Na Dotto Mwaibale, Singida WAFUGAJI Tisa akiwamo mtoto mdogo wa jamii ya Kimasai wametua katika Jimbo
la Singida Mashariki lililopo wilayani Ikungi mkoani Singida linaloongozwa na
Miraji Mtaturu baada ya kupata taarifa kuwa mwaka jana mbunge huyo alikuwa
akitoa msaada wa chakula. Wamasai hao waliwasili mjini Ikungi wakitokea Kata ya Inokanoka Halmashauri
ya Wilaya ya Ngorongoro na kupokelewa katika kitongoji cha Misri Kijiji cha
Ikungi ambapo waliuliza watawezaje kumuona Mbunge Mtaturu. Wafugaji hao ambao walikuwa katika hali ya kudhoofu kutokana na njaa na
safari ndefu, mwenyeji wao aliyewapokea aliyetambulika kwa jina la Hanifa Mwiko
‘ maarufu Mama Saiduni’ aliwapatia
chakula kabla ya kwenda kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa
kitongoji hicho ambaye naye alikwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi. Baada ya polisi kujiridhisha kuwa wageni hao walikuwa na nia ya kumuona
Mbunge Mtaturu mwenyeji wao Mama Saiduni aliwapa chumba ambapo walilala hadi
siku iliyofuata ambayo mbunge huyo alifika akitokea bungeni Dodoma na
kuzungumza nao na baadae kuwapa msaada wa chakula. Mama wa familia hiyo ya jamii ya kimasai alisema wao walikuwa hawamjui Mbunge Mtaturu walikuwa wakilijua jina lake
tu baada ya kusikia alipokuwa akiwasaidia watu chakula mwaka jana. "Tulikuwa hatumfahamu Mtaturu tulikuwa tunalijua jina lake tu baada ya
kusikia ni mtu mwema na anawasaidia watu
kuwapa chakula kutokana na kuishi bila ya kula kwa kukosa chakula tukaona tuje
tumtafute kwani tuliambiwa ni mbunge wa Igunga lakini watu walitueleza kuwa ni
wa Ikungi," alisema mama huyo wa
Kimasai. Mama huyo alisema kufuatia nyumbani kwao kuwa na hali ngumu ya maisha
wanaomba hata wapewe vibarua vya kulima na kazi nyingine ili waweze kupata
fedha za kujikimu kimaisha. Akizungumza na wananchi hao Septemba 17, 2023 baada ya kuwapatia chakula
Mtaturu aliwapa pole kwa safari ndefu hadi kufika Ikungi lakini aliwaomba mara
baada ya kufika nyumbani kwao waende eneo la Msomera wilayani Handeni mkoani
Tanga ambalo wametengewa na Serikali na kuwekewa miundombinu mizuri kwa ajili
ya kuishi na kupata mahitaji muhimu ya kibinadamu. "Ninyi wenyewe mmekiri kuwa eneo mnaloishi hamuwezi kufanya kilimo na
hakuna huduma niwaombe mkirudi nendeni mlikotengewa na Serikali itakuwa rahisi kusaidiwa,"
alisema Mtaturu. Baadhi ya wananchi wa wilaya ya Ikungi walimpongeza Mbunge Miraji Mtaturu
kwa hatua ya haraka aliyoichukua ya kutoka bungeni Dodoma kwenda Ikungi kuonana
na wageni hao na kuwafanyia kitendo hicho cha huruma kwa kuwapa msaada huo kwa
kuangalia zaidi utaifa kwani ingekuwa kwa watu wengine wangeweza kuwaacha tu
waende zao bila ya kuwasaidia. Aidha, alipongezwa Mama Saiduni kwa moyo wa upendo wa kuwapokea wageni hao na kuwapa mahali pa kulala na jinsi alivyowasiliana na viongozi wa kitongoji hicho na baadae kwenda kutoa taarifa kituo cha Polisi kwa ajili ya tahadhari na usalama. |
Mbunge wa Jimbo la Singida, Mashariki, Miraji Mtaturu kipenzi cha Wananchi wa jimbo lake na maeneo mengine ya nchi akiwa katika moja ya mikutano yake wilayani Ikungi.
No comments:
Post a Comment