WABUNGE wameishauri Serikali kuanza kufikiria kujenga barabara za tozo zitakazo kuwa njia nyingine mbadala wa kuwaingizia fedha za ukarabati wa barabara zake. Ushauri huo umetolewa leo na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu jijini Dar es Salaam alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara njia nane kutoka Kimara jijini Dar es Salaam hadi Kibaha mkoani Pwani, ambao kwa sasa umekamilika kwa kiasi kikubwa.
Akizungumza mara baada ya kutembelea mradi wa barabara hiyo ya njia nane kilomita 19.2 kutoka Kimara hadi Kibaha, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Selemani Kakoso alitolea mfano ujenzi wa barabara hizo tangu awali ungeainisha barabara moja ya kulipia ambayo ingekuwa ikiipatia fedha Serikali na kutumika kwa ajili ya ukarabati.
"...Wajumbe hapa wameelezea umuhimu wa kuanza na barabara zenye tozo, mimi naamini kabisa kama tungekuwa tumejipanga kwa hizi hizi njia nane ni lazima tungekuwa na njia ambazo nyingine ni za kulipia, yaani barabara za tozo ili tuongeze mapato duniani kote barabara nyingi zinajengwa kwa mfumo huu.
Sheria inatukataza kujenga barabara za tozo kama hauna barabara mbadala lakini hapa kuna njia mbadala kwanini msingelianza na hizi hapa tukawa na barabara za kulipia. Hii ni sawa na lile Daraja la Tanzanite tuliishauri Serikali wangelifanya kuwa la tozo yaani kila anayepita atozwe maana daraja mbadala ambalo ni Salender lipo, kwa hiyo lazima haya myafanyie kazi," alishauri Mhe. Kakoso.
Alisema kamati yake inaunga mkono juhudi zote zinazofanywa na Serikali katika uboreshaji wa miundombinu hasa ubunifu uliofanywa katika mradi wa Barabara ya njia nne kutoka kimara hadi Kibaha unaojengwa na kampuni ya Kitanzania (Mkandarasi ESTIM) chini ya usimamizi wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kwani wananchi wanatamani wapate huduma nzuri na endelevu.
Hata hivyo alishauri barabara zinazojengwa kuwa na mfumo mzuri wa mifereji ya maji ya mvua ili mvua zinaponyesha kipindi cha mvua maji yaweze kuchukuliwa na kupelekwa sehemu stahiki, kwani kutokuwa na mifereji bora kunasababisha maji hayo kwenda hovyo pembezoni mwa barabara na wakati mwingine kwenda kwenye makazi ya watu na kuwa kero.
"Barabara mnazijenga vizuri lakini pamoja na uhimarishaji mzuri wa barabara zetu lazima mjenge mifereji mizuri ya maji taka kwa ajili ya kuzilinda," alisema Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Kakoso.
Awali akiwasilisha maendeleo ya mradi huo kwa wabunge, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Rogatus Mativila alisema ujenzi wa barabara ya njia nne Kimara – Kibaha (km 19.2) chini ya Mkandarasi ESTIM umekamilika kwa asilimia 98 hadi sasa na kinachomaliziwa ni ufungaji wa taa za pembezoni mwa barabara hiyo.
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasilino Wakala wa Barabara nchini (TANROADS).
No comments:
Post a Comment