Na Eleuteri Mangi-WUSM
MSANII maarufu katika kughani mashairi nchini Tanzania Mrisho Mpoto, maarufu 'Mjomba’ amepeperusha vema bendera ya Tanzania Tamasha la Tano la Sanaa na Utamaduni la Jumuiya ya Afrika Mashariki (JAMAFEST) nchini Burundi.
Msanii Mjomba amekonga nyoyo za washiriki wa Tamasha la JAMAFEST na wananchi wa Burundi kwa wimbo wake wa “Wewe ni nani” wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Evariste Ndayishimiye ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa tamasha hilo.
Akishangiliwa na mamia ya watu waliohudhuria ufunguzi wa tamasha hilo Setemba 5, 2022 katika uwanja wa michezo wa Intwari Bujumbura, Mjomba amesisitiza wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutambua thamani ya utamaduni wao ambao ndiyo alama inayowapa heshima na kujitofautisha na mataifa mengine.
Katika ufunguzi huo, kila nchi mwanachama wa Jumuiya hiyo walikaribishwa kutoa ujumbe na kuburudisha hadhira, ndipo zamu ya Tanzania ilipofika ilikuwa shangwe na nderemo kumuona msanii Mpoto akiingia akiwa taika mavazi ya asili na kucheza kwa mtindo wa Kiafrika kwa kuonesha sarakasi safi, kutumia moto bila kuungua na kuuzima, kuonesha umahiri wa kuchezesha vifaa kwa kutumia miguu ikiwemo kuzungusha ngoma na kubeba meza.
Tamasha la JAMAFEST linafanyika kwa mzunguko ambapo mwaka 2022 ni zamu ya nchini Burundi baada ya kufanyika tamasha la 4 kufanyika kwa mafaniko makubwa jijini Dar es Salaam 2019.
No comments:
Post a Comment