ya deni la nje kwa Pato la Taifa ni asilimia 19.0 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 40; na thamani ya sasa ya deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 113.2 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 180.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na mijadala kuhusu Deni la Serikali ambalo mara nyingi limepotoshwa na kutumiwa kisiasa kama silaha ya kuwatia hofu watanzania kuhusu mwenendo wa deni letu. Mara kwa mara, ongezeko la deni limekuwa likitajwa bila kueleza sababu zake halisi na jinsi fedha hizo zinavyotumika. Napenda kusahihisha rekodi hiyo leo ili kuweka kumbukumbu sawa. Mheshimiwa Spika, ongezeko la deni letu la Taifa limechangiwa na sababu kadhaa za msingi na za kimaendeleo. Kwanza, tumepokea fedha kutoka mikopo ya zamani pamoja na mikopo mipya. Fedha hizo, zimeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo yenye manufaa kwa Taifa letu, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli ya kisasa, viwanja vya ndege, na miradi ya umeme, elimu na afya. Kwa kipindi cha kuanzia tarehe 1 Aprili 2021 hadi 31 Machi 2024, Serikali ilipokea (net inflow) jumla ya shilingi bilioni 17,218.21.
Pili, kupungua kwa thamani ya Shilingi dhidi ya dola ya Marekani kumechangia ongezeko la deni la nje. Kuanzia tarehe 31 Machi 2021 hadi 31 Machi 2024, thamani ya shilingi dhidi ya dola moja imepungua kutoka shilingi 2,309.96 hadi shilingi 2,569.66, sawa na kupungua kwa thamani kwa asilimia 11.24. Hii imesababisha ongezeko la deni la nje kwa shilingi bilioni 5,428.92.
Tatu, ongezeko la deni la ndani lilisababishwa na kutoa hatifungani maalumu zenye thamani ya shilingi bilioni 2,176.7 mwaka 2021/22 kwa ajili ya kulipa deni la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), linalohusu michango ya watumishi waliokuwa kwenye utumishi kabla ya mwaka 1999.
Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo, ni muhimu kuelewa sababu za ongezeko la deni kabla ya kutoa hukumu au kueneza hofu. Serikali yetu inaendelea kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha kwamba mikopo inayochukuliwa inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kwa manufaa ya taifa letu. Hatua hizi zinaenda sambamba na juhudi zetu za kulipa madeni kwa wakati, hali inayotuweka katika nafasi nzuri ya kifedha na kuendeleza uaminifu wetu kimataifa.
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwamba uwiano wa maendeleo ndani ya nchi yetu haukuwa sawa kwa muda mrefu. Baadhi ya mikoa imekuwa na miundombinu bora zaidi, kama vile barabara nzuri, idadi kubwa ya shule za msingi na sekondari, vyuo vingi, na huduma bora za maji na umeme ikiwemo umeme unaofika hadi kwenye mabanda ya mifugo. Wakati huo huo, mikoa mingine inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa umeme katika makazi ya watu. Katika kutatua tofauti hizi, Serikali ya Awamu ya Sita imechukua hatua madhubuti kwa kuingia mikataba ya mikopo ya fedha ili kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta tofauti. Nitaeleza kwa undani zaidi kuhusu miradi hiyo na jinsi fedha hizo zilivyotumika, hivi punde.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, tumekopa jumla ya shilingi bilioni 17,218.21 kutoka katika vyanzo vya nje kwa lengo la kugharamia shughuli mbalimbali za maendeleo. Fedha hizo zimeelekezwa kwenye miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo: Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kwa vipande mbalimbali pamoja na ununuzi wa mabehewa na vichwa vya treni. Mikoa itakayonufaika na mradi huu ni pamoja na Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Katavi na Kigoma. Miradi hii pia itafungua fursa za kiuchumi kutoka nchi jirani kama vile Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/24, sekta ya ujenzi ilitengewa jumla ya shilingi bilioni 4,164.96. Fedha hizo zimeelekezwa kwenye miradi mbalimbali ya ujenzi inayotekelezwa katika mikoa tofauti nchini. Chini ya uongozi wa Mama yetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kwa ushirikiano na washirika wetu wa maendeleo, tumeweza kuendelea na utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya barabara na viwanja vya ndege zaidi ya 14. Miradi hiyo ina thamani ya dola za Marekani bilioni 2.81, sawa na shilingi trilioni 7.34, ikijumuisha mikopo nafuu na misaada kutoka kwa Washirika wa Maendeleo kama Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), Benki ya Dunia, JICA, Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait, na Mfuko wa Maendeleo wa OPEC.
Mheshimiwa Spika, baadhi ya barabara zinazojengwa kwa fedha za washirika hawa ni pamoja na: Ujenzi wa Barabara ya Mabasi ya Haraka (BRT) Awamu ya Pili (Kariakoo - Mbagala), Tatu (Posta - Gongolamboto) na Nne (Posta - Tegeta) Jijini Dar es Salaam; Mradi wa Barabara za Mzunguko kwa Jiji la Dodoma; barabara ya Mnivata - Masasi - Newala; barabara ya kikanda ya Tanzania - Burundi, Rumonge Gitaza kabingo - Kasulu Manyovu; barabara ya kikanda ya Bagamaoyo - Horohoro/Lunga Lunga - Malindi; barabara za Malagarasi - Ilunde - Uvinza, Kazilambwa - Chagu, Kasekese - Ikola - Karema; Barabara ya Kahama -Bulyanhulu - Kakola; barabara za Rusahunga - Rusumo, Mtwara - Mingoyo - Masasi, Rutukila - Songea, Iringa - Msembe; pamoja na ujenzi wa daraja la Jangwani. Ujenzi huu, unaenda sambamba na ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato na viwanja vya ndege vya Tanga, Ziwa Manyara na Iringa. Miradi hii ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji wake na baadhi yake inategemewa kukamilika katika mwaka 2024/25.
Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kuboresha huduma za jamii, jumla ya shilingi bilioni 4,063.31 zilielekezwa kwa ajili ya kupambana na athari za UVIKO-19. Fedha hizi zimeelekezwa katika ujenzi wa madarasa ya shule za msingi na sekondari, kuboresha huduma za afya, na ufufuaji wa sekta ya utalii, miradi ambayo imetekelezwa nchi nzima.
Mheshimiwa Spika, katika sekta ya elimu, shilingi bilioni 2,427.42 zilielekezwa kwenye miradi muhimu ikiwemo Mradi wa Maboresho ya Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi, ambao unatekelezwa na vyuo vikuu vyote vya umma Tanzania Bara na Zanzibar. Aidha, tunaendeleza Mradi wa Kuboresha Elimu Msingi Zanzibar ili kuimarisha misingi ya elimu katika eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa sekta ya maji, shilingi bilioni 1,012.06 zilikopwa kwa ajili ya miradi ya maji inayotekelezwa Tanzania Bara na Zanzibar. Miradi hii inajumuisha Mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini - Sustainable Rural Water Supply and Sanitation kwa upande wa bara, na Mradi wa Usambazaji Maji Mijini kwa upande wa Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kuimarisha miundombinu ya nishati nchini, shilingi bilioni 2,051.32 zilielekezwa kutekeleza miradi mbalimbali ya sekta ya nishati. Kwenye sekta ya mawasiliano, shilingi bilioni 1,631.84 zimeelekezwa kwenye miradi kama Mradi wa Digital Tanzania, unaotekelezwa nchi nzima kuboresha upatikanaji na ubora wa mawasiliano.
Mheshimiwa Spika, katika sekta ya kilimo, shilingi bilioni 1,379.68 zimeelekezwa kutekeleza miradi katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar, ikiwemo mradi wa Tanzania Food Systems Resilience Program na Agricultural Inputs Support Project, ambayo inalenga kuongeza uzalishaji na usalama wa chakula. Aidha, jumla ya shilingi milioni 2,433.98, zimeelekezwa katika sekta nyingine kama ardhi, afya, utawala bora, maendeleo ya jamii na sekta ya fedha ili kuboresha huduma na miundombinu muhimu.
Mheshimiwa Spika, kwa maelezo haya, ni dhahiri kwamba Serikali ya Awamu ya Sita imeingia mikataba ya mikopo ya fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kiasi kikubwa ukiachilia mbali ile sehemu ya deni iliyoongezeka kwa sababu za msukosuko wa uchumi duniani.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, kampuni kubwa za kimataifa za Moody’s Analytics na Fitch Ratings ziliifanyia nchi yetu tathmini ya uwezo wa nchi kukopa na kulipa madeni. Matokeo ya tathmini ya awamu ya kwanza ya mwaka 2023 yalibainisha kuwa Tanzania inakopesheka na ina uwezo wa kulipa madeni. Kampuni ya Moody’s ilifanya mapitio ya pili ya mwenendo wa uchumi wa Tanzania Machi 2024. Kufuatia mapitio hayo, Tanzania imepandishwa Daraja la uwezo wa nchi kukopesheka kutoka B2 ikiwa na mtazamo chanya (Positive Outlook) hadi B1 ikiwa na mtazamo thabiti (Stable Outlook). Daraja hili ni la juu kabisa katika ukanda wa Afrika Mashariki na inatokana na jitihada za Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini ya uongozi thabiti wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji pamoja na ukuaji wa uchumi. Faida za kupandishwa daraja kwa Tanzania ni pamoja na: kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje; na kuongeza upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Serikali na sekta binafsi katika masoko ya fedha ya kimataifa. Aidha, Kampuni ya Fitch imeanza kufanya mapitio kama haya mwezi Mei 2024.
TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2023/24
Mwenendo wa Mapato
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka 2023/24, Serikali ilitarajia kukusanya jumla ya shilingi trilioni 44.39 kutoka katika vyanzo vya ndani na nje. Hadi Aprili 2024, jumla ya shilingi trilioni 35.25 zilipatikana kutoka vyanzo hivyo, sawa na asilimia 79.4 ya lengo la mwaka. Mchanganuo wa mapato yaliyopatikana ni kama ifuatavyo:
Mapato yaliyokusanywa kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania yalikuwa ni shilingi trilioni 21.31, sawa na asilimia 79.7 ya lengo la mwaka;
Mapato yasiyo ya kodi yanayokusanywa na Wizara, Wakala na Taasisi za Serikali yalifikia shilingi trilioni 1.91, sawa na asilimia 54.4 ya lengo la mwaka;
Mapato yanayokusanywa na Mamlaka za Serikali za Mitaa yalifikia shilingi bilioni 931.0, sawa na asilimia 81.4 ya lengo la mwaka;
Misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo ilifikia shilingi trilioni 4.93, sawa na asilimia 90.1 ya lengo la mwaka;
Mikopo ya kibiashara kutoka vyanzo vya ndani ilikuwa shilingi trilioni 4.61, sawa na asilimia 84.8 ya lengo la mwaka; na
Mikopo ya kibiashara kutoka vyanzo vya nje ilikuwa shilingi trilioni 1.56, sawa na asilimia 74.5 ya lengo la mwaka.
Mwenendo wa Matumizi
Mheshimiwa Spika, makadirio ya matumizi yaliyoidhinishwa na Bunge lako Tukufu kwa mwaka 2023/24 ni shilingi trilioni 44.39, ambapo shilingi trilioni 30.31 ni matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 14.08 ni matumizi ya maendeleo. Katika kipindi cha Julai 2023 hadi Aprili 2024, jumla ya shilingi trilioni 35.63 zimetolewa, sawa na asilimia 80.3 ya lengo la mwaka. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 23.29, sawa na asilimia 76.8 ya lengo la mwaka zilikuwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Aidha, jumla ya shilingi trilioni 12.34, sawa na asilimia 87.7 ya lengo la mwaka zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, baadhi ya maeneo yaliyopelekewa fedha katika kipindi cha marejeo ni pamoja na: ulipaji wa deni la Serikali shilingi trilioni 8.84; ulipaji wa mishahara ya watumishi shilingi trilioni 8.28; ujenzi wa barabara, madaraja, na viwanja vya ndege shilingi trilioni 1.27; ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya reli ikiwemo mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) shilingi trilioni 1.71; utekelezaji wa mradi wa Kufua Umeme katika Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) MW 2,115 na mradi wa kusambaza umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) shilingi trilioni 1.02; ugharamiaji wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu na vyuo vya kati shilingi bilioni 570.3; ugharamiaji wa Programu ya Elimumsingi na Sekondari bila Ada shilingi bilioni 333.0; utekelezaji wa mradi wa Kuboresha Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) ikijumuisha ununuzi wa ndege shilingi bilioni 244.8; na utekelezaji wa miradi ya maji mijini na vijijini shilingi bilioni 457.4.
Mheshimiwa Spika, utakumbuka kuwa nchi yetu ilikumbwa na janga la mvua za El-Nino ambazo ziliharibu kwa kiasi kikubwa miundombinu ya barabara, madaraja na reli. Kufuatia hali hiyo, Serikali makini ya Awamu ya Sita ilifanya jitihada za makusudi kurejesha hali ya awali ya miundombinu hiyo kwa kutoa jumla ya shilingi bilioni 136.2 kupitia TANROADS na TARURA. Nipende kuwahakikishia watanzania kuwa Serikali itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya kugharamia ukarabati wa miundombinu iliyoharibiwa. Aidha, nazielekeza taasisi zote zinazohusika na ujenzi wa miundombinu kuhakikisha zinafanya usanifu wa miradi kwa kuzingatia mabadiliko ya tabianchi.
Ulipaji wa Malimbikizo ya Madeni
Mheshimiwa Spika, hadi Aprili 2024, Serikali imelipa madeni yaliyohakikiwa ya jumla ya shilingi trilioni 1.19. Kati ya kiasi hicho, madeni yatokanayo na mashauri ya kimahakama na hati za makubaliano (deed of settlement) ni shilingi bilioni 535.8, wazabuni shilingi bilioni 268.0, makandarasi shilingi bilioni 263.3, watumishi shilingi bilioni 106.7 na watoa huduma shilingi bilioni 14.6. Ulipaji huu wa madeni umesaidia kuongeza ukwasi na hivyo kuchochea shughuli za kiuchumi. Aidha, ili kuipunguzia Serikali gharama za malipo ya madeni, nazielekeza taasisi zote za Serikali kuhakikisha zinawasilisha hati za madai Wizara ya Fedha kwa wakati na kufuata taratibu inapolazimu kuvunja mikataba.
MIKAKATI YA KUONGEZA MAPATO KWA MWAKA 2024/25
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, itaendelea na jitihada za kuongeza mapato ya ndani ikiwa ni pamoja na kuanza utekelezaji wa Mkakati wa Muda wa Kati wa Kuongeza Mapato (2024/25 - 2026/27) kwa lengo la kupunguza utegemezi wa kibajeti na kuzidi kuliletea maendeleo Taifa letu. Mkakati huo umejikita katika kuongeza wigo wa kodi, kuendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi na ukusanyaji wa mapato pamoja na kuhamasisha umma juu ya umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari.
Mheshimiwa Spika, katika kuongeza wigo wa mapato, Serikali itaendelea kuboresha vyanzo vya mapato kwa kuhakikisha vinaakisi misingi ya ukusanyaji mapato. Aidha, utoaji elimu kwa umma kuhusu ulipaji kodi utakuwa endelevu ili kuongeza uhiari na kuhakikisha kodi stahiki inakusanywa. Vilevile, kupitia fursa za uwekezaji zinazoibuliwa, Serikali itaendelea kutambua walipakodi wapya ikiwemo kusajili kampuni za kimataifa zinazoendesha biashara kidijitali hapa nchini kupitia mfumo wa usajili uliorahisishwa.
