WATENDAJI WAZEMBE, WAVIVU, WIZARA YA MALIASILI NA UTALII WAKALIA KUTI KUTI KAVU - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday 23 May 2023

WATENDAJI WAZEMBE, WAVIVU, WIZARA YA MALIASILI NA UTALII WAKALIA KUTI KUTI KAVU

Waziri wa Maliasili  Dk. Mohammed Mchengerwa, akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Mwongozo wa Usimamizi wa Hifadhi za nyuki katika hafla ya kufunga Maadhimisho ya Siku ya Nyuki yaliyofanyika Viwanja vya Bombadia mkoani Singida,May 21, 2023.Wengine kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Dk.Ezekiel Mwakalukwa, Naibu Waziri wa wizara hiyo,Mary Masanja, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Thomas Apson na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Singida, Lusia Mwiru.

Dotto Mwaibale na Selemani Msuya, Singida

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Mohammed Mchengerwa amesema katika uongozi wake hatawavumilia watendaji wazembe na wavivu, huku akitoa miezi miwili kwa watendaji wa sekta ya misitu na nyuki, kuja na mpango mkakati wa ‘Achia Shoka Kamata Mzinga’ ambao utawezesha uzalishaji wa asali nchini kuongezeka hadi kufikia tani 138,000. 

Mchengerwa ameyasema hayo, May 21, 2023 katika hafla ya kufunga Maadhimisho ya Siku ya Nyuki yaliyokuwa yanafanyika katika Viwanja vya Bombadia mkoani Singida ambapo pia alizindua Mwongozo wa Usimamizi wa Hifadhi za nyuki, na vibanda maalum vya kuuzia asali pia ametoa Tuzo 5 za wadau wenye mchango mkubwa kwenye Sekta ya nyuki na ametoa vyeti kwa wanafunzi walioandika nsha nzuri kuhusu ufugaji wa nyuki.

Waziri huyo alisema iwapo kuna watendaji ambao wanafanya kazi kwa mazoea na hawataki kubadilika, hawatakuwa na nafasi katika uongozi wake.

Alisema iwapo kila mtumishi akifanya kazi kwa bidii na kuachana na utendaji wa mazoea ni wazi kuwa Tanzania itaweza kuzalisha zaidi ya tani 138,000 ya asali na kuondoka katika tani 35,000 iliyopo sasa.

“Iwapo kila mmoja wetu ataacha kufanya kazi kwa mazoea, wizara yetu itaweza kuchangia pato la taifa kwa asilimia 30 hadi 50 na kuodoka kwenye asilimia 23. Niwaombe kwamba katika uongozi wake uzembe na uvivu, sitaviruhusu, nataka kuona mipango ya ubunifu, sio kuleta madokezo ya kutaka kusafiri nje ya nchi.

Nataka kuona ni namna gani wizara hii itachangia kundi kubwa la vijana linaondoka katika dimbwi la umaskini, mimi ni waziri mtendaji na tofauti, nataka matokeo, uadilifu na uchapakazi, mheshimiwa naibu waziri kawaambie watendaji wabadilike,” alisema.

Waziri Mchengerwa alisema taasisi zote za wizara zikitekeleza majukumu yake ipasavyo, Tanzania itapata maendeleo ya haraka.

Alisema wizara hiyo inasimamia asilimia 33 ya misitu, hivyo ni lazima tafsiri yake ionekane kwa vitendo na kwamba kinyume na hapo, itawalazimu baadhi yao kuwapisha kwani wameshindwa kuonesha walichoaminiwa nacho.

Mchengerwa alisema Tanzania ni nchi ya pili kwa uzalishaji wa asali Afrika na ya nne duniani, ila matarajio yake ni kuona inakuwa ya kwanza duniani kwa kuwa ina rasilimali misitu mingi ambayo inaweza kuzalisha zao hilo.

Alisema asali ya Tanzania ina soko kubwa ndani na nje ya nchi, hivyo hakuna sababu ya kushindwa kutumia fursa hiyo muhimu.

“Kauli mbiu ya Siku ya Nyuki mwaka huu inasema ‘Tuwalinde Nyuki kwa Ustawi wa Mazingira na Usalama wa Chakula, inaakisi kuwa tafiti zinaonesha asilimia 80 ya chakula kinatokana na uchavushaji wa nyuki,” alisema.

