DAKTA, MPANGO AWEKA JIWE LA MSINGI BARABARA YA MIANZINI-NGARAMTONI JUU KM 18 - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday 20 May 2023

DAKTA, MPANGO AWEKA JIWE LA MSINGI BARABARA YA MIANZINI-NGARAMTONI JUU KM 18

Makamu wa Rais Dakta, Philip Mpango akisisitiza jambo kwa wananchi hawapo pichani wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi ujenzi wa barabara ya Mianzini-Ngaramtoni juu KM 18 wilayani Arumeru mkoani Arusha.

Makamu wa Rais Dakta, Philip Mpango akisalimiana na Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya (wapili kulia), na viongozi wengine alipokwenda kuweka jiwe la msingi ujenzi wa barabara ya Mianzini-Ngaramtoni juu KM 18 wilayani Arumeru mkoani Arusha.



Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya akifafanua jambo wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi ujenzi wa barabara ya Mianzini-Ngaramtoni juu KM 18 wilayani Arumeru mkoani Arusha.

MAKAMU wa Rais Dkt. Philip Isdor Mpango amezungumzia umuhimu wa wananchi kutumia kwa usahii barabara zinazojengwa kwa kiwango cha lami ili kuepuka ajali na kuzilinda barabara hizo kwa kutunza mazingira.

Akizungumza wakati akiweka jiwe la msingi barabara ya Mianzini-Ngaramtoni juu KM 18 inayojengwa kwa kiwango cha lami jijini Arusha Dakta, Mpango amesema ni vema jamii ikatambua kuwa barabara zinajengwa kwa fedha nyingi za wananchi hivyo wanalazimika kuzilinda na kuzitunza ili zidumu na kuleta tija kwa wananchi.

“Tunajenga barabara za lami kila mahali hivyo nitoe wito kwa watumiaji wa barabara kuwa makini na kuendesha vyombo vya moto kwa tahadhari ili kuepuka ajali, ulemavu na vifo na wananchi kuacha shughuli za binadamu zinazofanyika kwenye njia za maji kwani husababisha mafuriko wakati wa mvua  na kuharibu barabara”, amesisitiza  Makamu wa Rais Dakta, Mpango.

Aidha amemtaka mkandarasi anayejenga barabara hiyo kutoa kipaumbele cha ajira wa vijana wa mkoa wa Arusha ili waweze kunufaika kiuchumi na kitaalam na hivyo kuulinda mradi huo.

Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya amesema barabara Mianzini-Ngaramtoni juu KM 18 ikikamilika licha ya kupunguza msongamano katikati ya jiji la Arusha pia itawezesha wafanyabiashara na watalii kufikia masoko na vivutio vya utalii kwa urahisi.

“Ujenzi wa barabara hii unalenga kuzifungua barabara za Wilaya ya Arumeru kwa kupita katika maeneo ya uzalishaji na hivyo kukwepa msongamano katikati ya jiji la Arusha”, amesisitiza.

Mtendaji Mkuu wa TANROADS Eng. Rogatus Mativila amesema ujenzi wa barabara ya Mianzini-Ngaramtoni juu KM 18 umegawanywa katika sehemu tano ili kurahisisha kazi ya ujenzi na utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 22 utakapokamilika.


No comments:

Post a Comment