RUTH ZAIPUNA: MIAKA MIWILI YA MAFANIKIO MAKUBWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 20 March 2023

RUTH ZAIPUNA: MIAKA MIWILI YA MAFANIKIO MAKUBWA

TAREHE 19 ya mwezi Machi, ni siku muhimu sana kwa taifa letu, watu wake na historia ya nchi yetu. Kama nchi, tunaungana kusherehekea kwa dhati mafanikio na hatua muhimu za utawala wa mwanamke shupavu. Mwaka huu, tunaadhimisha miaka miwili ya uongozi uliotukuka na mabadiliko chanya tangu Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan aingie madarakani.

Utekelezaji wa ajenda ya diplomasia ya uchumi, juhudi endelevu za kuboresha mazingira ya biashara, na jitihada zake sahihi za kuleta zama mpya ya kisiasa nchini kupitia falsafa inayozingatia Maridhiano, Uthabiti, Mageuzi na Kujenga Upya nchi kwa pamoja, kumelifanya  taifa kuchukua uelekeo wa maendeleo ya kiuchumi na ustawi jumuishi.

Kwa hakika, miaka miwili ya kwanza ya utawala wa Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan inaweza kuelezewa kama kipindi cha mambo matano yafuatayo:

Kuimarisha, Kufufua na Kuweka Msingi wa Ukuaji endelevu wa Uchumi

Azma mpya ya Diplomasia ya Uchumi kama chanzo cha ukuaji na ustawi

Mageuzi ya ya Kisiasa yanayolenga kujenga umoja wa kitaifa, utawala bora na demokrasia

Juhudi za makusudi na za pamoja kuleta usawa wa kijinsia na maendeleo ya kiuchumi kwa wanawake

Ufanisi wa kihistoria wa kiutendaji wa sekta ya kibenki Tanzania

Kimarisha Kuufufua na kuweka Msingi wa Ukuaji wa Uchumi wa Muda Mrefu Baada ya Uviko-19

Mwaka 2021 wakati Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani, dunia ilikuwa imegubikwa na Janga la Uviko-19. Katika mazingira hayo, azma yake kubwa ya muda wa kati ikawa kuulinda uchumi wa Tanzania dhidi ya athari za Uviko huku kipaumbele chake cha muda mrefu kikiwa ni kujenga uchumi upya kwenye msingi mpya (wa Diplomasia ya Uchumi).

Kupitia sera rafiki za kibiashara na zenye manufaa makubwa, Mheshimiwa Rais Dkt Samia ameiongoza nchi kuwa na mazingira tulivu ya uendeshaji biashara yanayolenga ukuaji unaoongozwa na ushirikiano na sekta binafsi.

Hatua alizozichukua kuchochea shughuli za kuongeza kipato baada ya Janga la Uviko-19  zimechangamsha sekta nyingi na kuimarisha utendaji wa benki za biashara ambazo ni kiunganishi muhimu cha wenye amana na wanaohitaji mikopo kwenye uchumi wa nchi.

Katika kuitafakari miaka miwili ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi Ruth Zaipuna, anautaja muda huo kuwa ni “kipindi cha mafanikio makubwa” huku akiwa na matarajio lukuki kwamiaka ijayo.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi Ruth Zaipuna.

Bi Zaipuna amesema katika kipindi hichi cha miaka miwili sekta ya kibenki Tanzania imeendelea kuwa imara, tulivu na yenye faida. 

Sekta imetoka kwenye msukosuko wa ugonjwa wa UVIKO-19 ikiwa imara, na ikiwa na mizania (balance sheet) iliyokua kwa kiwango cha asilimia 19 kwa muhula kufikia rekodi ya mali yenye thamani ya Shilingi Trilioni 45.99.  

Sekta ya kibenki pia imeweka rekodi ya faida Shilingi Trilioni 1.7 kabla ya kodi kwa mwaka 2022. 

Katika hali ya kuimarika kwa mazingira ya biashara, Benki ya NMB imeendelea kuwa kiongozi kwenye soko kwa kuweka rekodi ya faida ya Shilingi Bilioni 426 baada ya kodi kwa mwaka 2022. Hii ni faida kubwa zaidi kuwahi kufikiwa na benki katika miaka 25 ya historia yake na inawakilisha ongezeko la asilimia 47 mwaka hadi mwaka, ukuaji wa kihistoria ukilinganisha na benki nyingine katika ukanda huu wa Afrika Mashariki .

“Utendaji huu umechangiwa na mazingira wezeshi ya biashara nchini pamoja na maono ya NMB katika kutoka suluhu imara za kifedha kwa wateja wake na jamii kwa ujumla,” alisema Bi Zaipuna.

