Mkuu waTaasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida, Mzalendo Widege, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi wa taasisi hiyo ya kipindi cha Januari hadi Machi 2023, katika mkutano uliofanyika leo May 18, 2023.
Na Dotto Mwaibale, Singida
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
nchini (TAKUKURU) Mkoa wa Singida imebaini kuwepo kwa mianya ya rushwa katika baadhi ya
halmashauri ikiwemo ya Mkalama ikihusishwa na ukusanyaji wa michango kutoka kwa
wananchi na matumizi yake.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida, Mzalendo Widege wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi wa taasisi hiyo katika maeneo yote matatu yaani, Uzuiaji wa Vitendo vya Rushwa, Elimu kwa Umma na Uchunguzi kwa kipindi cha Januari – Machi 2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa leo May 18, 2023.
Widege alisema Takukuru imebaini fedha za michango zinatumika kabla ya kuingizwa kwenye akaunti za vijiji, baadhi ya wananchi hawapewi stakabadhi hasa kama ametoa mchango pungufu, fedha zinatumika kinyume na madhumuni ya mchango, wenyeviti wa vitongoji na watendaji wa vijiji wanatumia fedha kwa matumizi binafsi.
Aidha, Widege alisema wamebaini mianya ya rushwa katika usimamizi wa fedha za miradi ya maji chini ya kamati za maji za jumuiya za watumia maji ambapo wajumbe wa bodi wanajilipa posho kubwa, hakuna mwongozo wa viwango vya posho na mishahara na ukaguzi wa mahesabu haufanyiki.
"Baada ya kukaa nao tumekubaliana
fedha za miradi ya maji zinazo kusanywa ziingizwe kwenye akaunti kabla ya
kuanza kutumika na wananchi wapewe stakabadhi kama taatibu
zinavyoelekeza," alisema Widege.
Widege akizungumzia uendeshaji wa masoko katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni alisema wamebaini mambo kadhaa kuwa hakuna sheria ndogo za halmashauri zinazosimamia uendeshaji wa masoko,kuna usimamizi hafifu wa soko kupelekea vizimba kuwa wazi na wafanya biashara wachache kulipa kodi.
Alitaja mambo mengine waliyoyabaini kuwa ni matumizi hayafuati taratibu, mfano ununuzi wa umeme na malipo ya mhudumu, baadhi ya mapato hayaingizwi katika mfumo wa mapato, kama mapato yatokanayo na maji na choo, rejesta ya wafanyabiashara hazihuishwi na kuna malalamiko ya mpango wa uboreshaji wa soko ambapo kila mfanyabiashara atatakiwa kutoa Sh 4,000,000 ili kujengewa kibanda kipya na Halmashauri.
Akizungumzia kuhusu uendeshaji na usimamizi wa vyama vya walimu Manispaa ya Singida alisema wamebaini walimu wanakatwa makato ya CWT bila ridhaa yao na bila kujaza fomu TUF 15, ukinzani wa maslahi, mjumbe wa chama kuhusika katika kupitisha notice pale mwanachama anapotaka kujitoa, Wanachama kuendelea kukatwa kama wanachama wa CWT wakati tayari notisi ya kujitoa uanachama imewasilishwa ofisi ya mkurugenzi na imekubaliwa kwa kutoa uthibitisho wa barua.
Alitaja mambo mengine waliyoyabaini ni kuwepo kwa mkataba wa uwakala baina ya Manispaa ya Singida na chama chenye wanachama wengi ambayo haijapitiwa kwa muda mrefu (kuhuishwa),mwajiri kukata fedha ya uwakala kwa wanachama na kuwasilisha CWT bila kuwa na akaunti maalumu kwa ajili ya fedha ya uwakala na watumishi wa serikali kukaimu nafasi ya katibu nafasi ambayo haipo kisheria .
Akielezea eneo la Uzuiaji Rushwa Widege alisema kwa kuzingatia kwamba miradi ya maendeleo ni mali ya wananchi na Serikali inapeleka fedha nyingi katika eneo hilo, taasisi hiyo mkoani hapa imefuatilia utekelezaji wa miradi Ishirini na nane yenye thamani ya zaidi Sh.Bilioni 3 katika sekta za Elimu na Barabara ambayo inajumuisha miradi ya Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19 na Serikali Kuu.
Aliitaja miradi hiyo na thamani yake
kuwa ni Miradi ya Elimu iliyokaguliwa ilikuwa saba yenye thamani ya Sh.
