SERIKALI YA UINGEREZA YATANGAZA MIKAKATI MIPYA USHIRIKIANO NA TANZANIA KUBORESHA UWEKEZAJI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday 5 April 2024

SERIKALI YA UINGEREZA YATANGAZA MIKAKATI MIPYA USHIRIKIANO NA TANZANIA KUBORESHA UWEKEZAJI

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba na Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Maendeleo na Afrika Mhe. Andrew Mitchell wakishuhudia zoezi la upandishwaji wa bendera za mataifa hayo mawili kwenye hafla ya ufunguzi wa Ofisi ya Ubalozi wa Uingereza jijini Dodoma

Serikali ya Uingereza imetangaza mipango na mikakati mipya ya ushirikiano na Serikali ya Tanzania ili kuzimarisha ushirikiano katika Sekta za Afya, Uwekezaji na Biashara na kusaidia miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi.


Mipango hiyo imetangazwa leo tarehe 05 Aprili 2024 jijini Dodoma na Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Maendeleo na Afrika, Mhe. Andrew Mitchell wakati wa hafla ya ufunguzi wa Ofisi Ndogo za Ubalozi wa Uingereza jijini hapa.


Akitangaza mipango hiyo, Mhe. Mitchell amesema Serikali ya Uingereza  imechangia kiasi cha Dola za Marekani milioni 18.9 kwenye Mpango wa Miaka Mitano wa Afya kwa Wote unaotekelezwa nchini  ili kuimarisha mifumo ya afya, kuimarisha ustahimilivu wa huduma za afya,  kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika na kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

Kadhalika, Uingereza imetoa kiasi cha Dola za Marekani milioni 15 kwa ajili ya kushirikiana na Serikali ya Tanzania kwenye masuala ya maboresho ya  Afya ya Uzazi ikiwemo kuboresha huduma za uzazi wa mpango kwa lengo la kuwafikia takribani watu 900,000.

Katika kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili hususan kwenye kuboresha hali ya maisha ya Watanzania, Serikali hiyo imeahidi kuendelea kusaidia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) ambao hutoa ruzuku kwa asilimia 15 kwa kaya maskini zaidi katika mikoa yote ya Tanzania ili kuimarisha uchumi, upatikanaji wa chakula na kuboresha mazingira kwa kaya hizo.


Kadhalika Serikali hiyo imepongeza juhudi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika utunzaji wa  mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambapo nchi hiyo  katika kuunga mkono jitihada hizo imeahidi kuchangia kiasi  cha Dola za Marekani milioni 6.9 hadi mwaka 2026 ili kuwezesha upatikanaji wa nishati safi na kukuza teknolojia safi ya kupikia kwa utunzaji mazingira.


Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba ameishukuru Serikali ya Uingereza kwa ushirikiano uliopo baina ya nchi hizi mbili na kwa kutangaza mipango na ufadhili kwa miradi mbalimbali ya manufaa kwa wananchi wa Tanzania.

Pia ameipongeza nchi hiyo kwa kufungua Ofisi Ndogo za Ubalozi jijini Dodoma ikiwa ni mwitikio wa wito wa Serikali ya Tanzania wa kuhamishia Makao Makuu yake jijini humo. 

Amesema mbali na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali ikiwemo ujenzi wa miundombinu kama Reli ya Kisasa na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa jijini Dodoma, Serikali itaendelea kuwekeza katika kuboresha jiji hilo  ili kuwa na hadhi stahiki ya makao makuu ya nchi.

Wakati huohuo, Tanzania na Uingereza zimesaini Hati ya Makubaliano kuhusu Ushirikiano unaozingatia Maslahi ya Pande Zote Mbili. Hati hii pamoja na mambo mengine inalenga kuongeza ushirikiano katika maeneo ya uwekezaji kutoka Uingereza; Kuongeza biashara baina ya Tanzania na Uingereza; Kuhamasisha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati pamoja na kuisaidia sekta ya madini nchini.

Kwa upande wa Tanzania Hati hiyo imesainiwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida huku Uingereza ikiwakilishwa na Balozi wa Uingereza nchini, Mhe. David Concar. Utiaji saini huo umeshuhudiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo na Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Maendeleo na Afrika, Mhe. Andrew Mitchell.

Mhe. Mitchell ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili amekutana pia kwa mazungumzo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda na Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu.

No comments:

Post a Comment