Na Saidina Msangi, WF, Busan, Korea Kusini
TANZANIA imeikaribisha
Jamhuri ya Korea ya Kusini kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo nishati na
kilimo nchini Tanzania ili iweze kufikia lengo la kuwa na maendeleo endelevu.
Wito huo umetolewa na
Balozi wa Tanzania Jamhuri ya Korea Kusini Mheshimiwa Togolani Mavura,
alipokuwa akitoa wasilisho kuhusu fursa zinazopatikana Tanzania wakati wa vikao
vya mkutano wa saba wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Korea Kusini na Nchi za
Afrika (KOAFEC), Mjini Busan, Korea Kusini.
Alisema kuwa Tanzania
ni nchi yenye uchumi tulivu, amani na usalama na pia ina jiografia ya kimkakati
ambapo nchi sita zinazopakana nayo zinategemea Tanzania kama mlango mkuu wa
bahari.
‘‘Tanzania ina ardhi
kubwa kufanikisha kilimo endelevu chenye kujali mazingira na ni nchi yenye
vyanzo vingi vya kuweza kuzalisha umeme wa nishati jadidifu isiyochafua
mazingira hasa ikizingatiwa kuwa dunia inakabiliwa na mabadiliko ya
tabianchi’’, alisema Mhe. Balozi Mavura.
Pia alisema kuwa
Tanzania ina madini ya kimkakati ya graphite, nickel na lithium ambayo ndio
madini yanayohitajika zaidi katika kuzalisha miundombinu na mitambo ya
kuzalisha umeme wa nishati jadidifu.
Aidha, alizungumzia
fursa zilizopo katika uchumi wa buluu na bahari ambazo zinaweza kutumiwa na
Korea kuja kuwekeza katika maeneo hayo ili kwa pamoja kuweza kufikia maendeleo
endelevu.
Alifafanua kuwa kwa
upande wa kilimo Tanzania inajielekeza katika maeneo manne ambayo ni uzalishaji
wa ngano, mafuta ya kupikia, uzalishjaji wa matunda hasa parachichi, nyama na
maziwa ambapo tayari Serikali imewekeza katika mradi wa mashamba makubwa
kuwezesha vijana kulima kibiashara (BBT).
‘‘Tanzania ina fursa
kubwa ya kuwa shamba la Afrika kuzalisha chakula kwa ajili ya Bara la Afrika
ikiwa uwekezaji sahihi utafanyika katika kilimo cha kisasa,’’aliongeza Mhe. Balozi
Mavura.
No comments:
Post a Comment