305,906,524.63. Miradi ya Barabara iliyokaguliwa ilikuwa mitatu yenye thamani
ya shs. 742,786,600.00,Miradi ya Afya iliyokaguliwa ilikuwa kumi na moja yenye
thamani ya Sh. 2,036,228,500.
Alisema ufuatiliaji mwingine
uliokaguliwa ulikuwa ni matumizi ya asilimia kumi ya mapato ya ndani
ya Halmashauri za Singida, Manyoni, na Ikungi
kwa ajili ya makundi maalumu (wanawake,
vijana na watu wenye ulemavu) ambapo kiasi cha Sh.
422,331,613.00 kilitengwa.m
Alitaja miradi mingine mitano iliyokaguliwa
yenye thamani ya Sh. 1,279,506,500 na kukutwa na ilikutwa na mapungufu
mbalimbalimbali kuwa ni ujenzi wa Kituo cha Afya Kisiriri katika Halmashauri ya Wilaya ya Iramba ambayo ilipokea Sh. 500,000,000.
Alisema
mradi huo umechelewa kukamilika bila
sababu zozote za kitaalamu kubainishwa na umekuwa na usimamizi usiokidhi
viwango.
Alisema katika ufuatiliaji wa matumizi ya asilimia kumi ya mapato ya ndani ya nyaraka kwa ajili ya makundi maalum vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika Halmashauri ya Wilaya ya Iramba walibaini kutekeleza miradi kinyume na andiko la maombi, ucheleweshaji wa nyaraka kwa walengwa na ukosefu wa nyaraka katika kikundi husika ambapo Takukuru iliwashauri wahusika kuhakikisha wanafuata sheria kauani na taratibu zilizowekwa.
Katika
ufuatiliaji wa matumizi ya fedha hizo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
ambapo Sh.Milioni 52
zilitengwa walibaini walengwa
kupewa fedha kidogo tofauti na maombi yao.
Alitaja mradi mwingine kuwa ni ujenzi
wa Zahanati ya Kijiji cha Wembere katika Halmashauri ya Wilaya ya Iramba ambayo ilipokea Sh.Sh. 271,000,000 Mradi umechelewa kukamilika bila sababu zozote za kitaalamu kubainishwa.
Mradi
mwingine ambao ulionesha kutokidhi viwango ni ujenzi wa kivuko cha chini cha
watembea kwa miguu Kibaoni-Manispaa ya Singida ambao gharama yake ni Sh.
Milioni 388
uliotekelezwa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuwa na baadhi ya maeneo yalionekana kuwa na ukamilishaji
usiokuwa mzuri.
Mradi
mwingine ni ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Tutu katika Halmashauri ya Wilaya ya Iramba ambao umegharimu
Sh.68,506,500
kutotekelezwa kwa kiwango
kilichotarajiwa na Wananchi waliochangia fedha pamoja na Serikali.
Widege alisema Takukuru Mkoa wa Singida wamefanya Warsha
nne kuhusiana na chambuzi za mifumo zilizofanyika kwa kushirikiana na wadau
kama kikao cha kujadili mianya ya rushwa iliyobainika katika uchambuzi wa mfumo
wa usimamizi wa fedha za miradi ya maji chini ya kamati za maji za jumuiya ya
watumia maji.
Kikao cha kujadili mapungufu mbalimbali yaliyobainishwa kupitia miradi ya Afya, elimu na Barabara kwa Wilaya ya Singida.
Kikao cha kujadili matokeo ya uchambuzi wa mfumo wa
uendeshaji wa masoko katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni.
Kikao cha kujadili kuhusu mapungufu yaliyobainika katika manunuzi ya umma katika miradi ya maendeleo ya halmashauri ya wilaya ya Ikungi.
Widege alisema ufuatiliaji wa utekelezaji wa maazimio hayo
ulifanyika kupitia kikao cha wazazi na Kamati ya Shule ya Msingi Bomani Halmashauri
ya Wilaya ya Iramba.
Vikao vilivyojadili mapungufu mbalimbali yaliyobainishwa
kupitia miradi ya Afya, Elimu na Barabara kwa Wilaya ya Singida.
Kikao kilichojadili
mianya ya rushwa katika ukusanyaji wa michango kwenye minada na kikao
kilichojadili mianya ya rushwa katika ukusanyaji wa mapato kwa njia ya POS.
