SERIKALI
imewahakikishia Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya
Kazi, kuwa inayachukulia kwa uzito mkubwa, maoni na mapendekezo yao kuhusu
maboresho ya Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi
Kauli hiyo ya Serikali
imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye
Ulemavu, Mhe. Profesa Joyce Ndalichako, wakati akifunga Kikao Kazi cha Mafunzo
ya Uelimishaji kwa Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya
Kazi, Kanda ya Kusini na Watendaji wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) mjini
Songea, Februari 10, 2024.
Akieleza zaidi Mhe.
Profesa Ndalichako amesema tayari inayafanyia kazi baadhi ya mapendekezo ya
maboresho ya sheria yaliyotolewa na waheshimiwa Majaji kwenye kikao kazi kama
hicho kilichofanyika mjini Bagamoyo mwezi Julai, 2023
“Mapendekezo ya
kuboresha kifungu cha 39 (2) cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi [Sura 263]
kilichoweka ukomo wa muda wa kuwasilisha madai bila kutoa wigo wa kupokea madai
hayo iwapo kuna sababu za msingi za kucheleshwa, tumeyafanyia kazi na
tunataraji muswada wa marekebisho kuwasilishwa bungeni hivi karibuni.” Amesema
Mhe. Profesa Ndalichako.
Aidha, Mhe. Profesa
Ndalichako amesema Ofisi yake kupitia Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi inatarajia
kupokea maoni zaidi kutoka kwa waheshimiwa majaji kwa lengo la kuongeza ufanisi
wa utekelezaji wa Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi [Sura 263].
“Natamani kuona kuwa
kati ya mapendekezo yenu katika mafunzo haya iwe ni namna gani rahisi tunaweza
kutumia sheria kuwezesha waajiri wote ambao hawajajisajili WCF, kufanya hivyo
mara moja,” amesema
Mhe. Profesa
Ndalichako pia amebainisha kuwa Serikali ya awamu ya Sita chini ya Uongozi
mahiri wa Mheshimiwa Daktari Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania inatambua na kuthamini mchango wa wafanyakazi katika sekta zote na
ndio maana imeendelea kutekeleza na kuboresha masuala ya fidia kwa wafanyakazi
katika sekta binafsi na umma
Amesema, katika
kipindi kifupi cha Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita kumeshuhudiwa
mabadiliko mbalimbali katika sekta ya hifadhi ya jamii ikiwemo kupunguza
kiwango cha uchangiaji kwa waajiri wa sekta binafsi kutoka asilimia 1 ya
mshahara wa mfanyakazi kila mwezi hadi kufikia asilimia 0.5;
Awali akifungua mafunzo
hayo mwishoni mwa juma, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.
Mustapher Siyani aliwahimiza waajiri nchini kujisajili WCF na kutoa taarifa za
ajira za wafanyakazi wao ili kulinda haki za wafanyakazi hao pindi wanapopatwa
na majanga wakiwa kazini.
"Pamoja na uwepo
wa sheria inayowabana waajiri wanaoshindwa kuwasajili wafanyakazi wao WCF
lakini bado kuna waajiri ambao hawatoi taarifa za ajira za wafanyakazi wao na
hivyo kuuweka mfuko katika nafasi ngumu ya kutekeleza majukumu yake,"
alifafanua
Jaji Siyani ametoa
mfano wa kisa cha mfanyakazi mmoja aliyekuwa akifanya kazi kwenye kampuni moja
ya ujenzi mkoani Lindi ambaye aliumia akiwa kazini na kupelekea kupoteza
baadhi ya viungo vyake na kumsababishia ulemavu wa kudumu kwa zaidi ya asilimia
75 lakini alikosa vigezo vya kupata fidia kwa kuwa mwajiri wake hakuwa
amejisajili na kuwasilisha michango WCF kwa mujibu wa sheria.
“Licha ya kijana huyo
kufanya kazi kwa zaidi ya miaka miwili lakini taarifa zake hazikuwepo WCF na
hivyo kukosa haki ya kupata fidia yoyote” ameeleza Jaji Siyani; na kuongeza
kuwa iwapo zingekuwepo taarifa za mfanyakazi huyo, bila shaka angepata fidia
bora zaidi ya ile iliyotokana na majadiliano na maridhiano na mwajiri wake.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma,
amesema Mahakama ya Tanzania ni wadau muhimu wa Mfuko huo katika utekelezaji wa
majukumu yake kwa kuwa Mfuko unategemea maamuzi mbalimbali ya mahakama katika
utekelezaji wake wa majukumu ikiwemo maamuzi ya kesi za mirathi.
Dkt. Mduma amesema
kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Serikali
yanayozitaka taasisi zake kuhakikisha zinashirikiana kwa karibu kwa
dhumuni la kuongeza tija na huduma bora kwa wananchi.
Pia, mafunzo hayo
yanatoa fursa ya kubadilishana uzoefu baina ya wataalam wa Mahakama na WCF
kupitia mada mbalimbali zitakazowasilishwa ambapo washiriki wanaweza kuja na
mapendekezo yatakayoboresha utendaji kazi wa Mfuko huo.
"Ni matarajio
yangu kuwa mafunzo haya yataleta manufaa makubwa kwa pande zote mbili, ikiwemo
kuimarisha mahusiano kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi na kuchangia
kukuza uchumi wa nchi yetu na hasa kupunguza umasikini kwa wafanyakazi
watakaopata majanga yanayotokana na kazi zao," amesisitiza Dkt. Mduma.
Mafunzo hayo ambayo ni
ya awamu ya nne yamewaleta pamoja washiriki kutoka mikoa ya Ruvuma, Mtwara,
Iringa, Mbeya, Songwe na Rukwa ambapo miongoni mwa mada zinazotarajiwa
kuwasilishwa ni kuhusu sheria ya fidia kwa wafanyakazi, taratibu za
uwasilishaji na ushughulikiaji wa madai ya fidia kwa wafanyakazi.

No comments:
Post a Comment