Karagwe - Kageara
KAMATI ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi Wilaya Karagwe imemshukuru na kumpongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa na kumteua kuwa Waziri wa Ujenzi.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi wilaya Karagwe, Ndugu Paschal Rwamugata katika Kikao cha Kamati hiyo ya Siasa wilaya Karagwe kilichofanyika katika Makao Makuu ya CCM Kayanga, Karagwe, leo tarehe 21 Septemba 2023.
“Kamati ya Siasa tunamshukuru Mwenyekiti Wetu wa CCM Taifa, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kukuamini wewe Mbunge wetu na kukupeleka katika Wizara ya Ujenzi ili umsaidie katika Utekelezaji wa Ilani ya CCM” amesema Rwamugata
Rwamugata amesema Utekelezaji wa Ilani ya CCM katika wilaya ya Karagwe unaendelea kwa kasi kubwa na kuwafanya Wananchi kuendelea kuwa na imani Kubwa na Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi.
Aidha, Rwamugata ameipongeza Serikali kwa kuendelea kusimamia kikamilifu miradi ya kimkatakati inayoendelea kutekelezwa katika Wilaya Karagwe ikiwa ni pamoja na miradi ya Maji, Barabara, Elimu na uboreshaji wa utoaji wa huduma za Afya kwa Wananchi.
Kwa Upende wake, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Mbunge wa Jimbo la Karagwe ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameipongeza Kamati ya Siasa ya Wilaya Karagwe kwa kuendelea kusimamia kimamilifu utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi wilayani Karagwe.
“Ninawashukuru na Kuwapongeza kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kuendelea kuisimamia Serikali katika Utekelezaji wa miradi yote hasa ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa katika wilaya yetu” amesema Bashungwa.
Bashungwa ameeleza kuwa Shukrani na Pongezi za Kamati ya Siasa ya Wilaya atazifikisha kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na akaahidi imani Kubwa aliyopewa atahakikisha anafanya kazi kwa uaminifu na weledi Mkubwa.
No comments:
Post a Comment