Alisema kupitia Programu ya TAKUKURU RAFIKI yenye lengo
la kuongeza wigo wa kuwashirikisha wadau kwenye mapambano dhidi ya rushwa kwa
kutumia njia za kuzuia na kupambana na rushwa katika utoaji wa huduma za
kijamii na utekelezaji wa miradi ya maendeleo. vikao 10 na wadau vilifanyika
katika kata 10 ambapo wadau waliibua kero 140. Ambapo
Idadi ya kero zilizotatuliwa ni 41.
Akizungumzia elimu kwa umma alisema inafanyika ili kuielimisha jamii kuhusu madhara ya rushwa kwa jamii na Taifa kwa ujumla. Elimu kwa umma pia inafanyika kwa madhumuni ya kuipa jamii uelewa na hivyo kuihamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa.
Alisema Takukuru Mkoa wa Singida kupitia Dawati la Elimu
kwa Umma hutumia mbinu mbalimbali katika kuelimisha kwa kuwashirikisha
wanajamii wa makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na vijana wa shule za Msingi,
Sekondari, Vyuo, Watumishi wa Umma na jamii kwa ujumla.
Akielezea kuhusu uchunguzi na mashitaka alisema jumla ya taarifa za malalamiko 47
yalipokelewa ambapo taarifa 31 zilihusu vitendo vya rushwa na taarifa 16
hazikuhusu vitendo vya rushwa.
Alisema mkakati wa utendaji kazi wa Takukuru Mkoa wa Singida kwa robo ya nne ya mwaka 2022/2023 inayoanzia Aprili hadi Juni, 2023 ni kufuatilia matumizi ya fedha za Serikali zinazoelekezwa Mkoa wa Singida kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo hasa fedha za Mradi wa “BOOST’’
Kuzuia rushwa kwenye hutoaji wa huduma, kufanya uchunguzi pale itakapobainika kuwa katika ufuatiliaji huo wa matumizi ya fedha za Serikali zinazoelekezwa Mkoa wa Singida vitendo vya rushwa vimejitokeza; na kuendelea na uelimishaji unaolenga kushirikisha jamii katika uzuiaji wa vitendo vya Rushwa ikiwa ni pamoja na kuendelea kutekeleza Programu ya Takukuru – Rafiki.
Widege alisema Takukuru Mkoa wa Singida inatoa rai kwa wananchi wote kwa ujumla kujiepusha na vitendo vya Rushwa na kushiriki kikamilifu katika Kuzuia vitendo vya Rushwa vinavyotokea katika maeneo mbalimbali ya kutolea huduma za kijamii na miradi ya maendeleo.
Aidha, aliwataka wananchi kutoa taarifa za vitendo vya Rushwa kwa njia mbalimbali ikiwemo,
kufika Ofisi za Takukuru Singida Mkoa na Wilaya Iramba.Ikungi, Mkalama na
Manyoni na kupiga simu ya bure 113 au kupiga simu kwa Mkuu wa Takukuru Mkoa wa
Singida Namba 0738-150-208, Mkuu wa Takukuru Mkalama 0738150 212, Mkuu wa
Takukuru Ikungi 0738150 213, Takukuru
Iramba 0738 -150 210 na MkuuTakukuru Manyoni 0738-150 211 na kuhakikisha
wanatoa ushirikiano kwenye uchunguzi na kushiriki kutoa ushahidi Mahakamani.
Aidha Widege alisema katika Mkoa wa
Singida, kama ilivyo kwa mikoa mingine, kumekuwepo na wimbi la watu
wanaojifanya Maafisa wa Takukuruna kujipatia fedha kwa kuwahadaa kuwa wanaweza
kuwasaidia kupata huduma au nafuu zozote kutoka mamlaka mbalimbali za Serikali.
Takukuru Mkoa wa Singida inawataadharisha matapeli wote wanaowatapeli au wanaopanga kuwatapeli wananchi kwa kujifanya Maafisa wa taasisi hiyo au vyombo vingine vya dola kuacha kwa sababu watakapobainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ikiwemo kuwafikisha Mahakamani.
Kaimu Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Singida, Sifa Mwanjala, akijitambulisha kwa waandishi wa habari wakati wa mkutano huo ambapo aliwaomba waendelee kushirikiana na taasisi hiyo katika kutangaza kazi mbalimbali inazozifanya za kuzuia na mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa..
Maafisa wa Takukuru Mkoa wa Singida wakiwa kwenye mkutano huo na waandishi wa habari.Maafisa wa Takukuru wakiwa kwenye mkutano huo.
Mkutano ukiendelea.
Taswira ya mkutano huo.
No comments:
Post a Comment