Mheshimiwa Spika, katika kurahisisha ulipaji kodi, ada na tozo mbalimbali na kuongeza uhiari wa ulipaji wa kodi, Serikali inaendelea kufanya maboresho ya mifumo ya taasisi zenye sura ya utoaji wa huduma kwa pamoja ili kutoa ankara jumuishi ya malipo itakayorahisisha upatikanaji wa mapato kwa wakati na kupunguza muda wa utoaji wa huduma kwa wananchi. Aidha, Serikali imeendelea kuwekeza kwenye matumizi ya TEHAMA ili kuhakikisha mifumo ya Serikali inabadilishana taarifa kwa usahihi, kuondoa urudufu na kuimarisha ufuatiliaji na usimamizi wa fedha za umma. Niendelee kuzihimiza taasisi kuhakikisha malipo yote yanakusanywa kwa kutumia Kumbukumbu Namba ya Malipo ili kudhibiti upotevu wa mapato.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na tabia kwa baadhi ya wafanyabiashara kukwepa kulipa kodi kwa kutumia mbinu mbalimbali. Jambo hili linamsikitisha sana Mheshimiwa Rais kama alivyozungumza katika Baraza la Eid mwezi Aprili 2024, naomba ninukuu “Inasikitisha kuona kwamba baadhi ya wafanyabiashara wanatumia mbinu mbalimbali kukimbia kulipa kodi, hawatoi risiti wanapouza au wakitoa risiti ni zenye upungufu, na wanunuzi wa bidhaa nao hawadai risiti wanaponunua bidhaa au huduma. Naomba mniruhusu nitumie jukwaa hili kusema kwamba ulipaji wa kodi ni jambo la halali kidini. Mwenyezi Mungu ametuwekea mfumo madhubuti wa kiuchumi unaoeleza namna ya bait-ul-mal au hazina ya Serikali zinavyopaswa kukusanya kodi ili ziwe na uwezo wa kuwahudumia wananchi wake”. Mwisho wa kunukuu. Nitumie fursa hii kukemea vikali tabia hiyo na Serikali itachukua hatua kali za kisheria dhidi ya wale wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya ukwepaji kodi.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee, napenda kuwashukuru wananchi wanaoendelea kulipa kodi kwa hiari. Hakika moyo huu wa kizalendo unawezesha Serikali kutekeleza majukumu yake ya kuleta maendeleo ya nchi yetu. Kwa Pamoja Tujenge Taifa Letu! Aidha, Serikali inakusudia kuanzisha Tuzo ya Uzalendo kupitia Mfumo wa Usimamizi wa Risiti za Kielektroniki ili kuhamasisha tabia ya wananchi kudai risiti stahiki pindi wanapofanya ununuzi, na wafanyabiashara kutoa risiti kwa hiari pale wanapofanya mauzo. Tuzo hizo zitatolewa kwa mtindo wa bahati nasibu ambapo zawadi mbalimbali zitakuwa zinatolewa kwa kuchezesha droo ili kuwapata washindi waliotoa na waliodai risiti kwa kipindi husika. Vilevile, Serikali inaendelea kuhimiza juu ya umuhimu wa kuzingatia sheria za kodi pale taasisi za umma, mashirika, watu binafsi na makampuni yanapofanya ununuzi ama kuuza bidhaa na huduma.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendeleza juhudi za kuboresha mazingira wezeshi ya ufanyaji biashara na uwekezaji kwa kurahisisha taratibu na kanuni za uanzishaji na uendeshaji. Aidha, kwa kutambua umuhimu wa biashara ya kimataifa na uwekezaji wa kigeni, Serikali itaendelea kuimarisha na kukuza uhusiano na mataifa mengine, taasisi za kimataifa na jumuiya za kikanda pamoja na kuimarisha utekelezaji wa sera ya diplomasia ya uchumi.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitoa misamaha ya kodi kwa lengo la kuvutia uwekezaji nchini. Hata hivyo, kumekuwa na changamoto ya matumizi yasiyo sahihi ya misamaha hiyo. Hivyo, Serikali inaendelea kuhimiza matumizi sahihi ya misamaha inayotolewa katika uwekezaji na miradi mbalimbali nchini. Aidha, katika kuhakikisha uwazi na ufanisi wa misamaha inayotolewa, Serikali itaendelea kufanya mapitio ya misamaha na vivutio vya kodi vinavyotolewa kwa wawekezaji na kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali. Lengo likiwa ni kubaini faida na umuhimu wake kwa ukuaji wa uchumi wa Taifa, na pale itakapobainika kuwa misamaha hiyo imetumika kinyume na malengo yaliyokusudiwa itafutwa mara moja ili kunusuru upotevu wa mapato.
Mheshimiwa Spika, kama ilivyobainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuwa, baadhi ya taasisi na mashirika ya umma yamekuwa yakipata hasara mwaka hadi mwaka na kusababisha Serikali kutopata mapato stahiki na kuiongezea mzigo kwa kuendelea kupewa ruzuku. Hivyo, nazielekeza taasisi na mashirika ya umma kuweka mikakati ya kuongeza ufanisi ili kusaidia kurejesha fedha za uwekezaji na kuongeza mapato na hatimaye kupunguza mzigo kwa Serikali. Aidha, Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi na tathmini ya utendaji wa taasisi na mashirika ya umma ili kuongeza ufanisi.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha malengo ya ukusanyaji mapato ya Serikali yanafikiwa, nazielekeza taasisi zilizopewa dhamana ya kukusanya mapato ya Serikali kuhakikisha mapato yanakusanywa kupitia mifumo rasmi na kodi stahiki inalipwa kwa mujibu wa sheria kama alivyosisitiza Mheshimiwa Rais, naomba kunukuu “Ahadi yangu kwa watanzania ni kuendelea kusimamia haki kwenye ukusanyaji wa kodi, kuboresha mifumo na kuleta wepesi katika ulipaji na ukusanyaji wa kodi na kuhakikisha kuwa kodi inayokusanywa inatumika ipasavyo kwa manufaa ya wananchi”. Mwisho wa kunukuu. Hivyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge na watanzania wote kwa ujumla tumuunge mkono Mheshimiwa Rais katika kulipa kodi bila shuruti kwa maendeleo ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, kufuatia mvua za El-Nino zilizonyesha nchini kuanzia Septemba, 2023 pamoja na kimbunga Hidaya, barabara mbalimbali za kitaifa katika mikoa 26 zimeathirika. Barabara 68 zilikuwa zimejifunga, barabara 106 zilikuwa zinapitika kwa shida na barabara 168 ziliathirika lakini zinaendelea kupitika kwa shida baada ya kufanyiwa matengenezo ya dharura. Maeneo yaliyoathirika katika barabara hizo yanakadiriwa kufikia kilometa 520. Aidha, madaraja na makalavati yapatayo 189 yalikuwa yamekatika na mengine kuharibika vibaya. Tathmini iliyofanyika inaonesha gharama za kurejesha miundombinu hiyo ni shilingi trilioni 1.07. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 728.0 ni kwa ajili ya kufanya matengenezo ya kurejesha miundombinu ya barabara ili zirudi katika hali yake ya awali na shilingi bilioni 158.0 ni kwa ajili ya matengenezo ya dharura ili barabara hizo ziweze kupitika. Aidha, shilingi bilioni 184.14 ni kwa ajili kurejesha miundombinu iliyoathiriwa na kimbunga Hidaya. Mahitaji hayo ya kurejesha miundombinu iliyoharibika katika hali yake ya kawaida hayakuwepo kwenye bajeti ya mwaka 2023/24 yaliyoidhinishwa na Bunge lako Tukufu na upo uwezekano majanga kama haya kuendelea kujitokeza miaka ijayo.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kurekebisha Sheria ya Mfuko wa Dharura (Contigency Fund) ili uwe na sifa za mfuko maalum kwa ajili ya kugharamia matengenezo ya dharura ya miundombinu ya barabara inayoharibika tukianza na mwaka huu wa fedha ambapo miundombinu ya barabara imeharibika kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Napendekeza vyanzo vya mfuko huu iwe tozo ya miundombinu (infrstructure levy), mapato yatokanayo na tofauti ya kushuka kwa bei za mafuta (the windfall gain in fuel price decrease, asilimia moja ya matumizi ya Serikali kila mwezi na vyanzo vingine vitakavyopangwa na Waziri mwenye dhamana ya Fedha). Undani zaidi utaelezwa kwenye majedwali ya hatua za kikodi.
MABORESHO YA MFUMO WA KODI, ADA, TOZO NA HATUA NYINGINE ZA MAPATO
Mheshimiwa Spika, nchi inatekeleza miradi mikubwa ya kimkakati kwa mara moja kuliko nchi yeyote ukanda wa Afrika kwa mfano, reli yetu ya kisasa SGR itakuwa reli ya tano duniani kwa urefu baada tu ya China km 40,493, Hispania km 3,917, Japani km 3,146, Ufaransa km 2,735 na Tanzania km 2,080, ikifuatiwa na Ujerumani km 1,631, Uturuki km 1,232 na Finland km 1,120. Na itakuwa reli ndefu kuliko reli zote duniani kwa nchi zinazoendelea. Aidha, Tanzania inatekeleza mradi mkubwa wa umwagiliaji na uzalishaji wa mbegu. Tunatekeleza pia mabadiliko makubwa ya mitaala kwa kiwango kikubwa kufanyika katika historia ya nchi yetu na mpango wa elimu bila ada na ruzuku kwenye elimu ngazi zote kwa idadi kubwa ya wanafunzi kuliko kipindi chochote katika historia ya nchi yetu. Vilevile, tunatekeleza maandalizi ya Bima ya Afya kwa wote ambapo Bunge lako Tukufu lilipitisha Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote Na. 13 ya Mwaka 2023 ambayo ni programu kubwa zaidi kwenye sekta ya afya katika historia ya nchi yetu. Kadhalika, tunatekeleza programu kubwa ya miradi ya kufua na kusambaza umeme nchini na tunajenga barabara mijini na kufungua barabara nyingi vijijini kuliko kipindi chochote katika historia ya nchi yetu. Hayo ni baadhi tu!
Mheshimiwa Spika, hii inatuambia nini? haya ni mambo ya kujivunia kwa kila mtanzania. Tusijidharau wenyewe na kwamba sote tuna kazi ya kufanya kukamilisha haya yote. Hii inatupa jukumu la kila mmoja anayestahili kulipa kodi kutimiza wajibu huu kikamilifu. Hivyo, niendeleee kutoa rai kwa watanzania wote kwa kila mmoja wetu kuona umuhimu wa kulipa kodi kwa kuwa kodi yako ndio inayoenda kufanikisha hayo yote. Mheshimiwa Spika, Sheria za ukusanyaji wa kodi zilizotungwa na Bunge lako Tukufu na kusimamiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zinamtaka kila mwananchi kulipa kodi stahiki. Zipo aina mbili za kodi. Aina ya kwanza ni ile ya moja kwa moja (direct taxes) ambazo zinatozwa na sheria za kodi kutoka kwa mlipakodi na kumtaka yeye awasilishe ritani na kulipa kodi husika kwa wakati uliowekwa kisheria. Lakini pia zipo aina za kodi ambazo sio za moja kwa moja (indirect taxes) ambazo Serikali kupitia TRA hukusanya kwa kutumia mawakala.
Mheshimiwa Spika Mathalani, kodi ya PAYE ni kodi kwa mtumishi sio kodi kwa mwajiri. Mwajiri kama ni Kampuni au Shirika linaowajibu wa kumlipa mtumishi mshahara wake na kisha kuzuia shehemu ya mshahara wake kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Mapato SURA Na. 332 na kuiwasilisha ritani na malipo yaliyokatwa kama kodi kwa mtumishi kila ifikapo tarehe 7 ya mwezi unaofuata. Kadhalika, Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni kodi inayotozwa kwa mujibu wa Sheria ya Ongezeko la Thamani SURA Na. 148 kwa wananchi wa kawaida kila wanaponunua bidhaa ama kununua huduma. Kodi hii hukusanywa na wauzaji ambao sheria inawapa wajibu wa kuikusanya na kuiwasilisha TRA kila ifikapo tarehe 20 ya mwezi unaofuata.
Mheshimiwa Spika, Serikali imebaini kuwepo kwa wimbi la wafanyabiashara na Taasisi ambao wana wajibu wa uwakala wa ukusanyaji wa kodi ambao sio waaminifu katika kutimiza wajibu wao uliowekwa kisheria. Mawakala hao wamekuwa wakikusanya kodi hizo na kutokuziwasilisha inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria za kodi. Ni vyema ikafahamika kuwa kodi hii sio kodi ya mfanyabiashara au wakala yeyote, na pia si yeye anayelipa ila yeye anatumika kama mkusanyaji wa kodi ya Serikali na anatakiwa kuiwasilisha Serikali ndani ya muda unaotakiwa kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni za kodi. Ifahamike kuwa, wafanyabiashara hawa wenye wajibu wa uwakala wanaamua kwa makusudi kwenda kinyume na utaratibu wa kisheria, na kwa kufanya hivyo, wanazitumia kodi za walipakodi hawa wa kawaida kwa matumizi binafsi ya biashara zao na hatimae kuonekana kuwa ndio matajiri kumbe wanatumia fedha za watanzania wenzao. Mawakala wanaofanya vitendo hivi wanaihujumu Serikali na jitihada za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuiletea maendeleo nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, ninatoa rai kwa mawakala hao iwe ni waajiri binafsi au Taasisi za Serikali wakiwemo wale waliosajiliwa kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), Kodi ya Zuio (Withholding Tax) na Ushuru wa bidhaa (Excise Duty) kuacha mara moja tabia hiyo ya kuzuia kodi zilizokusanywa kwa wengine na kuzitumia wao badala ya kuziwasilisha TRA kwa mujibu wa sheria. Pia, naelekeza Mamlaka ya Mapato Tanzania kuchukua hatua kali za kisheria kwa mawakala ambao hawatawasilisha ritani na malipo ya kodi hizi ndani ya wakati ikibidi kuwapeleka mahakamani. Hatua hizi zitasaidia kukomboa kodi ya Serikali kwa wakati na kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari ili kuiletea maendeleo nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, kodi ni wajibu wa kila mmoja anayestahili kulipa kodi. Kuna mazingira yasio na usawa ambayo yamezoeleka katika utozaji wa kodi. Mfano, mtu mwenye kima cha chini cha mshahara anayepata shilingi 300,000 kwa mwezi anatozwa kodi sawa na ilivyo kwa mfanyabiashara mdogo mwenye mapato ghafi yanayozidi shilingi 330,000 kwa mwezi. Inatokea makundi mengine kwenye sekta za uzalishaji ambayo kimsingi yanatumia kodi kuboresha shughuli zao lakini hayalipi kodi. Hii haiko sawa na haina usawa. Kwa mfano, mtu mwenye ng'ombe 9,000 kutokulipa kodi na kutaka kujengewa josho au bwawa kwa ajili ya mifugo yake kwa kodi ya mtu mwenye kipato cha shilingi 300,000 kwa mwezi, sio sawa. Mtu mwenye kipato cha milioni 200 au 300 kutokana na kuuza mazao yake kutokulipa kodi na kupokea ruzuku ya mbolea, mbegu au skimu ya umwagiliaji kutokana na kodi ya mtu mwenye kipato cha shilingi 300,000, sio sawa.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kila halmashauri zenye idadi kubwa ya mifugo kuratibu ushirika wa mifugo na kuanzisha mfuko wa kuendeleza huduma za ugani za mifugo na miundombinu ya mifugo kama majosho kwa kutumia mifuko hiyo na magari ya Serikali ya kuchimba mabwawa na visima yalioko mikoani mwetu. Vyama vya wafugaji na wafugaji wakubaliane kuhusu utaratibu wa uendeshaji wa mifuko hiyo kama inavyofanyika kwenye vyama vya ushirika kwenye mazao ya kilimo mfano korosho, tumbaku pamba na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, sasa nijielekeze kwenye mapendekezo ya maboresho ya mfumo wa kodi, ada na tozo mbalimbali kwa mwaka 2024/25. Maboresho hayo yanatarajiwa kujibu maswali na kukidhi kiu ya jamii ya Watanzania katika kuchachua uwekezaji kwenye shughuli mbalimbali za uzalishaji mali ndani ya nchi na kuweka mkazo katika sekta za kimkakati kama vile viwanda, kilimo, madini, utalii, ufugaji na uvuvi, miundombinu ya umeme, uchukuzi na usafirishaji na sekta za kijamii za elimu na afya. Maboresho haya yanalenga pia kukuza uchumi jumla, kukuza ajira na hatimaye kupunguza ukali wa maisha ya wananchi (“Macro economic objectives for inclusive economic growth”). Aidha, Hatua hizo zinalenga pia kuimarisha usimamizi, ukusanyaji wa mapato ya ndani ya nchi na kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali (“Domestic Revenue Mobilization and Improvements in Tax Administration”). Marekebisho yanayopendekezwa yanahusu Sheria zifuatazo:
Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148;
Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332;
Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147;
Sheria ya Usimamizi wa Kodi, SURA 438;
Sheria ya Kuendeleza Ufundi Stadi, SURA 82;
Sheria ya Serikali za Mitaa ya Utozaji wa Kodi ya Majengo, SURA 289;
Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania, SURA 197;
Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha, SURA 342;
Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha, SURA 407;
Sheria ya Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma, Mwaka 2018;
Sheria ya Ushuru wa Barabara na Mafuta, SURA 220;
Sheria ya Mtoto, SURA 13;
Sheria ya Bandari, Mwaka 2004;
Sheria ya Sukari, Namba 6;
Sheria ya Korosho, Namba 18;
Sheria ya Madini, SURA 123;
Sheria ya Michezo ya Kubahatisha, SURA 41;
Sheria ya Reli, Mwaka 2017;
Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, SURA 157;
Sheria ya Magari (Ada ya Usajili na Uhamishaji), SURA 124;
Sheria ya Usimamizi wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004;
Sheria ya Kudhibiti Uingizwaji wa Bidhaa Nchini, SURA 276;
Sheria ya Usafirishaji Bidhaa Nje ya Nchi, SURA 196;
Maboresho ya Ada na Tozo mbalimbali za Taasisi za Serikali pamoja na Utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Kufanya Biashara (Blueprint); na
Marekebisho madogo madogo katika baadhi ya Sheria za Kodi na Sheria nyingine mbalimbali.
Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura 148 kama ifuatavyo:
Kufanya marekebisho kwenye Kipengele cha 18 cha Sehemu ya Kwanza ya Jedwali la Msamaha ili kujumuisha magari pamoja na vifaa vinavyotumiwa na Jeshi la Wananchi (military and armed forces). Lengo la hatua hii ni kuwezesha Jeshi la Wananchi kutekeleza majukumu yake ya ulinzi na usalama wa nchi. Aidha, msamaha utatolewa baada ya kupata uthibitisho wa Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Ulinzi ili kuhakikisha msamaha husika unatumika kwa manufaa ya Jeshi la Wananchi na si vinginevyo;
Kujumuisha wazalishaji na waunganishaji wa ndege nchini kwenye wigo wa msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani unaotolewa kwenye matengenezo kinga ya ndege (aircraft mantainance), uuzaji na ukodishaji wa ndege, injini za ndege na vifaa vyake vinavyouzwa nchini. Lengo la hatua hii ni kufanya wazalishaji na waunganishaji wa ndege nchini kuwa shindani sokoni, kuvutia uwekezaji nchini, kuchochea ukuaji wa tasnia ya Anga pamoja na kuunga mkono juhudi za kuhamasisha Sekta ya Utalii Hatua hii inatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 7.1;
Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye madawa ya kutibu na kusafisha maji, dira za maji na huduma ya uondoshaji wa maji taka (sewage). Msamaha utatolewa kwa Mamlaka za Maji baada ya kupata ridhaa ya Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Maji. Lengo la hatua hii ni kufanikisha utoaji wa huduma ya maji safi na salama nchini;
Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye uingizwaji wa vifaa vya kiteknolojia kwa ajili ya kuwasaidia waamuzi (Video Assistant Referee equipment and accessories). Lengo la hatua hii ni kuhakikisha nchi inapata vifaa muhimu vya michezo kwa kuzingatia kuwa, Tanzania ni moja ya nchi mwenyeji zitakazohusika katika maandalizi ya michuano ya fainali ya kuwania kombe la mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027 na hivyo kunufaika na ongezeko la akiba ya fedha za kigeni, kukuza taswira ya nchi kimataifa na uwepo wa fursa kwa makampuni ya ndani kutangaza biashara zao. Aidha, msamaha utatolewa baada ya vifaa hivyo kupata idhini ya Waziri mwenye dhamana ya masuala ya michezo ili kuhakikisha kuwa msamaha huo unatumika kama ilivyokusudiwa na si vinginevyo;
Kuweka takwa la marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT Refunds) kulipwa ndani ya siku 30 kutoka tarehe ya kuwasilishwa kwa maombi ya marejesho hayo. Hatua hii inalenga kuchochea ulipaji kodi wa hiari na kuongeza uwajibikaji kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania;
Kujumuisha trekta lenye ekseli moja (single axle tractors/ power tiller) linalotambulika kwa HS Code 8701.10.00 kwenye wigo wa zana na vifaa vya kilimo vinavyopata msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani. Marekebisho haya yanalenga kuakisi mawanda ya bidhaa zilizosamehewa pamoja na kuoanisha H.S Codes zilizomo kwenye kitabu cha Viwango vya Pamoja vya Ushuru cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (East African Community Common External Tariff) cha mwaka 2017 na zile zilizomo kwenye kitabu cha mwaka 2022;
Kufanya marekebisho kwenye Sehemu ya Kwanza ya Jedwali la Misamaha ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa kuondoa baadhi ya vifaa vyenye matumizi mbadala kwenye wigo wa vifaa vya kilimo vinavyopata msamaha wa kodi. Vifaa hivyo vinatambulika kwa HS Code 8201.10.00 (chepe); 8201.30.00 (sururu). Lengo la hatua hii ni kuendana na azma ya Serikali ya kupunguza misamaha isiyo na tija kwa lengo la kulinda mapato ya Serikali na kupunguza matumizi yanayohusiana na utoaji wa misamaha ya kodi (tax expenditure). Aidha, tathmini iliyofanywa imebaini kuwa, msamaha husika haujafikia malengo kutokana na vifaa hivyo kuwa na matumizi mbadala. Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 4,250;
Kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa kiwango cha asilimia 0 kwenye madini ya dhahabu yatakayouzwa kwa Benki Kuu ya Tanzania. Lengo la hatua hii ni kuhamasisha uuzaji wa dhahabu kwa Benki Kuu ya Tanzania, na hivyo kuongeza akiba ya nchi ya fedha za kigeni na kupunguza tatizo la uhaba wa dola za Marekani. Aidha, hatua hii inalenga pia kuchochea ukuaji wa viwanda vya kusafisha madini (refineries) nchini kwa kuwa Benki Kuu ya Tanzania hununua dhahabu baada ya kusafishwa na viwanda hivyo pekee;
Kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa kiwango cha asilimia 0 kwenye madini ya dhahabu yatakayouzwa kwa Viwanda vya Kusafishia Dhahabu Nchini (refineries). Lengo la hatua hii ni kuchochea ukuaji wa viwanda hivyo nchini kwa kuhakikisha kuwa vinapata malighafi za kutosha (feed stock). Aidha, pendekezo hili pia linalenga kutimiza azma ya Serikali ya kuhakikisha kuwa madini ghafi ya dhahabu yanasafishwa nchini na kuongezewa thamani kabla ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi;
Kufuta Msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye madini ya thamani, madini ya vito na madini mengine ya thamani yanayouzwa kwenye vituo vya kusafishia dhahabu (refineries) vilivyopo nchini. Lengo la hatua hii ni kuongeza mchango wa Sekta ya Madini katika ukuaji wa Pato la Taifa. Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 18,150;
Kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa kiwango cha asilimia 0 kwenye mbolea inayozalishwa ndani ya nchi kwa kipindi cha mwaka mmoja. Lengo la hatua hii ni kuleta unafuu kwa wakulima na walaji hasa katika kipindi hiki cha mdororo wa uchumi duniani;
Kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa kiwango cha asilimia 0 kwenye bidhaa za nguo zinazotengenezwa kwa kutumia pamba inayolimwa nchini kwa kipindi cha mwaka mmoja. Lengo la hatua hii ni kuleta unafuu kwa wakulima wa pamba na viwanda vinavyotengeneza nguo nchini hasa katika kipindi hiki cha mdororo wa uchumi;
Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye mafuta ya kula yanayozalishwa ndani ya nchi kwa kutumia mbegu zinazozalishwa nchini kwa muda wa mwaka mmoja. Hapo awali, msamaha huu ulitolewa kwa kipindi cha mwaka mmoja (1) kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2023 na ukomo wake ni tarehe 30 June 2024. Lengo la hatua hii ni kuendeleza unafuu wa bei ya mafuta ya kula iliyopanda kutokana na mdororo wa uchumi pamoja na vita ya Urusi na Ukraine vilivyosababisha uhaba wa mafuta hayo; na
Kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye huduma ya data zinazotolewa mtandaoni (online data service). Mabadiliko haya yanaenda sambamba na kuweka tafsiri ya maneno online data services na kujumuisha huduma hiyo kwenye wigo wa utozaji wa huduma za kidijitali. Lengo la hatua hii ni kuongeza wigo wa kodi na kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia. Hatua hii inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 16,397.
Hatua zote za Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 22,393.
Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332 kama ifuatavyo:
Kujumuisha Taasisi zinazofanya shughuli za uboreshaji wa huduma za afya (advancement of health) na utunzaji wa mazingira kwenye wigo wa Taasisi zinazotoa huduma za hisani (Charitable Organisations) ili ziweze kupata nafuu ya ukokotoaji wa Kodi ya Mapato kulingana na matakwa ya Sheria. Lengo la hatua hii ni kuchochea huduma za hisani kwenye eneo la afya na utunzaji wa mazingira hususan katika kipindi hichi ambacho dunia inakabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi;
Kufanya marekebisho ya kifungu cha 4(8) cha Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura. Na. 332, ili kuondoa takwa la kulipa kodi ya mapato mbadala (Alternative Minimum Tax) kwa makampuni yanayochakata mazao ya Chai, ambayo yanatengeneza hasara kwa kipindi cha miaka mitatu (3). Lengo la hatua hii ni kuleta unafuu kwenye Sekta ya Chai ambayo kwa sasa inakabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa hasara unaosababishwa na bei ya zao hilo kushuka katika soko la dunia;
Kufanya marekebisho kwenye Kifungu cha 11 cha Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332 kwa kuweka takwa la risiti za kielektroniki kutumika katika kuthibitisha manunuzi yaliyofanywa kwenye mwaka husika wa mapato ambayo yamechangia katika uzalishaji wa mapato. Hatua hii haitahusisha muuza bidhaa au mtoa huduma ambaye ni raia wa kigeni na hayupo Tanzania au mtu yeyote ambaye hayupo katika wigo wa kutoa risiti za kielektroniki. Lengo la hatua hii ni kuhimiza utoaji risiti za kielektroniki na kulinda mapato ya Serikali;
Kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332 kwa kuruhusu michango ya asilimia 15 inayolipwa na Taasisi za Serikali kwenda Mfuko Mkuu wa Serikali kuwa miongoni mwa sehemu ya gharama za Taasisi kwenye ukokotoaji wa kodi ya mapato (deductible expenditure). Lengo la hatua hii ni kupunguza changamoto zilizopo katika ukokotoaji wa kodi hiyo kwa kuwa fedha hizo huingizwa Mfuko Mkuu wa Serikali. Hatua hii inatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Shilingi milioni 1,000;
Kufanya maboresho kwenye Jedwali la Kwanza la Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332, kwa kurekebisha viwango elekezi vya kodi vinavyotumika kwa wasafirishaji wa abiria ambao mauzo ghafi yao hayazidi kiasi cha shilingi milioni mia moja na ambao hawawajibiki kuandaa hesabu kisheria. Maboresho haya yanalenga kutoa unafuu wa kodi kwa wafanyabishara wa Kundi/ Daraja A na kuendana na hali halisi ya utekelezaji wa shughuli hizo hususan za usafirishaji kupitia daladala. Hatua hii inatarajia kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 2,265;
Jedwali: Utaratibu wa kukadiria kodi ya mapato
unaopendekezwa kwa wasafirishaji wa Abiria kwa kutumia viwango elekezi vya kodi kwa kila Gari
Kuweka takwa kwa raia wa kigeni (non-resident) kukusanya kodi ya zuio kwa kiwango cha asilimia 5 kwenye malipo yanayofanywa kwenda kwa mtengeneza maudhui mkaazi (resident digital content creator). Lengo la hatua hii ni kuongeza wigo wa kodi na kuzingatia kanuni za usawa za utozaji wa kodi. Hatua hii inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 675;
Kutoza Kodi ya Zuio kwa kiwango cha asilimia mbili kwenye malipo yanayotokana na ununuzi wa madini ya viwandani (industrial minerals). Aidha, utozaji huu hautahusisha chumvi, madini ya metaliki au madini mengine ya thamani kama yalivyotafsiriwa kwenye Sheria ya Madini, SURA 123 yatakayouzwa na mmiliki wa Leseni ya Uchimbaji Mdogo wa Madini (Primary Mining Licence) au mchimbaji mdogo wa madini (Artisanal Miner). Lengo la hatua hii ni kuongeza wigo wa kodi na kuzingatia kanuni za usawa za utozaji kodi;
Kutoza Kodi ya Zuio kwa kiwango cha asilimia 3 kwenye mapato yatokanayo na uhamishaji au ubadilishanaji wa mali za kidijitali (digital assets). Mabadiliko haya yanaenda sambamba na kuweka tafsiri ya maneno “mali za kidijitali”. Aidha, Mmiliki wa jukwaa au mtu yeyote atakayefanikisha zoezi la uhamishaji au ubadilishanaji, atawajibika kuwa wakala wa kukusanya kodi hiyo na kuiwasilisha kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania. Raia wa kigeni anayemiliki jukwaa linalotumika kufanikisha uhamishaji au ubadilishanaji wa mali za kidijitali, atapaswa kujisaliji chini ya mfumo uliopo wa simplified tax regime. Lengo la hatua hii ni kuongeza wigo wa kodi na kuzingatia kanuni za usawa za utozaji wa kodi. Hatua hii inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 465;
Kutoza Kodi ya Zuio kwa kiwango cha asilimia 5 kwenye malipo ya biashara ya kutengeneza maudhui ya kidijitali (digital content creators) yanayofanywa na wakaazi (resident business). Lengo la hatua hii ni kuongeza wigo wa kodi na kuzingatia kanuni za usawa za utozaji wa kodi. Hatua hii inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 968;
Kutoza Kodi ya Mapato kwa kiwango cha asilimia 2 kwenye malipo yatakayofanywa na WAFANYABIASHARA WA KATI kutokana na ununuzi wa bidhaa za kilimo, ufugaji, uvuvi na misitu. Kodi inayopendekezwa itakuwa ni kodi ya mwisho na mpokeaji wa mapato hatawajibika kukatwa tena kodi kwa mapato ambayo yameshakatwa kodi hiyo;
Kufanya marekebisho kwenye Kifungu cha 56(5)(a) cha Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332 ili kubainisha kuwa, mabadiliko ya umiliki wa Kampuni iliyopo nchini (resident entity) uliosababishwa na ugawaji wa hisa mpya hautatozwa Kodi ya Mapato kwa mujibu wa Kifungu cha 56. Lengo la hatua hii ni kutoa ufafanuzi wa kifungu hicho na kuondoa changamoto zilizopo katika utekelezaji na usimamizi wa kifungu hicho baada ya kufanyiwa marekebisho kupitia Sheria ya Fedha ya 2023;
Kufanya marekebisho ya Kifungu cha 19 (2) cha Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332 ili kuongeza wigo wa faida itakayotozwa kodi kuanzia mwaka wa nne kwa mfanyabiashara anayepata hasara mfululizo kutoka asilimia 30 hadi asilimia 40. Lengo la hatua hii ni kuiwezesha Serikali kukusanya kodi mapema zaidi bila kuathiri hasara za nyuma za biashara zitakazobakia ambazo mfanyabiashara ataruhusiwa kuzidai kwenye miaka ya mapato itakayofuatia;
Kutoa msamaha wa Kodi ya Zuio kwenye malipo ya riba yanayofanywa na Taasisi za Kifedha za ndani ya nchi (Resident Financial Institutions) kwenda Taasisi za Kifedha au Mifuko ya Kifedha ya nje ya nchi (Non Resident Financial Institutions or Funds) zenye mikataba na Serikali ya kutoa mikopo ya riba nafuu kwa Taasisi za Kifedha za ndani ya nchi. Aidha, msamaha utatolewa pale ambapo mkataba uliosainiwa umekidhi matakwa ya Sheria za nchi na una kipengele kinachobainisha msamaha wa kodi hiyo. Lengo la hatua hii ni kuchochea ukuaji wa uchumi kwa kuhakikisha upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu kwa wananchi pamoja na kuwezesha benki za ndani ya nchi kupata mikopo kwa gharama nafuu kutoka Benki za nje ya nchi; na
Kuweka utaratibu kupitia Kanuni wa utambuzi na ufutaji wa mikopo chechefu kwa taasisi za Kibenki nchini. Lengo la hatua hii ni kutatua changamoto zinazojitokeza katika utambuzi na ufutaji wa mikopo chechefu hususani wakati wa ukokotoaji wa kiasi cha Kodi ya Mapato kinachopaswa kulipwa na Benki husika;
Hatua hizi za Kodi ya Mapato kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 31,738;
Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2023 ilifanya marekebisho ya viwango maalum vya ushuru (specific duty rates) kwa kiwango cha asilimia 10 ya bei kwenye bidhaa zisizo za petroli, na asilimia 20 ya bei kwenye bidhaa za bia na tumbaku ikiwa na lengo la kuakisi mabadiliko ya thamani ya mapato ya Serikali kulingana na mfumuko wa bei. Maboresho hayo hayakujumuisha utozaji Ushuru wa Bidhaa kwa kiwango cha asilimia ya thamani ya bidhaa (advalorem rates) kwa kuwa thamani ya bidhaa inazingatia mfumuko wa bei. Vilevile, Serikali ilianzisha utaratibu wa kurekebisha viwango vya Ushuru wa Bidhaa kila baada ya miaka mitatu (3) kuanzia mwaka wa fedha 2023/24 ili kuiwezesha nchi kuwa na sera za kodi zinazotabirika na kuweka mazingira bora ya uwekezaji nchini. Aidha, napendekeza pia kufanya marekebisho kwa bidhaa nyingine kama ifuatavyo: -