Makala haya yamezungumza kwa kina na Zaipuna kuhusu uongozi wa Rais Samia katika miaka hii miwili. Fuatilia mazungumzo haya kufahamu mtizamo wa mkurugenzi huyu mwanamke anayeiongoza taasisi kubwa ya fedha nchini.

Tangu aingie madarakani Machi 2021, uongozi wa Rais Dr Samia Suluhu Hassan umekuwa ukihamasisha biashara na uwekezaji. Kwa kifupi, unazionaje sera za uongozi wa Rais Samia na sera zake za kuimarisha mazingira ya biashara nchini hasa kwa utendaji wa benki za biashara?

Sera za Serikali kuhamasisha biashara na uwekezaji zimeendelea kuwa na manufaa kwenye uchumi wa Tanzania ambao kwa mwaka 2022 pato la Taifa lilikua kwa asilimia 4.5 likichangiwa zaidi na ufanisi ulioshuhudiwa kwenye sekta mbalimbali muhimu.

Kwa kipindi hiki, mfumuko wa bei umeendelea kuhimilika na kufikia asilimia 4.8 Desemba 2022 ambao ulikuwa ni wa chini zaidi kwa ukanda wa Afrika Mashariki. Hili lilitokana na juhudi za Serikali kupunguza makali ya bei ya bidhaa za zilizoagizwa kutoka nje pamoja na mahitaji ya kila siku ya watu.

Kutokana na mazingira rafiki yaliyopo, sekta ya kibenki imeendelea kukua kwa kasi nzuri. Mwaka 2022 faida ya jumla ya sekta hii ilivuka Shs trilioni 1 kwa mara ya kwanza katika historia ya mabenki Tanzania na kufika Sh1.2 trilioni.

Thamani ya mali za benki pamoja na amana za wateja nazo zimeimarika sambamba na ubora wa mali hizo huku ikishuhudia uwiano wa mikopo isiyolipika ikilinganishwa na jumla ya mikopo yote iliyotolewa ukishuka mpaka asilimia 5.8 Desemba 2022 kutoka asilimia 8.5 katika kipindi kama hicho mwaka 2021. Upatikanaji wa huduma za fedha umeendelea kuimarika nchini, ukishuhudia kuongezeka kwa miamala ya wateja hasa wanaotumia huduma mbadala za kibenki

Mikopo iliyotolewa kwa sekta binafsi iliongezeka kwa asilimia 22.5 kwa mwaka mpaka Desemba 2022 hali inayodhihirisha kurejea kwa shughuli za uchumi baada ya janga la Uviko-19 lililosababisha kudorora kwa biashara duniani. Haya yote yametokea kutokana na sera nzuri za fedha na kodi. Kukuaji umekuwa mzuri kwenye sekta nyingi muhimu nchini, huku mikopo iliyotolewa kwenye sekta ya kilimo ikipanda kwa kasi kubwa. Kwa ujumla, sekta ya kibenki imeendelea kuwa imara licha ya vihatarishi vilivyojitokeza, na benki zenyewe zikibaki na mtaji wa kutosha. Benki zimeendelea kuwa na ukwasi unaokubalika kisheria na zinapata faida inayoongezeka kila mwaka. Matarajio ni mazuri kwa siku zijazo.

 
Benki ya NMB ikisaidia utekelezaji wa miradi ya kijamii ikiwemo elimu. 

Kutokana na uchumi wa Taifa kukua, sekta ya kibenki imenufaika kwa kuongeza ukopeshaji na kuwafungulia wajasiriamali wengi zaidi fursa za kukuza miradi yao. Rais Samia amekuwa akisisitiza ukuaji endelevu wa uchumi katika mazingira rafiki. Benki ya NMB kama mbia wa kimkakati katika kuhamasisha ajenda za Mazingira, Jamii na Utawala (ESG), imekuwa ikitoa dhamana za benki  kwa Utaratibu huu umewezesha kuhamasisha maendeleo endelevu huku benki ikiendelea kutoa mikopo kwa wateja wake.       

Miezi minne tu baada ya Dr Samia kuapishwa kuwa Rais (Julai 2021), Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilichukua hatua kadhaa ikiwamo kutenga Sh1 trilioni maalumu kwa ajili ya kuzikopesha benki na taasisi za fedha nchini ili izikopeshe kwa sekta binafsi – katika jitihada za kuongeza ukwasi sokoni na kuimarisha ukopeshaji. Kwa mtizamo wako, unaona hatua hizo zimekuwa na manufaa yoyote hasa katika ukopeshaji wa benki na taasisi za fedha, Benki ya NMB ikiwa mfano?

