Na Wizara ya Madini- Bangkok
NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo ameinadi Minada ya Madini kwa Wafanyabiashara Wakubwa nchini Thailand ikiwa ni maandalizi ya Serikali kuirejesha tena baada ya kuifungia kwa muda.
Mbibo amewafahamisha wafanyabiashara hao kwenye Semina iliyofanyika Septemba 8, 2023 jijini Bangkok katika maonesho ya 68 yanayoendelea nchini humo ambapo semina hiyo imejadili fursa zilizoko katika tasnia ndogo ya madini ya vito na usonara kwa nchi za Mashariki ya Kati ambazo ni miongoni mwa nchi zilizobobea kwenye shughuli za uongezaji thamani madini, nchi wanunuzi na watumiaji wakubwa wa madini ya vito na usonara duniani.
Ameieleza hadhira hiyo kuwa, Tanzania ikiwa mzalishaji mkubwa wa madini ya vito na wao kama wafanyabiashara wakubwa wa madini hayo, wanayo nafasi kubwa ya kushiriki moja kwa moja katika minada ya madini ambayo inatarajiwa kurejeshwa tena mapema mwaka 2024, ikiwemo kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali za kibiashara, uongezaji thamani madini na kushirikiana katika kuongeza ujuzi kwa watanzania waweze kuzalisha bidhaa zenye ubora na zinazokidhi viwango vya kimataifa kwenye soko la dunia na hatimaye kuchochea hamasa kwa watanzania kujikita katika eneo hilo.
Hivi sasa Serikali iko katika hatua za mwisho za mchakato wa kuwasilisha mapendekezo ya maboresho ya Sheria na Kanuni ili kuwezesha maonesho na minada ya vito kurejea ikiwemo marekebisho ya Kanuni za Eneo Tengefu la Mirerani za Mwaka 2021 ambazo zilizuia kuuzwa kwa madini ya Tanzanite nje ya Mirerani.
Kufanyika kwa minada hiyo kuna manufaa makubwa kwa Tanzania ambapo pamoja na mambo mengine itasaidia kuyatambulisha madini yanayozalishwa nchini, kuchangia fedha za kigeni, kuyaongezea thamani, kuongeza tija katika sekta ya madini na kuwahamasisha wauzaji na wanunuzi wakubwa wa madini duniani kununua moja kwa moja kutoka nchini.
Aidha, Mbibo ametumia jukwaa hilo baada ya Tanzania kupata heshima ya kuzungumza katika semina hiyo ambapo amewakaribisha kushiriki katika Jukwaa la Kimataifa la Uwekezaji katika Sekta ya Madini linalotarajiwa kufanyika tarehe 25 na 26 mwezi Oktoba, 2023 jijini Dar es Salaam.
Ameongeza kwamba, jukwaa hilo litawapa nafasi ya kukutana na wauzaji, kufahamu fursa za kibiashara zilizopo nchini, kujenga mahusiano ya kibiashara na wadau kutoka pande mbalimbali duniani na kufahamu kwa kina kuhusu utajiri wa rasilimali madini uliopo Tanzania ambayo ni miongoni mwa nchi wazalishaji wakubwa wa madini ya vito ambapo nchi husika ni walaji.
Katika hatua nyingine, katika mazungumzo yake na wadau hao, amesema wameonesha nia ya kushirikiana na Serikali kuhusu namna ya kuendesha minada hiyo ili kuifanya kuwa na sura ya kimataifa na hivyo wameiomba Wizara iharakishe mchakato wa kurejeshwa kwake. "Wafanyabiashara hawa pia wameonesha utayari wa kushirikiana na sekta binafsi kuendeleza Sekta ya Madini nchini katika eneo hilo,’’ amesema Mbibo.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) Daniel Kidesheni ametoa wito kwa vijana wa Tanzania kuigeukia tasnia ndogo ya uongezaji thamani madini kutokana na fursa nyingi za kibiashara na ajira zilizopo katika eneo hilo kutokana na utajiri mwingi wa madini ambao nchi ya Tanzania imebarikiwa kuwa nao.
Ameongeza kwamba, semina hiyo imeongeza ujuzi kwa Kituo hicho kuona namna bora ya kuwaendeleza vijana wa kitanzania kupitia mafunzo yanayotolewa, matumizi ya teknolojia za kisasa na namna ambavyo ukanda huo ulivyofanikiwa kurithisha taaluma hiyo kwa vizazi na vizazi
Shughuli za uongezaji thamani madini ya vito ni biashara ambayo imeshamiri kwa kiasi kikubwa katika eneo la nchi zilizopo Mashariki ya Kati ikiwemo nchi ya Thailand ambayo ni maarufu katika utengenezaji wa vito vya rangi za kuvutia na imekuwa ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya mapato kwa nchi hizo ikiwemo ajira.
Semina hiyo imehusisha wadau wa madini ambao ni wabobezi Katika biashara ya Vito, shughuli za uongezaji thamani Madini ambapo wamejadili masuala mbalimbali ikiwemo namna ya kuongeza utaalam zaidi katika eneo hilo.
No comments:
Post a Comment