Kupunguza Ushuru wa Bidhaa kutoka shilingi 63.80 kwa lita hadi shilingi 56 kwa lita ya maji ya kunywa yaliyosindikwa kwenye chupa yanayozalishwa nchini. Maji hayo yanatambulika kwa Hs Code 2201.10.00 na 2201.90.00. Lengo la hatua hii ni kuchochea ukuaji wa viwanda vidogo vinavyozalisha maji nchini, kupunguza gharama kwa walaji na kuchochea matumizi ya maji safi na salama. Hatua hii inatarajia kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 474;
Kutoza Ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha shilingi 7,000 kwa kila lita ya Un-denatured Ethyl Alcohol yenye kilevi cha asilimia 80 au zaidi inayotoka nje ya nchi, na shilingi 5,000 kwa kila lita ya Un-denatured Ethyl Alcohol yenye kilevi cha asilimia 80 au zaidi inayozalishwa ndani ya nchi. Bidhaa hiyo inatambulika kwa HS Code 2207.10.00. Utozaji huo hautahusisha Un-denatured Ethyl Alcohol inayotumika kwa matumizi mengine yasiyohusu uzalishaji wa vilevi baada ya kupata ridhaa ya Waziri mwenye dhamana ya masuala husika. Aidha, viwango tofauti vinapendekezwa kwa lengo la kulinda viwanda vya ndani. Lengo la hatua hii ni kuongeza mapato ya Serikali. Hatua hii inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 154,550;
Kutoza Ushuru wa Bidhaa kwa kiwango cha asilimia 10 kwenye thamani ya dau la kamari (value of the stake on betting) kwenye Michezo ya Kubahatisha na Bahati Nasibu ya Taifa. Mapato yatakayokusanywa kutoka chanzo hiki ni kwa ajili ya kugharamia bima ya afya kwa watu wasio na uwezo na makundi maalum hususan wanawake wajawazito na watoto wa umri chini ya miaka mitano. Hatua hii inatarajia kupeleka kiasi cha shilingi milioni 29,522 katika Mfuko huo;
Kutoza Ushuru wa Bidhaa kwa kiwango cha asilimia 10 kwenye ada ya matangazo ya biashara za Michezo ya Kubahatisha na Bahati Nasibu ya Taifa yanayotangazwa kupitia vituo vya televisheni, redio, na tasnia ya uchapishaji. Lengo la hatua hii ni kuongeza wigo wa kodi. Hatua hii inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 9,150;
Kutoza Ushuru wa Bidhaa kwa kiwango cha Shilingi 300 kwa kilo ya tomato sauce na tomato ketchup (HS Code 2103.20.00), pamoja na chilli sauce na chilli ketchup (HS Code 2103.90.00) zile zinazotoka nje ya nchi. Lengo la hatua hii ni kuongeza mapato ya Serikali na kupata fedha za fidia ya athari hasi zinazotokana na matumizi ya sukari na chumvi iliyopo katika bidhaa hizo. Hatua hii inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 634;
Kutoza Ushuru wa Bidhaa kwa kiwango cha Shilingi 500 kwa kilo moja ya rangi za mafuta (solvent based paints and vanishes) zinazotoka nje ya nchi. Rangi hizo zinatambulika kwa heading 32.08. Lengo la hatua hii ni kuongeza mapato ya Serikali na kupata fedha za fidia ya athari hasi zinazotokana na matumizi ya bidhaa hizo. Hatua hii inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 2,433;
Kutoza Ushuru wa Bidhaa kwa kiwango cha Shilingi 963.90 kwa lita ya bia isiyochujwa, yaani opaque ya mfano wa Kibuku (HS Code 2206.00.20) zinazoingizwa kutoka nje ya nchi, na Shilingi 2,959.74 kwa lita ya pombe zenye mchanganyiko wa matunda (HS Code 2206.00.90) zinazotoka nje ya nchi. Lengo la hatua hii kuleta usawa katika utozaji Kodi. Hatua hii inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 327;
Kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura 147 ili kuelekeza asilimia 2 ya mapato ya Ushuru wa Bidhaa yanayokusanywa kutoka kwenye bidhaa za urembo, vinywaji laini (carbonated drinks) na vileo (bia na pombe kali) kwenye Bima ya Afya kwa wote. Lengo la hatua hii ni kuongeza fedha zitakazotumika kwa ajili ya kugharamia bima ya afya kwa watu wasio na uwezo na makundi maalum hususan wanawake wajawazito na watoto wa umri chini ya miaka mitano. Hatua hii inatarajia kupeleka kiasi cha shilingi milioni 18,800 katika Mfuko huo; na
Kuweka takwa kwenye Kanuni za Stempu ya Kodi Kielektroniki za mwaka 2018, linaloelekeza Leseni ya uzalishaji wa bidhaa zinazotozwa Ushuru wa Bidhaa kutolewa baada ya mfumo wa kutoa stempu za kielektroniki kusimikwa na kiwanda kuanza uzalishaji. Takwa hili litaenda sambamba na ukaguzi utakaokuwa ukifanyika mara kwa mara ili kuhakikisha bidhaa zote zinazozalishwa zinawekwa stempu za kielektroniki na kulipiwa kodi stahiki. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vya ndani dhidi ya biashara ya bidhaa feki sokoni, kuboresha usimamizi wa ukusanyaji wa ushuru wa bidhaa na kuzuia upotevu wa mapato ya Serikali.
Hatua hizi za Ushuru wa Bidhaa kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 196,142.
Kuongeza kiwango cha currency points kutoka shilingi 15,000 hadi shilingi 20,000. Lengo la hatua hii ni kuakisi mabadiliko ya thamani ya mapato ya Serikali kwa kuwa utozaji wa currency point kwa kutumia kiwango maalum (specific rates) usiporekebishwa hupoteza thamani ya fedha na hivyo kupunguza mapato ya Serikali. Njia bora inayotumika kuondoa mapungufu hayo ni kurekebisha kiwango hicho ili kuendana na thamani ya fedha; na
Kufanya marekebisho kwenye Kifungu cha 86(1) cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi kwa kuweka ukomo wa faini ya juu ya kosa la kutokutoa risiti wa kiasi cha currency points 1000 (sawa na shilingi 15,000,000). Lengo la hatua hii ni kuleta unafuu kwa walipakodi na kuchochea ulipajikodi kwa hiari.
Sheria ya Kuendeleza Ufundi Stadi, SURA 82
Mheshimiwa Spika, Kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kuendeleza Ufundi Stadi, Sura 82 ili kutokujumuisha gharama za vibarua wanaotumika katika utekelezaji wa miradi ya maji inayosimamiwa na Mamlaka za Maji katika wigo wa kukokotoa Kodi ya Kuendeleza Ufundi Stadi. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za utekelezaji wa miradi na kuongeza ufanisi wa usambazaji wa maji nchini.
Sheria ya Serikali za Mitaa ya Utozaji wa Kodi ya Majengo, SURA 289
Mheshimiwa Spika, Napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Serikali za Mitaa ya Utozaji wa Kodi ya Majengo, Sura 289 ili kuelekeza asilimia 20 ya mapato yanayokusanywa kutoka kwenye kodi ya majengo na kodi ya pango la ardhi ipelekwe moja kwa moja kwenye akaunti za Mamlaka ya Serikali za Mitaa (Halmashauri) husika badala ya utaratibu wa sasa ambapo mapato yote yanaingia Mfuko Mkuu wa Serikali na kisha Halmashauri kuomba kurejeshewa asilimia 20 ya mapato hayo. Lengo la hatua hii ni kuwezesha Mamlaka ya Serikali za Mitaa kugharamia masuala ya ufatiliaji na ukusanyaji wa Kodi ya Majengo na Kodi ya Pango la Ardhi kwa ufanisi na kwa wakati.
Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania, SURA 197;
Mheshimiwa Spika, Napendekeza kufanya marekebisho kwenye vifungu vya 32(2)(b); 35(1); 41 na 42(2) vya Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania, Sura 197 kwa kuongeza maneno ‘return’ or ‘profit’ katika vifungu hivyo. Lengo la hatua hii ni kuwezesha benki na taasisi za fedha zisizo toza riba kutumia fursa zinazotolewa kama ilivyo kwa benki na taasisi zinazotoa huduma za kibenki kwa kufuatia mfumo wa kawaida wa kibenki.
Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha, SURA 342
Mheshimiwa Spika, Napendekeza kufanya marekebisho kwenye kifungu cha 24(g)(iv) cha Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha, Sura 342 kwa kuongeza maneno ‘return’ or ‘profit’. Lengo la hatua hii ni kuruhusu benki zisizo toza riba kufanya biashara kwa kutumia akaunti zao au akaunti za wateja kwenye hati zinazotumika kuzalisha.
Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha, SURA 407
Mheshimiwa Spika, Napendekeza kufanya marekebisho kwenye kifungu cha 4(3) cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania, Sura 407 kwa kuongeza maneno ‘return’ or ‘profit’ ili kuwezesha taasisi au makampuni yanayojihusisha na utoaji wa huduma ndogo za fedha kuweza kutoa huduma hizo kwa misingi ya kutotoza riba.
Sheria ya Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma, Mwaka 2018.
Mheshimiwa Spika, Napendekeza kufanya maamuzi ya muda mfupi ya kugharamia malipo ya nyongeza ya mkupuo kwa asilimia 7 ili kufikia asilimia 40 kwa kundi ambalo lilikuwa linalipwa asilimia 50 kabla ya kuunganishwa kwa mifuko ya pensheni. Vile vile, napendekeza kuongeza kikokotoo kwa asilimia 2 ili kufikia asilimia 35 kwa kundi ambalo lilikuwa linalipwa asilimia 25 kabla ya kuunganishwa kwa mifuko ya pensheni. Nyongeza hizo zitaanza kulipwa kwa wastaafu waliostaafu kuanzia mwaka 2022/23 na kuendelea hadi watakaostaafu mwaka 2029/30 na baada ya hapo mfuko wa PSSSF uchukue jukumu la kuendelea kuwalipa mafao. Lengo la hatua hii ni kutoathiri mfumo mzima wa pensheni kwa kuwa na uwiano wa mafao kwa wanachama na kuupa Mfuko muda wa kuangalia uhimilivu wake. Hatua hii inatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 155,400.
Sheria ya Ushuru wa Barabara na Mafuta, SURA 220
Mheshimiwa Spika, Napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Ushuru wa Barabara na Mafuta, Sura 220 ili kutoza shilingi 382 kwa kila kilo ya gesi asilia inayotumika kwenye magari. Lengo la hatua hii ni kuongeza mapato yatakayotumika katika kufanya matengenezo ya barabara pamoja na kuleta usawa kwa kuwa magari yanayotumia mafuta tayari yanachangia mapato kwa ajili ya matengenezo ya miundombinu ya barabara. Mapato yatakayotokana na chanzo hiki yatapelekwa Mfuko wa Barabara. Hatua hii inatarajia kuongeza Mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 9,500.
Mheshimiwa Spika, Napendekeza pia Kuweka utaratibu wa kutenga fedha kwa ajili ya maendeleo ya miundombinu ya barabara katika kipindi ambacho kutakuwa na punguzo la bei ya mafuta ya petroli sokoni ambapo badala ya bei hizo kushuka fedha hizo zitaelekewa kwenye Mfuko wa Barabara. Utaratibu huu utatekelezwa na Kamati Maalum itakayoundwa na Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Nishati kwa kushirikiana na Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Fedha kwa lengo la kupendekeza kiasi kitakachotengwa kwa kuzingatia wastani wa bei iliyopo sokoni. Aidha, mapato yatakayotokana na utaratibu huu yatapelekwa Mfuko wa Barabara. Lengo la hatua hii ni kuongeza mapato ya Serikali yatakayotumika katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya barabara nchini.
Sheria ya Bandari, Mwaka 2004
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Bandari ya mwaka 2004 ili kurejesha jukumu la kukusanya tozo ya matumizi ya miundombinu ya bandari (wharfage) kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA). Aidha, mapato yatakayotokana na tozo hizo yatawekwa katika akaunti maalum ya TPA iliyopo Benki Kuu ya Tanzania na matumizi yake yatafanyika baada ya kuomba na kupata idhini ya Mlipaji Mkuu wa Serikali. Lengo la hatua hii ni kuiwezesha Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania kupata fedha kwa wakati kwa ajili ya maboresho ya miundombinu ya Bandari na hivyo kuongeza ufanisi wake.
Sheria ya Sukari, Namba 6
Mheshimiwa Spika, Napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Sukari, Namba 6 kama ifuatavyo:
Kuiwezesha Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kununua kuratibu na kuhifadhi pengo la sukari kwenye hifadhi ya chakula ya Taifa. Lengo la hatua hii ni kuwezesha upatikanaji wa Sukari nchini na kuondoa uhodhi kwa baadhi ya wenye viwanda bila kuathiri dhamira ya Serikali ya kulinda viwanda vya ndani;
Kufanya marekebisho kwenye kanuni ya NFRA kwa kuijumuisha sukari kuwa sehemu ya usalama wa chakula; na
Kutoza shilingi 50 kwa kilo ya mabaki (by products) yanayotakana na uzalishaji wa sukari. Lengo la hatua hii ni kuongeza mapato yatakayoiwezesha Bodi ya Sukari kutekeleza majukumu yake ikiwemo kuendeleza mafunzo na kukuza ujuzi katika sekta ya sukari pamoja na kusimamia uzalishaji wa sukari nchini kupitia upanuzi wa viwanda vilivyopo na kuhamasisha uwekezaji mpya.
Sheria ya Korosho, Namba 18
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Korosho ili mapato yatokanayo na tozo ya kusafirisha korosho ghafi nje ya nchi yapelekwe Bodi ya Korosho kwa asilimia 100 kwa kipindi cha miaka mitano. Lengo la hatua hii ni kuchochea maendeleo ya Sekta ya kilimo na kusaidia upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya ruzuku na tafiti pamoja na kuongeza mchango wa zao katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
Mheshimiwa Spika, vilevile ninapendekeza kuipa Mamlaka ya Mapato Tanzania jukumu la kukusanya tozo za kusafirisha mazao nje ya nchi na tozo za kuingiza mazao nchini pamoja na kubainisha mgawanyo wa mapato yatokanayo na tozo hizo kama ifuatavyo: asilimia 70 pelekwe mfuko wa kilimo (ADF); na asilimia 30 ipelekwe mfuko mkuu wa Serikali. Lengo la hatua hii ni kuongeza ufanisi katika ukusanyaji, kuchochea maendeleo ya Sekta ya kilimo na kusaidia upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya majukumu mbalimbali ya Serikali.
Sheria ya Madini, SURA 123
Mheshimiwa Spika, Napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Madini, Sura 123 kama ifuatavyo:
Kufanya marekebisho kwenye Kifungu cha 90A (3) cha Sheria ya Madini, SURA 123 ili kutoa msamaha kwa Benki Kuu ya Tanzania wa kulipa ada ya ukaguzi ya asilimia 1. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za ununuaji wa madini na kuhamasisha uuzaji wa dhahabu kwa Benki ya Tanzania ili kuongeza akiba ya nchi ya fedha za kigeni kwa lengo la kupunguza tatizo la upatikanaji wa dola zinazotumika kwa ajili ya majukumu mbalimbali;
Kupunguza mrabaha unaotozwa kwenye madini ya dhahabu yatakayouzwa kwa Benki Kuu ya Tanzania kutoka asilimia sita (6) hadi asilimia mbili (4) . Marekebisho haya yanaenda sambamba na kuweka takwa la malipo ya mrabaha unaolipwa kwenye madini ya dhahabu yanayouzwa kwa Benki Kuu ya Tanzania kuwa ni malipo ya mwisho (final payments). Lengo la hatua hii ni kuhamasisha uuzaji wa dhahabu kwa Benki Kuu ya Tanzania kwa lengo la kuongeza akiba ya nchi ya fedha za kigeni na kupunguza tatizo la upatikanaji wa dola zinazotumika kwa ajili ya majukumu mbalimbali. Vile vile, hatua hii inalenga kuleta usawa baina ya vituo vya kusafishia madini (refineries) na Benki Kuu ya Tanzania kwa kuwa tayari vituo hivyo vinanufaika na msamaha;
Kuweka takwa la wamiliki wa leseni za uchimbaji wa madini na wafanyabiashara wa madini kutenga kiasi cha madini kwa ajili ya kuchakatwa, kuyeyushwa, kusafishwa na kuuzwa nchini. Aidha, kiasi kitakachopaswa kutengwa kitabainishwa na Waziri mwenye dhamana ya masuala ya madini kwenye Kanuni za Masoko ya Madini za mwaka 2019 ambapo kwa kuanzia kiasi cha asilimia 20 ya sehemu ya dhahabu inayozalishwa nchini kitapaswa kutengwa. Aidha, takwa hili halitahusisha Kampuni za Uchimbaji wa Madini zilizoingia mikataba na Serikali kwa lengo la kutekeleza miradi ya uchimbaji wa madini ya dhahabu nchini ili kuheshimu makubaliano hayo. Serikali itafanya majadiliano na Kampuni hizo ili kuona uwezekano wa kutekeleza takwa la kutenga kuanzia asilimia 20. Hatua hii inalenga kuongeza akiba ya fedha za kigeni nchini na kupunguza tatizo la uhaba wa dola zinazotumika kwa ajili ya majukumu mbalimbali. Vile vile, hatua hii inalenga pia kuchochea ukuaji wa viwanda vya kusafisha madini kwa kuhakikisha vinapata dhahabu ya kusafisha ikiwa ni moja ya hatua za kupata ithibati za kimataifa; na
Kuitambua Benki Kuu ya Tanzania kama mnunuzi wa madini nchini. Lengo la hatua hii ni kuondoa mkinzano uliopo baina ya Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania na Sheria ya Madini na kuiwezesha Benki Kuu ya Tanzania kutekeleza jukumu lake la kisheria la kununua madini ya dhahabu kwa ajili ya kuongeza akiba ya nchi ya fedha za kigeni.