Aidha, Waziri huyo ameilekeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), kuhakikisha maeneo yenye uoto wa misitu, yanatambuliwa na kuhifadhiwa, wananchi wanapata elimu ya uhifadhi na ufugaji kibiashara na vijiji vyote viwe na mpango bora wa matumizi ya ardhi.

Pia aliitaka TFS kuandaa maeneo ambayo yatatumika kufuga nyuki kwa njia ya kiutalii, ambapo amewataka waende kujifunza nchini Slovenia namna ambavyo wananufaika na utalii wa nyuki.

Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi TFS, Profesa Dos Santos Silayo, alisema wakala hiyo imejipanga kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya Waziri Mchengerwa, ili kuhakikisha sekta hiyo inachangia ukuaji wa uchumi.

Alisema TFS imekuwa ikitoa elimu kwa umma kuhusu ufugaji nyuki wa kisasa, ambapo kwa mwaka wawanatumia tkaribani milioni 90 kuhakikisha asali ya Tanzania inapata ithibati ya kuuzwa soko la dunia.

“Sisi kwa kushirikiana na wadau wa nyuki tutahakikisha mnyororo wa thamani wa mazao ya nyuki unaongezeka, ili mchango wa wizara hii uweze kuongezeka,” alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Thomas Apson ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, alisema mkoa huo umepata mafanikio kupitia ufugaji wa nyuki ambapo zaidi ya wananchi 12,133 wanajihusisha katika eneo lenye ukubwa wa hekta 476,361 za misitu ya asili na vichaka vya Itigi.

“Ufugaji wa nyuki umeingiza shilingi 890 zilizotokana na uzalishaji wa asali tani 89 na tani 20 za nta, hivyo tunaamini zao hili ni muhimu katika mkoa wetu. Ila uzalishaji huu unabeba kauli mbiu yetu ya Achia Shoka, Kamata Mzinga,” alisema.

Vijana wa Skauti wakifanya itifaki ya kumvika skafu, Waziri wa Maliasili  Dk. Mohammed Mchengerwa baada ya kuwasili kufunga Maadhimisho ya Siku ya Nyuki mkoani Singida.

Waziri wa Maliasili  Dk. Mohammed Mchengerwa (kulia) akivuta pazia kuachiria uzinduzi wa kibanda maalumu cha kuuzia mazao ya nyuki ikiwemo asali.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja, akizungumza kwenye maadhimisho hayo.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, akizungumza kwenye maadhimisho hayo.

Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Dk.Ezekiel Mwakalukwa, akizungumza kwenye maadhimisho hayo.

Kwaya ya Chuo cha Utumishi wa Umma, Mkoa wa Singida ikitoa burudani kwenye maadhimisho hayo.

Waziri wa Maliasili  Dk. Mohammed Mchengerwa, akisalimiana na Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Singida, Ahmed Kaburu.

Waziri wa Maliasili  Dk. Mohammed Mchengerwa, akisalimiana na Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro.

Mhifadhi Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kassim Ally (kulia) , akitoa maelezo kwa Waziri wa Maliasili  Dk. Mohammed Mchengerwa alipotembelea banda la TFS.

Utembeleaji wa mabanda ukiendelea wakati wa maadhimisho hayo.

Meneja Mahusiano Mwandamizi  ya Kilimo, kutoka Benki ya NMB, akitoa maelezo kwa Waziri wa Maliasili  Dk. Mohammed Mchengerwa, alipotembelea banda la benki hiyo.

Mratibu wa Enabel-Bevac  Project inayofanya shughuli zake katika mikoa ya Tabora, Singida na Shinyanga, Deogratias Kimena, akitoa maelezo kwa Waziri wa Maliasili  Dk. Mohammed Mchengerwa, alipotembelea banda lao.

Viongozi meza kuu pamoja na mgeni rasmi Waziri wa Maliasili  Dk. Mohammed Mchengerwa (katikati) wakishiriki kuimba wimbo wa Taifa na wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati wa maadhimisho hayo.

Wimbo wa Taifa ukiimbwa.

Viongozi wa idara mbalimbali wakiwa kwenye maadhimisho hayo.

Viongozi wa idara mbalimbali wakiwa kwenye maadhimisho hayo.

Baadhi ya Madiwani wa Manispaa ya Singida wakijitambulisha kwenye maadhimisho hayo.

Maadhimisho yakifanyika

Taswira ya maadhimisho hayo. Waliovaa suti ni Wanafunzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Mkoa wa Singida. 

No comments:

Post a Comment