TICTS KUONDOKA BANDARINI KUANZIA JANUARI MOSI, TPA YAWEKA WAZI...! - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday 22 December 2022

TICTS KUONDOKA BANDARINI KUANZIA JANUARI MOSI, TPA YAWEKA WAZI...!

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Juma Kijavara akizungumza mjini Bagamoyo alipokuwa akifunga semina ya siku mbili kwa waandishi wa habari wanaoandika habari za bandari kutoka maeneo anuai yenye bandari nchini Tanzania.
Mgeni rasmi ambaye pia ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Bagamoyo Kasilda Mgeni (katikati walio kaa) pamoja na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Juma Kijavara katika picha ya pamoja na waandishi wa habari wanaoandika habari za bandari kutoka maeneo anuai yenye bandari nchini Tanzania.

MAMLAKA ya Usimamizi Bandari nchini (TPA) imesema imeamua kutoendelea tena kumipangisha Kampuni ya Kimataifa ya Kuhudumia Makontena Tanzania (TICTS) bandarini baada ya mkataba wa awali kumalizika hivyo, kuanzia Januari Mosi shughuli za kampuni hiyo zitasimamiwa moja kwa moja na TPA wenyewe.

Taarifa hiyo imetolewa na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Juma Kijavara mjini Bagamoyo alipokuwa akifunga semina ya siku mbili kwa waandishi wa habari wanaoandika habari za bandari kutoka maeneo anuai yenye bandari nchini Tanzania. 

Alisema mkataba kati ya TICS na TPA umemalizika na kwa sasa TPA haiko tayari kupangisha tena eneo hilo bali itafanya kazi hizo chini ya usimamizi wake kwa maboresho zaidi. 

"...Nataka kuweka wazi kuwa mkataba kati yetu na TICS umeisha muda wake na kuanzia Januari Mosi tutaendesha wenyewe shughuli zilizokuwa zikifanywa na kampuni hiyo, na huduma zitaboreshwa zaidi" alisisitiza Mhandisi Kijavara.

Alisema licha ya TPA kuchukua usimamizi wa shughuli hizo wafanyakazi wote waliokuwa wakifanya kazi chini ya TICS wataendelea na kazi zao kama kawaida lakini hivi sasa wakiwa chini ya usimamizi wa TPA yenyewe. 

Alibainisha kuwa kilichomalizika ni mkataba wa TICS na TPA na si shughuli za uhudumiaji wa kontena, hivyo wafanyakazi wote wataendelea na kazi kama ilivyokuwa awali kwa kuwa kinachobadilika hakiathiri shughuli za kuhudumia makotena bandarini. 


No comments:

Post a Comment