Fungu hili maalumu lililotengwa na Serikali na kuwekwa Benki Kuu ya Tanzania limekuwa na mchango mkubwa katika ukopeshaji hasa kwa wajasiriamali wadogo,  na wa kati (MSME). Mara nyingi, biashara hizi hukumbwa na changamoto zinapotafuta mikopo kutokana na uchanga wao na kukosa dhamana. Hata hivyo, kutokana na fungu hili lililotolewa kwa benki na taasisi za fedha nchini, liliongeza kiasi cha fedha zilizopo kwa ajili ya kuzikopesha kwa wajasiriamali waliokusudiwa hivyo kuwawezesha kupanua biashara zao na kutoa ajira nyingi zaidi.

Hii imekuwa muhimu hasa kwa kipindi hiki cha mdororo wa uchumi duniani kinachoshuhudia biashara nyingi ndogo zikihangaika kufufuka kutokana na athari za janga la Uviko-19. Kwa NMB, fungu hili lilielekezwa kwa wateja wetu waliopo kwenye sekta ya kilimo ambayo ndio sekta kubwa zaidi kuliko zote ikiajiri zaidi ya asilimia 60 ya nguvukazi iliyopo.

Katika miaka miwili iliyopita, Benki ya NMB ilitenga Sh100 bilioni maalumu kwa ajili ya kuzikopesha kwa mnyororo wa biashara zilizopo kwenye sekta ya kilimo kwa riba ya asilimia tisa kwa mwaka. Baadaye tuliongeza kiasi kingine, Sh150 bilioni na kufanya jumla ya mikopo hii yenye riba nafuu kuwa Sh250 bilioni. Mpaka sasa, zaidi ya asilimia 93 ya kiasi hicho kimeshakopeshwa kwa wahitaji.

Fungu hili limeisaidia benki kuimarisha utoaji na kurahisisha upatikanaji wa mikopo hivyo kuchangia ukuaji wa sekta, kuongeza uzalishaji kwenye mnyororo wa thamani wa sekta ya kilimo, na ajira kwa vijana.

Kwa ujumla, fungu hili maalumu lililotengwa na Serikali limechangia kwa kiasi kikubwa ukopeshaji wa wajasiriamali wadogo na wa kati ambao ndio wengi nchini na wanaoendesha uchumi wa Taifa wakiongoza kwa kutoa ajira nyingi pia. Uwezeshaji huu wa ukopeshaji utakuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi kwa muda mrefu ujao.

Katika kipindi hiki, Benki ya NMB imeendelea kuwa mbia muhimu wa maendeleo kwa kuwezesha miradi iliyopo kwenye sekta ya nishati kwa kutoa Sh300 bilioni. Vilevile, tulitoa Sh100 bilioni kwenye mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Mwendo Kasi) na Sh50 bilioni kwenye miradi ya ujenzi wa nyumba.

Licha ya kuongezeka kwa faida, mikopo iliyotolewa na amana za wateja, miaka miwili iliyopita imeshuhudia kushuka kwa kiwango cha mikopo chechefu. Unadhani kwa kiasi gani sera za Rais Samia zimechangia kufanikisha hili?

Kwa ujumla, sera za Mheshimiwa Rais Samia zimekuwa na mchango mkubwa katika kushusha kiwango cha mikopo isiyolipika nchini na Benki ya NMB kimahsusi katika miaka miwili iliyopita. Pamoja na sababu nyingine mfano usimamizi makini uliofanywa na uongozi wa Benki lakini mazingira rafiki ya kufanya biashara yamekuwa na mchango mkubwa.

Sera za Mheshimiwa Rais Samia zimekuwa na mchango mkubwa katika kuchochea shughuli za uchumi na maendeleo ambazo zimeongeza urejeshaji wa mikopo iliyotolewa hivyo kushusha kiwango cha mikopo chechefu. Vilevile, kuchukuliwa kwa hatua mahsusi kama vile kutengwa kwa fungu maalumu kwa ajili ya sekta ya kilimo na ujenzi kulikofanywa na Serikali ili kuziongezea benki ukwasi, kulirahisisha upatikanaji wa mikopo kwa wajasiriamali.

Mtizamo wa Rais Samia kuhamasisha ujumuishaji wananchi kwenye huduma za fedha na kupanuka kwa upatikanaji wa huduma hizo kumechangia pia kushusha kiwango cha mikopo isiyolipika. Vilevile, juhudi za Serikali kuimarisha sheria na kanuni zinazoongoza sekta ya benki kumesaidia kuondoa baadhi ya changamoto zilizokuwa zinachangia kuifanya mikopo isilipike, ukiwamo usimamizi duni wa vihatarishi vya mikopo.