Hatua hizi kwa pamoja zinatarajia kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 114,519.
Sheria ya Michezo ya Kubahatisha, SURA 41.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Michezo ya Kubahatisha, Sura 41 kama ifuatavyo:
Kuanzisha ada ya maombi ya cheti cha uwakala (dealer’s certificate) wa michezo ya kubahatisha ya shilingi 10,000 na ada ya cheti ya shilingi 20,000. Lengo la hatua hii ni kuongeza mapato yatakayowezesha ufanisi na udhibiti bora wa watu binafsi au mawakala wanaofanya biashara katika tasnia ya michezo ya kubahatisha;
Kuanzisha ada ya usajili wa vituo vya bahati nasibu ikiwemo Bahati Nasibu ya Taifa kwa kiwango cha shilingi 30,000. Lengo la hatua hii ni kuongeza mapato yatokanayo na Bahati Nasibu ya Taifa yatakayowezesha ufanisi na udhibiti bora wa michezo ya kubahatisha; na
Kuanzisha ada ya leseni ya uuzaji au usambazaji wa tokeni zinazotumika kwenye mashine za sloti kwa kiasi cha shilingi 500,000 ikiwa ni ada ya maombi ya leseni, na shilingi 1,000,000 ikiwa ada ya leseni kwa mwaka. Lengo la hatua hii ni kuongeza mapato yatakayowezesha Bodi ya Michezo ya Kubahatisha kuongeza ufanisi na udhibiti wa tasnia ya michezo ya kubahatisha.
Hatua hizi kwa pamoja zinatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 180.
Sheria ya Reli, ya Mwaka 2017
Mheshimiwa Spika, Napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Reli ya mwaka 2017 kwa kuongeza kiwango cha Tozo ya Maendeleo ya Reli (Railway Development Levy) kinachotozwa kwa bidhaa zote zinazoingia na kutumika nchini kutoka asilimia 1.5 ya thamani ya mzigo (CIF) hadi asilimia 2 ya thamani ya mzigo (CIF). Aidha, asilimia 50 ya mapato yatakayotokana na chanzo hicho yatapelekwa kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Reli na asilimia 50 itapelekwa kwenye Mfuko wa Barabara. Lengo la hatua hii ni kuongeza mapato yatakayotumika katika kuboresha na kujenga miundombinu ya reli na barabara zilizoathiriwa na mvua za El-Nino. Hatua hii inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 216,898;
Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania SURA 157
Mheshimiwa Spika, Napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Sura 157 kama ifuatavyo:
Kuanzisha ada ya matumizi ya huduma mahsusi za hali ya hewa katika shughuli za ujenzi ya shilingi 500,000/= kwa mradi wenye thamani kuanzia milioni 500 hadi bilioni 1; ada ya shilingi 1,500,000 kwa mradi wenye thamani kuanzia shilingi bilion 1.1 hadi bilioni 10; na ada ya shilingi 5,000,000 kwa mradi wenye thamani zaidi ya bilion 10. Lengo la hatua hii ni kuongeza mapato yatakayowezesha utoaji wa huduma mahsusi za hali ya hewa kwa lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na kuboresha usalama wa watu na mali katika maeneo ya miradi/ujenzi. Hatua hii inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 1,600; na
Kuanzisha ada ya matumizi ya huduma mahsusi za hali ya hewa katika shughuli za usimamizi wa rasilimali maji kwa kiwango cha shilingi 500,000 kwa mwezi kwa kila Bodi ya Maji ya Bonde yenye uwezo mkubwa kifedha na shilingi 200,000 kwa mwezi kwa kila Bodi ya Maji ya Bonde yenye uwezo mdogo kifedha. Lengo la hatua hii ni kuongeza mapato yatakayowezesha utoaji wa huduma mahsusi za hali ya hewa kwa ufanisi kwenye mabonde ya maji pamoja na kuboresha utendaji kazi kwa kuongeza ufanisi katika usimamizi wa rasilimali maji. Hatua hii inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 36.
Sheria ya Magari (Ada ya Usajili na Uhamishaji), SURA 124
Mheshimiwa Spika, Napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Magari (Ada ya Usajili na Uhamishaji) Sura 124 kwa kujumuisha magari ya umeme kwenye wigo wa ulipaji wa ada ya usajili wa magari. Lengo la hatua hii ni kuzingatia kanuni za usawa za utozaji wa kodi na kuendana na mabadiliko ya teknolojia.
Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004
Mheshimiwa Spika, Napenda kukufahamisha kwamba, kikao cha Mawaziri wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki cha Maandalizi ya Bajeti (EAC Pre-Budget Consultative Meeting of Ministers of Finance) kilichofanyika tarehe 17 Mei 2024 jijini Arusha, pamoja na masuala mengine kilipendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Usimamizi wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004 pamoja na Viwango vya Pamoja vya Ushuru wa Forodha vya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Common External Tariff) kwa mwaka wa Fedha 2024/25. Mapendekezo hayo yanalenga kuendeleza mageuzi ya kiuchumi kupitia uimarishaji wa Sera za bajeti na uwekezaji katika kuhimili na kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi kwa maendeleo ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, mapendekezo ya Mawaziri wa Fedha ya kufanya marekebisho kwenye Viwango vya Pamoja vya Ushuru wa Forodha yanahusisha hatua mpya na zinazoendelea ambazo zimekuwa zikitekelezwa katika Mwaka wa Fedha 2023/24. Hatua hizo ni kama zifuatazo:
Mapendekezo ya hatua mpya za Viwango vya Ushuru wa Forodha ni kama ifuatavyo: -
Kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kwa kiwango cha asilimia 0 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye betri za umeme (Lithium-ion Electric accumulators) zinazotambulika kwa HS Code 8507.60.00 zinazotumiwa na wazalishaji au waunganishaji wa magari na pikipiki nchini. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu pamoja na kuchochea uwekezaji katika uzalishaji au uunganishaji wa magari na pikipiki hapa nchini ili kuwezesha upatikanaji wa bidhaa ya mwisho kwa bei nafuu;
Kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kwa kiwango cha asilimia 0 badala ya asilimia 10 kwa mwaka mmoja kwenye runinga ambazo hazijaunganishwa (Unassembled Television(CKD)) zinazotambulika kwa HS Codes 8528.72.10; 8528.73.10. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa waunganishaji wa runinga nchini ili kurahisisha upatikanaji wa bidhaa hiyo kwa gharama nafuu, kuongeza ajira pamoja na kuhamasisha uwekezaji nchini;
Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimekubaliana kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kwa kiwango cha asilimia 0 kwenye malighafi (inputs) zinazotumika katika uzalishaji au uunganishaji wa simu za mkononi. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa wazalishaji na waunganishaji wa simu ndani ya Jumuiya ili kurahisisha upatikanaji wa bidhaa hiyo kwa gharama nafuu, kuongeza ajira pamoja na kuhamasisha uwekezaji;
Kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kwa kiwango cha asilimia 10 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye karatasi zinazotambulika kwa HS Code 4811.90.00 zinazotumiwa na wazalishaji wa lebo na karatasi za kutolea risiti za kielektroniki. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu wa ushuru wa forodha kwenye viwanda vinavyotumia malighafi hii;
Kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kwa kiwango cha asilimia 10 badala ya asilimia 35 kwa mwaka mmoja kwenye malighafi za kutengeneza vioo vigumu (toughened glass) zinazotambulika kwa HS Codes 7005.10.00; 7005.21.00; 7005.29.00; na 7005.30.00. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa watengenezaji wa vioo hivyo nchini;
Kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kwa kiwango cha asilimia 0 badala ya asilimia 25 au asilimia 35 kwa mwaka mmoja kwenye vifungashio vinavyotumiwa na wazalishaji wa maziwa kwa joto la juu yanayodumu kwa muda mrefu (UHT Milk), yoghurt na maziwa ya unga vinavyotambulika kwa HS codes 3923.50.90; 4819.20.90; 4819.30.00; 4819.50.00; 4821.90.00; 7607.19.90. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa wazalishaji wa maziwa hapa nchini, kuongeza ajira pamoja na kuhamasisha uwekezaji kwenye sekta ya maziwa nchini;
Kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kwa kiwango cha asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye malighafi zinazotumiwa na wazalishaji wa Optical Fiber Cables zinazotambulika kwa HS codes 3215.19.00; 3403.99.00; 3506.91.00; 3818.00.00; 3907.99.00; 3907.99.00; 3916.90.00; 3917.39.00; 3919.90.90; 3920.69.90; 3920.99.90; 3921.14.90; 3921.90.90; 5402.11.00; 5404.90.00; 7019.90.90; 8536.90.00; 8544.49.00. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa wazalishaji wa Optical Fiber Cables hapa nchini ili kurahisisha upatikanaji wa mawasiliano kwa gharama nafuu, kuongeza ajira pamoja na kuhamasisha uwekezaji kwenye sekta ya mawasiliano;
Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimekubaliana kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kwa kiwango cha asilimia 0 kwenye malighafi (inputs) zinazotambulika kwa HS Codes 4817.30.00; 4819.10.00; 5407.51.00; 3921.19.90 zinazotumika katika uzalishaji dawa za mbu (mosquito repelants). Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa wazalishaji wa dawa hizo ndani ya Jumuiya ili kurahisisha upatikanaji wa bidhaa hiyo kwa gharama nafuu, kuongeza ajira, kuhamasisha uwekezaji pamoja na kuongeza juhudi za kupambana dhidi ya malaria;
Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimekubaliana kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kwa kiwango cha asilimia 10 badala ya asilimia 25 kwenye malighafi (inputs) zinazotambulika kwa HS Code 2106.90.20 zinazotumika kwenye uzalishaji wa vyakula na vinywaji. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa wazalishaji wa vyakula na vinywaji ndani ya Jumuiya;
Kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 35 badala ya asilimia 10 kwenye vioo vya kawaida na vigumu (float, toughened and multiple-walled insulating units of glass) vinavyotambulika kwa HS Codes 7005.10.00; 7005.21.00; 7005.29.00; 7005.30.00; 7007.19.00; 7007.29.00 na 7008.00.00 kwa mwaka mmoja. Hatua hii inalenga kulinda wazalishaji wa vioo hivyo hapa nchini ili viweze kuwa shindani dhidi ya vioo kutoka nje ya nchi;
Kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 35 au dola za Marekani 3.0 kwa kila mita moja ya mraba (square meter) kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa badala ya asilimia 35 pekee kwa mwaka mmoja kwenye marumaru zinazotambulika kwa HS Codes 6907.21.00; 6907.22.00; na 6907.23.00. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vya ndani vinavyozalisha marumaru, pamoja na kudhibiti udanganyifu wa thamani halisi ya bidhaa hizo kutoka nje;
Kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 25 au dola za Marekani 300 kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton) kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa badala ya ushuru wa asilimia 25 au dola za Marekani 200 kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton) kwa mwaka mmoja kwenye bidhaa za mabati zinazotambulika kwa HS codes 7210.49.00; 7210.61.00; 7210.69.00; 7210.70.00; 7210.90.00; na 7212.30.00. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vya ndani, kuongeza ajira pamoja na mapato ya Serikali;
Kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 25 au dola za Marekani 300 kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton) kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa badala ya asilimia 35 kwa mwaka mmoja kwenye bidhaa za mabati zinazotambulika kwa HS codes 7212.40.00; na 7212.50.00. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vya ndani, kuongeza ajira pamoja na mapato ya Serikali;
Kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 10 au dola za Marekani 300 kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton) kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa badala ya asilimia 10 kwa mwaka mmoja kwenye bidhaa za mabati zinazotambulika kwa HS code 7212.60.00. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vya ndani, kuongeza ajira pamoja na mapato ya Serikali;
Kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 25 au dola za Marekani 300 kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton) kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa badala ya kiwango cha asilimia 10 kwenye bidhaa za chuma zinazotambulika kwa HS Codes 7225.91.00; 7225.92.00; na 7225.99.00 kwa mwaka mmoja. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vinavyozalisha nondo hapa nchini, kuongeza ajira pamoja na mapato ya Serikali;
Kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 35 au dola za Marekani 500 kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton) kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa badala ya kiwango cha asilimia 35 kwenye mabati yanayotambulika kwa HS Codes 7210.41.00 kwa mwaka mmoja. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vinavyozalisha mabati hayo ndani ya nchi, kuongeza ajira pamoja na mapato ya Serikali;
Kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 50 badala ya kiwango cha asilimia 35 au asilimia 25 kwenye chumvi inayotambulika kwa Heading 25.01 kwa mwaka mmoja. Lengo la hatua hii ni kulinda wazalishaji wa chumvi nchini;
Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 au dola za Marekani 300 kwa kila tani moja (Metric ton) kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa kwenye bidhaa za chuma zinazotambulika kwa HS Code 7226.99.00 kwa mwaka mmoja badala ya ushuru wa asilimia 10 pekee. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vya ndani, kuongeza ajira, kuvutia uwekezaji, kuongeza mapato ya Serikali pamoja na kudhibiti udanganyifu wa thamani halisi ya bidhaa hizo kutoka nje;
Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 au dola za Marekani 500 kwa kila tani moja ya ujazo (Metric ton) kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa badala ya asilimia 35 kwa mwaka mmoja kwenye mafuta ya kula yaliyochakatwa kwa kiwango cha mwisho (refined edible oils) yanayotambulika kwa HS codes 1507.90.00; 1508.90.00; 15.09; 15.10; 1511.90.30; 1511.90.90; 1512.19.00; 1512.29.00; 1513.19.00; 1513.29.00; 1514.19.00; 1514.99.00; 1515.19.00; 1515.29.00; 1515.50.00; 1515.60.00 na 1515.90.00. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vya ndani na kuhamasisha uchakataji wa mbegu na mafuta ghafi yaliyoingizwa nchini ili kuongeza thamani ya bidhaa (value addition), kukuza ajira, pamoja na kuongeza mapato ya Serikali; na
Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimekubaliana kufanya marekebisho kwenye muundo wa tariff lines za magari yanayotumia nishati ya umeme na mafuta (hybrid) zinazotambulika kwenye HS Codes 8703.40.00; 8703.50.00; 8703.60.00; na 8703.70.00 ili magari yanayoingizwa nchini yakiwa hayajaunganishwa (unassembled) yatozwe ushuru wa forodha kwa kiwango cha asilimia 0. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa waunganishaji wa magari hayo nchini na kuhamasisha uwekezaji.
