Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Singida, Peter Njau (kulia) akitoa elimu ya kupinga ukeketaji kwa wananchi katika mnada wa Kijiji cha Nkwae Kata ya Msisi uliofanyika Oktoba 3, 2023 kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali la Women Wake-Up (WOWAP)
Na Dotto Mwaibale, Singida
SHIRIKA lisilo la Kiserikali la Women Wake-Up (WOWAP) lenye makao yake
makuu Dodoma linalojishughulisha na utetezi wa haki za wanawake na watoto na
utoaji wa msaada wa kisheria bure kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya
Singida mkoani Singida limetoa elimu ya kupinga vitendo vya ukeketaji kwa
wananchi katika Mnada wa Kijiji cha Nkwae unaofanyika kila mwezi Kata ya Msisi.
Kupitia ufadhili wa Shirika la Women Action Against FGM (WAAF) Japan
shirika WOWAP wanatekeleza mradi wa kupinga ukeketaji kwa kutoa elimu katika
makundi ya jamii kwenye wilaya hiyo.
Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Singida, Peter Njau akizungumza na
waandishi wa habari wakati wa utoaji elimu
katika mnada huo alisema wilaya humo bado kunachanga changamoto kubwa ya
ukeketaji na kuwa licha ya kutoa elimu ya kupinga vitendo hivyo dhidi ya watoto
wa kike na wanawake uelewa wa jamii ni mdogo.
“Jamii ya maeneo haya bado inauelewa mdogo na inaendelea na vitendo vya
ukeketaji ndio maana shirika la WOWAP limeanzisha kampeni ya kuzunguka kwenye
kila mnada kwa ajili ya kutoa elimu hii ambayo tunaamini itawafikia watu wengi
zaidi kwa wakati mmoja,” alisema Njau.
Alisema elimu hiyo imekuwa ikiwahusisha viongozi wa dini, wazee maarufu,
wanafunzi, wanawake, viongozi wa vijiji na kata, wakunga wa jadi na ngariba
wastaafu.
Njau alisema kampeni hiyo ni endelevu na itakuwa ikifanyika katika kila
mnada wilayani humo lengo ni kuhakikisha vitendo hivyo vinakwisha kama sio
kumalizika kabisa.
Afisa Ustawi wa Jamii wa wilaya hiyo, Felix Maigo alisema vitendo vya
ukeketaji vinafanyika kutokana na sababu za kidesturi, dini, kuhifadhi
utamaduni, bikra, usafi, kulinda heshima ya familia na kukubalika kwenye jamii
haswa kuhusiana na ndoa.
Akielezea ukeketaji alisema ni ukataji wa sehemu za siri za mwanamke ambao
unahusisha maeneo nyeti na kuwa aina ya kwanza ya ukeketaji ni kuondolewa kwa
kinembe (kisimi) na kuwa aina ya pili ni kuondolewa kwa sehemu au jumla ya
kisimi na midomo ya ndani ya uke.
Alitaja sehemu ya tatu kupunguza au kukata kwa ujumla uke na nne ni taratibu
zote zenye madhara ikiwa ni pamoja kukata, kuchoma, kurarua, kutoboa na kutanua
sehemu za siri za uke.
Alisema hivi sasa ukeketaji kwa watoto hufanyika kwa siri kubwa kwa
wahusika kuogopa kufikiwa na mkono wa sheria kutokana na vyombo mbalimbali vya
dola na mashirika yasiyo ya kiserikali kupigia kelele jambo hilo.
Maigo alitaja baadhi ya madhara ya ukeketaji kuwa ni makubwa ikiwa na
kusababisha kifo kutokana na mfanyiwaji kutoka kwa damu nyingi na maumivu
makali, uharibifu wa mfumo wa nje wa viungo vya uzazi, na maambukizi, msongo wa
mawazo, kupungua hamu ya kufanya mapenzi, kuongeza hatari ya kujifungua kwa
njia ya upasuaji, watoto kuzaliwa kabla ya muda, kuongezeka kwa vifo vya uzazi
na madhara mengine mengi yanayofanana na hayo.
Maigo alitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa kila mwana jamii katika eneo
analoishi kupiga vita vitendo hivyo vya ukeketaji na kutoa taarifa kwa kupiga bure
namba ya simu 116.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Maghojoa, Godwin Mgitu alisema moja ya kazi kubwa
wanayoifanya ni utoaji wa elimu ya kupinga vitendo vyote vya ukatili katika
kata hiyo na vinapotokea wahusika uchukuliwa hatua na alilipongeza shirika hilo
kwa hatua walioichukua ya kuanzisha kampeni hiyo ya utoaji wa elimu kwenye
minada.
“Niliwaombe WOWAP warudi tena kutoa elimu hii ili wananchi waweze kuelewa
zaidi kutokana na kuwepo kwa changamoto hiyo katika maeneo yetu,” alisema
Mgitu.
Mkazi wa Kijiji cha Kinyagigi, Amiri Jumanne alisema hivi sasa vitendo
hivyo vimepungua kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma alilishukuru
Shirika la WOWAP kwa kuanziasha kampeni hiyo ya kutoa elimu kwenye minada na
kueleza kuwa ni nzuri na itawafikia watu wengi hasa katika maeneo ya vijijini.
“Kipekee nilishukuru shirika la WOWAP kwa kazi hii kubwa wanayoifanya pia
nimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake kwa kushirikiana na
mashirika yasiyo ya kiserikali katika shughuli mbalimbali za kijamii kwa ajili
ya kukabiliana na vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia ukiwemo ukeketaji,”
alisema Jumanne.
Mkazi wa Maghojoa Mrisho Ramadhan alisema vitendo hivyo havikubaliki hata
kidogo hivyo aliliomba shirika hilo kuifanya kampeni hiyo ya kutoa elimu
minadani kuwa endelevu.
Mrisho alisema moja ya majukumu yao kama viongozi wa dini ni kukemea
vitenndo hivyo katika maeneo yao ya ibada na kuwa wanapata mafanikio baada ya
jamii kuonesha kubadilika.
Wananchi wengine walioipongeza kampeni hiyo ni Saimon Ghalanda, Khalidi Samwel na Zaituni Salim kutoka Kijiji cha Msimii.
No comments:
Post a Comment