Na Elimu ya Afya Kwa Umma
IKIWA Wizara ya Afya inaendelea na kampeni ya chanjo ya Surua kwa watoto waliochini ya umri wa miaka 5 Kwa njia ya magari ya matangazo, Mganga wa Tiba Asili katika kijiji cha Ikulwe kata ya Majimoto Halmashauri ya Mpimbwe Wilayani Mlele Mkoani Katavi Mihangwa Lubana ari maarufu Halawa amehamasika na kuruhusu watoto wake 12 kupatiwa chanjo ya Surua.
Akizungumza nyumbani kwake mara baada ya kutembelewa na wawakilishi kutoka wizara ya afya pamoja wawakilishi kutoka Halmashauri ya Mpimbwe, Lubana amesema amepata hamasa hiyo baada ya kupata ujumbe wa elimu ya ugonjwa na hamasa ya chanjo ya Surua unaotolewa na Elimu ya Afya kwa Umma, Idara ya Kinga, Wizara ya Afya Kwa njia ya Magari kwa ushirikiano na Halmashauri ya Mpimbwe.
"Nimekuwa nikisikia tu matangazo kwenye magari na ujumbe mkubwa nilioupata ni kwamba si Magonjwa yote yanatibiwa kwa waganga wa Tiba Asili hasa ugonjwa wa Surua, hivyo naishukuru sana Wizara ya Afya kwa kuniletea huduma hii nyumbani kwangu" amesema Lubana.
Aidha, Lubana ametoa wito kwa waganga wa Tiba Asili wengine kuacha kuwarubuni na kuwakataza watu kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya pindi watoto wao wanaposumbuliwa na maradhi mbalimbali.
"Unakuta Mganga mwingine anajua kabisa ugonjwa alio nao mteja hawezi kumtibu kama vile Surua hivyo nawasihi na waganga wenzagu wa Tiba Asili tusiwang'ang'anie wateja, tufunguke tuwe wa wazi kuwaambia Ili watoto waweze kupata huduma za Afya mapema" amesema.
Naye mke wa Halawa kati ya wake watatu, Holo Salu amesema hatua inayofanywa na Wizara ya Afya ya kutembea nyumba kwa nyumba kutoa huduma ya chanjo ya Surua itafikia watoto wengi hasa Sehemu za vijijini .
"Hatua hii ya Wizara ya Afya ya kampeni ya chanjo ya Surua itafikia watoto wengi naipongeza sana Wizara ya Afya kwa Msaada wenu watoto wangu wote wamepata chanjo"amesema Holo.
Mmoja wa wananchi aliyepata fursa ya kupatiwa chanjo watoto ya Surua watoto wake baada ya kuliona gari la matangazo na kulifuata Mayunga Matondo mkazi wa Migunga B amesema ameamua kuwaleta watoto kupata chanjo baada ya kupata elimu ya uhamasishaji wa chanjo.
“Ninashukuru sana kwa kuwapatia chanjo watoto wangu nina imani sasa watakuwa na kinga dhidi ya Surua nawasihi wazazi wengine wawapeleke watoto kupatiwa chanjo ya Surua” amesema.
Ikumbukwe kuwa kampeni ya uhamasishaji wa chanjo ya Surua kwa watoto waliochini ya umri wa miaka 5 Mkoani Katavi ilizinduliwa hivi karibuni na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu baada ya kuripotiwa watoto 13 kupoteza Maisha Halmashauri ya Mpimbwe kutokana na ugonjwa huo.
No comments:
Post a Comment