HUMAN LIFE INTERNATIONAL LAWATAKA WAZAZI KUEPUKA MANENO MABAYA MBELE YA WATOTO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday 24 January 2023

HUMAN LIFE INTERNATIONAL LAWATAKA WAZAZI KUEPUKA MANENO MABAYA MBELE YA WATOTO

Wakufunzi wa Pro-Life kutoka Mikoa mbalimbali katika Picha ya Pamoja na Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Kutetea Uhai (HLI) Emil Hagamu na Paroko wa Parokia Teule ya Mtakatifu Anthony Padua Vigowa Jimbo Kuu la Dar es Salaam Padri Constantine Baraka, O.FM Cap.

Na Frida Manga, Dar es Salaam

SHIRIKA la Kimataifa la Kutetea Uhai la Human Life International (HLI) limewataka Wazazi na Walezi kuepuka kutoleana Maneno mabaya mbele ya Watoto (Kukashifiana) kwani Maneno hayo yanaharibu ukuaji wao.

Malezi bora kwa Watoto ndiyo matokeo ya Wazazi na Walezi wa Kesho, ikiwa Wazazi na Walezi watakuwa na Maneno maovu mbele ya Watoto wao basi hao Watoto na wao katika maisha yao watakuwa Wazazi wa aina hiyohiyo, alisema Mkurugenzi wa HLI, Kanda ya Afrika kwa nchi zinazozungumza Kiingereza, Emil Hagamu katika warsha ya tathimini ya utendaji kazi wa Uzazi Wajibifu iliyowashirikisha Wakufunzi wa Shirika hilo, hivi karibuni.

Alisema neno “Mtoto wangu” halipaswi kutumika katika familia, bali wazazi na walezi wanapaswa kusema kwa "Mtoto Wetu”, ikimaanisha mtoto ni wa baba na mama, na hivyo katika malezi Wazazi wote wanahusika na ukuaji wa mtoto ama watoto.

Hagamu aliwataka kuzingatia afya ya Mwili na Roho kwa Watoto wao tangu kutungwa Mimba, Kuzaliwa, kuwahudumia watoto, pamoja na kuwaandaa kwa maisha bora ya baadae. Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo aliwataka Watanzania kutambua mateso, maumivu na hali yeyote ngumu anayopitia Binadamu iwe ni katika ugonjwa, Uzee na hata ulemavu ni mpango na kusudi la Mungu.

"Kutamani kufa, au kuua mtu aliye katika hali ya ugonjwa wa muda mrefu na mateso(yutanasia), Uzee na Ulemavu au kuuza Mtoto aliye tumboni ni chukizo na mbele za Mungu, pia ni Ushetani, Alisema Hagamu.

“Tunapaswa kuheshimu na kuthamini Uhai wa Kila Binadamu katika hali yeyote ile,” Alisisitiza.

Kwa upande wake Mratibu wa Mpango wa Uzazi Wajibifu katika Shirika la Kutetea Uhai Tanzania, (Pro-Life) Elmina Kalunga, alisema uzazi wajibifu unalinda afya ya Mama kwani hazina madhara ya mwili kwa Mama na hata Mtoto na hivyo amewataka wanandoa kutumia njia hiyo katika kupanga uzao ambayo pia hazina gharama kiuchumi.

Alisema licha ya changamoto ambazo wanakutana nazo katika kuelimisha wanandoa namna ya kutumia njia hiyo wajibifu katika kupanga uzao wameendelea kutoa elimu hiyo kwa mafanikio ambapo wanandoa wameona faida ya kutumia njia wajibifu katika kupanga uzao.

Katika Warsha hiyo Wakufunzi wa Pro-Life kutoka Mikoa mbalimbali walielezea changamoto zinazowakabili katika kutelekeza wajibu wa Utume huo, ambapo Lulu Hagamu kutoka Ifakara alisema Imani potofu, ulevi kwa wanaume na kutovumilia husababisha wanandoa kuishia njiani wakati wa mafundisho ya njia wajibifu na ya asili kupanga uzao.

Warsha hiyo ya siku mbili kuanzia Ijumaa Januari 20 hadi Jumamosi Januari 21; 2023 ilifanyika Jijini Dar es Salaam ambapo imehitimishwa kwa Shirika hilo kuweka mpango mkakati wa Utendaji Kazi.


No comments:

Post a Comment