Mapendekezo ya kuendelea na utekelezaji wa Viwango vya Ushuru wa Forodha vya mwaka 2023/24 ni kama ifuatavyo:
Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 10 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye mashine za kielektroniki zinazotumika kukusanya mapato ya Serikali (Cash registers, Electronic Fiscal Device (EFD) Machines and Point of Sale (POS) machines) zinazotambulika kwa HS Codes 8470.50.00 na 8470.90.00. Lengo la hatua hii ni kuhamasisha matumizi ya vifaa hivi katika kuhasibu mapato ya Serikali;
Kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kwa kiwango cha asilimia 0 badala ya asilimia 10 kwa mwaka mmoja kwenye vifuniko vya chupa za mvinyo (corks and stoppers) vinavyotambulika kwa HS Code 4503.10.00. Hatua hii inalenga kuwapunguzia gharama wazalishaji wa mvinyo ili kuhamasisha na kuendeleza kilimo cha zao la zabibu nchini pamoja na kuongeza ajira;
Kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 10 badala ya asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye unga wa kakao unaoingizwa kutoka nje unaotambulika kwa HS Code 1805.00.00. Lengo la hatua hii ni kuhamasisha kilimo cha zao la kakao nchini pamoja na kuongeza mapato ya Serikali;
Kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kwa kiwango cha asilimia 0 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye vifungashio vya kuhifadhia kahawa vinavyotambulika kwa HS codes 7310.21.00; 6305.10.00; 3923.50.10; 3923.50.90 na 3920.30.90 vinavyotumiwa na viwanda vya kusaga kahawa nchini. Hatua hii inalenga kuongeza thamani kwenye zao la kahawa na kutoa unafuu wa gharama kwenye viwanda vinavyosaga kahawa hapa nchini;
Kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kwa kiwango cha asilimia 0 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye vifungashio vya kuhifadhia korosho vinavyotambulika kwa HS code 3923.21.00. Hatua hii inalenga kuongeza thamani katika zao la korosho na kupunguza gharama kwenye viwanda vinavyochakata korosho hapa nchini;
Kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kwa kiwango cha asilimia 0 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye vifungashio vya kuhifadhia pamba (cotton lint) vinavyotambulika kwa HS codes 3920.30.90; 6305.39.00 na 7217.90.00. Hatua hii inalenga kuvutia uwekezaji ili kuongeza thamani ya zao la pamba nchini;
Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimekubaliana kuendelea kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kwa kiwango cha asilimia 0 badala ya asilimia 10 au asilimia 25 kwenye malighafi mbalimbali za kutengeneza taulo za kike pamoja na taulo za watoto. Hatua hii inalenga kutoa unafuu wa gharama za uzalishaji na kuongeza ajira;
Kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kwa kiwango cha asilimia 0 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye vifungashio vya mbegu vinavyotambulika kwa HS codes 3923.29.00; 6305.10.00; 4819.40.00; 7310.29.90; 6305.33.00; 6305.20.00; 6304.91.90 na 7607.19.90. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa wazalishaji wa mbegu hapa nchini;
Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 au dola za Marekani 125 kwa kila tani moja ya ujazo (Metric ton) kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa badala ya ushuru wa asilimia 10 pekee kwenye bidhaa za chuma kwa mwaka mmoja. Bidhaa hizi zinatambulika kwa HS Codes 7209.16.00; 7209.17.00; 7209.18.00; 7209.25.00 7209.26.00; 7209.27.00; 7209.28.00; 7209.90.00; 7211.23.00; 7211.90.00; 7225.50.0 na 7226.92.00. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vya ndani vinavyozalisha bidhaa hizo pamoja na kukuza ajira;
Kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 25 au dola za Marekani 250 badala ya kiwango cha asilimia 25 au dola za Marekani 200 kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton) kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa kwenye bidhaa za chuma zinazotambulika kwa HS Codes 7213.10.00; 7213.20.00; 7213.99.00; 7306.30.00; 7306.50.00; 7306.61.00; 7306.69.00; na 7306.90.00 kwa mwaka mmoja. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vinavyozalisha nondo hapa nchini, kuhamasisha uwekezaji, kuongeza ajira pamoja na mapato ya Serikali;
Kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 10 badala ya asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye fito za plastiki zijulikanazo kama PVC Profiles zinazotambulika kwa HS Codes 3916.10.00; 3916.20.00; na 3916.90.00 zinazotumika kutengenezea fremu za milango, madirisha. Lengo la hatua hii ni kuongeza mapato ya Serikali;
Kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 25 badala ya asilimia 10 kwa mwaka mmoja kwenye karatasi zinazotambulika kwa HS code 4804.29.00. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vinavyozalisha karatasi hizo hapa nchini;
Kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kwa kiwango cha asilimia 10 badala ya asilimia 35 kwa mwaka mmoja kwenye ngano inayotambulika kwa HS Codes 1001.99.10 na 1001.99.90. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama kwa Viwanda vinavyozalisha unga wa ngano;
Kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kwa kiwango cha asilimia 0 badala ya asilimia 10 kwa mwaka mmoja kwenye malighafi ya kutengeneza sabuni ijulikanayo kama RBD Palm Stearin zinazotambulika kwa HS Code 1511.90.40 kwa viwanda vinavyotengeneza sabuni nchini. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa viwanda vya kuzalisha sabuni nchini;
Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au dola za Marekani 1.35 kwa kila kilo moja ya viberiti (safety match boxes) vinavyotambuliwa kwenye HS code 3605.00.00 kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa badala ya asilimia 25 pekee kwa mwaka mmoja. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vinavyozalisha viberiti nchini dhidi ya bidhaa zenye ruzuku kutoka nje na hivyo kuwa na ushindani sawa katika soko;
Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 60 badala ya asilimia 35 kwa mwaka mmoja kwenye maji ya kunywa (mineral water) yanayotambulika kwa HS code 2201.10.00. Hatua hii inalenga kulinda viwanda vinavozalisha maji ya kunywa nchini;
Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 badala ya asilimia 0 kwenye Gypsum Powder inayotambulika kwa HS code 2520.20.00 kwa mwaka mmoja. Lengo la hatua hii ni kulinda wazalishaji wa Gypsum Powder nchini;
Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 35 au dola za Marekani 0.40 kwa kilo moja kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa kwa mwaka mmoja kwenye mitumba inayotambulika kwa HS Codes 6309.00.10; 6309.00.20; na 6309.00.90 inayoingia kutoka nje. Hatua hii inalenga kutoa unafuu kwa watumiaji wa bidhaa hii hapa nchini;
Kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwenye malighafi, vipuri na mashine vinavyotumika katika kutengeneza viatu vya ngozi na nguo. Lengo la hatua hii ni kuhamasisha ukuaji wa sekta ya nguo na viatu vya ngozi nchini;
Kutoza ushuru wa Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 25 badala ya asilimia 10 kwa mwaka mmoja kwenye matairi mapya ya pikipiki (new pneumatic tyres of rubber) yanayotambulika kwa HS Code 4011.40.00. Lengo la hatua ni kuhamasisha uzalishaji wa matairi hayo nchini kwa kuwa kuna malighafi za kutosha;
Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye mikebe ya kubebea maziwa (milk cans) inayotambulika kwa HS Codes 7310.10.00 na 7310.29.90. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu wa vifungashio vya kuhifadhia maziwa ili kuwalinda walaji nchini;
Kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kwa kiwango cha asilimia 0 badala ya asilimia 10 au asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye malighafi za kutengeneza sabuni (Organic surface-active agents) zinazotambulika kwa HS Codes 3402.31.00; 3402.39.00; 3402.49.00. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa wazalishaji wa sabuni za unga na maji nchini;
Kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kwa kiwango cha asilimia 0 badala ya asilimia 25 au asilimia 10 kwa mwaka mmoja kwenye malighafi za kuchakata ngozi zinazotambulika kwa HS Codes 3208.20.10; 3208.20.20; 3208.90.20 na 3210.00.10. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa wachakataji wa ngozi nchini;
Kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kwa kiwango asilimia 0 badala ya asilimia 25 au asilimia 10 mwaka mmoja kwenye malighafi za kutengeneza mbolea zinazotambulika kwa HS Codes 2710.99.00, 2528.00.00 na 3505.20.00. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa wazalishaji wa mbolea nchini;
Kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kwa kiwango asilimia 0 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye vifungashio vya tumbaku iliyochakatwa vinavyotambulika kwa HS Code 5310.10.00. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa wachakataji wa tumbaku nchini;
Kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kwa kiwango asilimia 0 badala asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye vifungashio vya chai iliyochakatwa vinavyotambulika kwa HS Codes 4819.20.90, 5407.44.00 na 3923.29.00. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa wachakataji wa chai (tea blenders) nchini;
Kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kwa kiwango asilimia 10 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwa waunganishaji wa pikipiki za matairi matatu bila kujumuisha fremu ili ziweze kutengenezwa na kuunganishwa hapa nchini (CKD for three-wheel motorcycles excluding chassis and its components) zinazotambulika kwa HS Code 8704.21.90. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa waunganishaji wa pikipiki hizo nchini ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo;
Kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kwa kiwango asilimia 0 badala ya asilimia 25 au asilimia 10 kwa mwaka mmoja kwenye malighafi za kutengeneza mabomba ya plastiki (glass reinforced plastic pipes) zinazotambulika kwa HS Codes 3920.61.10, 7019.39.00, 7019.31.00, 6006.90.00, 7019.12.00, 3920.10.10, 4016.93.00, na 3907.91.00. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa watengenezaji wa mabomba hayo nchini ili kupunguza gharama za uzalishaji na kuwezesha ujenzi wa miundombinu ya maji;
Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimekubaliana kuendelea kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kwa kiwango cha asilimia 10 badala ya asilimia 100 au dola za Marekani 460 kwa kila tani moja ya ujazo (metric tone) kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa kwenye sukari ya matumizi ya viwandani (sugar for industrial use) inayotambulika kwa HS Codes 1701.99.10 na 1701.99.20. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwenye viwanda vinavyotumia bidhaa hii kama malighafi;
Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 au dola za Marekani 125 kwa kila tani moja (Metric ton) kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa kwenye mabati yanayotambulika kwa HS Code 7212.20.00 kwa mwaka mmoja badala ya ushuru wa asilimia 10 pekee. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vya ndani, kuongeza ajira pamoja na mapato ya Serikali;
Kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye taulo za watoto (Baby Diapers) zinazotumbulika kwa HS code 9619.00.90. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vinavyozalisha bidhaa hii nchini, kuongeza ajira pamoja na mapato ya Serikali;
Kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 25 badala ya asilimia 10 kwa mwaka mmoja kwenye nyuzi za pamba (cotton yarn) zinazotambulika kwa Headings 52.05, 52.06 na 52.07 isipokuwa nyuzi za pamba zinazotambulika kwa HS Code 5205.23.00. Lengo la hatua ni kulinda viwanda vinavyozalisha bidhaa hiyo na kuongeza thamani ya zao la pamba (value addition) nchini;
Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye bidhaa za mbogamboga na matunda zinazotambulika kwa HS code 0604.20.00; 0604.90.00; 0808.10.00; 0808.30.00 kwa mwaka mmoja. Hatua hii inalenga kilinda wazalishaji wa bidhaa za mbogamboga na matunda hapa nchini;
Kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kwa kiwango cha asilimia 0 badala ya asilimia 10 kwa mwaka mmoja kwenye malighafi za kutengeneza viongeza ladha kwenye vyakula na vinywaji (food flavors) zinazotambulika kwa HS Code 1901.90.10; 3302.10.00; na 3505.10.00. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa watengenezaji wa vyakula na vinywaji nchini;
Kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kutoka asilimia 25 au asilimia 10 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye karatasi zinazotambulika kwa HS Codes 4804.39.00; 4805.11.00; 4805.19.00; 4805.24.00; 4805.25.00; zinazotumika kama malighafi ya kutengeneza vifungashio aina ya maboksi (corrugated boxes). Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa wazalishaji wa vifungashio hivyo hapa nchini ili wananchi waweze kuvipata kwa urahisi na kwa bei nafuu;
Kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kutoka asilimia 35 hadi asilimia 10 kwa mwaka mmoja kwenye malighafi za kutengeneza sabuni (toilet soap) zinazotambulika kwa HS Code 3401.20.10. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa wazalishaji wa sabuni nchini, kuhamasisha uwekezaji, kuongeza ajira pamoja na mapato ya Serikali;
Kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kwa kiwango cha asilimia 0 badala ya asilimia 25 au asilimia 10 kwa mwaka mmoja kwenye malighafi za kutengeneza nyaya za umeme (electrical cables) zinazotambulika kwa HS Codes 7312.10.00; 7217.20.00; 7408.19.00; 7409.11.00; 7605.21.00; 2710.19.56; 3815.90.00; 5402.19.00; 5903.90.00; 7907.00.00; na 2712.10.00. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa watengenezaji wa nyaya hizo pamoja na kuvutia uwekezaji nchini;
Kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 25 badala ya asilimia 10 kwenye kamba zinazotengenezwa kwa nyuzi zenye asili ya plastiki (Twine of other synthetic fibers) zinazotambulika kwa HS Code 5607.50.00 kwa mwaka mmoja. Lengo ni kulinda viwanda vinavyozalisha bidhaa mbadala hapa nchini pamoja na kuongeza ajira;
Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye kadi janja (smart cards) zinazotambulika kwa HS Code 8523.52.00 zitakazoingizwa nchini na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA). Hatua hii inalenga kupunguza gharama za uingizaji wa kadi hizo ili kurahisisha upatikanaji wa vitambulisho vya Taifa kwa wananchi;
Kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 25 au dola za Marekani 250 kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton) kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa badala ya ushuru wa asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye mabati yanayotambulika kwa HS code 7210.30.00. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vya ndani, kuongeza ajira pamoja na mapato ya Serikali;
Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka kiwango cha asilimia 50 hadi asilimia 35 kwa mwaka mmoja kwenye vitenge vinavyotambulika kwa HS Codes 5208.51.10; 5208.52.10; 5209.51.10; 5210.51.10; 5211.51.10; 5212.15.10; 5212.25.10; 5513.41.10; na 5514.41.10. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwenye uagizaji wa vitenge ili kulinda walaji;
Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au dola za Marekani 0.25 kwa kila mita moja kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa badala ya asilimia 25 pekee kwa mwaka mmoja kwenye vitambaa vya pamba (cotton grey fabric) vinavyotambulika kwa HS Codes 5208.11.00; 5208.12.00; 5208.13.00; 5208.19.00; 5209.11.00; 5209.12.00; 5209.19.00; 5210.11.00; 5210.19.00; 5211.11.00; 5211.12.00; 5211.19.00; 5212.11.00; na 5212.21.00. Lengo la hatua hii ni kuchochea uzalishaji wa vitambaa hivyo kwa kutumia pamba inayozalishwa hapa nchini, kuongeza ajira pamoja na mapato ya Serikali;
Kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 25 badala ya asilimia 10 kwenye karatasi za kutolea risiti za kielektroniki zinazotambulika kwa HS Code 4811.90.00 kwa mwaka mmoja. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vya ndani vinavyozalisha bidhaa hii;
Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye mabasi ya abiria yanayotambulika kwa HS Codes 8702.10.99 na 8702.20.99 yanayoingizwa nchini kwa ajili ya mradi wa mabasi yaendayo haraka. Hatua hii inalenga kupunguza gharama za uingizaji wa mabasi hayo ili kurahisisha huduma ya usafiri kwa wananchi;
Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 au dola za Marekani 350 kwa kila tani moja ya ujazo (Metric ton) kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa badala ya asilimia 35 pekee kwa mwaka mmoja kwenye misumari zinazotambulika kwa HS code 7317.00.00. Hatua hii inalenga kulinda viwanda vinavyozalisha bidhaa hizo nchini, kuhamasisha uwekezaji wa bidhaa za chuma, kuongeza ajira pamoja na mapato ya Serikali;
Kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 35 badala ya kiwango cha asilimia 100 au dola za Marekani 460 kwa kila tani moja ya ujazo kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa kwa mwaka mmoja kwenye sukari ya matumizi ya kawaida (consumption sugar) inayotambulika kwa HS Code 1701.14.90 inayoagizwa kutoka nje ya nchi kwa vibali maalum kwa lengo la kuziba pengo (gap) la uzalishaji hapa nchini;
Kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kutoka asilimia 35, asilimia 25 au asilimia 10 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye malighafi za kuzalisha bidhaa mtaji (capital goods) zinazotumika viwandani zinazotambulika kwa headings 72.14; 72.15; 72.16; 32.08; 73.07; 83.11; 85.44; 68.06; 74.19; 72.08; 73.06; 73.12; 73.15; 73.18; 84.82; 84.83; 72.22; 73.04; 84.81; 84.84; 73.25; 40.10; na 76.06. Hatua hii inalenga kutoa unafuu kwa wazalishaji wa bidhaa mtaji hapa nchini ili bidhaa hizo ziweze kupatikana kwa unafuu kwa viwanda vya ndani pamoja na kuchochea uwekezaji wa kuzalisha bidhaa hizo hapa nchini;
Kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kwa kiwango cha asilimia 0 badala ya asilimia 35, asilimia 25 au asilimia 10 kwa mwaka mmoja kwenye malighafi za kutengeneza rejeta (radiators) za vyombo vya moto zinazotambulika kwa HS Codes 7409.11.00; 7409.19.00; 7410.11.00; 7410.12.00; 7409.21.00; 8001.10.00; 3810.90.00. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu pamoja na kuchochea uwekezaji katika uzalishaji wa rejeta hapa nchini;
Kutoa unafuu wa Ushuru wa Forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kwa kiwango cha asilimia 0 badala ya asilimia 10 au asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye malighafi za kutengeneza wiring harnesses za vyombo vya moto zinazotambulika kwa HS Codes 8538.90.00; 4016.99.00; 8205.59.00; 8536.10.00; 8536.69.00; 8536.90.00; 8547.20.00; 3926.90.90; 3917.32.00; na 8544.30.00. Hatua hii inalenga kutoa unafuu kwa wazalishaji pamoja na kuchochea uwekezaji katika uzalishaji wa wiring harnesses nchini; na
Kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 10 kwa mwaka mmoja badala ya asilimia 0 kwenye mafuta ghafi ya soya, karanga, nazi, mnyonyo, haradali n.k yanayotambulika kwa HS codes 1507.10.00; 1508.10.00; 1513.11.00; 1513.21.00; 1514.11.00; 1514.91.00; na 1515.11.00. Lengo la hatua hii ni kuoanisha viwango vya mafuta ghafi haya vifanane na viwango vya mafuta ghafi ya alizeti, pamba, mahindi na mafuta ghafi mengineyo ambayo viwango vyake ni asilimia 10. Aidha, hatua hii pia inalenga kulinda na kuhamasisha uzalishaji wa mbegu za mafuta ya kula nchini, kuongeza ajira pamoja na kulinda fedha za kigeni zinazotumika kuagiza mafuta hayo nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, Napendekeza kuanzisha utaratibu wa Serikali kusaini Mikataba ya Utekelezaji (Performance Agreement) na viwanda vinavyolindwa na Serikali kwa kupewa unafuu wa kodi ikiwemo Ushuru wa Forodha kupitia utaratibu wa Duty Remission, Kodi ya Ongezeko la Thamani kupitia utoaji wa msamaha au utozaji wa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa kiwango cha asilimia sifuri (Exemption au Zero Rated) pamoja na viwanda vitakavyolindwa na Serikali kutokana na sera za kuongeza kodi kwenye bidhaa zinazotoka nje ya nchi. Hatua hii inalenga kuhakikisha malengo ya utoaji wa unafuu wa kodi husika yanafikiwa na hatimaye kuleta manufaa tarajiwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
Hatua hizi kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 205,727.