Kwa ujumla, sera za Rais Samia zimekuwa muhimu katika kuweka mazingira rafiki kwa benki kufanya biashara zao hivyo kuimarisha utoaji mikopo na urejeshaji wake hivyo kupunguza mikopo chechefu. 

Tukiangalia miaka miwili ijayo kutoka sasa, unaionaje sekta na Benki ya NMB hasa kwenye suala la ufanisi?

Kutokana na mafanikio niliyoyaeleza wakati najibu maswali yaliyotangulia, benki za biashara ikiwamo NMB zimeshuhudia kuongezeka kwa mikopo inayotolewa, amana za wateja na faida huku uwiano wa mikopo isiyolipika ikishuka. Kwa mfano, mpaka Desemba 2022, uwiano wa mikopo chechefu wa Benki ya NMB ulikuwa asilimia 3.3 ambazo ni chini ya asilimia tano ambao ni ukomo unaopendekezwa na Benki Kuu.

Nikiitizama miaka kadhaa mbele kutoka sasa, iwapo hali hii ya kuimarika kwa uchumi itaendelea na Serikali ikazidumisha sera zake za kuwezesha biashara, sekta ya kibenki itaendelea kufanya vizuri. Kwa kuongezea, fedha zilizotolewa na Benki ya Dunia hivi karibuni kufanikisha upatikanaji wa maji, miradi ya mazingira na afya, zitakuwa na mchango mkubwa kwa nguvukazi, ufanyaji biashara, na uchumi mzima kwa ujumla.

Utekelezaji wa mpango mkakati wetu wa muda wa kati ni kipaumbele cha kwanza. Tutaendelea kuwekeza kwenye maeneo tunayofanya vizuri ili kuimarisha mizania yetu, kuwa na mtaji wa kutosha, mtandao wa matawi yetu pamoja na huduma za kidijitali kufanikisha malengo yetu ya kibiashara.  

Tutaendelea kusimamia ajenda ya ujumuishaji wananchi katika huduma za fedha huku tukitoa huduma bora zaidi kwa wateja wetu. Tunajielekeza katika kuhakikisha wanahisa wetu wanapata faida nzuri tukijipanga kuendelea kuwahudumia kwa ubora wateja wetu tukielekea robo ya pili ya mwaka 2023 na kuendelea. 

Benki ya NMB imefanya nini kusaidia utekelezaji wa miradi ya kijamii ndani ya miaka miwili iliyopita chini ya uongozi wa Rais Samia? Mmetumia kiasi gani kufanikisha miradi hiyo ya kijamii katika miaka hii miwili?

Uwekezaji kwenye miradi inayoisaidia jamii umekuwa ni utaratibu wetu ambao tunauendeleza siku zote. Tumekuwa tukitenga asilimia moja ya faida ya benki baada ya kodi kila mwaka kwa ajili ya kufanikisha hili. Kwa miaka miwili iliyopita ya uongozi wa Rais Samia, tumewekeza zaidi ya Sh5 bilioni kufanikisha maeneo matano ya kipaumbele kwa jamii ambayo elimu, afya, mazingira, kilimo na kukabili majanga. Tunafanya hivi kuhakikisha tunaleta matokeo chanya kwa jamii tunayoihudumia.

Kwa mwaka 2022 pekee, tumetumia zaidi ya Sh2.9 bilioni kwenye miradi ya kijamii katika sekta ya elimu kwa kuchangia madawati 68,850 katika shule 459 hivyo kuwanufaisha zaidi ya wanafunzi 206,500. Vilevile, tulitoa msaada wa vitanda 720 vilivyowanufaisha wanafunzi 1,440 wa bweni. Kwenye sekta ya afya nako, tulivisaidia vituo 42 vya afya kwa kuvipelekea vitanda vya wagonjwa, vitanda vya kujifungulia pamoja na mashuka hivyo kuwanufaisha zaidi ya watu 210,000. Kuhusu elimu ya fedha, program zetu za Wajibu na GonaNMB zilitoa majukwaa kwa wananchi hasa vijana kujengewa uwezo. Zaidi ya watu 147,630 wakiwemo vijana walinufaika na elimu hii.

Kwa kipindi chote hiki, tumeendelea kuchangia kuwawezesha wanawake kufanikisha malengo yao kwa kukusanya Shs bilioni moja tulizozielekeza kwenye matibabu ya wenye Fistula. Fedha hizi zilizotolewa kipindi cha uongozi wa Rais Samia, zilipatikana kwenye “Mwendo wa Upendo Marathon.”

No comments:

Post a Comment