Na Mwandishi wetu, Mara
Wajumbe wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) wameonesha kuridhishwa na zoezi la Uboreshaji wa majaribio wa
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unaoendelea katika Kata ya Ikoma iliyopo
Halmashauri ya Wilaya ya Rorya Mkoani Mara ambapo hadi kufikia jana Wapiga Kura
1,613 wamejitokeza.
Wajumbe hao wa Tume, Mhe. Jaji
Asina Omar, Mhe. Jaji wa Rufaa Mwanaisha Kwariko na Mhe. Magdalena Rwebangira
wametembelea vituo vya uboreshaji katika Kata ya Ikoma na kushuhudia ufanisi wa
zoezi hilo.
Wakizungumza wakati wa ziara
hiyo, Jaji Asina Omar amesema mwitikio wa wananchi kujitokeza kujiandikisha na
kuboresha taarifa zao ni mkubwa na mawakala wanashiriki kikamilifu katika zoezi
hilo ikiwa ni pamoja na kuwabaini wananchi wasio na sifa za kuandikishwa kuwa
Wapiga Kura.
“Zoezi linakwenda vizuri,
tumeshuhudia katika vituo tulivyotembelea hakuna changamoto na zilizopo
zimetatuliwa na wataalam kwa kushirikiana na makawala wa vyama waliopo vituoni
jambo ambalo linaonesha lengo la zoezi hili kutimia kama ilivyo kusudiwa,”
alisema Mhe. Jaji Asina.
Jaji Asina amesema, muda
unaotumika kuandikisha au kuboresha taarifa za Mpiga Kura unazidi kuwa mfupi na
kuimarika kwa huduma vituoni hivyo kuleta ufanisi zaidi siku hadi siku na
kuonesha uwezo wa vifaa vinavyotumika.
Kwa upande wake Mjumbe wa Tume
ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Magdalena Rwebangira amesema ameridhishwa namna
zoezi linavyofanyika hivyo lengo la zoezi hilo la kufanyia majaribio vifaa vya
uboreshaji pamoja na mifumo ya uboreshaji wa Daftari linatimia kwani changamoto
zinabainika na kutatuliwa mapema.
Akitoa taarifa ya siku nne za
uboreshaji huo wa majaribio katika Kata ya Ikoma, Mkurugenzi wa Idaya ya
Usimamizi wa Uchaguzi, Ndg. Grayson Orcado kwa niaba ya Mkurugenzi wa Uchaguzi
alisema, zoezi hilo linakwenbda vizuri na kwa ufanisi mkubwa kwani hadi sasa
wananchi 1,613 wamejitokeza vituoni ambapo kati ya hao 1,356 wamejiandikisha
kuwa wapiga kura na wapiga kura 257 wameboresha taarifa zao huku hakuna
walioondolewa katika Daftari.
Orcado amesema, mawakala wa
vyama wanaonesha ushirikiano wa hali ya juu hasa katika changamoto za utambuzi
wa wakazi wa maeneo yao kwa kuzingatia kuwa Kata ya Ikoma inamwingiliano wa
raia wanchi jirani.
Kwa mujibu wa mawakala wa
vyama waliokuwepo katika kituo cha kujiandikisha wapiga kura cha Shule ya
Msingi Nyamasanda, walieleza kuwabaini raia 8 wakigeni kutoka nchi jirani ambao
walikiri kuwa si watanzania na hivyo Mwandishi Msaidizi hakuweza kuwaandikisha
kuwa wapiga kura.
Wakala wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (CHADEMA) Silvanus Owan’ge aliyepo katika Kituo cha Ofisi ya
Mtendaji Kata ya Ikoma amesema, wanarisdhishwa namna zoezi hilo lilivyo la
uwazi na kupongeza Tume kwa namna inavyofanya kazi kwa kushirikiana nao.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi
inaendesha zoezi la uboreshaji wa majaribio wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
katika Kata ya Ikoma iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Mkoa wa Mara na
Kata ya Ng’ambo iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Mkoa wa Tabora
kuanzia tarehe 24 hadi 30 Novemba, 2023.

No comments:
Post a Comment