Sheria ya Kudhibiti Uingizwaji wa Bidhaa Nchini, SURA 276
Mheshimiwa Spika, Napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kudhibiti Uingizwaji wa Bidhaa Nchini, Sura 276 kwa kuanzisha Tozo ya Maendeleo ya Viwanda (industrial Development Levy) kwa baadhi ya bidhaa zinazoingizwa nchini kama ifuatavyo: kiwango cha asilimia 10 kwenye wire rods zinazotambulika kwa HS Code 7213.91.10 na 7213.91.90; asilimia 10 kwenye bia zinazotambulika kwa heading 22.03 pamoja na mvinyo (wine); asilimia 5 kwenye bia zisizo na kilevi (non-alcoholic beer) zinazotambulika kwa HS Code 2202.91.00; asilimia 5 kwenye vinywaji vya kuongeza nguvu (energy drinks) vinavyotambulika kwa HS Code 2202.99.00; asilimia 10 kwenye sabuni za unga (detergents) zinazotambulika kwa HS Code 3402.50.00 na sabuni za maji zinazotambulika kwa HS Code 3402.90.00. Tozo hii haitatozwa kwenye bidhaa zinazozalishwa katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Partners States) ambazo zinakidhi vigezo vya uasilia (Rules of Origins). Aidha, Serikali itaendelea kufanya tathmini na tafiti kwenye bidhaa nyingine zinazozalishwa kwa wingi nchini kwa lengo la kuzijumuisha katika wigo wa utozaji. Lengo la hatua hii ni kuvutia uwekezaji nchini, kuchochea mauzo nje ya nchi na kulinda uzalishaji wa ndani kwa kuwa bidhaa husika zinazalishwa kwa wingi nchini. Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 11,147.
Sheria ya Usafirishaji Bidhaa Nje ya Nchi, SURA 196
Mheshimiwa Spika, Napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Usafirishaji wa Bidhaa Nje ya Nchi, Sura 196 kama ifuatavyo:
Kutoza ushuru kwa kiwango cha asilimia 10 kwenye mafuta ghafi ya kula ya alizeti (Crude Sunflower Oil), mashudu yanayotokana na mbegu za alizeti (Sunflower Cake) pamoja na mbegu za alizeti (Sunflower Seeds) zinazosafirishwa kwenda nje ya nchi. Lengo la hatua hii ni kuwezesha upatikanaji wa bidhaa za mafuta kwa bei nafuu nchini pamoja na kulinda wazalishaji wa ndani kwa kuhakikisha wanapata mbegu za alizeti za kutosha ambazo zinatumika kama malighafi katika viwanda hivyo. Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 2,048;
Hatua hizi kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 2,048
Maboresho ya Ada na Tozo mbalimbali za Taasisi za Serikali pamoja na Utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Kufanya Biashara (Blueprint).
Mheshimiwa Spika, Napendekeza kufanya maboresho ya sheria na kanuni mbalimbali, kufuta au kupunguza ada na tozo mbalimbali zinazotozwa na Wizara, Idara na Taasisi zinazojitegemea ili kuleta usimamizi bora wa sekta mbalimbali na kuboresha mazingira ya biashara nchini. Hatua hizi pia ni moja ya sehemu ya mwendelezo wa utekelezaji wa Mpango wa kuboresha Mfumo wa udhibiti wa Biashara (Blueprint for Regulatory Reforms to Improve the Business Environment). Marekebisho hayo ni kama ifuatavyo:
Tume ya nguvu za mionzi Tanzania
Kufanya marekebisho kwenye ada ya Utambuzi wa Mionzi kama ifuatavyo:
Kuweka takwa la kutoza kiwango cha asilimia 0.1 ya malipwani kwenye bidhaa za mifugo na chakula inayosafirishwa kwenda nje ya nchi pale ambapo nchi hizo zina sharti la uhitaji wa cheti cha utambuzi wa mionzi au msafirishaji ameomba cheti hicho. Pendekezo hili linaondoa takwa la ulazima wa msafirishaji kulipia tozo hiyo hata pale ambapo cheti cha utambuzi wa mionzi hakihitajiki na nchi zinapopelekwa bidhaa hizo; na
Kupunguza ada ya mionzi kutoka asilimia 0.4 ya Malipwani hadi asilimia 0.2 ya malipwani kwa bidhaa za mwisho zinazoingizwa nchini. Lengo la hatua hizi ni kupunguza tozo kero na gharama za biashara na hivyo kuchochea uzalishaji na kukuza uwekezaji nchini sambamba na kupunguza uingizaji wa bidhaa hizo nchini kwa njia ya magendo. Hatua hii inatarajia kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 42.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji
Kufanya marekebisho ya Sheria ya Jeshi ya Zimamoto na Uokoaji, SURA 427 kwa kupunguza tozo ya mafunzo ya kinga na tahadhari za moto kwa wasimamizi (wardens) kutoka Shilingi 500,000 hadi Shilingi 200,000. Marekebisho haya yanaenda sambamba na kuweka sharti la mafunzo hayo kufanyika kwa msimamizi mmoja na kuendelea kwa kila mwaka badala ya utaratibu wa sasa wa wasimamizi zaidi ya wawili. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za ufanyaji biashara na uwekezaji nchini.
Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania
Kutoza ada ya kuhuisha leseni za uendeshaji wa ndege za kiusalama (Air Operators Certificates - AOC) kwa kiwango cha dola za Marekani 600 kwa Kampuni kwa mwaka badala ya kiwango kinachotozwa sasa cha dola za Marekani 600 kwa kila ndege kwa mwaka. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za ufanyaji wa biashara katika sekta hiyo na kuchochea ukuaji wa Sekta ya Anga.
Wizara ya Maliasili na Utalii
Kufanya marekebisho kwenye Kanuni ya Ada na Tozo za Utalii ya mwaka 2015 kama ifuatavyo:
Kutoza ada ya Leseni za Biashara za Utalii Tanzania kwa Shilingi ya Tanzania badala ya dola za Marekani. Mapendekezo haya yanaenda sambamba na kuweka takwa la ada hizo kulipwa katika kipindi cha miezi 12 kuanzia siku ya malipo ya mwisho ya leseni ya biashara yalipofanyika; na
Kupunguza ada ya Leseni ya Biashara za Utalii Tanzania inayolipwa na wakala wa wapandisha watalii mlimani (mountain climbing) kutoka dola za Marekani 2,000 kwa mwaka hadi shilingi milioni 3 kwa mwaka. Aidha, ada hiyo italipwa kwa thamani ya shilingi ya Tanzania.
Lengo la hatua hizi ni kurahisisha mfumo wa ulipaji wa ada za utalii, kupunguza gharama za uendeshaji, kuvutia uwekezaji katika tasnia ya utalii na kuendana na matakwa ya Kifungu cha 26 cha Sheria ya Benki kuu ya Tanzania kinachoelekeza malipo yanayofanywa nchini kutumia shilingi ya Tanzania.
Wizara ya Mifugo na Uvuvi
Sekta ya Mifugo
Kufanya marekebisho kwenye ada ya kibali cha kusafirisha mifugo katika minada kutoka shilingi 30,000 hadi shilingi 31,000 kwa kila ng’ombe; na shilingi 6,500 hadi shilingi 7,000 kwa kila mbuzi na kondoo. Ongezeko hilo ada litapelekwa Halmashauri kwa lengo la kuongeza usimamizi katika minada husika.
Sekta ya Uvuvi
Kufanya marekebisho ya tozo mbalimbali kwenye Sekta ya Uvuvi kama ifuatavyo:
Kupunguza ada ya kibali cha kusafirisha samaki na mazao ya uvuvi (dagaa, furu) samaki wakavu,wabichi na waliogandishwa kutoka Shilingi 100 kwa kila kilo moja hadi shilingi 50 kwa kila kilo moja. Aidha, Samaki na mazao ya uvuvi yaliyokaushwa yenye uzito chini ya kilo 20 pamoja na yale mabichi au yaliyogandishwa yenye uzito chini ya kilo 30 hayatatozwa ada hiyo;
Kupunguza ada ya kibali cha kusafirisha mazao ya mabondo kutoka shilingi 2,500 hadi shilingi 2,000 kwa kilo ya Mabondo mabichi na kutoka shilingi 3,500 hadi shilingi 2,800 kwa kilo ya Mabondo makavu; na
Kuongeza ushuru wa kusafirisha mabondo nje ya nchi (export royalty) kutoka Dola za Marekani 2.7 hadi Dola za Marekani 3.0 kwa kilo kwa mabondo mabichi na Dola za Marekani 3.3 hadi Dola za Marekani 3.5 kwa kilo kwa mabondo makavu.
Hatua hizi kwa pamoja zinatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 554.
Mheshimiwa Spika, pamoja na maboresho ya sheria mbalimbali yaliyofanywa na Serikali ili kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara kwa kupunguza mwingiliano wa majukumu baina ya taasisi mbalimbali za udhibiti nchini na kufuta/kupunguza ada na tozo kero, bado kumekuwa na changamoto ya taasisi nyingi za udhibiti zinazosimamia sekta mbalimbali kuongeza kero za ufanyaji biashara na uwekezaji kutokana na ada, tozo na adhabu mbalimbali wanazotoza pamoja na kaguzi nyingi na zisizokuwa na tija. Ili kuondoa kero hizo, Serikali ipo katika hatua za kuanzisha mfumo wa pamoja wa ukusanyaji wa ada, tozo na adhabu za taasisi za udhibiti (Single Window Payment System) na kuweka utaratibu kwa taasisi hizo kufanya kaguzi kwa namna ambayo haitaleta usumbufu na bila kuathiri majukumu ya msingi yanayofanywa na taasisi husika.
Marekebisho madogo madogo katika baadhi ya Sheria za Kodi, Sheria nyingine na Kanuni mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho mengine madogo madogo yasiyo ya kisera katika sheria mbalimbali za kodi, sheria nyingine pamoja na Kanuni za Sheria mbalimbali ili ziwe sanjari na azma ya kurahisisha utekelezaji wake. Marekebisho hayo yataainishwa katika Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2024 na Matangazo ya Serikali (Government Notices).
Tarehe ya Kuanza Kutekeleza Hatua Mpya za Kodi.
Mheshimiwa Spika, hatua hizi za kikodi zinazopendekezwa zitaanza kutekelezwa tarehe 1 Julai, 2024, isipokuwa pale itakapoelezwa vinginevyo.
SURA YA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2024/25
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2024/25, Serikali inatarajia kukusanya na kutumia jumla ya shilingi trilioni 49.35, sawa na ongezeko la asilimia 11.2 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2023/24. Ongezeko la bajeti kwa kiasi kikubwa limetokana na kugharamia: deni la Serikali ambalo limeongezeka kutokana na kushuka kwa thamani ya shilingi, kuongezeka kwa viwango vya riba na kuiva kwa mikopo ya zamani; ajira mpya; ulipaji wa hati za madai; Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2024; maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025; na maandalizi ya michuano ya mpira wa miguu ya mataifa ya Afrika (AFCON) ya mwaka 2027 ikiwemo ujenzi na ukarabati wa viwanja.
Mapato
Mheshimiwa Spika, mapato ya ndani yanakadiriwa kuwa jumla ya shilingi trilioni 34.61, sawa na asilimia 70.1 ya bajeti yote na asilimia 15.7 ya Pato la Taifa. Kati ya mapato hayo, mapato yatakayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania yanakadiriwa kuwa shilingi trilioni 29.41, mapato yasiyo ya kodi yatakayokusanywa na Wizara, Taasisi na Idara zinazojitegemea shilingi trilioni 3.84 na mapato yatakayokusanywa na Mamlaka za Serikali za Mitaa shilingi trilioni 1.36. Mikakati ya kufikia malengo haya ya mapato ni kama nilivyoeleza hapo awali.
Mheshimiwa Spika, misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo inakadiriwa kuwa shilingi trilioni 5.13. Naomba nizitambue nchi wahisani zilizoahidi kuchangia bajeti ya mwaka 2024/25 ambazo ni pamoja na: Australia, Austria, Canada, China, Denmark, Finland, India, Ireland, Italia, Japan, Korea ya Kusini, Marekani, Norway, Poland, Sweden, Ubelgiji, Ufaransa, Uhispania, Uholanzi, Uingereza, Ujerumani na Uswisi. Aidha, taasisi na Mashirika ya Kimataifa yaliyoahidi kuchangia ni pamoja na: Benki ya Dunia; Shirika la Fedha la Kimataifa; Benki ya Maendeleo ya Afrika; Benki ya Kiarabu kwa Maendeleo ya Kiuchumi katika Afrika; Benki ya Uwekezaji ya Ulaya; Mfuko wa Abu Dhabi; Mfuko wa Kuwait; Mfuko wa Kimataifa wa Kusaidia Mapambano Dhidi ya Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria; Mfuko wa OPEC kwa Maendeleo ya Kimataifa; Mfuko wa Mazingira Duniani; Adaptation Fund; Mfuko wa GRMF; Umoja wa Mataifa na mashirika yote yaliyopo chini yake; Umoja wa Ulaya; na Shirikisho la GAVI.
Mheshimiwa Spika, kwa dhati kabisa, napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru washirika wetu wa maendeleo kwa misaada na mikopo nafuu wanayoendelea kutupatia katika kutekeleza miradi na programu mbalimbali za maendeleo nchini. Ni matarajio yetu kuwa rasilimali zilizoahidiwa na marafiki zetu hawa zitatolewa kwa wakati na kwa kiasi kilichoahidiwa. Nasi, kwa upande wa Serikali tunaahidi kusimamia ipasavyo matumizi ya fedha hizo kama ilivyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika, Serikali inakadiria kukopa shilingi trilioni 6.62 kutoka soko la ndani ambapo shilingi trilioni 4.02 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva na shilingi trilioni 2.60 kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Aidha, Serikali inakadiria kukopa shilingi trilioni 2.99 kutoka soko la nje kwa masharti ya kibiashara kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa spika, katika kuhakikisha soko la mitaji la ndani linaendelea kuwa chanzo muhimu cha fedha, Serikali itaendelea kutoa hati fungani kizio (benchmark bonds) kwa lengo la kujenga viwango vya bei rejea na shindani katika soko la fedha na mitaji nchini. Aidha, Serikali itaendelea kufungua wigo kwa wawekezaji kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika.
Matumizi
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2024/25, Serikali imepanga kutumia jumla ya shilingi trilioni 49.35. Kiasi hicho kinajumuisha: shilingi trilioni 15.74 kwa ajili ya ulipaji wa deni la Serikali na gharama nyingine za Mfuko Mkuu; shilingi trilioni 11.77 kwa ajili ya mishahara ikiwemo ajira mpya pamoja na upandishaji wa madaraja kwa watumishi; shilingi trilioni 2.17 kwa ajili ya mifuko ya reli, barabara, maji, REA na TARURA; na ruzuku ya maendeleo ya shilingi trilioni 1.19 kwa ajili ya kugharamia mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu na vyuo vya kati pamoja na Programu ya Elimumsingi na Sekondari bila Ada.
Mheshimiwa Spika, sura ya bajeti kwa mwaka 2024/25 ni kama inavyoonekana katika Jedwali Na. 1.
