MKURUGENZI MKUU TTCL AWASHUKURU WADAU KWENYE SADAKA YA FUTARI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday 5 April 2024

MKURUGENZI MKUU TTCL AWASHUKURU WADAU KWENYE SADAKA YA FUTARI







Na Rehema Nyangasa- Mwanza

MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania-TTCL, Mhandisi Peter Ulanga amewashukuru wadau waliojumuika pamoja katika hafla maalum ya kufuturisha Wafanyakazi na wadau mbalimbali wa sekta ya Mawasiliano iliyofanyika Aprili 4, mwaka huu.

Katika hafla hiyo ya ibada iliyofanyika kwenye Hoteli ya Malaika jijini Mwanza, Mhandisi Ulanga aliwakumbusha waumini walioshiriki kujitahidi kufuata maagizo ambayo wanapewa na Mwenyezi Mungu kupitia mawaidha kutoka kwa viongozi wa dini.

"Tumeipokea heshima kubwa ya kujumuika nasi na ni faraja kubwa sana kwetu, Sisi kama Shirika la Mawasiliano tumeona ni vyema kutimiza maagizo ya Mwenyezi Mungu kwa kujumuika na Wadau wetu katika iftari ili kukumbushana maagizo mbalimbali ambayo tunaelekezwa na Mwenyezi Mungu.” Amesema Mhandisi Ulanga.

Pamoja na hayo, ametoa wito kwa Mashirika ya Umma, Taasisi binafsi na wabunifu katika masuala ya teknolojia kutumia fursa ya uwepo wa huduma ya Faiba Mlangoni Kwako kuboresha utendaji wao wa kazi na kuongeza ufanisi katika majukumu yao.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, Bw. Hassan Masalla akizungumza kwenye hafla hiyo, iliyoandaliwa na Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL, Bi. Zuhura Snare Muro, amepongeza juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kukuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya mawasiliano ili kurahisisha huduma za kiuchumi na kijamii.

Hata hivyo, amepongeza kitendo cha Shirika la TTCL kupitia kwa Mwenyekiti wake wa Bodi cha kufuturisha huku akisema jambo hilo pamoja na mambo mengine ni tendo la ibada ambalo pia linahimarisha na kujenga uhusiano mazuri kati ya Wafanyakazi na wateja wao. 

Ametoa pongezi kwa Mwenyekiti wa Bodi na Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Ulanga kwa kuona umuhimu wa kufanya jambo hilo ambalo ni moja ya nguzo kuu katika dini ya Kiislam, ambapo katika kipindi cha mfungo wa Ramadhani watu binafsi, Taasisi, Mashirika na Kampuni wanatumia kipindi hiki kutoa sadaka hasa kufuturisha makundi mbalimbali katika jamii.

“Nawapongeza sana kwakufanya jambo hili la kufuturisha na naomba niwaambieni hii imekuwa fursa nzuri kukutana na wadau wenu na kuimarisha upendo, umoja na mahusiano yenu na jamii mnayoihudumia,” amesema Masalla.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL, Bi Zuhura Sinare Muro amewashukuru wote waliohudhuria katika hafla hiyo ya Iftari ambayo ni mara ya kwanza kufanyika nje ya Dar Es Salaam.

Amesema TTCL ni Shirika la Wananchi hivyo kwa muktadha huo Watumishi wa Shirika hilo wanapaswa kutambua kuwa wamebeba dhamana kubwa ya ulinzi na usalama wa nchi kupitia miundombinu ya Mawasiliano.

Amesema kila Mtumishi katika nafasi yake anapaswa kuhakikishe anaongeza bidii, ubunifu na uzalendo wa hali ya juu ili kuhakikisha huduma ya mawasiliano inapatikana kwakuzingatia ubora, urahisi na unafuu wa gharama.

Kwa upande mwingine amemshukuru Mhe. Dkt. Samia kwa kitendo chake cha kuliamini shirika hilo na kulipa dhamana ya kutunza na kuendesha miundombinu ya kimkakati ya mawasiliano na kuwataka Watumishi wa TTCL kutokumwangusha katika utekelezaji wa majukumu hayo makubwa.

"Tumebeba dhamana kubwa ya kulinda na kutunza miungombinu tuliyokabidhiwa kazi yetu kubwa ni kuhakikisha hatumwangushi Rais wetu na ahadi yetu ni kuwa jukumu hili tunalibeba kwa weledi wa hali ya juu,”. Alisisitiza Bi. Sinare Muro.

No comments:

Post a Comment