Na Frida Manga, Dar
PAROKO wa Parokia ya Mtakatifu Bonaventura Kinyerenzi, Padri Francis Hiza, OFMCap amesema mafanikio siku zote hayaji kwa Nguvu wala mkono wa mtu mwenyewe bali kwa Nguvu za Mungu.
Padri Francis aliyasema hayo wakati akitoa homilia yake kwenye adhimisho la Sadaka ya Misa Takatifu ya kumshukuru Mungu kwa Mahafali ya Wanafunzi wa Shule ya Awali, Msingi na Sekondari ya St. Rosalia iliyoko Kinyerezi Jijini Dar es Salaam.
Alisema ikiwa mafanikio ya mtu hayana Nguvu ya Mungu basi mafanikio hayo ni batili na watu wanaoishi na mafanikio yasiyo na nguvu ya Mungu wanakuwa ni chukizo katika Jamii kwa kufanya mambo maovu.
"Ni vizuri katika Jamii zetu watoto wapewe fursa ya kusoma, kuwa na Elimu nzuri na hatimaye kazi nzuri lakini mambo yote hayo yaambatane na kumtegemea Mungu" Alisema Padri Hiza.
Mbali na kuwapongeza Wakurugenzi wa Shule hiyo Bwana Paul Mfungahema na mkewe Lilian Asela Mfungahema, waalimu, wafanyakazi na Wanafunzi kwa ujumla kwa kumtanguliza Mungu katika mafanikio hayo, Padri Francis amewataka Wahitimu wa Darasa la Saba kusoma kwa bidii na kuendelea kumtanguliza Mungu katika Maisha yao.
Padri Francis anasema yapo mabadiliko chanya kwa mtu anaye mcha Mungu katika Imani yoyote, kwani anakuwa mnyenyekevu, mpole, mtii na Mwenye Afya njema ya roho na mwili na hatimaye anakuwa mtu mwenye mafanikio mazuri yanayompendeza Mungu.
Pia aliwataka wazazi na walezi kuwekeza katika elimu kwa watoto wao na kuhakikisha kwamba wanapata Elimu bora kwa maendeleleo yao kwa sababu kumcha Mungu huleta Baraka na mafanikio katika maisha ya mwanadamu.
Alibainisha kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu wameendelea kuhakikisha kwamba upatikanaji wa elimu bora kwa watoto ni jambo la msingi na la kupewa kipaumbele.
Alisisitiza kwamba kila mtu anapaswa kuhakikisha kuwa elimu anayoipata inamsaidia kuchangia maendeleo ya jamii husika, sanjari na kukuza uelewano, uvumilivu na urafiki kati ya watu na mataifa mbalimbali na kwa njia hii watu wanaweza kujenga misingi ya haki na amani.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shule ya St. Rosalia Paul Mfungahema anasema elimu ya nyakati hizi lazima imuandae mwanafunzi kwa ajili ya maisha ya baadae ambayo hakuna mtu anayeweza kuyatabiri.
Alikazia kwamba maisha ya mbeleni yatatatuliwa na teknolojia ambayo haijagunduliwa bado na ni muhimu kumpa mtoto elimu bora ili kumjengea maisha bora ya baadae na elimu ni lazima ikidhi misingi ya jamii na mahitaji ya mwanafunzi lazima yapewe kipaumbele ipasavyo.
"Shule zetu haziko kwa lengo la biashara tu, bali tunataka kuhakikisha kila Mzazi ama mlezi anatimiza lengo la kumsomesha mwanae kwenye shule bora na kupata elimu bora inayokidhi matakwa ya Dunia na si bora elimu” . Mfungahema alionyesha Taswira
Aliyasema hayo wakati wa sherehe za mahafali ya Tisa kwa Darasa la Saba na ya Saba kwa Darasa la Awali, sherehe zilizofanyika shuleni hapo Jumamosi Oktoba 15; 2022.
Shule ya Awali, Msingi na Sekondari ya St Rosalia ni miongoni mwa wadau ambao wamekuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi za serikali katika sekta ya elimu.
Shule ya St Rosalia ilianzishwa rasmi mnamo 06/01/2014 ikiwa na wanafunzi 20, walimu 6 na wafanyakazi wasio walimu wa 4, na kusajiliwa mwaka huohuo kwa namba ya usajili EM 15952 na hii ni baada ya ukaguzi wa ubora wa shule uliofanyika.
Mfungahema alieleza kuwa kwa sasa Shule hiyo ina jumla ya Wanafunzi 634 wakiwemo Wavulana 298 na Wasichana 336 na idadi ya watumishi 66 kati yao Walimu ni 34.
Miundombinu bora na Moyo wa Ibada uliojengwa kwa wanafunzi wa dini zote na Watumishi ni jambo kubwa wanalojivunia lililosaidia katika maendeleleo ya Watoto kitaaluma pamoja na nidhamu.
“Tunajivunia mafanikio tuliyoyapata tangu kuanzishwa kwa Shule hii, kama vile, kusimamia swala la nidhamu, kuzingatia matakwa ya Taifa katika kutoa elimu bora inayokidhi vigezo na inayo waandaa Vijana kwa elimu ya juu na kuanzishwa kwa Shule ya Sekondari”. Alisema Mfungahema
Mbali na kusimamia ubora wa elimu, Shule hiyo inasimamia vyema suala la usalama na ulinzi wa watoto kwa kufunga camera za CCTV, ili kufuatilia mwenendo wa watoto wawapo katika maeneo ya shuleni.
Elimu kwa maana pana ni tendo au uzoefu wenye athari ya kujenga akili, tabia ama uwezo wa kimaumbile wa mtu binafsi, katika dhana ya kiufundi, elimu ni njia ambayo hutumiwa makusudi na jamii kupitisha maarifa, ujuzi na maadili kutoka kwa kizazi kimoja hadi kingine.
“Elimu ni urithi pekee usio hamishika kwa mwanadamu” alisisitiza Mfungahema, Lengo kuu la elimu ni kuhakikisha kwamba mwanadamu anapata maendeleo endelevu katika maisha yake ya uzima wa sasa na wa baadae, ili kulinda na kudumisha utu wake na kuendelea kuimarisha haki zake za msingi.
No comments:
Post a Comment