Jedwali Na. 1: Sura ya Bajeti ya Mwaka 2024/25
Chanzo: Wizara ya Fedha
Vihatarishi vya Utekelezaji wa Bajeti
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/25 unaweza kuathiriwa na vihatarishi mbalimbali vinavyohusisha mabadiliko ya sera za uchumi, fedha, bajeti, siasa na mahusiano ya kidiplomasia. Aidha, utekelezaji wa bajeti unaweza kuathiriwa na masuala mtambuka hususan mabadiliko ya tabianchi, majanga ya asili, magonjwa ya mlipuko na athari za vita baina ya mataifa. Vihatarishi katika bajeti ya mwaka 2024/25 ni pamoja na: kudorora kwa uchumi wa dunia; mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma; mabadiliko ya riba katika masoko ya fedha ndani na nje ya nchi; mabadiliko ya viwango vya kubadilisha fedha; madeni sanjari; siasa na mahusiano ya kidiplomasia; na mabadiliko ya tabianchi, majanga ya asili na magonjwa ya mlipuko.
Mheshimiwa Spika, endapo vihatarishi hivyo vitatokea, athari zinazoweza kujitokeza ni pamoja na: kutokufikiwa kwa lengo la ukusanyaji wa mapato; kasi ndogo ya utekelezaji wa miradi; kuongezeka kwa gharama za bidhaa, malighafi, huduma na utekelezaji wa miradi; kuongezeka kwa gharama za kuhudumia deni la Serikali; na kuongezeka kwa gharama za mikopo ya kibiashara katika masoko ya fedha. Athari nyingine ni: kupungua kwa misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo; kuongezeka kwa nakisi ya bajeti; kupungua kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo; uharibifu wa miundombinu; na kuongezeka kwa madai na madeni ya wazabuni na watoa huduma.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na vihatarishi vinavyoweza kujitokeza ili kufikia malengo na shabaha za utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2024/25. Hatua hizo ni pamoja na: kuendelea kusimamia sera ya fedha na bajeti; kuimarisha mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji mapato; kuboresha mazingira ya uwekezaji wa ndani na nje; kuendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Mikopo, Misaada na Dhamana, Sura 134; kuimarisha hifadhi ya chakula ya Taifa; kusimamia utekelezaji wa Mwongozo wa Taifa wa Kuandaa na Kusimamia Mfumo wa Usimamizi wa Vihatarishi katika Taasisi za Umma; kuendelea kuimarisha na kusimamia Mfuko wa Taifa wa Maafa; kuimarisha utawala bora na utawala wa sheria; na kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Kuimarisha Upatikanaji wa Fedha za Kigeni.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imepata mafanikio makubwa kutokana na kuwepo kwa sera madhubuti za Serikali ya Chama Cha Mapinduzi zilizolenga kuimarisha uchumi. Katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake, Mheshimiwa Rais amedhihirisha kuwa ni kiongozi mwadilifu, msikivu, makini, shupavu, mchapa kazi na aliye na dhamira thabiti ya kuendelea kuiletea nchi yetu maendeleo makubwa kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati. Hakika MAMA Mitano Tena! Aidha, niwashukuru wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kudumisha amani na utulivu hapa nchini ambayo imetusaidia sana kuwatumikia vyema na kufanikisha mafanikio yaliyopatikana katika kipindi chote cha miaka mitatu ya MAMA.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitatu ya MAMA, bado wananchi wana kiu ya kuona huduma za jamii kama vile barabara, maji, afya, elimu na umeme zinaendelea kuwa bora zaidi. Bajeti ya mwaka 2024/25 inalenga kuwawezesha watanzania kuwa na maisha bora kwa kuendeleza juhudi za kujenga msingi wa uchumi wa viwanda ili kupanua fursa za ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa na ustawi endelevu wa jamii. Katika kufikia malengo hayo, Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti ikiwemo: kuboresha miundombinu ya nishati, usafiri na usafirishaji; kuimarisha mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji kupitia sera madhubuti ili kuwezesha ushindani huria wa sekta binafsi; kuboresha mifumo ya elimu na mafunzo; na kuunganisha tafiti na maendeleo na shughuli za kiuchumi zenye tija.
Mheshimiwa Spika, ili kufikia matamanio haya, rai yangu kwa Watanzania wenzangu, na hasa sisi viongozi ni lazima tujitoe kuijenga Tanzania kwa kumuunga mkono Rais wetu kwa vitendo. Hivyo, ni lazima tufanye kazi kwa bidii tukijielekeza kutekeleza malengo tuliyojiwekea ya kujenga uchumi imara unaotengeneza ajira ili kila mtanzania anufaike na matunda ya jasho lake.
Mheshimiwa Spika, kama mnavyofahamu, nchi yetu ipo katika mchakato wa kidemokrasia wa kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024 na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. Nipende kulihakikishia Bunge lako Tukufu na wananchi kwa ujumla kuwa Serikali imejipanga kikamilifu kugharamia mchakato mzima wa chaguzi hizo. Nitoe rai kwa viongozi wa vyama vya siasa na wananchi kwa ujumla kuhakikisha kuwa tunatumia haki yetu ya kikatiba kuchagua au kuchaguliwa kwa amani, undugu na upendo. Aidha, tuhakikishe kuwa viongozi tunaowachagua wawe ni waadilifu, wasikivu, wazalendo, wachapa kazi na wanaotoka ndani ya chama cha siasa kinachotetea maslahi na haki za wanyonge na chama hicho ni Chama Cha Mapinduzi!
Mheshimiwa Spika, napenda kutoa pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kutimiza miaka mitatu tangu aingie madarakani mwezi Machi 2021 na kuendelea kuliongoza vyema Taifa letu kwa umahiri mkubwa huku tukishuhudia mafanikio makubwa katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii kama nitakavyoelezea hapo baadae.
Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia mafanikio ya miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita, hatuwezi kumsahau Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo, naomba nitumie nafasi hii kumpongeza kwa kumsaidia vyema Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuongoza shughuli za Serikali ambazo matokeo yake yanaonekana na tunajivunia.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kwa uongozi wake thabiti alioonesha tangu kuchaguliwa kwake. Hakika Zanzibar ya Uchumi wa Buluu Inameremeta! Aidha, nitoe pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Ruangwa, pamoja na Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko, Naibu Waziri Mkuu, Waziri wa Nishati na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, kwa kuendelea kuratibu na kusimamia shughuli za Serikali kwa weledi na umahiri mkubwa. Hakika Safu hii Imesheheni Viongozi Makini, Kazi Iendelee!
Mheshimiwa Spika, nitumie tena fursa hii kukupongeza wewe binafsi Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson Mwansasu, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani. Kuchaguliwa kwako kumeliletea heshima kubwa Taifa letu kwa kuwa mwanamke wa kwanza kutoka Bara la Afrika kushika wadhifa huo. Hongera sana! Tunakutakia kila la kheri katika majukumu hayo na unapoendelea kuliheshimisha Taifa letu katika nyanja za siasa za kimataifa. Nikupongeze pia Mheshimiwa Spika pamoja na Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu, Naibu Spika na Mbunge wa Jimbo la Ilala, kwa kuendelea kutekeleza kikamilifu majukumu ya kuliongoza Bunge letu Tukufu. Hakika mmeendelea kuonesha ukomavu, ustahimilivu na weledi wa hali ya juu katika kusimamia na kuendesha shughuli za Bunge.
Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania; Mheshimiwa Mustapher Mohamed Siyani, Jaji Kiongozi – Mahakama kuu ya Tanzania; Prof. Elisante Ole Gabriel, Mtendaji Mkuu wa Mahakama na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama; na Mheshimiwa Eva Kiaki Nkya, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, kwa kazi nzuri ya kuongoza mhimili wa Mahakama.
Mheshimiwa Spika, nawapongeza pia waheshimiwa wabunge waliopata heshima ya kuteuliwa kushika nafasi mbalimbali serikalini mwaka 2023/24. Wabunge hao ni: Mheshimiwa Doto Mashaka Biteko (Mb), Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati; Mheshimiwa Deogratius John Ndejembi (Mb), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu; Mheshimiwa Jerry William Silaa (Mb), Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Mheshimiwa Zainab Athuman Katimba (Mb), Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Mheshimiwa Stanslaus Haroon Nyongo (Mb), Naibu waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji; Mheshimiwa Daniel Baran Sillo (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi; Mheshimiwa Judith Salvio Kapinga (Mb), Naibu Waziri wa Nishati; Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile (Mb), Naibu Waziri Uchukuzi; Mheshimiwa Alexander Pastory Mnyeti (Mb), Naibu waziri Kilimo; na Dunstan Luka Kitandula (Mb), Naibu Waziri Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee kabisa nimpongeze Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi kwa kuaminiwa na kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi. Hakika, uzoefu na umahiri wake katika siasa na diplomasia ya kimataifa hauna shaka yoyote katika kusimamia kwa weledi na umahiri utekelezaji wa mipango ya Serikali na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020. Kidumu Chama Cha Mapinduzi!
Mheshimiwa Spika, niwapongeze Mheshimiwa Deodatus Philip Mwanyika, Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini, na Mheshimiwa Dkt. Joseph Kizito Mhagama, Mbunge wa Jimbo la Madaba, kwa kuchaguliwa na kuungana na Mheshimiwa Najma Murtaza Giga, Mbunge wa Viti Maalumu, kuwa wenyeviti wa Bunge. Nawatakia utendaji mwema katika majukumu yao. Aidha, nimpongeze Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini, kwa kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti pamoja na makamu wake Mheshimiwa Twaha Ally Mpembenwe, Mbunge wa Jimbo la Kibiti. Ni matumaini yangu wataendeleza ushirikiano na umakini mkubwa katika kupitia, kuchambua na kushauri wakati wote wa maandalizi ya Bajeti ya Serikali. Vilevile, ninawashukuru Wenyeviti, Makamu Wenyeviti na Wajumbe wa Kamati zote za Kudumu za Bunge kwa michango yao waliyoitoa kupitia vikao vya Kamati za Kisekta katika kuboresha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara mbalimbali na Serikali kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwapongeza na kuwashukuru kwa dhati kabisa wakuu wote wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa uzalendo na utumishi wao uliotukuka. Naomba niwatambue kwa majina: Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Jacob John Mkunda; Inspekta Jenerali wa Polisi, Camillus Mongoso Wambura; Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Balozi Ali Idi Siwa; Kamishna Jenerali wa Magereza, Mzee Ramadhani Nyamka; Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Peter Makakala; Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji, John William Masunga; Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, CP Salum Rashid Hamduni; na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas James Lyimo. Aidha, niwapongeze Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mheshimiwa Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi na Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Nalija Luhende kwa kazi zao nzuri za kuwatumikia wananchi.
Mheshimiwa Spika, nawapongeza Waheshimiwa Mawaziri wenzangu na Naibu Mawaziri kwa kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. Aidha, namshukuru Katibu Mkuu Kiongozi, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Taasisi pamoja na wataalam wote wa Serikali na sekta binafsi kwa ushirikiano na michango waliyotoa katika kila hatua ili kukamilisha bajeti hii.
Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru viongozi na watumishi wenzangu wa Wizara ya Fedha kwa ushirikiano mkubwa walionipa na kwa kujituma katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara hususani katika maandalizi ya bajeti hii. Kipekee ninamshukuru Mheshimiwa Hamad Hassan Chande (Mb), Naibu Waziri wa Fedha na Mbunge wa Jimbo la Kojani; Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Katibu Mkuu HAZINA na Mlipaji Mkuu wa Serikali pamoja na Naibu Makatibu Wakuu, Amina Khamis Shaaban, Elijah Greenton Mwandumbya na Jenifa Christian Omolo. Aidha, namshukuru Ndugu Emmanuel Mpawe Tutuba, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, kwa kusimamia sekta ya fedha kwa ustadi. Pia nimshukuru Ndugu Alphayo Japan Kidata, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, kwa jitihada kubwa anazofanya za kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Vilevile, namshukuru CPA Charles Edward Kichere, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, kwa kazi nzuri ya kukagua hesabu za taasisi mbalimbali za Serikali. Nimshukuru pia Dkt. Albina Andrew Chuwa, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, kwa kusimamia vizuri Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii pia kuwashukuru kwa dhati wananchi wa Jimbo langu la Iramba Magharibi kwa kuendelea kuniunga mkono na kutambua wajibu wa kitaifa nilionao na dhamana niliyokabidhiwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, niwashukuru Watanzania wote kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita ambayo inaendelea kutekeleza kwa dhati dhamira ya kujenga uchumi wa nchi na kuboresha hali ya maisha ya kila mtanzania. Kwa namna ya pekee, nawashukuru viongozi na waumini wa dini zote kwa kuendelea kuliombea Taifa letu na kumuombea Rais wetu pamoja na viongozi wote wa Serikali katika utekelezaji wa majukumu yao. Niwaombe tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu bila kuchoka.
Mheshimiwa Spika, niipongeze timu ya Azam kwa kushika nafasi ya pili katika mashindano ya Ligi kuu ya NBC na kufuzu kushiriki mashindano ya Klabu Bingwa ya Afrika. Aidha, niipongeze timu ya Coastal Union kwa kufuzu kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya muda mrefu. Kwenye mafanikio ya timu ya Coastal Union, nimpongeze kwa dhati Mheshimiwa Ummy Ally Mwalimu, Mbunge wa Tanga Mjini kwa kujitoa kwa hali na mali ikiwa ni pamoja na kuhudhuria katika uwanja wa Mkwakwani na viwanja vingine bila kukosa na kushirikiana na wadau wengine kuiwezesha timu hiyo kufuzu kushiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika. Mheshimiwa Spika, ni vyema kuwakumbusha wanatanga walikotoka maana kiubinadamu nyumba ikipendeza kuna wakati sifa huwa zinakwenda kwa fundi rangi tu na kuwasahau aliyechora ramani, aliyejenga msingi imara, ukuta imara na aliyepaua na kumpa fursa anayepaka rangi akiwa kwenye kivuli.
Mheshimiwa Spika, kwa umaalum kabisa nimpongeze GSM kwa uwekezaji mzuri alioufanya ambao umebadilisha kabisa taswira na uwezo wa kiuchezaji wa timu ya Yanga. Mafanikio hayo yametokana na uwekezaji mzuri uliofanywa na GSM; GSM wewe ni mwamba, ujengewe Sanam/Mnara pale Makao Makuu ya Yanga. Napenda nitoe pongezi kwa Menejimenti Bora ya timu chini ya Eng. Hersi Saidi kwa kuiongoza vyema timu ya wananchi Yanga na kuipeperusha bendera ya nchi yetu katika medani za kimataifa. Kama tunavyofahamu, Tanzania iliingiza timu mbili katika hatua ya robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika, ikiwa ni kwa mara ya kwanza katika historia ya soka nchini. Pamoja na kwamba wenzetu Simba walipigwa ndani nje katika hatua hiyo lakini ni sehemu ya kujifunza na kujipanga upya. Kipekee, niipongeze timu ya YANGA kwa kuitoa jasho timu ya Mamelodi Sundowns. Nina hakika siku ile ya mechi ya mwisho kule Afrika Kusini, wale wachezaji wa Mamelodi Sundowns walilala na viatu kufuatia kitu kizito walichokumbana nacho uwanjani.
Mheshimiwa Spika, mafanikio haya yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na hamasa ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo amekuwa akitoa shilingi milioni tano kwa kila goli linalofungwa katika hatua ya makundi na shilingi milioni kumi kuanzia hatua ya robo fainali. Hivyo, kwa namna ya pekee naomba nitoe pongezi kwa MAMA yetu kwa ubunifu huo ambao umeliletea Taifa letu sifa na heshima kubwa katika nyanja ya michezo. Ni rai yangu kuwa tuendelee kuhamasisha michezo mingine ili nchi yetu iweze kushiriki katika mashindano mbalimbali ya kimataifa na hatimaye kurudi na tuzo au makombe. Aidha, napenda kutumia fursa hii kuipongeza timu ya YANGA kwa kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya kandanda nchini kwa mara ya tatu mfululizo na Kombe la Shirikisho la Benki ya CRDB. Yanga ni wafalme wa soka la Tanzania, natamani kumshauri Gavana wa Benki kuu kuweka nembo ya klabu ya Yanga kwenye noti ya shilingi 100 kuyaenzi mafanikio haya.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee kabisa nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kunijalia afya njema katika utekelezaji wa majukumu yangu. Naomba pia kumshukuru mke wangu na rafiki yangu kipenzi Bi. Neema Mwigulu Nchemba pamoja na watoto wetu kwa maombi yao na kunipa faraja inayoniwezesha kutekeleza wajibu niliopewa wa kuwatumikia watanzania.
Mheshimiwa Spika, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, Viongozi na Wananchi wote kwa kunisikiliza.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
VIAMBATISHO
No comments:
Post a Comment